NA IS-HAKA OMAR, DODOMA.
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania
(UWT) Taifa, Gaudencia Kabaka amewataka wanawake wa umoja huo kuvunja makundi
ya ngazi zote yaliyojengeka wakati wa uchaguzi na badala yake wafanye kazi za
kuwatumikia kwa ufanisi wapiga kura waliowapa ridhaa ya kuongoza.
Pia, amesema UWT kupitia uongozi wake mpya ulioingia kwa
sasa ni lazima irejeshe heshima yake ya kuwa chombo cha kuwaunganisha wanawake
wote wa mijini na vijijini Tanzania ili wapate maendeleo.
Wito huo ameutoa katika hafla ya mapokezi ya uongozi huo
yalioandaliwa na UWT Mkoa wa Dodoma katika viwanja vya White house Makao Makuu
ya CCM Dodoma.
Amesema bila kuvunja makundi Umoja huo hautopata maendeleo na
watatumia muda mwingi kulaumiana, kuangaishana na hamaye kukosa muelekeo wa
kutekeleza ahadi walizotoa kwa mamilioni ya wanawake wa Tanzania.
Kabaka ameeleza kwamba Umoja wa Wanawake Tanzania ni chombo cha
CCM kinachotakiwa kuwa nguzo na muhimili mkuu katika kusimamia na kulinda
maslahi ya Chama kisiasa, kiuchumi na kijamii.
"Furaha yangu ni kwamba mlituchagua kihalali bila ya kutumia
rushwa, hivyo nasi tuna deni la kuwalipa ambalo ni lazima tutimize utumishi
bora na uliotukuka kwa miaka mitano ya uongozi wetu.
Pia nakuombeni tushirikiane kwa pamoja kupinga rushwa na ufisadi
ndani ya UWT na Chama kwa ujumla kama tunavyopinga makundi ya kuhatarisha uhai
wa Chama cha Mapinduzi", amesema Mama Kabaka.
Amesema jopo la viongozi wa ngazi mbali mbali wa UWT
waliochaguliwa hivi karibuni ndio jeshi la kisiasa la Akina Mama wanaotakiwa
kuongoza mapambano ili CCM ishinde na kubaki madarakani katika uchaguzi
mkuu wa mwaka 2020.
Kupitia hotuba yake Mwenyekiti huyo, ameagiza miradi yote ya
UWT Tanzania iorodheshwe ndani ya miezi miwili kwa lengo la kuijua ipo mingapi
na kuweka utaratibu rasmi ili iwanufaishe akina mama wote.
"Mbali na miradi ya kiuchumi iliyopo Makatibu wa ngazi mbali
mbali tafuteni takwimu sahihi zinazohusu masuala ya huduma za kijamii hasa
zinazowahusu wanawake." ameagiza Mwenyekiti huyo.
Pamoja na hayo ametoa shukrani zake kwa wajumbe wote wa Mkutano
Mkuu wa Tisa wa Umoja huo kwa kuwaamini kisha kuwachagua kwa kura nyingi
viongozi wote wa ngazi ya Taifa.
“Natoa ahadi yangu tena kwenu kwamba mmeniamini nami nitatenda
mema kwenu kwa kurejesha matumaini ya kutenda na kusimamia mambo yote yenye
manufaa kwa wanawake wa Tanzania.
Naye Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa, Thwaiba Kisasi amesema
dhamira ya UWT ni kuzitatua changamoto mbali mbali zinazowakabili Akina mama
ili wanufaike na matunda ya kuwa mwanachama wa Umoja huo.
Ameeleza kwamba viongozi hao hawatowaangusha kiutendaji bali
watatumia uzoefu na taaluma zao kuleta maendeleo endelevu ndani UWT.
Akizungumza Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Dodoma, Neema Majule amesema
Umoja huo umevuna wanachama wapya 5000 kupitia Chaguzi za ngazi mbali mbali
zilizofanyika katika Mkoa huo.
Amesema UWT imejipanga kuanzisha miradi mikubwa ya kiuchumi
kuanzia ngazi za Wilaya za Mkoa huo na mwanamke mmoja mmoja kwa lengo la
kujikomboa kiuchumi.
Mapema katika hafla hiyo jumla ya wanachama wapya 1700
wamekabidhiwa kadi za CCM kwa lengo la kuitumikia jumuiya na Chama kwa ujumla.
Viongozi mbali mbali walioudhuria katika hafla hiyo ni pamoja na
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Hakson,
Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Tabia Maulid Mwita na Katibu Mkuu wa UWT
Taifa, Amina Makilagi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni