Jumatano, 1 Novemba 2017

WAZIRI SOUD, KHATIB WASEMA SERA ZA CCM CHACHU YA USTAWI WA KARAFUU PEMBA.

              

MAWAZIRI wasiokuwa na Wizara Maalum wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Said Soud na Juma Ali Khatibu wamesema maendeleo yaliyofikiwa Kisiwani Pemba katika Nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa yanatokana na usimamizi mzuri wa Sera za Chama Cha Mapinduzi.

Hayo waliyabainishwa katika ziara Maalum ya kukagua uchumaji wa zao la Karafuu  katika Mikoa mbali mbali ya Pemba, walisema CCM ndio mkombozi wa wananchi kwani bila Chama hicho kuwa madhubuti  katika kusimamia siasa zake nchi isingeweza kupata maendeleo  yaliyopo hivi sasa.

Akizungumza Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum Juma Ali Khatib alielezea kuridhishwa kwao na juhudi za wakulima wa zao la Karafuu kuwa zinaenda sambamba malengo ya Serikali katika kuongeza thamani ya zao hilo Kibiashara.

Khatib, alieleza Kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar , inayoongozwa na Dkt, Ali Mohammed Shein, imewajengea mazingira mazuri Wakulima wa Karafuu kwa kuwapandishi bei kubwa ambayo itawanufaisha na hivyo iko tayari kupambana na wale wote wenye nia  na dhamira mbaya ya kulihujumu zao hilo kwa njia yoyote ile. 

“Serikali imeongeza bei ya zao la karafuu kwa makusudi kwa ajili ya kuwainua wakulima wa karafuu kwa kuwapa asilimia 80% na Serikali kubakia na asilimia 20%, hivyo kwa thamini juhudi hizo ni vyema wakulima wakauza zao hilo katika vituo vilivyoruhusiwa Kisheria” alisema Juma.

Naye  Mwanasiasa Mkongwe  kutoka Chama cha Wakulima AFP  Said Soud, ambaye ni Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar Dk. Shein, amewasihi wananchi wa Kisiwa cha Pemba kuendelea kutunza Amani na Utulivu wa nchi ili wapate muda mzuri wa kufanya shughuli za kuingiza kipato zikiwemo za kilimo hasa cha karafuu.

Alitamka wazi kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kutekeleza kwa nguvu zote Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 Mijini na Vijijini  bila kujali tofauti za kisiasa, kidini na kikabila  na wao wakiwa ni wasaidizi wa Rais wa Zanzibar  Dk. Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar  ili wananchi wapate maendeleo endelevu.

Aliwasihi wakulima na wananchi kwa ujumla wa Kisiwa hicho kulinda na kuthamini zao hilo kuwa ndio nyenzo pekee ya kuwakomboa katika wimbi la umasikini wao pamoja na vizazi vyao vijavyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni