Jumatano, 7 Septemba 2016

TAARIFA YA WAZEE KWA VYOMBO VYA HABARI

KAULI YA BARAZA LA WAZEE WA CCM ZANZIBAR KUUNGA MKONO NA KUMPONGEZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI KWA HOTUBA YAKE ALIYOITOA KWA WAZANZIBARI WOTE KUPITIA MIKUTANO YA HADHARA ILIYOFANYIKA UWANJA WA GOMBANI CHAKE PEMBA TAREHE 02/09/2016 NA VIWANJA VYA DEMOKRASIA MJINI UGUJA TAREHE 03/09/2016

Baraza la wazee wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kwa niaba ya wazee wote wa CCM Unguja na Pemba wapenda amani na utulivu nchini unampongeza kwa dhati Rais wetu mpendwa kwa hotuba yake mwanana aliyoitoa kwenye mikutano ya hadhara miwili iliyofanyika visiwani humu kwenye tarehe tofauti.

Wazee tumehamasika kwa kauli mwanana sahihi iliyotolewa na Rais wetu mpendwa na tunaiunga mkono kwa dhati kabisa na tunashauri iwe ni dira kwa wanasiasa wote wa Tanzania, tunashauri viongozi na watendaji wakuu wa Serikali zetu zote mbili  kuzingatia na kutekeleza dhamira za Rais wetu kuleta Maendeleo ya haraka kwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
-    Kwa upande wa Zanzibar Mhe. Rais amehimiza mipango kadhaa, kama vile kusambaza maji safi na salama visiwani mote.
-    Kupanua miundo mbinu ya mawasiliano hasa uendelezaji wa ujenzi wa bara bara za lami visiwani.
-    Ujenzi wa viwanda kufanikisha Sera ya kuifikisha nchi yetu kwenye uchumi wa kati na kuifanya Tanzania kua ni nchi ya viwanda.
-    Kuhimiza uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, Zanzibar kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa nchini na Sheria husika zilizotungwa na Bunge na BLW.
-    Lakini pia kuhakikisha usalama na utulivu hapa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.  Mhe. Rais alikemea choko choko zisifanyike nchini petu ili kuhakikisha ukombozi wa uchumi wetu unafikiwa kikamilifu.
-    Sisi wazee, tunaamini na kukubaliana na kauli ya Rais Magufuli kwamba bila ya Amani na utulivu hayo yote hayataweza kufikiwa.
-    Kwa hiyo, tunaunga mkono kauli yake thabiti ya kuviagiza na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama viwe makini kuhakikisha Zanzibar inabaki kua tulivu na yenye Amani daima milele, kwa kuzingatia ukweli kwamba Uchaguzi Zanzibar umekwisha na uchaguzi unaofuata utafanyika mwaka 2020.
-    Kwa pamoja wazee wa CCM Zanzibar tunatoa heko kwa Rais wetu kutoa maagizo muhimu kwa maisha ya Watanzania wote na kuwa na msimamo madhubuti wa kuwatumikia wananchi wote na hasa kuwapendelea wananchi masikini wafikie kwenye ukombozi kamili.
-    Na mwisho tunampongeza Mhe. Rais kwa kuulinda Muungano wetu.  Pamoja na pongezi zetu wazee, tunawanasihi wananchi wenzetu wawe pamoja nasi kuona ukweli wa dhamira na vitendo vya Rais wetu kutekeleza kauli yake ya “Hapa kazi tu” na tushirikiane nae kuongeza bidii katika shughuli zetu za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
-    Tunamtakia Rais wetu afya njema, maisha marefu na uzima.KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!
UDUMU MUUNGANO WA TANZANIA
MAPINDUZI DAIMA!
 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni