Na Is-haka Omar, Picha na Abeid Machano Kh - Zanzibar.
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM),Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein
amewataka viongozi watakaochaguliwa kupitia Mkutano Mkuu wa Chama katika
Mkoa wa Kusini Unguja, kuwa karibu na wananchi kwa kufuatilia na kushughulikia
matatizo yanayoikabili jamii.
Pia,amefafanua kuwa kila mwanachama anayepata nafasi ya uongozi ndani ya
CCM ni lazima awe na sifa ya kufuatilia masuala mbalimbali hususan kero
zinazowakabili wananchi ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu na
mamlaka husika.
Rai hiyo aliitoa jana wakati akifungua Mkutano Mkuu maalum wa Uchaguzi wa CCM,
katika Mkoa huo, uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Coconut Tree
huko Marumbi Wilaya ya Kati Unguja.
Amewambia wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kuwa wanatakiwa kuwachagua viongozi
wabunifu ambao watanzisha miradi ya maendeleo itakayoongeza nguvu za kiuchumi
ndani ya Chama na kutoa ajira za kudumu kwa wananchi.
Dk.Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
amewasisitiza wajumbe wa mkutano huo kutumia vizuri haki yao ya kikatiba
kwa kuchagua viongozi imara wenye misimamo isiyoyumba katika kusimamia
Sera za Chama na serikali kwa maslahi ya wanachi wote.
“CCM ina uzoefu mkubwa katika kufanya mageuzi ya kisera, kifikra,
kiitikadi pamoja na kimkamkati kulingana na mabadiliko ya nyakati
yanavyokwenda.
Ameongeza kuwa ndio maana hivi karibuni chama kimefanya mabadiliko makubwa
katika Katiba ya Chama ili miongozo ya kikanuni iendane na mahitaji ya
wananchi ambao ndio wapiga kura wa kuiweka CCM madarakani kwa kila uchaguzi
mkuu.
Katika maelezo yake amesema viongozi watakaopewa dhamana ya kuongoza kwa
kipindi cha miaka mitano wanatakiwa kutambua kuwa wao ni miongoni mwa
wapiganaji wanaounda jeshi la CCM litakalofanikisha ushindi katika mwaka 2020.
Akitoa nasaha kwa wanachama wanaogombea na watakaoshindwa kupata nafasi za
uongozi katika ngazi mbalimbali amewasihi wasivunjike moyo bali washirikiane
na wenzao walioshinda na kwamba CCM ni Chama cha watu wote.
Mbali na hilo, amesema hali ya kisiasa nchini
imeendelea kuwa na mvuto wa kipekee kwa wananchi na ushahidi wa jambo
hilo ni ushindi uliopatikana katika uchaguzi mdogo wa madiwani Tanzania bara
ambapo CCM kimeshinda kata 42 kati ya 43.
Amesema CCM sio Chama cha mtu mmoja kama ilivyo kwa baadhi ya vyama vingine
vya kisiasa nchini vilivyopoteza muelekeo kwa kupokonyana nafasi za uongozi.
“ Viongozi mtakaochaguliwa kemeeni makundi ya kuhatarisha uhai wa chama pamoja
na rushwa ili kuendeleza misingi imara ya ukombozi iliyofanywa na waasisi wa
ASP wakiongozwa na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume aliyepigania
wanyonge wa Zanzibar kupitia mapinduzi ya mwaka 1964.”, alieleza Makamu
Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika Mkoa huo,
amesifu juhudi za viongozi mbalimbali wa Chama na serikali katika kusimamia
vizuri upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo kuimarika kwa sekta za elimu,
afya, miundombinu ya maji safi na salama pamoja na barabara.
Dk.Shein amesema kupitia mradi wa Ras Al – Khaimah unaodhamini uchimbaji wa
visima vya maji safi na salama, Serikali ya SMZ imejidhatiti kumaliza kero
ya ukosefu wa huduma hiyo kwa wananchi wa Mkoa huo kwa kipindi kifupi kijacho.
Ameeleza kwamba utoaji wa huduma bora za kijamii na kiuchumi ndio kipimo muhimu
cha kuipima serikali na kukitathimini Chama cha Mapinduzi kama kimetekeleza
kwa ufanisi mambo kilichoyaahidi kwa wananchi.
“ Ni wajibu wa kila kiongozi ndani ya chama na Serikali kufanya kazi kwa
kujituma na kwa bidii kubwa, ili wananchi wanapotutathimini na kutuhoji
waridhike na majibu yetu kwani yatakuwa yanaendana kile tulichoahidi
katika kampeni za uchaguzi uliopita”, amesisitiza Dk.Shein.
kwa upande wake Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan,ameeleza matarajio yake
katika uchaguzi huo ni kuchaguliwa kwa viongozi makini na watakaoivusha salama
CCM kwa kila jambo linalotakiwa kutekelezwa kwa maslahi ya Chama.
Samia ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, amesema viongozi hao
ambao watachaguliwa wataisaidia kuondoa utendaji wa mazoea visiwani humo
na kwamba kuleta mabadiliko ya kimaendeleo kwenye nyanja mbalimbali.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi
amesema uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi na jumuia zake kuanzia ngazi za
mashina hadi Mikoa umeendelea kufanyika vizuri na kwa kufuata matakwa ya
miongozo ya kanuni za uchaguzi.
Ameeleza kuwa kupitia uwezo na uzoefu wa viongozi wanaochaguliwa katika Uchaguzi
huo kuna matumaini makubwa ya Chama cha Mapinduzi kupata ushindi wa
kihistoria katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
“Kupitia uchaguzi huu Chama kimefanya kazi ya ziada kuhakikisha viongozi wote
wanaoteuliwa kugombea nafasi za uongozi hawana sifa chafu za makundi ya
usaliti,rushwa na kupanga safu za wagombea uongozi.” ameeleza Dk.Mabodi.
Katika uchaguzi huo nafasi zinazogombewa katika Mkoa huo ni nafasi za Mwenyekiti, Katibu wa Siasa na Uenezi, Wajumbe wa Halmashauri
Kuu ya Mkoa nafasi tano(5) kutoka kusini pamoja na nafasi tano(5) kutoka kati.
MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza katika mkutano huo. |
NAIBU Katibu
Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akizungumza katika mkutano Mkuu huo
uliofanyika katika hoteli ya Coconut Tree Marumbi Mkoa wa Kusini Unguja.
|
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein(kushoto)akimkabidhi taarifa ya utekelezaji ya miaka mitano ya Mkoa huo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi. |
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar akimkabidhi taarifa ya utekelezaji ya miaka mitano ya Mkoa huo pamoja na nyaraka mbali mbali za Chama, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Mhe. Samia Suluhu Hassan. |
WAJUMBE wa
Kamati ya siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kusini waliomaliza muda wao
wa uongozi kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. |
MAKAMU
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali
Mohamed Shein akipiga kura ya kuwachagua viongozi wa ngazi hiyo akiwa ni
miongoni mwa wajumbe wa mkutano huo. |
MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipiga kura ya kuwachagua viongozi mbali mbali wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni