Alhamisi, 30 Novemba 2017

NAGMA GIGA- AFUNGUA MKUTANO WA UCHAGUZI WAZAZI, ASISITIZA USHIRIKIANO KUDHIBITI UDHALILISHAJI

Na Is-haka Omar, Zanzibar.
             
NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Nagma Giga amewataka wazazi na walezi kuunga mkono juhudi za serikali na wanaharakati kwa kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto nchini.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Wazazi katika Mkoa wa Mjini, uliofanyika Amaani Unguja.

Amesema wazazi ndio walezi na waangalizi wa malezi ya makundi yote katika jamii hivyo ni lazima wawe mstari wa mbele kupinga vitendo vyote vinavyoensda kinytume na maadili, mila desturi na utamaduni visiwani humo.

Amefafanua kwamba ushindi dhidi ya vitendo vya udhalilishaji itafanikiwa endapo jamii itakuwa tayari kushirikiana na Serikali na vyombo vingine vya kisheria ili kudhibiti uhalifu huo unaochafua heshima na sifa ya nchi kitaifa na kimataifa. 

"Hii ni vita yetu sote kila mzazi amuone mtoto wa mwenziwe kama wake hapo ndipo tutakapoweza kuwalinda watoto wetu ili wakue katika malezi bora yasiyokuwa na vikwazo vya kukatisha malengo yao ya baadae.

Wanawake na watoto wengi wamekuwa ni wahanga kubakwa,kulawitiwa na kutelekezwa hali inayosababisha wengi wao kuathirika kisaikolojia ” Ameeleza kwa uzuni Nagma. 

Pia aliwasihi wazazi, viongozi wa dini na wanasiasa nchini kuhakikisha wanakemea kuporomoka kwa maadili kwa baadhi ya vijana wanaovaa nguo zinazokwenda kinyume na utamaduni sambamba na kutumia lugha zisizofaa katika jamii. 

Akizungumzia Uchaguzi wa Mikoa mbali mbali ya jumuiya hiyo, Nagma amewasisitiza wajumbe wa mikutano hiyo kuwachagua viongozi imara na wenye dhamira ya kweli katika kuleta mabadiliko ya kimaendeleo ndani ya jumuiya na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla.

Amesema wasimamizi wa uchaguzi huo kutenda haki na wapiga kura kuwa na uadilifu wakati wa kutekeleza wajibu wao wa kidemokrasia kwa kuchagua viongozi wanaowataka bila ya kufanya vurugu.

Naibu Katibu Mkuu huyo, amesema Jumuiya hiyo ina majukumu mawili makubwa ya kuhakikisha CCM inashinda na kubakia madarakani kupitia uchaguzi mkuu wa Dola sambamba na kusimamia mwenendo wa elimu, malezi, utamaduni na mazingira kwa jamii.

Ameeleza kuwa  nchi zilizoendelea Ulimwenguni ni zile zilizowekeza katika sekta ya elimu inayozalisha wataalamu wa fani mbali mbali za kuleta maendeleo ya haraka katika kukuza uchumi wa nchi kupitia mfumo wa uzazilishaji mali katika sekta za viwanda vinavyotegemea mfumo wa sayansi na teknolojia.

“Kila wana CCM anatakiwa kuchukua jukumu la kuwaelimisha vijana wetu wasome kwa bidii ili Chama na jumuiya zetu ziwe na wanachama wengi wenye uwezo mzuri wa kitaaluma watakaoweza kusimamia maslahi ya taasisi zetu bila kuyumba.

Mikakati hiyo itafanikiwa kama tutapata viongozi makini kupitia uchaguzi huu ambao ni wapambanaji wasiochoka wala kukata tama katika uwanja wa kisiasa.” Amefafanua Naibu Katibu Mkuu Giga. 

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Amani ambaye ni mjumbe wa Mkutano huo, Abdi Ali Mzee ‘’Mrope’’ amesema wakati umefika wa Chama cha Mapinduzi na jumuiya zake kuwa na ajenda moja ya kutumia vizuri rasilimali zinazomilikiwa na Chama kuanzisha miradi mikubwa itakayozalisha kipato na kutoa ajira za kudumu kwa vijana.

Kwa upande wake mjumbe wa Mkutano huo, Salma Abdi Ibada amewashauri viongozi watakaochaguliwa kupitia uchaguzi huo wawe mfano wa kuigwa katika kuleta maendeleo ndani ya jumiya na kupiga vita vitendo vya rushwa na makundi ya kuhatarisha uhai wa Chama. 

Uchaguzi huo umefanyika katika Mikoa yote jumuiya ya Wazazi nafasi ambazo zinashindaniwa ni Wenyeviti wa Mikoa, nafasi ya Mkutano mkuu taifa/Baraza la wazazi taifa, nafasi mkutano mkuu wa CCM mkoa, pamoja na nafasi za Baraza kuu la wazazi Mikoa kutoka kila Wilaya.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini Mohamed Omar Nyawenga(kushoto) Naibu katibu Mkuu wa Jumuiya ya wazazi Zanzibar Nagma Giga (katikati) na viongozi wengine wa jumuiya ya wazazi.

 BAADHI ya wajumbe wa Mkutano huo wakisikiliza kwa makini hotuba ya ufungunguzi ya mgeni rasmi


Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Amani, Abdi Ali Mzee “Mrope” akiwasalimia wajumbe wa mkutano huo wa uchaguzi jumuiya ya wazazi Mkoa wa Mjini.


Jumatano, 29 Novemba 2017

DK.MABODI AWATAKA UVCCM KUCHAGUA VIONGOZI WANAOUZIKA KISIASA

Na Is-haka Omar, Zanzibar.
       
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi, amewataka Umoja wa Vijana UVCCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, kuwachagua viongozi wa jumuia hiyo ambao ni waadilifu, wabunifu na wachapakazi watakaolinda na kutetea maslahi mapana ya UVCCM. 

Wito  huo  ameitoa leo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa UVCCM, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo alisema viongozi watakaochaguliwa kupitia uchaguzi huo. 

Dk. Mabodi amesema  Vijana wanapaswa kuwa wabunifu kwa kuandaa mazingira rafiki ya kuwavutia vijana kujiunga na CCM kutoka vyama vya upinzani.

Amesema viongozi watakaopatikana kupitia uchaguzi huo ndio watakaounda jeshi la ukombozi wa kisiasa litakalosaidia kupata ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

 Naibu huyo aliongeza kuwa wajumbe ambao watachagua viongozi hao wanapaswa kuhakikisha watekeleza sera na Ilani ya CCM.

 Katika maelezo yake Dk. Mabodi alisema UVCMM inapaswa kuzingatia ibara ya tano ya Chama ambapo inaelekeza kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola hivyo ni wajibu wao kama vijana kutekeleza.

 "Chama kinatoa kipaumbe cha kupatia nafasi mbalimbali za uongozi kwa vijana ili waweze kusimamia kwa uadilifu sera na miongozo ya chama na serikali kwa maslahi ya wananchi wote,"alisema.

 Amesema  jukumu kubwa ni kuhakikisha vijana wanashawishi wenzao ili kujiunga ndani ya chama hivyo lazima viongozi watakaopatikana wawe wabunifu na wachapakazi wa kuifikisha CCM ushindi wa mwaka 2020.

 "Ikimbukwe kuwa viongozi ambao watakaoshinda ndio wameaminiwa na chama hivyo wajibu wao ni kutengeneza siasa ya mkoa kwa ajili ya ushindi wa mwaka 2020,"amesema. 

 Mbali na hilo,  amesema  ikumbukwe kuwa wakati huu ni wamapambano makali hivyo ni lazima vijana watambue kuwa ni CCM ya mabadiliko na kwamba hakuna kulala hadi kuhakikisha ushindi wa uchaguzi mkuu ujao. 

 Dk.Mabodi amesisitiza jumuia hiyo kuendeleza na kusimamia kwa uadilifu mambo mema yaliyonayo na kufafanua kuwa moja ya malengo makuu ya chama cha siasa chochote ni kushinda uchaguzi mkuu kwa kuendelea kushika dola. 

 "Na hiyo ndio sababu ya msingi ya CCM kuandaa jeshi lake la kisiasa kupitia uchaguzi wa chama ndani ya jumuia hii UVCCM na hivyo ni lazima vijana wawe daraja la kuwaunganisha vijana wenzake na kuwashawishi kujiunga ndani ya CCM kutoka vyama vya upinzani,"amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti ambaye amemaliza muda wake, Bakari Musa Vuai, amewasisitiza wajumbe wa mkutano huo kuchagua viongozi watakaoisaidia ushindi wa uchaguzi ujao. 

Amesema  viongozi watakaopatikana ndani ya jumuia hiyo ya UVCCM wanapaswa kuwa wenye sifa kama kanuni na katiba inavyotaka na kwamba jambo ni kujenga jumuia mpya.

Akizungumza Mjumbe wa Kamati Maalum ya CCM Taifa, Khadija Hassan Aboud alisema  vijana kutumia vizuri fursa za uongozi wanazopewa ndani ya CCM na jumuiya zake ili kujenga heshima ya kundi hilo katika jamii.

Pamoja na hayo amesema  CCM ndio chama pekee kinachopigania haki za wananchi wa makundi yote bila ya ubaguzi hivyo na kwa viongozi watakaochaguliwa wanatakiwa kuendeleza utamaduni huo ili kuimarisha jumuiya hiyo. 

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa UVCCM Mkoa wa Kaskazini Unguja wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano huo.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Mhe Khadija Hassan Aboud akizungumza katika Mkutano Mkuu Maalum wa UVCCM Mkoa wa Magharibi uliofanyika katika ukumbi wa Peace Building huko Welezo Unguja.

MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi UVCCM Mkoa wa Mjini akipiga kura katika uchaguzi huo.

Jumanne, 28 Novemba 2017

UWT NGAZI ZA MIKOA ZANZIBAR WAFANYA UCHAGUZI

Na Is-haka Omar , Zanzibar.

JUMUIYA ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) ngazi za Mikoa ya Zanzibar leo wamefanya uchaguzi wa kuwapata viongozi mbali mbali watakaoongoza Jumuiya hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Akizungmza katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa UWT Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais Mama Asha Suleiman Idd,uliofanyika katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, amewataka wagombea ambao watashinda katika nafasi mbalimbali kuwa chachu ya kuendeleza Umoja na mshikamano ndani ya jumuiya hiyo.


Alisema uchaguzi huo ni muhimu kwa kila mwanachama wa  jumuiya hiyo kwani viongozi watakaochaguliwa ndio wenye dhamana ya kuunda jeshi la kisiasa litakalofanikisha ushindi wa CCM mwaka 2020.

Hata hivyo amewasihi wagombea watakaoshindwa katika uchaguzi huo wawe na subra na wasiinunie jumuiya wala kukisusia Chama kwani uongozi unatokana na majaliwa ya mwenyezi Mungu.

 Amesema uchaguzi si uhasama na kwamba baada ya mchakato huo kuisha kinachotakiwa ni kuendelea kushikamana kwa ajili ya ushindi wa mwaka 2020 wa CCM.
 Aliongeza kwa kufafanua kuwa haina maana wagombea hao kukinunia chama ama kususa kutokana na ushindani ulioko ndani ya jumuia.

Katika maelezo yake Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais, alisema kinachotakiwa katika uchaguzi huo ni kuwapata viongozi wapiganaji ambao watafanya kazi kwa pamoja ili kuleta mabadiliko makubwa katika jumuia hiyo.

“Maendeleo ndani ya UWT yataletwa na wanawake wa CCM na sio taasisi wala watu wengine, hivyo tuendelee kutumia nguvu na ushawishi tulionao kuhakikisha miaka mitano ijayo jumuiya inakuwa na mabadiliko makubwa ya kimaendeleo.

 Wagombea hao wanapaswa kutambua kuwa lazima wakubaliane na matokeo ya uchaguzi ambao wajumbe watawachagua kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa chama. ” Alisema Mama Asha.

Aliwataka akina mama hao kuwashawishi idadi kubwa ya wanawake kuingia ndani ya CCM na kwamba wajiulize chama wamekifanyia nini jibu lake ni kukiongezea nguvu kubwa kwa kwavuta wanachama wapya kujiunga na Chama.

Mbali na nasaha hizo, alieleza kuwa matokeo ya ushindi wa uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata mbali mbali huko Tanzania Bara unatokana na sera ya Rais Dk.John Magufuli aliyoingianao hivyo ni vyema UWT mkoa huo ujitathmni na kuhakikisha wanafanya mikakati ya ushindi wa mwaka 2020.

“Tujifunze kuwa siasa zetu za huku na za Bara tofauti hivyo tujifunze kuwa watu wanataka maendeleo na si huku watu wanamtaka mtu ndio maana sasa matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani umejionesha wazi hivyo sisi kazi yetu huku ni kuonesha na kuwashawishi wananchi waone maendeleo yanayofanywa na CCM ili iwei rahisi katika ushindi wa mwaka 2020,”alisema.

Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza Kuu UWT, Panya Ali Abdalla, aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha wanachagua viongozi madhubuti ambao watakisaidia chama katika kuleta mabadiliko ndani ya chama na jumuia hiyo.

Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Kaskazini, ambaye muda wake umekwisha, Miza Ali Kombo, alisema wajumbe ambao watapiga kura katika uchaguzi huo ni 129 na kwamba waliohudhuria ni 118 katika majimbo tisa ndani ya mkoa huo.

Mapema Akifungua Mkutano Mkuu wa UWT, Mkoa wa Mjini Unguja, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuwachagua viongozi bora wasiokuwa na makundi ya kuhatarisha uhai wa chama na jumuiya hiyo.

Aliwataka viongozi watakaoshinda katika uchaguzi huo wahakikishe wanakwenda sambamba na kasi ya utendaji wa CCM katika kusimamia vizuri utekelezaji wa sera zake kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Kwa upande wake Katibu wa UWT Mkoa wa Kusini Unguja, Sitamili Omar  Dendego alisema uchaguzi umefanyika vizuri katika mkoa huo na wanatarajia kuwapata viongozi watakaolinda maslahi ya jumuiya na CCM kwa ujumla.

Uchaguzi huo uliofanyika katika Mikoa yote ya UWT Zanzibar na Tanzania kwa ujumla nafasi ambazo zinashindaniwa  ni Wenyeviti wa Mikoa, Wajumbe wa Baraza kuu Taifa nafasi nne,Wajumbe wa Baraza Kuu Mkoa nafasi 10, Mwakilishi wa Umoja wa Vijana(UVCCM) nafasi moja na Jumuia ya Wazazi nafasi moja.
Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mama  Asha Suleiman Idd akifungua mkutano mkuu wa UWT Mkoa wa kaskazini Unguja.

 Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa UWT Mkoa wa Kaskazini Unguja.

 Baaadhi ya Wajumbe wa  Mkutano Mkuu wa  UWT Mkoa wa Mjini Unguja.
Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu  wa UWT Mkoa wa Kusini Unguja wakifuatilia kwa umakini mchakato wa uchaguzi unaoendelea katika Mkoa  huo.

Mjumbe kutoka kundi la Vijana akiomba kura katika Mkutano Mkuu wa  UWT Mkoa  wa  Kusini Unguja.

    

Jumatatu, 27 Novemba 2017

REJA- WATUMISHI SOMENI KATIBA CCM NA KANUNI

Na Is-haka Omar, Zanzibar.

               


WATUMISHI na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Zanzibar  wameshauriwa  kuzisoma, kuzielewa na kuzifanyia kazi kwa vitendo Katiba ya CCM ya mwaka 1977 pamoja na Kanuni zake.

Pia, wamesisitizwa kutumia miongozo hiyo ikiwemo mabadiliko ya Katiba hiyo yaliyofanywa hivi  ambayo ni nyenzo muhimu ya kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Chama na rasilimali watu kwa ujumla.

Akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo Watumishi wa Afisi Kuu ya CCM Zanzibar,  Mkufunzi kutoka Makao Makuu ya CCM Dodoma Salum Khatib Reja, amesema  Katiba ya Chama ndio chombo pekee kinachoeleza kwa upana wajibu na haki za kila mwanachama.

Amesema ukitaka kuijua CCM ni lazima uzisome na kuzielewa vizuri Katiba na Kanuni zake ni miongoni mwa vyombo vinavyosimamia ustawi wa Chama na Jumuiya zote.

Mkufunzi  Reja, ameongeza kuwa endapo watumishi hao watafuata maelekezo yaliyotolewa katika miongozo hiyo itasaidia kumaliza malalamiko na tuhuma zisisokuwa za lazima kwani kila kitu kitakuwa kimeamliwa kwa kufuata matakwa ya kikatiba.

Amesema siri ya kuimarika kwa Demokrasia ndani ya CCM ni kutokana na utamaduni wake wa kufuatwa kwa misingi ya Kikatiba badala ya matakwa binafsi ya viongozi ama Watendaji wa Chama.

“ Kila mtumishi anatakiwa kujitathimini na kutafakari kwa kina ni kwa namna gani atasaidia kuleta maendeleo ndani ya Chama ili taasisi hiyo iendelee kuwa chama bora cha kisiasa barani Afrika na Ulimwenguni kote”. Alisema.

Akitoa mada ya majukumu ya Idara ya Itikadi na Uenezi Mkufunzi  Eva Degeteki, amesema miongoni mwa majukumu ya msingi ya Idara hiyo ni kuendeleza mahusiano mema na vyombo vya habari nchini ili vitangaze na kuripoti  kwa usahihi matukio na habari mbali mbali za Chama.

Kupitia mafunzo hayo, Eva amewataka watumishi hao kuendelea kujifunza itikadi na miongozo ya CCM ili kufikia malengo na shabaha za taasisi hiyo kwa ufanisi zaidi.

Akitoa neno la Shukrani Mtumishi wa CCM ,  Catherine Peter amewahi watendaji wenzake kuongeza bidii katika utekelezaji wa majukumu yao ili chama kiweze kushinda katika uchaguzi Mkuu ujao.

Kwa upande wake Muhsin Daud Suleiman,  ambaye ni miongoni mwa washiriki wa Mafunzo hayo, amesema mada zilizotolewa zimekidhi mahitaji ya watumishi hao kwani wamejifunza mambo muhimu yatakayosaidia kuongeza kasi ya kiutendaji kazini.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, idara ya Organizesheni CCM Zazibar , Haji Mkema Haji akifungua Mafunzo hayo yaliyofanyika Afisi Kuu CCM  Kisiwandui Unguja.

Mkufunzi wa mafunzo hayo Eva Degeteki akitoa ufafanuzi juu ya mada ya majukumu ya Idara ya Itikadi na Uenezi kwa Watumishi hao katika Mafunzo Afisi Kuu CCM, Kisiwandui Zanzibar.

Mkufunzi Ali Juma Makoa akifafanua umuhimu wa matumizi mazuri ya rasilimali fedha kwa watumishi katika mafunzo hayo.
Mkufunzi wa mafunzo hayo Filbert Mdaki Mampwepe akisisitiza suala la kujituma na ubunifu kwa watendaji hao.

Mshiriki wa mafunzo hayo Catherine Peter Nao akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake.
Mshiriki wa mafunzo hayo Muhsin Daud Suleiman akizungumza kwa niaba ya Watumishi wapya katika mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi hao.

Jumapili, 26 Novemba 2017

AFISI KUU CCM ZANZIBAR WATWAA UBINGWA MASHINDANO YA MAJIMBO

Na Is-haka Omar, Zanzibar.
               
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa ameeleza kuwa mchezo wa soka ni miongoni mwa masoko huria linatoa nafasi kwa vijana nchini kujiajiri wenyewe.

Akihutubia mamia ya wapenzi wa soka katika fainali za mashindano ya majimbo ya Unguja kwa mchezo huo iliyofanyika katijka uwanja wa michezo wa Amaan Zanzibar.

Amesema mchezo huo umekuwa maarufu ulimwenguni na unatoa fursa mbali mbali kwa vijana ambao wana vipaji vya mchezo huo.

Aidha Mhe. Majaliwa amepongeza waandaaji wa mashindano hayo kwa kubuni mashindano la kuwakutanisha vijana katika jukwaa moja kupitia sekta ya michezo bila kujali tofauti zao kisiasa kiuchumi na kijamii.

Waziri Mkuu Majaliwa ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, amesema CCM imekuwa ni mlezi bora wa kulea makundi mbali mbali ya kijamii hususani vijana ambao kitakwimu ni wengi kuliko makundi mengine na kuwataka wawe na maadili mema yatakayosaidia kukuza sekta za utamaduni na uchumi.

Ametoa wito kwa majimbo mbali mbali ya CCM kwa upande wa Tanzania bara  kuiga mfano wa majimbo ya Zanzibar  kwa kuandaa mashindano ya michezo mbali mbali kwa vijana ili kuibua vipaji vitakavyoendelea kuijenga heshima ya  nchi kimichezo katika anga za kimataifa.

“Kupitia mchezo huu nimeona vijana wengi wenye vipaji wanaoweza kucheza katika timu kubwa zilizopo nchini, hivyo endeleeni kujitokeza na kushikamana na michezo ili kujiepusha na vikundi viovu kwani mtapoteza muelekeo wa maisha yenu’’, alisema Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.

Mapema  Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Abdulla Juma Mabodi alisema  mchezo huo umeongeza mahusiano mema kwa  majimbo yote yaliyoshiriki  katika mashindano hayo.

Dk. Mabodi alisema CCM kitaendele kuwa karibu na waandaji wa mashindano hayo  katika ligi zijazo kwa lengo la kudumisha amani, utulivu na mahusiano mazuri kwa vijana nchini.

Mashindano hayo yalianza kutimua vumbi toka mwezi Mach 24 mwaka huu yalizinduliwa na Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein yakiwa na timu 18 za Majimbo ya Unguja.

Katika fainali hiyo timu ya Afisi Kuu CCM Zanzibar imefanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano hayo baada ya kuifunga timu ya Jimbo la Kwahani magoli 3 – 1 yaliyofungwa na Kheir Makame mnamo dakika za 25, 32 na Haidham Khamis ksatika dakika ya 65 wakati goli la Kwahani lilifngwa na Yusuf  Juma katika dakika ya 15.

 Kufuatia ushindi wa timu ya Afisi Kuu CCM Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Mabodi amewapongeza wachezaji wa timu ya Afisi Kuu kwa kutwaa ubingwa huo na kuipa zawadi ya shilingi Milioni tano.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (kushoto) akikabidhi Gari ndogo aina ya Carry kwa nahodha wa timu ya Afisi Kuu CCM Zanzibar, Vuai Makame Jecha.

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (kushoto) akimkabidhi ufunguo Gari ndogo aina ya Carry nahodha wa timu ya Afisi kuu CCM Zanzibar Vuai Makame Jecha mara baada ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya Majimbo Zanzibar baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 3 – 1 dhidi ya timu ya Kwahani.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir Ali Maulid akikabidhi zawadi ya mchezaji bora wa mashindano ya majimbo nahodha wa timu ya Afisi Kuu CCM Zanzibar Vuai Makame Jecha.

Viongozi mbali mbali wa Serikali na CCM wakiwa jukwaa kuu la Uwanja wa Amaan Stadium wakifuatilia mchezo huo.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akiwa na kombe la ubingwa wa mashindano ya majimbo ya Zanzibar pamoja na wachezaji wa timu ya Afisi Kuu CCM Zanzibar mara baada ya kutwaa ushindi wa mashindano hayo.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika uwanja wa Amaan kuangalia mechi hiyo wakifuatilia kwa makini timu zao.

Ijumaa, 24 Novemba 2017

MH.KASSIM MAJALI MGENI RASMI FAINALI MAJIMBO CUP ZANZIBARNa Is-haka Omar, Zanzibar.

WAZIRI Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa  kesho Novemba 25, mwaka huu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mashindano ya fainali ya ligi za Majimbo ya Mkoa wa Mjini  Zanzibar.


Mchezo huo utakaotimua vumbi katika Kiwanja  cha Amaan Stadium Unguja, ambapo utazikutanisha timu mbili zilizofanikiwa kufika finali ambazo ni Timu ya Afisi Kuu CCM Zanzibar na Timu ya Jimbo la Kwahani.

Kabla ya mtanange huo mkali kutatanguliwa na mechi ya kumsaka mshindi wa tatu ambayo itachezwa na timu za jimbo la Kikwajuni na jimbo la Malindi kwa ajili ya kutafuta mshindi wa tatu.
Michezo hiyo inayotarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na uwezo wa kila timu katika masuala ya Soka.

Akizungumza na mwandishi wa Habari hizi Katibu wa Kamati ya mashindano hayo, Suzan Kunambi amesema maandalizi ya fainali hiyo tayari yamekamilika kwa upande wa Kamati yake na kwa timu zinazotarajiwa kushiriki zote zimedhibitisha ushiriki wao.

Ameeleza kwamba mashindano hayo yaliyoanza mwezi Machi 24 mwaka huu kwa kuzishirikisha timu 18 za majimbo pamoja na vikundi vya uhamasishaji vya CCM kutoka Mkoa wa Mjini pamoja na majimbo jirani yaliyoalikwa kutoka Mikoa yote ya Unguja.

Katibu huyo amefafanua kuwa mashindano hayo yalizinduliwa  na Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein na yanatarajiwa kufungwa na Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaaliwa.

Suzan ameyataja malengo ya mashindano hayo kuwa ni kujenga umoja na mshikamano kwa vijana mbali mbali waliopo majimboni ili wajikwamue katika changamoto za ukosefu wa ajira na makundi maovu kwa kujiajiri wenyewe kupitia vipaji vyao vya soka.

Amesema  mashindano hayo yamekuwa ni chachu ya kuibua vipaji vya soka ambapo wacheza mbali mbali wamepata fursa za kujiunga na timu kubwa zilizopo katika mashindano ya ligi za madaraja mbali mbali ya soka nchini.

“ Tunamshukru Makamo Mwenyekiti wetu Dk. Shein kwa mchango wake mkubwa wa kuthamini soka la vijana na kuimarisha sekta ya michezo nchini”, alitoa pongezi hizo Katibu huyo na kuongeza kuwa Kamati hiyo imejipanga kushirikisha timu nyingi zaidi ili mashindano yaendelee kuwa bora na kuwanufaisha vijana.

Akizungumzia zawadi zitakazotolewa kwa mshindi wa mwanzo hadi wa tatu amefafanua kuwa mshindi wa kwanza atapata Gari moja, Kikombe na medali ambapo mshindi wa Pili atapata fedha taslim shilingi milioni tatu na medali pamoja na mshindi wa tatu atapata shilingi milioni mbili na medali.

Sambamba na hayo aliwaomba wapenzi wa Soka wa ndani na nje ya Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa Amaan kushangilia timu zao kwani kiingilio ni bure.

 Mechi ya mwanzo itachezwa majira ya saa 8:00 mchana na ya pili ambayo ni fainali itachezwa kuanzia majira ya saa 10:00 jioni.