Jumatano, 13 Desemba 2017

BULEMBO-AMTAKA MRITHI WAKE UMOJA WA WAZAZI KWENDA NA KASI YA 4G



NA IS-HAKA OMAR, DODOMA.

MWENYEKITI Mstaafu Umoja wa Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Abdallah Bulembo, amesema anatamani kuona mrithi wake ndani ya Umoja wa Wazazi anafanya Mapinduzi ya kiuchumi yaliyomshinda yeye kuyatekeleza enzi za uongozi wake.

Akizungumza na mwandishi wa Habari hizi katika mahojiano Maalum mara baada ya kutangazwa Mwenyekiti mpya kupitia uchaguzi uliofanywa jana huko Ukumbi wa JK Dodoma, amesema anamini kwamba Umoja huo umepata viongozi imara watakaowavusha salama kuelekea ng’ambo ya mafanikio.

Bulembo ambaye pia ni Mbunge ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema kwa upande wake ametatua changamoto kadhaa za taasisi hiyo lakini bado zipo nyingine ambazo viongozi wapya wanatakiwa kuzibadilisha zikawa ni fursa za kimaendeleo kwa chama na serikali kwa ujumla.

Amesema viongozi waliochaguliwa ni lazima watekeleze kwa vitendo yale waliyowaahidi wapiga kura wao wakati wa kuomba ridhaa za uongozi kwani Chama cha Mapinduzi ni kiwanda cha kuzalisha viongozi makini na wenye uthubutu wa kuwaletea maendeleo ya kweli watu wanaowaongoza.

Aidha amesema katika kipindi chote akiwa Mwenyekiti wa jumuiya hiyo amefanya mengi na tokea alipoingia mpaka anapoondoka jumuiya haijawahi kuomba fedha yoyote kutoka chama kwa ajili ya kuendesha vikao.

“Viongozi waliochaguliwa wamepatikana kwa njia za kidemokrasia bila mizengwe wala choko choko za rushwa, husia wangu kwao watekeleze majukumu yao kwa kufuata misingi ya Katiba na kanuzi za umoja wetu kwa lengo la kuepuka migongano isiyokuwa ya lazima.”, ametoa nasaha Bulembo.

Amesisitiza Umoja na mshikamano kwa viongozi na wanachama wa Jumuiya hiyo na kuongeza kuwa hiyo ndio itakuwa njia pekee ya kufikia mafanikio ya kudumu kwa jumuiya hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni