Jumapili, 2 Agosti 2015

Maelfu ya Wananchi wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi wajitokeza katika Kura za maoni za Kuchagua Wabunge, Wawakilishi na Madiwani

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar jana walijitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura za maoni ndani ya chama hicho, ili waweze kuteuliwa viongozi  wa nafasi za ubunge , uwakilishi na udiwani watakaoweza kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha   uchaguzi mkuu wa dola unaotarajiwa kufanyika Octoba 25 mwaka huu.

Zoezi hilo lililoanza majira ya saa 2:30 asubuhi ya jana katika vituo mbali mbali vilivyokuwa katika matawi ya Chama hicho pamoja na shule kulimiminika wafuasi wa  CCM wakiwa na ari za kuwachagua viongozi bora watakaoweza kutatua changamoto zinazowakabili katika majimbo.

Akizungumza na UHURU Naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai mara baada ya kupiga kura katika Tawi la Magomeni Unguja, alisema ameridhishwa na muamko wa wanachama wa chama hicho jinsi walivyojitokeza katika vituo mbali mbali kwa lengo la kuwachagua viongozi wanaowaamini kuwa wana nia thabiti ya kuleta maendeleo na kusimamia Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa vitendo.

Alisema kuwa hali hiyo inaonyesha taswira halisi ya umoja na mshikamano uliopo ndani ya chama hicho unaoendelea kujenda demokrasia pana kwa kutoa fursa ya kira mwanachama kupata haki yake ya kuchagua na kuchaguliwa bila ya kuwekewa vikwazo.Vuai alifafanua kuwa matarajio ya chama hicho ni kuhakikisha kila kada mwenye sifa za kupiga kura ya maoni katika eneo husika wanapata haki hiyo bila ya kuwekewa vikwazo ili kuweza kukamilisha zoezi hilo kwa ufanisi na wakati uliopangwa.

“ Matumaini yetu ni kuhakikisha zoezi hili linafanyika vizuri na kumalizika bila ya matatizo licha ya kuwa mchakato wowote wa kidemokrasia hasa uchaguzi hauwezi kukosa kasoro kwa sababu ni jambo ambalo lipo katika usimamizi wa binadamu lakini kama kutajitokeza  changamoto lazima zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu.





CCM imetoa mafuzo mbali mbali kwa mawakala na wagombea wa nafasi mbali mbali pamoja na kuchapisha Makala mbali mbali zinazoelezea kanuni na taratibu za kura za maoni ndani ya chama chetu, hivyo bado tuna imani kuwa zoezi hili litafanyika kwa mujibu wa matarajio yetu kwa mujibu wa maandalizi yake.”, alisema Vuai na kuwapongeza wanachama wa Chama wa Zanzibar Unguja na Pemba  kwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura za maoni.

Naibu katibu mkuu huyo Vuai alitoa ufafanuzi  juu ya malalamiko ya baadhi ya wanachama kwa baadhi ya vituo kuchelewa kuanza kupiga kura hizo, alisema kuwa kasoro hizo haziwezi kuzuia wanachama hao wasipige kura kwani atafuatilia kwa makatibu wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanaongeza muda kwa vituo vilivyochelewa kuanza.

Vuai alisema kuwa baadhi ya maeneo ikiwemo Jimbo la Mahonda Wilaya ya kaskaszini “B’” Unguja mchakato huo umegubikwa na kasoro zilizosababisha kuhairishwa kupigwa kwa kura hizo mpaka viongozi watakapoweza kutatua kasoro hizo.

Alizitaja kasoro hilo kuwa ni kutokana na baadhi ya wagombea ndani ya jimbo hilo kuanza kuchafuana katika vituo vya kupigia kura hali iliyosababisha kuhairishwa kwa zoezi hilo mpaka kesho(leo).


Nao wananchi katika tawi la CCM Mpendae walilalamikia suala la kuchelewa kuanza kupiga kura hizo kutokana na kuchelewa kufikishwa vifaa jambo ambalo walisema linaweza kuharibu mchakato huo kwani baadhi ya wanachama wanaweza kususa kupiga kura.

Kwa upande wake Issa Hassan Masoud mkaazi wa jimbo la Mpendae alisema kuwa wananchi wamekaa katika kituo hicho kwa muda mrefu bila ya kupiga kura jambo ambalo linaweza kusababisha athari ya kuonekana CCM haikujipanga na zoezi hilo na kutoa fursa ya vyama vya upinzani kukichafua chama hicho.

Mkaazi kwa upande wake mkaazi wa Jang’ombe Urusi, Saada Kassim Haji alisema kuwa katika kituo hicho zoezi hilo limeendelea vizuri kwani vifaa na wasimamizi wa vituo wamefika mapema na kuanza kupiga kura hizo bila ya usumbufu.

Kwa upande wake Katibu wa wilaya ya Amani kichama Unguja,  Abdalla Mwinyi  alisema zoezi hilo limeendelea vizuri katika wilaya hiyo licha ya kujitokeza kwa changamoto ya kuchelewa kuanza kwa baadhi ya vituo kutokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wa kiutendaji wa wilaya hiyo.

“ Wanachama wanaendelea kupiga kura na tunapata faraja kuona wamejitokeza kwa wingi katika vituo mbali mbali vilivyopo katika wilaya yetu, hivyo matarajio yetu ni kuhakikisha zoezi hili linakamilika”, alisema Mwinyi.

Naye Katibu wa idara ya Itikadi na uenezi NEC Zanzibar, Waride Bakar  Jabu alizungumza na gazeti hili baada ya kumaliza kupiga kura katika kituo cha Tawi la Kiembe samaki, aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo vizuri kwa kuwachagua viongozi ambao wana nia ya dhati ya kutatua changamoto zinazowakabili.

Waride ambaye pia ni Mgombea wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Kiembe samaki Unguja, alisema kuwa zoezi hilo ni miongoni mwa hatua muhimu za kuwatafuta wagombea wa chama hicho wa ngazi mbali mbali kama kanuzi zilizomo ndani ya katiba ya CCM zinavyoelekeza.

Kwa upande wake msimamizi mkuu wa kituo cha Tawi la Kikwajuni Unguja, Pandu Ameir Kificho aliwashauri wafuasi wa chama hicho kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa katika vituo hivyo ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima.

Alisema katika kituo hicho wanachama wamejitokeza kwa wingi na kuhakikisha zoezi hilo linaendelea vizuri kwani mawakala na wasimamizi wengine wa uchaguzi wamekuwa na ushirikiano kwa kila hatua ili kuhakikisha zoezi hili linakamilika kwa wakati.

“Lazima tuhakikishe zoezi hili linakamilika kwa wakati na matokeo yanapatikana kwa muda uliopangwa kwani endapo patafanyika uzembe wa aina yoyote unaweza kusababisha athari ya kutokamilika kwa zoezi hilo kwa wakati”, alisema Kificho.


Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na  katika vituo mbali mbali umebaini kuwepo na demokrasia katika zoezi hilo kutokana na kila mwanachama mwenye sifa kupewa haki ya kupiga kura hizo bila ya kuwekewa vikwazo.

WAJUMBE WA NEC WAKIONGOZWA NA MWENYEKITI WA MKOA WA MJINI WAKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI