CHAMA cha mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema kwamba kitapambana kisiasa kuhakikisha kinadhibiti mbinu, njama na mipango ya wapinzani kuvuruga uchaguzi mkuu ujao haifanikiwi.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, alipokuwa akiwahutubia wana CCM na wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kwa Mabata, Magogoni Unguja.
Vuai amesema viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa mstari wa mbele katika kupanga njama chafu na kuanzisha vurugu kila kukikaribia uchaguzi mkuu ili waonekane mbele ya taasisi za kimataifa kuwa wanaonewa na CCM, jambo ambalo watafeli katika uchaguzi wa mwaka huu, kwani serikali imejipanga ipasavyo kudhibiti hali hiyo.
Alifafanua kwamba licha ya Viongozi na wafuasi wa kambi ya upinzani kutoa vitisho na propaganda za upotoshaji dhidi ya CCM na Serikali zake, chama hicho hakitoyumbishwa na mwenendo huo, bali kitajipanga vizuri na kuhakikisha kinashinda kwa kishindo chini ya demokrasia ya vyama vingi nchini.
“
Tunaviambia vyama siasa nchini CCM itaendeleza wimbi la ushindi na kukamata hatamu ya dola Tanzania Bara na Zanzibar kufuatia ushindi mkubwa na wa kihistoria na tunawambia kuwa wapinzani hawawezi tena bora wajitoe mapema, vyenginevyo wataaibika mbele ya watu wao wanaowadanganya na kuwapotosha." Alidai Vuai.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar alisisitiza haja kwa Wazanzibari kufahamu kwamba Zanzibar inahitaji kiongozi (Rais) mwadilifu na mwenye busara za hali ya juu ya kuwaongoza wananchi kwa misingi ya amani na utulivu na kamwe siyo kiongozi mwenye uchu wa madaraka na kutawaliwa na ndoto za kuingia Ikulu kwa ajili ya kulipiza visasi.
Alizungumzia kuhusu serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na CCM imepiga hatua kubwa za kimaendeleo ikiwemo upatikanaji wa huduma bora za kijamii pamoja na kupanuka kwa miuondombinu mijini na vijijini, Unguja na Pemba.
Alisema katika bajeti ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2015/2016, imetoa kipaumbe kwa huduma za msingi za kijamii ikiwemo afya, elimu na sekta zingine zinazogusa maisha ya wananchi wa hasa wa kipato cha chini.
Alisema katika bajeti hiyo, kwa mara ya kwanza wazee wote waliostaafu serikali na wale ambao hawakufanya kazi za utumishi serikali kuanzia umri wa miaka 70 wataanza kulipwa pensheni ya shilingi 20 kwa kila mwezi kwa lengo la kuwapunguzia ukali wa maisha.
Aidha alifafanua kwamba kuanzia mwaka 2011 serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitoa mikopo ya fedha kwa wanafunzi wa elimu ya juu zaidi ya shilingi bilioni 26, kwa lengo la kuzalisha wataalamu wa fani mbali mbali wenye uwezo na weledi wa kufanya kazi katika sekta mbali mbali nchini.
Kuhusu serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar (SUK) Vuai aliwambia viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani hasa CUF kwamba wao ndio wanaoanzisha choko choko za kuvuruga dhamira na malengo ya kuanzishwa kwa serikali hiyo.
“CCM tulitaka kuanzisha SUK mapema kutokana na CUF kukataa katika vikao vilivyofanyika Butiama mwaka 2008, baada ya mazungumzo baina ya CCM na Chama hicho yaliyochukua miezi 14 bila ya mafanikio.
Lakini wenzetu baadae wakarudi wenyewe kutaka tuanzishe serikali yenye mfumo huo (SUK) lakini kwa vile sisi CCM ni waungwana tukakubali lakini tulijuwa kuwa wenzetu wana nia na malengo ya kuingia Ikulu na siyo kujenga umoja na mshikamano wa Wazanzibari.”
Alisisitiza Naibu Vuai.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ya Taifa, Pandu Ameir Kificho, aliwasihi wananchi wa Wazanzibari kuweka kando ushabiki wa kisiasa na kufanya maamuzi yanayofaa kwa kuunga mkono katiba inayopendekezwa, ili kuipitisha kuwa katiba kamili kwani imebeba mambo ya msingi kwa maslahi ya jamii ya pande zote mbili za muungano.
Alisema kuwa baadhi ya viongozi wa kisiasa Zanzibar wamekuwa na utamaduni usiofaa wa kuwahamasisha wananchi kushiriki katika vitendo vya uvunjaji wa Amani na utulivu nchini.
“Lazima wananchi tujiepushe na utumwa wa kupandikizwa mbegu za chuki na kutugawa hasa katika kipindi hichi cha maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwani watu wote duniani wameelekeza masikio ya Zanzibar, kufahamu nini tutafanya.”Alishauri Kificho.
Naye Mwenyekiti wa Mkoa Magharibi Kichama, Yussuf Mohamed Yussuf aliwataka wafuasi wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kuendelea kujipanga kisaikolojia kwa kupima uwezo na sera za kila chama kiutendaji na hatimaye watajua wapi waunge mkono katika uchaguzi mkuu huo.
Yussuf alisema kuwa CCM ipo imara na ina uwezo wa kupambana na vikwazo vyote vilivyowekwa na CUF vikiwemo kupandikiza mbegu za chuki kwa wananchi kwa kubeza na kudharau kila jambo jema linalofanywa na serikali ya CCM, suala ambalo wananchi waliokuwa wengi wameshutuka na kuona wananyang’anywa ambao kwa sasa wanarudi katika chama cha mapinduzi chenye sera makini na zinazotekelezeka.
Katika hali isiyotarajiwa wakati mgeni rasmi kwenye mkutano huo akijiandaa kushuka kwenye jukwaa ghafla watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa chama cha CUF walianza kurusha mawe katika ya mkutano huo, lakini hali hiyo ilidhibitiwa mapema na askari wa jeshi la polisi na haikuleta madhara kwa wananchi waliokuwa katika mkutano huo.
Katika hali isiyotarajiwa wakati mgeni rasmi kwenye mkutano huo akijiandaa kushuka kwenye jukwaa ghafla watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa chama cha CUF walianza kurusha mawe katika ya mkutano huo, lakini hali hiyo ilidhibitiwa mapema na askari wa jeshi la polisi na haikuleta madhara kwa wananchi waliokuwa katika mkutano huo.