Jumamosi, 30 Desemba 2017

BALOZI SEIF ALI IDDI-ATOA NASAHA KWA WABUNGE NA WAWAKILISHI.



MAKAMU wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, ameshtukia mchezo mchafu ambao umeanza kufanywa na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), ambao wanataka kugombea nafasi za ubunge na uwakilishi, kuanza harakati za kutaka kuhama majimbo yao kwa ajili ya kugombea maeneo mengine baada ya kuharibu maeneo yao.

Amesema atahakikisha anafanya juhudi zote za kukishauri Chama kuhakikisha kuna kuwepo na msimamo thabiti kwa wagombea hao ambao watakaoanza kufanya harakati hizo kukatwa majina yao.

Balozi Seif amesema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa CCM, Mkoa wa Magharibi, ambapo amewataja baadhi ya viongozi hao kuwa hawana msimamo wala nia njema ya  kukitumikia chama na wananchikwa ujumla.

"Siasa sio biashara ama sehemu ya kujinufaisha mtu binafsi bali ni jukwaa la kusikiliza na kuratibu kero za wananchi na kuzifanyia kazi..,ni aibu kwa baadhi ya viongozi wetu kukwepa majukumu yao na badala yake wanaanza kutanga tanga huku na kule.

"Ikumbukwe kuwa kufanya hivyo ni kuhatarisha chama na kudhofisha jitihada za CCM katika kutekeleza ilani ya Chama hivyo kila Mbunge ama mwakilishi atakayegombea abaki kwenye jimbo lake husika kama umeharibu katika eneo lako ubaki huko usubirie wananchi waje kukuwajibisha kwa uliofanya,"alisema Makamu huyo wa Pili wa Rais.

Amesema wanachama hao ambao wagombea wa nafasi hizo ufikia uamuzi huo wa kuyakimbia majimbo yao ya zamani na kutaka kuhamia maeneo mengine baada ya kujibaini kutokuwatumikia vyema wanachama na wananchi katika kipindi walichoomba ridhaa ya kuwatumikia kwa vipindi vya awali.

Katika maelezo yake ameongeza kuwa imebainika uwepo wa baadhi ya wawakilishi na wabunge wanaoendelea na majukumu yao ndani ya majimbo yao ukumbwa na matatizo ikiwemo ushawishi, ftina na majungu kwa wale ambao wanataka kugombea nafasi hizo.

Akigusia suala la Uchaguzi ndani ya Chama Balozi Seif amesema  Wanachama wenye kufaa kuchaguliwa ndani ya Chama cha Mapinduzi   ni wale  waliojaa sifa za ziada kupita wengine katika kujenga Umoja na mshikamano kwenye Taasisi hiyo ya Kisiasa.

Ameeleza kuwa sifa hiyo ya Wanachama lazima iendane na uwezo wa Kiongozi huyo wa kuwashawishi wasiokuwa Wanachama kujiunga na Chama katika kukijengea nguvu za kuendeleza ushindi kwenye Uchaguzi mkuu wa Mwaka 2020.

Balozi Seif amesema  kazi ya Chama chochote cha Siasa ni kushika Dola. Hivyo kwa Mantiki hiyo CCM katika mabadiliko makubwa yanayoendelea kuyafanya katika kupanga safu za Uongozi kuanzia ngazi ya Shina hadi Taifa  kinahitaji Viongozi watakaokiletea ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu huo.

Makamu huyo amefahamisha kwamba Wanachama wanapaswa  kuzingatia muelekeo wa Viongozi wa Chama chao katika kuwachagua Wanachama watakaowapeleka huo kwenye chaguzi zilizobakia hata kama watakuwa na sura mbaya.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM amewasihi Viongozi watakaochaguliwa kuwa wabunifu hasa katika kukifanya chama kuwa na nguvu za ziada za kujitegemea kifedha badala ya kusubiri kutembeza bakuli kwa wahisani.

Balozi Seif amewatahadharisha wazi kwamba utegemezi siku zote unawajengea nguvu wale wanaowategemea, jambo ambalo baadhi ya wahisani hao wanaweza kutumia fursa hiyo kukiyumbisha Chama kirahisi.

Ametoa wito kwa Uongozi utakaochaguliwa uelewe fika kwamba utakuwa na jukumu la kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020 kwa kivitendo kama inavyoelezwa katika Sura ya nane.

Awali akisoma Risala ya Mkoa wa Magharibi Katibu wa CCM wa Mkoa huo, Aziza Ramadhan Mapuri, amesema uongozi wa CCM Mkoani humo umepata mafanikio makubwa katika kujenga upendo miongoni mwa Wanachama.

Aziza amesema upendo huo umeuwezesha Uongozi wa Mkoa huo kuisimamia vyema Serikali kwenye ngazi ya Mkoa katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 – 2020.

Mbali na hilo, amesema katika kipindi cha Miaka mitano inayomalizika, CCM Mkoa wa Magharibi umefanikiwa kupata eneo kwa ajili ya Ujenzi wa Ofisi ya Kisasa ya Mkoa itakayoambatana na uwepo wa vitega uchumi vitakachouwezesha Mkoa huo kujitegemea wenyewe na kujiepusha na utegemezi.

Akigusia changamoto zinazoukabili Mkoa huo Katibu huyo wa CCM Mkoa Magharibi amesema uhamiaji holela ambao unasababisah ujenzi holela ndani ya eneo hilo ambalo umeleta athari kubwa hat hususan kimazingira.

Kwa upande Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi,aliyemaliza muda wake, Yussuf  Mohamed Yussuf, amesema uchaguzi zilizokuwa zikiendelea ndani ya chama kuanzia ngazi ya Shina hadi Mkoa ni matukio muhimu ya kuendeleza Demokrasia ndani ya Chama.

Yussuf ameeleza kuwa katika kipindi chake cha utumishi wa nafasi hiyo katika kipindi cha miaka 15 ameshuhudia mabadiliko makubwa yaliyofanywa na CCM ndani ya kipindi kifupi jambo ambalo wanastahiki kupongezwa Viongozi pamoja  na Wanachama wenyewe.

Amesema Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuwa imara na chenye nguvu Tanzania endapo baadhi ya wanachama wake wataondokana na tabia za fitna na ubinafsi na badala yake wakafuata Katiba na Kanuni za CCM, na kuzifanyia kazi nasaha za Mwenyekiti wa Chama hicho Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.

TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA ILANI UCHAGUZI MKOA WA MJINI MAGHARIB

PICHA MALI MBALI ZA MATUKIO YA UCHAGUZI WA MAGHARIB

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi(kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharib  anayemaliza muda wake  Yussuf Mohamed Yussuf  katika  ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa Magharib Unguja. 



 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani kwa ajili ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu huo.

Ndugu Shaaban akisoma Qur-raan kutoka madrasa ya kamaria iliyopo kibanda hatari Jang'ombe Unguja.

 Katibu wa CCM Mkoa wa Magharibi Unguja Aziza Mapuri akisoma risala ya Mkoa huo.

 BAADHI ya wageni waalikwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu huo.

 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharib  anayemaliza muda wake  Yussuf Mohamed Yussuf  akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi

 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akiwahutubia wana CCM katika Mkutano huo
















Ijumaa, 29 Desemba 2017

TABIA AMTEMBELEA MWANA MAPINDUZI

MAKAMU MWENYEKITI WA UVCCM TAIFA TABIA MWITA-AMTEMBELEA MWANAMAPINDUZI RAMADHANI HAJI FAKI.

 MWASISI wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964, Brigedia Jenerali Mstaafu  Ramadhani Haji Fakii(kushoto) akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Mwita(kulia) alipofika nyumbani kwake Maisara Unguja kwa ajili ya kumtembelea.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

MAKAMU wa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Tabia Mwita amemtembelea  Brigedia Jenerali mstaafu Ramadhani Haji Faki, ambaye ni miongoni wa wanamapinduzi 14 waliofanikisha  Mapinduzi ya mwaka 1964.

Brigedia Jenerali  Faki  kati ya wanapinduzi  hao 14 ndiye  aliyebakia hai na pia alikuwa Waziri Kiongozi wa kwanza katika Baraza la Mapinduzi  baada ya Mapinduzi hayo kutokea.

Akizungumza  nyumbani kwake baada ya kutembelewa na Makamu huyo Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia, Mwanapinduzi huyo amesema kuna umuhumi wa kuhakikisha vijana wa sasa kuyaenzi na kulinda dhana ya mapinduzi hayo yaliyotekelezwa na vijana wa enzi za ASP.

"Nilimwambia Mzee Abeid Amani Karume kuwa lazima tuipindue serikali ya Sultan kwani ilikuwa wakiwadhalilisha  Waafrika ambao ni wazawa  na namshukru mungu mipango yetu ikafanikiwa  toka mwaka 1964 Zanzibar ilikuwa huru kiuchumi, kijamii, kimaendeleo na kisiasa.,"alisema.

Mwanapinduzi huyo amesema  baada ya kuipindua serikali ya Kisultani serikali ya Mapinduzi ilitangaza kuwa elimu ni bure na wananchi walihimizwa kusoma kutokana uamuzi wa serikali ya mapinduzi kutangaza bure ili kupata wataalamu wa kuiletea nchi maendeleo.

Faki alimtaka Makamu Mwenyekiti huyo ambaye ni kamanda mkubwa wa vijana Tanzania kuhakikisha vijana nchini wanapaswa kuyalinda kwa hali na mali.

"Sidhani kuwa kama kuna mtu atakuja kuyapindua Mapinduzi haya na kwamba labda ayafanyie nchi nyingine na si Zanzibar mapinduzi haya ni ya mwisho na sifikiri tena kama kuna mtu atakuja kuyafanya mapinduzi mengine,"alisema Faki.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti huyo Tabia, amemuhakikishia Mwanapinduzi huyo kuwa UVCCM itahakikisha yanayalinda  mapinduzi hayo ambayo yalitokea mwaka 1964.

Amesema  amejifunza mambo mengi kutoka kwa mwanamapinduzi huyo ambapo amebaini umuhimu wa kuwatumia vijana kuwafunza kuwa katika hali ya uimara na uzalendo mkubwa kwa kuyalinda mapinduzi hayo.

"Nikiwa mimi ni Makamu Mwenyekiti wa UVCCM,ninawaeleza vijana wenzangu kuwa hakutatokea Mapinduzi yeyote isipokuwa kuyaendeleza na kuyawekea mipango ya kufanya  kuleta maendeleo,"alisema

Makamu huyo amesema kupitia UVCCM mpya ambayo ni imara itaendelea kuyadumisha na kwamba yasifanyike mambo yakaleta fikra ya kutokea kwa mapinduzi mengine wakati yalishafanyika kwa mwaka 1964.

"Leo nimeona na nimesisimuka sana baada ya kupata historia ya kutokea kwa mapinduzi haya na kwamba yalikuwa lazima kutokea kutokana na unyama wa serikali ya Sultani aliyafanya na udhaifu wa kuongoza serikali,"alisema.

Tabia amefafanua  kuwa amekuja kujifunza taarifa za ndani za mahusiano ya ndani kati ya Chama Cha Mapinduzi(CCM), kilipotoka na kinapoelekea na kutoka Chama cha Afro shiraz Party (ASP) na TANU hadi CCM na kwamba elimu aliyopata ni umuhimu wa uzalendo kwa vijana katika kutetea nchi kwa kujitolea.


Alhamisi, 28 Desemba 2017

TABIA MWITA-AISHAURI SMZ KUONGEZA KASI UDHIBITI WA VITENDO VYA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA

 MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita (kusho) Msimamizi na mwandaji wa Vipindi vya  Shirika la Utangazaji Zanzibar ZBC Radio  Suzan Kunambi (kulia) akimfanyia mahojiano kiongozi huyo kuputia kipindi cha Asubuhi na ZBC huko katika Studio za Shirika hilo Rahaleo Unguja.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR 
 MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Tabia Maulid Mwita ameishauri serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuongeza kasi katika usimamizi wa mamlaka zinazohusika na uendeshaji wa kesi za udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake, watoto na watu wenye ulemavu kuhakikisha zinatenda haki.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akizungumza katika kipindi Maalum kinachorushwa mubashara kila siku asubuhi na ridhaa ya Taifa ya Zanzibar  ambayo ni Shirika la Utangazaji  Zanzibar (ZBC Radio) katika jengo la Shirika hilo lililopo Rahaleo Mjini Unguja.

Amesema miongoni mwa mikakati ya UVCCM ni kukemea vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, dawa za kulevya pamoja na vitendo viovu vinavyosababisha mmomonyoko wa maadili kwa vijana.

Tabia ameeleza kuwa Umoja huo umejipanga kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya taasisi hiyo kisiasa na kiuchumi.

Amesema wakati wa vijana kutumiwa kama ngazi ya kufikia mafanikio kwa baadhi ya watu umekwisha na badala yake vijana hao watumie fursa zilizowazunguka kujitafutia kipato.

“ Vijana tunatumiwa na baadhi ya wanasiasa hasa inapokaribia kipindi cha kampeni za uchaguzi na wanapopata nafasi hawaanzishi miradi ya maendeleo ya kulisaidia kundi hilo ambalo wengi wao hawana ajira za uhakika.

Sasa ifikie wakati na sisi tuwe na misimamo kwa kujiajiri wenyewe kupitia sekta ya ujasiria mali na ufundi na watushauri mambo mbali mbali ya kuimarisha taasisi yetu kisiasa.

Kupitia kipindi hicho Makamu Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa vijana wote nchini kuwaunga mkono viongozi wa Chama na Serikali hasa Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwani viongozi wanaojali maslahi ya vijana.

Amesisitiza wananchi kuheshimu utawala wa kisheria kwa kuepuka uvunjaji wa sheria na miongozo mbali mbali ya nchi.


Pamoja na hayo amewataka viongozi wa UVCCM kuwa mfano wa kuigwa kivitendo, kauli, maadili, hekima na busara ili vijana wengine waliopo katika vyama vya upinzani wavutike na kujiunga na umoja huo.

DK.MABODI-ATOA AHADI YA KUSHIRIKIANA NA UVCCM

VIONGOZI mbali mbali wa UVCCM pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi wakiomba dua katika Kaburi la Marehemu Mzee Abeid Amani Karume lililopo katika  eneo la Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  Dk. Abdalla Juma Saadalla(Mabodi)  amewahakikishia  Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM) kuwa ataendelea kushirikiana nao katika masuala  mbali mbali ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Ahadi hiyo ameitoa wakati akizungumza na viongozi wa UVCCM Taifa wakiongozwa na Mwenyekiti Kheir James na Makamu Mwenyekiti Tabia Maulid Mwita, waliofika  Afisi Kuu ya CCM Zanzibar kwa ajili ya kutembelea  na kuomba dua katika  kaburi  la aliyekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Aman Karume .

Dk. Mabodi aliwambia viongozi hao kwamba kumbukumbu  na historia ya Marehemu Mzee Abeid karume inatakiwa kulindwa na vijana wa CCM ambao wao ndio viongozi wa sasa na baadae wenye dhamana ya kulinda  serikali na Chama visichukuliwe na wapinzani.

Naibu Katibu Mkuu huo amemtaja  Marehemu Mzee  Abeid Karume kuwa alikuwa ni kiongozi  wa Mapinduzi mwenyekiti  aliyekuwa na azna kubwa ya busara na falsafa pana ya masuala ya uongozi na ubunifu ndani na nje ya ASP na Serikali kwa ujumla.

Amesema  Afisi Kuu ya CCM Zanzibar inayoongozwa na  Makamu Mwenyekiti Dk.Ali Mohamed Shein itatoa ushirikiano kwa UVCCM pamoja na jumuiya na taasisi zote za kisiasa na kiserikali ili wananchi waendelee kupata huduma bora za kijamii, kichumi na kisiasa.

Pia, ameueleza msafara huo wa viongozi wa UVCCM waliofika Zanzibar kwa mara ya kwanza toka wachaguliwe kupitia Mkutano Mkuu wa Tisa wa Umoja huo Taifa, kwamba maendeleo yaliyopatikana visiwani Zanzibar yanatokana na juhudi za CCM kuisimamia Serikali itekeleze  Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020.

“Kwanza karibuni sana Kisiwandui ambapo ndio sehemu pekee yenye historia na  Ofisi za waasisi wetu wa Afro Shiraz Party (ASP), walioanzisha harakati za ukombozi wa Waafrika wa visiwa vya Zanzibar na hatimaye  Januari 12, 1964 wakaung’oa utawala wa kisultani na kusimamisha  Dola huru iliyojali maisha na utu wa watu wote.

Nyinyi vijana ni azna kubwa kwa chama chetu hivyo fanyeni kazi kwa ufanisi ili kulinda heshima na dhamana mnazopewa kwa lengo la kuwanufaisha  vijana wenzenu ambao kwa njia moja ama nyingine hawajajaliwa kama zenu”, alisema Dk.Mabodi.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM  Taifa , Kheir James  amekipongeza Chama cha Mapinduzi Zanzibar kwa juhudi zake za kuimarisha taasisi hiyo ya kisiasa licha ya kuwepo na changamoto za kisiasa zinazosababishwa na wapinzani.

Mwenyekiti  Kheir amesema  yupo tayari kufanya kazi na viongozi wa Chama cha Mapinduzi na Serikali kwa ujumla ili changamoto mbali mbali zinazowakabili vijana ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na taasisi hizo.

Jumatano, 27 Desemba 2017

MWENYEKITI MPYA WA UVCCM TAIFA KHEIR JAMES- ATANGAZA VITA DHIDI YA WATU WANAOWATUKANA VIONGOZI WA CHAMA NA SERIKALI

MWENYEKITI wa UVCCM Taifa Kheir James akiwahutubia vijana wa UVCCM katika hafla hiyo.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.


UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) umetangaza rasmi mapambano  dhidi ya watu wanaokashfu na kuwadhalilisha viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi.

Akizungumza Mwenyekiti wa Umoja huo Taifa, Kheir James na Mamia ya vijana, viongozi wa Chama na Serikali waliojitokeza kupokea msafara wa viongozi wa Umoja huo huko katika ukumbi wa Gymkhana  Afisi Kuu ya UVCCM Zanzibar.

Amesema kuna baadhi ya watu wachache nchini wamekuwa wakijivisha joho la utukufu kwa kuwatukana na kuwadhalilisha viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar huku wakibeza na kudharau kila jambo jema linalotekelezwa  na serikali  hizo.

Mwenyekiti Kheir amewambia vijana wa UVCCM hasa viongozi kuwa wakati wa kuwavumilia  watu wa aina hiyo umekwisha na badala yake ni kuwachukulia hatua stahiki kupitia vyombo vya kisheria.

“Haiwezekani  viongozi wetu wapendwa wanaokesha wakiangaika kwa ajili ya wananchi wa nchi hii, watukanwe sisi tupo sasa kupitia hadhara hii natamka rasmi kwamba yeyote atakayethubutu tena kutukana basi tutamshughulikia,..haiwezekani…haiwezekani lazima tupambane nao.

Nawaagiza vijana wengangu yeyote atakayewavunjia heshima viongozi wetu na sisi tutavunja heshima yake, kwani viongozi wetu wamedhalilishwa mno na wamekuvumilieni sana..Umoja wa vijana tunasema lazima tuchukue hatua haraka iwezekavyo kwa lengo la kurejesha heshima ya Chama na Serikali.”, asisitiza Mwenyekiti huyo.

Ameeleza kuwa wanapotukanwa viongozi wa CCM vyombo vya ulinzi vinakaa kimya wala hakuna anayekamwatwa kwa uhalifu huo, lakini UVCCM ikijibu shutuma hizo vyombo vya ulinzi wanakuwa wakali huku wakida kuwa vijana wanahatarisha usalama wa nchi.

 Akizungumzia lengo la ziara hiyo ambayo ni ya kwanza kufika visiwani Zanzibar  toka uongozi huo uchaguliwe kupitia Mkutano Mkuu wa Tisa wa UVCCM uliofanyika Mjini Dodoma wiki kadhaa zilizopita, amesema lengo ni kuwashukru vijana wote wa UVCCM walioshiriki kwa njia moja ama nyingine kufanikisha uchaguzi uliowapa ridhaa ya kidemokrasia viongozi hao kuchaguliwa ili waongoze jumuiya hiyo kwa miaka mitano ijayo.

Amewasihi viongozi na wanachama wa UVCCM kushirikiana na uongozi huo ili waweze kutekeleza kwa vitendo ahadi walizotoa kwa vijana wakati wa kampeni za uchaguzi wa Umoja huo.

Amesema katika uongozi wake atahakikisha anakuwa ni kiongozi wa kusikiliza,kusimamia na kutafuta ufumbuzi wa kero zinazowakabili vijana na sio kutengeneza migogoro na makundi ya kuhatarisha umoja na mshikamano ndani ya UVCCM.

Amesisitiza umuhimu wa vijana wa Zanzibar kushikamana na kupendana ili waweze kunufaika na fursa mbali mbali zinazotokea ndani na nje ya umoja huo kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

SHAKA-ATOA YA MOYONI KATIKA HAFLA YA MAPOKEZI YA VIONGOZI WAPYA WA UVCCM ZANZIBAR

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Shaka Hamdu Shaka akizungumza katika hafla hiyo

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.


KAIMU Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Shaka Hamdu Shaka, amesema licha ya Umoja huo kupita katika misukosuko na mawimbi makubwa ya changamoto za kisiasa na kiutawala lakini bado viongozi wake wamebaki imara na wenye misimamo isiyopinda katika kusimamia maslai ya vijana.

Hayo ameyabainisha leo wakati akizungumza katika hafla ya mapokezi ya viongozi wa UVCCM Taifa waliofika Zanzibar leo kwa mara ya kwanza toka wachaguliwe kupitia Mkutano Mkuu wa Umoja huo uliofanyika hivi karibuni.  

Shaka amesema Umoja huo umepitia katika kipindi kigumu cha misukosuko ambayo wakati mwingine iliwayumbisha baadhi ya viongozi lakini baadae wakarudi katika mstari ulionyooka kutokana na nasaha za viongozi wa CCM.

Ameeleza kuwa maendeleo endelevu ya umoja huo yataletwa na vijana wenye nia, maono na uzalendo wa kweli katika kujenga hoja zenye uhalisia wa kuisaidia jumuiya hiyo na sio kuibomoa.

“ Namshukru mungu toka nimekuwa kiongozi ndani ya umoja huu nilipoanzia Zanzibar hadi kuteuliwa na kuhamishiwa Tanzania bara kwa wanaoijua UVCCM nilivyoikuta wanakiri kuwa kwa sasa ina maendeleo kuliko ilivyokuewa wakati wa nyuma.”, amefafanua Shaka.

Shaka amesema huu sio wakati wa maneno na porojo bali ni muda mwafaka wa kila kijana kutumia elimu, maarifa na mbunu mbadala katika kuishauri jumuiya iweze kufanya mambo mazuri yenye tija kwa maslahi ya Chama na Taifa kwa ujumla.

Ameahidi kuwa ataendelea kushirikiana na vijana wote bila kujali tofauti za kijinsia, umri, rangi,kabila na dini kwa lengo la kuhakikisha malengo ya UVCCM yanatimia kwa asilimia 100 kabla ya mwaka 2022.


MAKAMU MWENYEKITI UVCCM TAIFA TABIA MWITA - ASEMA UCHAGUZI UMEKWISHA KILICHOBAKI NI KUFANYA KAZI KWA BIDII

MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita akizungumza katika hafla ya  mapokezi hayo kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM)Taifa,  Tabia Maulid Mwita amewataka vijana kuvunja makundi yote yaliyoundwa wakati wa kampeni za uchaguzi na badala yake libaki kundi moja la UVCCM litakalotetea na kusimamia maslahi ya vijana wote wa Tanzania.

Rai hiyo ameitoa leo katika hafla ya mapokezi ya viongozi wa jumuiya hiyo ngazi ya Taifa waliofika Zanzibar kwa mara ya kwanza tokaka wachaguliwe kupitia Mkutano Mkuu wa Tisa wa UVCCM uliofanyika wiki kadhaa zilizopita Mjini Dodoma.

Amesema uchaguzi umekwisha na tayari viongozi wa ngazi mbali mbali wamechaguliwa hivyo kilichobaki kwa viongozi hao ni kuwatumikia vijana wa Umoja kwa ufanisi.

Amesema changamoto zinazoikabili UVCCM zitatafutiwa ufumbuzi wa kudumu endapo vijana mbali mbali wa umoja huo watakuwa tayari kushirikiana na viongozi wao katika kutathimini na kubuni mikakati mipya ya kuleta maendfeleo ndani ya umoja huo.

“ Ndugu zangu wapendwa na vijana wenzangu wa UVCCM nakupendeni sana lakini ushauri wangu kwenu ni kwamba tufanye kazi kwa bidii ili umoja wetu uendelee kuwa na heshima ya ndani na nje ya Chama cha Mapinduzi.

Pia uchaguzi umekwisha lakini pia makundi ya kuharisha uhai wa jumuiya yetu, rushwa na ufisadi tuyapige vita kwani hayatatusaidia bali yatatutafuna na kudhohofisha taasisi yetu.”, amesema Makamu Mwenyekiti huo.

Hata hivyo amewashukru vijana mbali mbali wa umoja huo wanaoendelea kuonyesha upendo na mshikamano kwa uongozi mpya wa ngazi ya taifa uliochaguliwa kuongoza kwa miaka mitano ijayo.


Amewambia mamia ya vijana waliojitokeza katika mapokezi hayo kwamba Umoja huo umejipanga kufanya mageuzi makubwa katika masuala ya  uongozi na kiuchumi kwa lengo la kufanya taasisi hiyo kuwa kimbilio la kudumu kwa vijana.

MAPOKEZI YA MWENYEKITI WA VIJANA ZANZIBAR

NATAKA VIJANA WAPAMBANAJI KATIKA UMOJA WA VIJANA





KUANZIA LEO VIJANA WA CCM NI MARUFUKU KULINDA HESHIMA ZA WATU WANAOVUNJA HESHIMA ZA VIONGOZI WETU NA TAIFA LETU.

PICHA MBALI MBALI ZA MAPOKEZI YA MWENYEKITI NA MAKAMU MWNYEKITI WA UVCCM ZANZIBAR

AFISA kutoka Idara ya Itikadi na Uenezi Asha choum (kulia wa mwanzo aliyevaa mtandio wa rangi ya kijani) akitoa historia ya aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar  Marehemu Mzee Abeid Karume kwa Msafara wa viongozi wapya wa UVCCM Taifa wakiongozwa na Mwenyekiti Kheir James na Makamu Mwenyekiti Tabia Mwita, katika eneo la kumbukumbu ambayo aliuwawa kiongozi huyo na wapinga maendeleo akiwa katika eneo la kucheza mchezo wa dhumna hapo Afisi Kuu ya CCM  Kisiwandui Zanzibar.

 VIONGOZI mbali mbali wa UVCCM pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi wakiomba dua katika Kaburi la Marehemu Mzee Abeid Amani Karume lililopo katika  eneo la Afisi Kuu ya CCM Zanzibar 

MSAFARA wa viongozi hao wakitoka katika kaburi la marehemu Mzee Karume mara baada ya kuomba dua. 

 MWENYEKITI wa UVCCM Taifa Kheir James(kushoto wa kwanza)  akitoa Shukrani kwa mapokezi aliyopewa na Uongozi wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar pamoja na SMZ kupitia Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed kama wanavyoonekana katika picha hiyo.

 MWENYEKITI  wa UVCCM Kheir James na Makamu Mwenyekiti Tabia Mwita wakivishwa sikafu na vijana wa Chipukizi mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Gymkhana.

 BAADHI ya vijana wa UVCCM waliobeba mabango yenye picha za viongozi wa UVCCM katika mapokezi hayo.

 MWENYEKITI wa UVCCM Taifa akisalimiana na viongozi na wanachama wa UVCCM na CCM kwa ujumla.



VIONGOZI wa UVCCM wakiwa meza kuu mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa Gmkhana.






 VIONGOZI wa UVCCM Taifa Makamu Mwenyekiti Tabia Maulid(kushoto) pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa wakivishwa maua maalum yanayobeba utamaduni wa Zanzibar ikiwa ni ishara ya kuwakaribisha visiwani humo.

 MWENYEKITI akipewa jezi na sikafu ya Zanzibar Heroes akiwa ni ishara ya kuwa ni mdau wa Soka la Zanzibar


 MAKAMU Mwenyekiti Tabia Mwita akipewa zawadi maalum iliyopo kwenye chupa ambayo ni zawadi maalum ya kumkaribisha nyumbani.

 BAADHI ya viongozi wa UVCCM na Jumuiya zingine za CCM Zanzibar.

 Kaimu Katibu Hamasa wa Chipukizi wa Umoja wa Vijana waChama cha Mapinduzi (UVCCM) Jokate Mwongelo.

 KAIMU Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Abdulghafari Idrissa Juma akizungumza katika mapokezi hayo.

 MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita akizungumza katika hafla ya  mapokezi hayo kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti.

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Shaka Hamdu Shaka akizungumza katika hafla hiyo

 MWENYEKITI wa UVCCM Taifa Kheir James akiwahutubia vijana wa UVCCM katika hafla hiyo.

 BAADHI ya viongozi wakongwe( MACOMRADE) wa Zamani wa UVCCM ambao kwa sasa ni viongozi wa Chama na Jumuiya zingine za CCM wakiwa katika hafla hiyo.



 BAADHI ya viongozi wa UVCCM walioudhuria katika hafla hiyo wakisoma dua.

VIONGOZI wa UVCCM wakisoma dua ya kuhitimisha hala hiyo.