Jumapili, 26 Mei 2019

DK.MABODI AONGOZA MAELFU YA WANANCHI MAZISHI YA MWENYEKITI MROPE -MAY 26,2019.


 VIJANA Maalum wa UVCCM wakiwa na Jeneza la aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Amani, Marehemu Abdi Ali Mzee 'Mrope'  kwa ajili ya Mazishi yake huko Kijijini kwao Jumbi Unguja.

 WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) na Wananchi mbali mbali wakiwa katika Mazishi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Amani, Marehemu Abdi Ali Mzee 'Mrope'  kwa ajili ya Mazishi yake huko Kijijini kwao Jumbi Unguja.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akiweka udongo katika Kaburi la aliyekuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Amani Marehemu Abdi Ali Mzee huko Jumbi.

Katibu wa UVCCM Wilaya ya Amani Ndugu Mohamed Ali Mohamed,akisoma Wasifu wa Marehemu mara baada ya Mazishi yaliyofanyika Kijijini Kwao Jumbi. 


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi, leo ameongoza Maelfu ya Wananchi katika Mazishi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Amani Unguja Marehemu Abdi Ali Mzee ‘Mrope’ aliyefariki Jana akiwa katika Matibabu huko Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es saalam na amezikwa leo kijijini kwao Jumbi Mkoa wa Kusini Unguja.
Viongozi mbali mbali wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali wameshiriki Mazishi hayo wakiwemo Katibu wa NEC,Idara ya Organazasheni Makao Makuu Ndugu Pereira Ame Silima,Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa CCM Zanzibar Mwl.Kombo Hassan Juma pamoja na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Zubeir Ali Maulid.
Wengine ni  Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mawaziri na Manaibu Mawaziri, Wabunge na Wawakilishi,Wakurugenzi wa Idara mbali mbali za SMZ,Wenyeviti na Makatibu wa CCM wa ngazi mbali mbali, Wana CCM na Wananchi kwa ujumla.
Katibu wa UVCCM Wilaya ya Amani Ndugu Mohamed Ali Mohamed,akisoma Wasifu wa Marehemu huyo amesema CCM na Jumuiya zake wamepokea kwa Huzuni na Masikitiko Taarifa ya Kifo cha Mwenyekiti huyo wa CCM Wilaya ya Amani Unguja.
Amesema Mwenyekiti Abdi Ali Mzee alizaliwa mwaka 1964 katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na kupata Elimu yake ya Msingi kuanzia mwaka 1978 katika Skuli ya Msingi Kidongo Chekundu pamoja na Elimu ya Sekondari katika Skuli ya Shangani mwaka 1981.
Amesema mwaka 1984 Abdi alijiunga na Chuo cha Ufundi wa Chuma huko Chang’ombe Dar es saalam na kuhitimu mafunzo hayo na akajiunga rasmi na Chama Cha Mapinduzi Mwaka 1983 katika Tawi la CCM Sogea.
Katika maelezo yake Katibu huyo, ameeleza kuwa Marehemu Enzi za Uhai wake alishika nyadhifa mbali mbali za Uongozi katika Chama Mwaka 1992 hadi 2007 alikuwa Balozi  wa Nyumba 10 Shina namba 7 katika Tawi la CCM Sogea,Mwaka 1997 hadi 2007 alikuwa Mwenyekiti wa CCM Tawi la Sogea,Mwaka 2007 hadi Mwaka 2012 alikuwa ni Mwenyekiti wa Jimbo la Magombeni.
Amesema Mnamo Mwaka  2012 hadi 2019 alikukuwa ndiye Mwenyekiti wa CCM wa mwanzo wa Wilaya ya Amani toka ilipoanzishwa na pia alikuwa Mkufunzi wa Makada katika Chuo cha Itikadi cha CCM Zanzibar na Mjumbe wa Bodi ya kudhibiti Kodi za Nyumba  Zanzibar.
Pamoja na hayo Mwenyekiti huyo licha ya kuwa Mwanasiasa pia alikuwa ni Mwanamichezo Mstaafu wa Mpira wa Miguu aliyewahi kuchezea Timu za African Kids,Wazee Sports Club hadi umauti unamkuta alikuwa ni Mwalimu wa Timu ya New Boko kutoka Mtaa wa Boko Zanzibar.
Sambamba na hayo Chama Cha Mapinduzi Taifa kupitia Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein wanatoa Salamu za Pole kwa Wafiwa na Watu wote walioguswa na Msiba huo na kuwaomba waendelee kuwa na subra katika kipindi hiki cha Maombolezo.
Marehemu ameacha Vizuka Wawili na Watoto Saba.
Mwenyezi Mungu Ailaze Roho ya Marehemu Mahala Pema Peponi Amin.
  
 
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni