Jumamosi, 11 Novemba 2017

Zaidi ya milioni 42 zimetumika katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo ya Umoja wa Vijana (UVCCM)


ZAIDI ya Shilingi milioni 42 zimetumika katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo ya  Umoja wa Vijana (UVCCM)  wa Jimbo la Kwahani  katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Hayo yameelezwa katika ziara mwendelezo  wa ziara ya  Mwenyekiti wa UVCCM  Wilaya ya Mjini alipotembelea  katika Jimbo hilo kwa lengo la kuimarisha jumuiya hiyo pamoja na kukagua utekelezaji wa ahadi za CCM ilizoahidi katika katika kampeni za uchaguzi Mkuu  uliopita.

Akisoma  risala Katibu wa UVCCM Jimbo hilo, Mariam Ramadhan Idd alisema  miradi hiyo iliyotekelezwa na Mbunge, Mwakilishi na Madiwani wa jimbo hilo ili isaidie kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili Vijana wa jimbo hilo.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na kuyajengea uwezo  Mabaraza ya Vijana ya wadi, kulipia gharama za masomo  vijana wanaosoma  kuanzia ngazi ya sekondari  hadi Shahada ya kwanza  pamoja na kuvisaidia vilabu vya michezo ndani ya jimbo hilo.

Katibu huyo alisema mara baada ya kuingia uongozi mpya wamejipanga kuendeleza madarasa ya Itikadi na kuongeza wanachama wapya ndani ya UVCCM na Chama kwa ujumla ili kupata wapiga kura wa uhakika watakaofanikisha Ushindi wa CCM mwaka 2020.

Alieleza kwamba vijana wa jimbo hilo bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira hivyo wanaomba CCM, serikali na watu wenye uwezo kuanzisha miradi ya kudumu itakayowasaidia vijana kujiajiri wenyewe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mjini, Hudhaima Mbarouk Tahir aliwashauri  Mbunge, Mwakilishi na madiwani  kuwashirikisha vijana ipasavyo pindi wanapotekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.

Alisema dhamira ya UVCCM ni kuhakikisha vijana wanaendelea kuwa mfano wa kuigwa kiutendaji,kimaadili na uongozi kwa lengo la kutekeleza kwa vitendo falsafa ya siasa shirikishi yenye maslahi kwa wananchi wote.

“ Nawapongeza vijana kwa juhudi zenu za kuipigania  UVCCM licha ya kukabiliwa na changamoto mbali mbali lakini bado mpo imara juu ya kulinda na kutetea maslahi ya CCM”, alisema.

Mapema Mwenyekiti huyo alipandisha bendera ya Chama  katika Maskani ya UVCCM inayojulikana kwa jina la ‘Chemba’ katika Tawi la Muungano ikiwa ni ishara ya kuunga mkono harakati za kisiasa za vijana wa Umoja huo.

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
  
 
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni