Ijumaa, 14 Aprili 2017

MAREKANI YAPONGEZA UKOMAVU WA CCM Z'BAR KISIASA, YAAHIDI FURSA ZA KIUCHUMI NA KIJAMII.


SERIKALI ya Marekani imesema itaendelea kutoa misaada ya Kiuchumi, Ustawi wa jamii na kisiasa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar   ili kuimarisha mahusiano ya nchi hizo  mbili.

Msimamo huo umeelezwa katika ziara ya Ujumbe wa Serikali ya Marekani uliotembelea Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya sera za kiuchumi, kisiasa na kijamii huko Afisi Kuu Kisiwandui Unguja.

Marekani ambayo ni miongoni mwa Taifa kubwa lililoendelea kiuchumi, kijamii na kiulinzi hata katika masuala ya Kisiasa limesema kasi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya saba Zanzibar, linaishawishi taifa hilo kutoa misaada binafsi na inayopitia katika ngazi za kimataifa, ili kuenzi kwa vitendo juhudi hizo.


Hayo yameelezwa na Kiongozi wa Msafara huo ambaye ni Afisa wa kusimamia Masuala ya sera za kijamii na kisisa katika Ukanda wa Nchi za Afrika zilizomo katika jangwa la sahara, Bw. Gregory Simpkims wakati Akizungumza na Viongozi na Maafisa wa CCM waliongozwa na Naibu  Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdallah Juma Abdallah “ Mabodi”  hapo Kisiwandui Unguja.

Bw. Simpkims  alieleza kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM)  kimekomaa kisiasa na kinaendelea kuimarika  tofauti na vyama vya kisiasa vya nchi nyingine , barani Afrika ambavyo baadhi yao vimeanza kupoteza nguvu na kuondolewa madarani na vyama vya upinzani.

“  Tuna nia ya kuendelea kuisadia Zanzibar misaada mbali mbali ili iweze kukuza uchumi wake katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kuimairisha mahusiano ya kibiashara.

Pia tunaamini kuwa vyama vya siasa vilivyopo Zanzibar  vitaendelea kulinda Amani ya Visiwa vya Zanzibar  bila kuruhusu ili viwe sehemu tulivu inayoshawishi kila taifa kufanya utalii na shughuli nyingine za kijamii.”, alisema Gregory.

Akitoa ufafanuzi  juu ya ugeni huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dkt. Abdallah Juma Abdallah “ Mabodi” alifafanua kwamba ujumbe huo pamoja na masuala mengine umesifu suala la serikali kuimarisha Amani na Utulivu wa nchi licha ya kuwepo kwa changamoto za kisiasa visiwani humo.

Pia ujumbe huo ulitaka kujua njia na sera zinazotumiwa na CCM kuendelea kuaminiwa na wananchi wa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla, hali inayopekea kuimarika kwa uchumi wa nchi hiyo.

Alisema kwamba ujumbe huo ulitaka kujua mambo mbali mbali yakiwemo suala la Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2015, siri ya kuimarika kwa CCM kisiasa na utekelezaji wa  Mipango(Programs) ya maendeleo na ustawi wa kiuchumi wa Taifa la  Marekani na sera za nchi za nje za taifa hilo kwa upande wa Zanzibar.

Alisema walizungumzia uimarishaji wa sera za kibiashara na kiuchumi ya Nchi za Afrika ambayo ni African Growth and Opportunity Act (AGOA), Mpango huo una Sheriainayorahisisha bidhaa kutoka Afrika ziingie katika soko la Marekani, na kueleza kuwa kwa sasa wapo tayari Zanzibar kunufaika na Mkakati huo ili Bidhaa zake zikauzwe katika soko hilo.

Dkt. Mabodi alisema ujumbe huo uliohoji kwa nini Taarifa ya wasimamizi wa kimataifa wa Uchaguzi (International Observers) wa mwaka 2015, ilikuwa tofauti na taarifa iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar  (ZEC).

Alifafanua kwamba jawabu la swala hilo Dkt. Mabodi ameeleza kwamba CCM inaamini  na kuunga mkono taarifa na maelekezo ya Tume hiyo kwani ndio iliyokuwa ikisimamia shughuli za Uchaguzi toka awali na ilibainisha sababu kuu zaidi ya Tisa zilizosababisha Uchaguzi huo kufutwa, na hao waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa walikuta mchakato huo ushaanza pia hawana uelewa wa kutoka juu ya siasa za Zanzibar.

Hata hivyo amesema kwamba pamoja na mambo mengine walitaka kujua kama ZEC wamewahi kutoa taarifa ya tathimini ya uchaguzi huo, na kuelezwa kuwa tayari imetolewa na kukabidhiwa rasmi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein.

Sambamba na hayo Kiongozi huyo wa CCM Zanzibar, ameweka wazi kuwa alichojifunza kupitia mazungumzo hayo ni kuwa siasa na sera za kimataifa ni tofauti na Tanzania, kwani Nchi hizo zinatambua uhalisia wa siasa za Zanzibar licha ya kuwepo na baadhi ya wanasiasa wanaopotosha  na kuchochea vurugu.

Ameeleza pamoja na hayo ujumbe huo wa Ubalozi wa Marekani ulitaka Viongozi wa CCM kukaa meza moja na CUF kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa uliozuka toka kufutwa kwa uchaguzi wa Octoba 2015, lakini Dkt. Mabodi akawafahamisha kwamba Chama chake kimeshamaliza Uchaguzi na Tayari Rais wa Zanzibar Dkt. Shein aliyepatikana kwa misingi ya kidemokrasia ataendelea kuongoza nchi hadi Uchaguzi wa 2020.

Amesema kuwa tayari baada ya Uchaguzi ulioharibika CCM kupitia viongozi wao waliitisha mazungumzo na CUF, lakini kabla ya kufikia makubaliano Maalim Seif Sharif Hamad alisusia mazungumzo hayo bila kutoa sababu za msingi.

Hata hivyo amesema Chama hicho kipo tayari kukaa na CUF kujadili utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 pamoja na sera mbali mbali za SMZ, lakini sio kwa suala la Uchaguzi Mkuu uliopita.

Pia aliwambia wageni hao kuwa CCM imekuwa ikijitahidi kuwambia wananchi walinde Amani na Utulivu wa nchi na waendelee na shughuli za ujenzi wa Taifa kimaendeleo , lakini vyama vya Upinzani navyo vimekuwa vikipandikiza mbegu za chuki kwa kuwambia baadhi ya wananchi kwa  maeneo tofauti  wagome kushiriki katika harakati hizo.

Hata hivyo ameishukru Nchi hiyo kwa kuisaidia Tanzania misaada mbali ikiwemo miradi mikubwa ambayo ni  mradi wa umeme wa MCC na miradi ya vyandarua pamoja na miradi mingine.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni