Jumanne, 19 Desemba 2017

DK.SHEIN, JPM NA MANGULA WAPATA USHINDI WA KIHISTORIA

 
 Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi uliofanyika jana katika ukumbi wa Jakaya Kikwete mjini Dodoma, Spika Job Ndugai.
WAJUMBE wa mkutano mkuu wa tisa wa CCM, jana wamemchagua Dk. John Pombe Magufuli kuwa Mwenyekiti wa chama hicho baada ya kupata  jumla ya kura 1,821 ambazo ni sawa na asilimia 100.

Wajumbe hao pia wamemchagua Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar kwa jumla ya kura 1,819  sawa na asilimia 100.

Philip Mangula alichaguliwa kuwa Makamu mwenyekiti wa CCM Bara kwa kupata jumla ya kura 1,826.

Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi uliofanyika jana katika ukumbi wa Jakaya Kikwete mjini Dodoma, Spika Job Ndugai, pia aliwatangaza wajumbe 15 kutoka Zanzibar na Tanzania Bara waliowania ujumbe kwenye Halmashauri Kuu ya CCM.

Kabla ya matokeo hayo ya uchaguzi, Mwenyekiti wa muda Rais mstaafu William Mkapa aliwaalika viongozi wastaafu kutoa nasaha zao ambapo akizungumza kwa niaba ya viongozi wastaafu, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, alisema  serikali zote mbili zimejiwekea mipango mizuri ambayo ikitekelezwa nchi itaweza kusonga mbele kimaendeleo.

“Mipango mizuri sana na sina shaka na watekelezaji, kwa sababu yapo mengine wameyatekeleza kwa ujasiri, maana mengine yalihitaji utafune jongoo kwa maeno,”alisema Kikwete.

Aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuwa na subira kwa kuwapa muda viongozi kwani matatizo yanayowakabili Watanzania wanayaelewa, hata hivyo hayawezi kumalizika kwa muda mfupi.

Kikwete alisema kwenye mchakato wa urais alitumia nguvu kubwa kumtetea Magufuli pamoja na kuwepo taarifa kuwa hajawahi kuwa hata kuwa Mwenyekiti wa CCM wa tawi.

“Waliniuliza vipi anawezaje kuwa Mwenyekiti wa CCM wakati hata hajaongoza tawi la CCM nikasema anafaa, kwa bahati nzuri kazi ya Mwenyekiti haina chuo cha kwenda kusomea,”alisema.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni