Ijumaa, 30 Juni 2017

WABUNGE NA WAWAKILISHI PEMBA WATAKIWA KUWEKEZA KATIKA ELIMU





Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka Wabunge na Wawakilishi kisiwani Pemba kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuwasaidia vijana wanaosoma kwenye shule na vyuo vya elimu ya juu vilivyopo katika kisiwa hicho.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdulla Juma Saadalla “Mabodi” katika mwendelezo wa ziara yake Pemba wakati akikagua ujenzi wa shule ya Msingi na Sekondari ya Kwale Mkoa wa Kusini Pemba.

Amesema viongozi hao wanatakiwa kubuni miradi itakayosaidia kuinua viwango vya elimu kwa vijana mbali mbali waliopo katika majimbo hayo ili waweze kupata taaluma zinakazowasaidia kujiajiri wenyewe.

Ameeleza kuwa  endapo kila jimbo litakuwa na wataalamu mbali mbali waliosomeshwa na viongozi wa majimbo hatua hiyo itaongeza kasi ya maendeleo kwa kupata wataalamu wa fani mbali mbali watakaohudumu kwenye sekta za umma na binafsi katika majimbo hayo.

Sambamba na hayo aliwaagiza Wabunge na wawakilishi hao kuongeza kasi katika kutatua kero zinazowakabili wananchi  ili kwenda sambamba na matakwa ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. 

Dkt.Mabodi alisema viongozi hao wanatakiwa kuwa wa kwanza kuratibu changamoto zinazowakabili wananchi kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kama walivyowaahidi wananchi hao katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Pamoja na hayo amewapongeza wananchi wa shehia ya Kwale Kisiwani Pemba kwa uzalendo wao wa kushiriki katika shughuli za kijamii zikiwemo ujenzi wa Skuli ya Kwale ambayo kwa sasa wanasoma watoto wa shehia hiyo na vitongoji vyake.

Kupitia ziara hiyo Dkt. Mabodi amechangia shilingi milioni tatu kwa lengo la kusaidia ujenzi wa madarasa ya shule ya Kwale.

NAGMA GIGA: AWATAKA WATENDAJI WA JUMUIYA YA WAZAZI KUWA WAADILIFU


JUMUIYA ya Wazazi ya CCM Zanzibar imewataka watendaji wake wa ngazi mbali mbali za jumuiya hiyo kuwa waadilifu wakati wa kuchuja majina ya wagombea wanaowania nafasi mbali mbali za uongozi kupitia uchaguzi unaoendelea ndani ya chama na jumuiya zake.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Bi.Nagma Giga wakati akikabidhi vitendea kazi ambavyo ni komputa na priter kwa Mikoa na Wilaya nane za jumuiya hiyo huko katika Afisi Kuu ya Wazazi Mpirani Kikwajuni Unguja.

Alisema watendaji wa ngazi za mikoa na wilaya za jumuiya hiyo ndio wasimamizi wakuu wa uchaguzi huo kwa ngazi mbali mbali za jumuiya hivyo wakati wa kuchuja wagombea ni lazima waweke kando urafiki na undugu na wawapitishe viongozi wenye sifa na uzalendo wa kukisaidia chama kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.


“mafanikio tuliyonayo ndani ya jumuiya yrtu yanatokana na juhudi zenu za kiutendaji hivyo nakupongezeni sana na muendelee na kasi hiyo hiyo hadi tupate viongozi imara watakaotetea maslahi ya CCM mwaka 2020”,.alisema Giga.

Aidha aliwasisitiza viongozi hao kuhakikisha wanatunza vizuri vifaa walivyopewa na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kurahisisha shughuli za kiutendaji za jumuiya.

Akitoa neno la shukrani Katibu wa Wazazi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Bi.Zaituni Bushiri Ussi aliahidi kuwa vifaa hivyo vitakuwa ni chachu ya kuharakisha maendeleo ya taasisi katika harakati za kiutendaji.

Vifaa hivyo ambavyo ni komputa nane zimekamilisha idadi ya komputa 19 ambazo Naibu Katibu Mkuu huyo aliahidi kutoa kwa Wilaya na Mikoa yote ya Jumuiya hiyo Zanzibar.





Alhamisi, 29 Juni 2017

DKT.MABODI: AWATAKA WANANCHI SHEHIA YA NDAGONI PEMBA WASIHARIBU MIUNDOMBINU YA MAJI.



NAIBU  Katibu  Mkuu   wa  CCM Zanzibar  Dkt. Abdulla  Juma  Saadalla “ Mabodi”  amewasihi  wananchi  wa  shehia ya Ndagoni  Mkoa wa Kusini Pemba kulinda miundombinu ya maji safi na salama isiharibiwe na baadhi ya watu wenye tabia  ya kuhujumu  miundombimu hiyo kwa makusudi.

Nasaha hizo  amezitoa  wakati  akikagua  miundombinu ya maji iliyotengenezwa na Mamlaka ya Maji Pemba baada ya kuharibiwa na watu wasiojulikana  ambayo  kwa sasa  imerudiswa katika hali ya kawaida na wananchi  wameanza kupata  huduma hiyo.

Dkt. Mabodi  alisema nishati ya maji ni muhimu kwa maisha ya kila siku kwa wananchi wote hivyo ni lazima miundombinu yake ithaminiwe na kuwekewa ulinzi wa kudumu  kwani  ikikosekana  wanaoteseka ni wananchi waiokuwa na hatia hasa wagonjwa na wazee wasiojiweza .

Naibu Katibu Mkuu huyo aliwambia wananchi hao kuwa siasa za chuki na migogoro zimepitwa na wakati hivyo  wabadilike  na kuanza kuishi kwa misingi ya umoja  na ushirikiano kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya  kisiwa hicho.

Aidha alieleza kwamba dhamira ya CCM ni kufanya siasa zenye ushindani  wa kutatua kero za wananchi ili waweze kupata huduma bora za kijamii zitakazowanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha  Dkt. Mabodi   ametoa  pole kwa wananchi wa Kisiwa Cha Pemba waliopata mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa za masika na kusababisha uharibifu wa mali na vifo, kuwambia kuwa  CCM inashirikiana kushirikiana na serikali kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hao.

“Mwezi mmoja uliopita nilikuja hapa na kutoa agizo kwa ZAWA washughulikie tatizo hili na wananchi wapate maji safi na salama, nakupongezeni kwa kutekeleza agizo langu kwa wakati na pia naendelea kupita katika maeneo  mengine kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM umefikia katika hatua gani”., alisema Dkt. Mabodi.

Pamoja na  hayo  Dkt. Mabodi alisema mbali na changamoto hizo  Chama hicho kitaendea   kuishauri serikali itafute ufumbuzi wa kudumu wa kumaliza  changamoto za masuala ya kilimo zinazowakabili wananchi wa Jimbo la Ole na vitongoji vyake.

Akizungumza katika  ziara hiyo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Pemba,  Bw. Omar  Mshindo alisema  mamlaka hiyo haitomvulimia mtu yeyote anayefanya vitendo vya uharibifu wa miundo mbinu hiyo na  atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.

Mapema  Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Pemba , Bi. Salama  Mbarouk  Khatib alimpongeza  Naibu Katibu Mkuu huyo kwa juhudi  zake za kusimamia utekelezaji  wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 ili wananchi wa mijini wapate maendeleo.

Jumamosi, 24 Juni 2017

DKT. MABODI AWATAKA WASOMI KUBUNI MIKAKATI ITAKAYOPUNGUZA TATIZO LA AJIRA NCHINI.

  
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdulla  Juma Saadalla akizungumza na vikundi sita vya vijana wa CCM wa Vyuo vikuu na taasisi za  Elimu ya Juu  Zanzibar,  hapo  Afisi Kuu CCM Kisiwandui.


 Baadhi ya vijana wa CCM wa Vyuo vikuu na taasisi za  Elimu ya Juu  Zanzibar wakifuatilia kwa umakini nasaha zinazotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdulla Juma Saadalla.


Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dkt. Abdulla Juma Saadalla “ Mabodi”  amewataka wasomi na wataalamu wa CCM waliopo katika taasisi za elimu ya juu kutumia taaluma zao kubuni mikakati endelevu itakayosaidia kupunguza tatizo la ajira na kuimarisha uchumi wa nchi.

Rai hiyo ameitoa wakati akizungumza na vikundi  sita  vya vijana na wasomi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu wa Chama hicho nchini huko Afisi kuu CCM Kisiwandui Zanzibar,  Dkt. Mabodi amesema maendeleo ya taifa lolote duniani yanatokana  na fikra za maendeleo  zinazobuniwa na wasomi.

Amewambia wasomi hao wa kada mbali mbali za Vyuo Vikuu kuwa ni lazima wakae pamoja na kupanga mikakati itakayoisaidia CCM na serikali zake kupiga hatua za kimaendeleo katika nyanja mbali mbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Ameeleza kuwa Chama Cha Mapinduzi kupitia sera zake kinaendelea kutoa vipaumbele katika sekta za elimu hasa vyuo vikuu kuhakikisha vinazalisha  wasomi wenye uwezo wa  kitaaluma  utakaoisaidia  nchi kujitawala yenyewe  kwa kila sekta ili kuenzi kwa vitendo fikra za  waasisi wa Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964.

Aidha  Dkt. Mabodi amesema  vijana hao ambao ni wataalamu watumie  nyenzo za kitaaluma zikiwemo fursa ya ujasiriamali kwa kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri ajira kutoka katika katika chanzo kimoja cha nafasi za ajira kutoka serikalini.

  

Wanawake nchini watakiwa kuwa msatri wa mbele




Wanawake Nchini wametakiwa kuwa mstari wa mbele kuisaidia Serikali katika kupiga vita vitendo vya udhalilishaji na watotozinavyoonekana kushamiri Nchini.

Hayo ameyasema Naibu Katibu Mkuu wa UWT Mhe. Salama Abuod Talib katika kikao cha viongozi, watendaji na watumishi wote wa UWT Mkoa na Wilaya kikao kilichofanyika katika Afisi Kuu ya CCM Kiswandui.

 Amesema wanawake wamekuwa mstrai wa mbele kukipa msukumo Chama bila kuchoka na ndio chache ya ushindi ya Chama Cha Mapinduzi. Amewataka wanawake wote kuhamasisha wanawake wenzao kujiunga na UWT kwani ndio chachu na mkombozi Nchini. 

 Salama amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuwaamini wanawake na kuwapa nafasi za uongozi ndani ya Chama na Serikali yake.

Jumamosi, 17 Juni 2017

DKT. MABODI: ASEMA CCM ITAENDELEA KUENZI SIASA ZA USHINDANI WA KISERA.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar , Dkt. Abdulla Juma Saadalla “Mabodi” akisalimiana na Mbunge wa Viti Maalum  Wanawake (CCM)  (MNEC) Bi. Khadija Hassan Aboud pamoja  na  viongozi  mbali mbali wa UWT Mkoa wa Mjini  Zanzibar mara baada ya kuwasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkoa wa Mjini CCM uliopo Amani Unguja.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar , Dkt. Abdulla Juma Saadalla “Mabodi” akiwahutubia  mamia  ya wanachama na viongozi  wa UWT Mkoa wa Mjini  Unguja, mara baada ya kufungua mafunzo ya Wanawake na Uongozi katika siasa huko  Ukumbi wa Mikutano wa Mkoa wa Mjini CCM uliopo Amani Unguja. 

 Baadhi ya Viongozi na wanachama wa UWT walioudhuria katika mafunzo hayo wakifuatilia kwa umakini nasaha za mgeni rasmi  Dkt. Abdulla Juma Saadalla “Mabodi”  wakati  akizungumza mara baada ya kufungua  mafunzo hayo.

Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mjini, Bi. Waridi Juma Othman akizungumza  na viongozi na wanachama  hao kabla ya kumkaribisha mgeni  rasmi afungue  mafunzo hayo  Ukumbi wa Mikutan    o wa Mkoa wa Mjini CCM uliopo Amani Unguja. 

 Mbunge wa Viti Maalum  Wanawake (CCM)  (MNEC) Bi. Khadija Hassan Aboud akitoa maneno ya shukrani kwa mgeni rasmi  Dkt. Abdulla Juma Saadalla “ Mabodi”  kabla ya kuanza mafunzo hayo.

 Katibu wa NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi  Bi. Waride  Bakar  Jabu  akiwapungia na kuwasalimia  washiriki wa mafunzo hayo  ambao ni viongozi na wanachama wa UWT Mkoa wa Mjini Unguja.

 Mkufunzi  wa Mafunzo  hayo  Bi. Emiley Nelson Fwambo  akizungumza na washiriki wa mafunzo  ya Wanawake  na Uongozi  katika siasa.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar , Abdulla Juma Saadalla “ Mabodi” amesema  CCM itaendelea kufanya ushindani wa sera za maendeleo kisiasa  zitakazowanufaisha wananchi wa makundi yote mijini na vijijini.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua Mafunzo ya Wanawake na Uongozi kwa wanachama na viongozi wa UWT Mkoa wa Mjini huko Amani Zanzibar, Dkt. Mabodi amesema  wananchi wa visiwa vya Zanzibar kwa sasa wanachohitaji ni siasa za ushindani wa Sera za maendeleo na sio sera za vurugu na migogoro.

Dkt. Mabodi ameeleza kuwa  taifa lolote linalotamani kuendelea kiuchumi ni lazima wananchi wake wakubali kwa vitendo dhana ya siasa za ustaarabu katika kudumisha amani na utulivu wa nchi ili kufanya kazi za kujiongezea kipato katika hali ya  Amani na utulivu.

Aidha  Naibu Katibu Mkuu huyo amesema  ushindi wa CCM katika chaguzi mbali mbali za dola unatokana na nguvu za Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi  katika kuunga mkono harakati mbali mbali za kisiasa hadi kuhakikisha chama kinaingia madarakani.

“ kila mtu ndani ya Chama Chetu anajua na kutambua mchango wa Wanawake katika medali za kisiasa, wao ndio wamekuwa mstari wa mbele kwa kila kitu ikiwemo kujitokeza kwa wingi kupiga kura halali za kuiletea ushindi CCM.

Pia naahidi kuwa nitakuwa nanyi bega kwa bega kwa lengo la kuimarisha chama na jumuiza zake sambamba na kusimamia vyema serikali itekeleze Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 ili wananchi mpate maendeleo ya kudumu.”, amesema Dkt. Mabodi.

Kupitia Mkutano huo Dkt. Mabodi amewasihi  viongozi na watendaji wa  Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kushuka ngazi za chini kiutendaji hasa matawi na mashina kwa lengo la kuratibu changamoto zinazowakabili  wananchi ili zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu na serikali.

Amewapongeza  viongozi wa UWT waliojitolea kuanzisha mafunzo ya uongozi kwa wanawake wenzao ili wapate ujuzi wa kufanya siasa za maendeleo zitakazowajengea ujasiri wa kujenga hoja imara zinazokubalika katika ulimwengu wa siasa za ushindani.

Sambamba na hayo aliwapongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar  ambaye pia ni Rais wa  Zanzibar  na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi kwa kutekeleza ipasavyo ilani ya Chama hicho hasa katika juhudi za kulinda rasilimali za nchi zisihujumiwe na baadhi ya watu wanaotanguliza mbele maslahi binafsi.

Akizungumzia Uchaguzi wa ngazi ya Wadi unaoendelea hivi sasa katika Chama na Jumuiya  Ameziagiza  kamati zinazosimamia zoezi hilo zifanye kazi ya ziada ya kuhakikisha wanapatikana viongozi safi wasiokuwa na sifa za usaliti.

Mapema akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mjini, Bi. Waridi  Juma Othman aliahidi kuwa wanawake hao watatumia vizuri mafunzo ya uongozi katika siasa kama muongozo wa kufanya kazi za kisiasa kwa ufanisi mkubwa.

Akitoa neno la shukrani  Mbunge wa Viti Maalum wanawake( MNEC), Khadija Hassan Aboud alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanawake wa CCM ili waweze kuzitumika vizuri fursa za uongozi zinazopatikana ndani ya chama na serikali kwa ujumla.

Mafunzo hayo ya siku moja  yameandaliwa na Mbunge wa Viti Maalum wanawake( MNEC), Khadija Hassan Aboud kwa kushirikiana na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini, Faharia Shomari Shomari Khamis  kwa lengo la kuwajengea uwezo wanawake wa UWT ili wapate ukomavu wa kisiasa utakaosaidia CCM kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2020.


Jumatatu, 12 Juni 2017

NAIBU KATIBU MKUU WA UMOJA WA WAZAZI CCM Z'BAR BI.NAJMA GIGA ATEKELEZA AHADI ZAKE KWA WILAYA SITA.

  Katibu Msaidizi wa Idara ya Organazesheni Umoja wa Wazazi Tanzania  anayefanyia kazi zake Zanzibar, Nd. Simba Haji Mcha akisoma taarifa fupi ya kukabidhi Komputa kwa Wilaya Sita za Umoja huo.

 Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Zanzibar ,  Nd. Mustafa Rashid Kumwala akitoa nasaha kwa  Makatibu wa Wilaya Sita za Umoja huo kabla ya kuwakabidhi komputa hizo.
 Baadhi ya Komputa zilizotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Zanzibar, Bi. Najma Giga kwa Wilaya Sita za Umoja huo.

 Kushoto ni Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Zanzibar , Mustafa Rashid akimkabidhi  Kopmputa  Katibu wa Wazazi Wilaya ya Kati Unguja  Bi. Husna Rashid.

Katibu wa Wazazi Wilaya ya Wete Pemba akikabidhiwa Komputa kwa niaba ya Katibu wa  Wazazi Wilaya  ya Chake Chake  na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Zanzibar , Mustafa Rashid.

 Kushoto ni Katibu wa Wazazi Wilaya ya Wete Pemba akikabidhiwa Komouta na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Zanzibar , Mustafa Rashid.
   Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Zanzibar , Mustafa Rashid akikabidhi  Kopmputa kwa  Katibu wa Wazazi Wilaya ya Amani, Bi. Mwanaisha Ame.
 Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Zanzibar , Mustafa Rashid akikabidhi  Kopmputa kwa  Katibu wa Wazazi Wilaya ya  Mfenesini,  Bi.  Mosi  Omar.
   Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Zanzibar , Mustafa Rashid akikabidhi  Kopmputa kwa  Katibu wa Wazazi Wilaya ya  Kaskazini “B” Unguja ,  Bi.  Salma Shaibu .


Baadhi ya Maafisa wa Afisi Kuu ya Wazazi Zanzibar  wakishuhudia zoezi hilo.
 Viongozi na Watendaji mbali mbali wa Wilaya, Mikoa  pamoja na Maafisa  wa Afisi Kuu ya Umoja wa Wazazi Zanzibar  wakiwa katika  picha ya pamoja mara baada ya hafla fupi ya kukabidhiwa  Komputa. (PICHA  NA AFISI KUU CCM ZANZIBAR) .

VIONGOZI  wa  Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Jumuiya  zake   wameshauriwa kutekeleza kwa wakati ahadi wanazotoa ndani ya chama na jumuiya zake ili kurahisha masuala ya kiutendaji katika taasisi hizo.

Ushauri huo umetolewa kwa nyakati tofauti na baadhi ya Makatibu wa Wilaya Sita za Umoja huo Zanzibar mara baada ya kukabidhiwa Komputa zilizotolelewa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi CCM Zanzibar, Bi. Najma Giga ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa ahadi alizowahi kutoa katika ziara zake alizofanya katika wilaya mbali mbali za Umoja huo Zanzibar.

Mmoja kati ya Makatibu hao ambaye ni  Katibu wa  Wazazi  Wilaya ya  Amani, Bi.Mwanaisha  Ame Mohamed amesema upatikanaji wa vifaa hivyo utaongeza ufanisi wa kiutendaji ndani ya umoja huo.

Aidha  Katibu huyo amewashauri  viongozi wa Chama Cha Chama na Jumuiya  zingine hasa  Wabunge, Wawakilishi na Madiwani  kufuata nyayo za kiongozi huyo   katika juhudi za kuharakisha maendeleo ya CCM kisiasa na kiuchumi.

Naye  Katibu wa Wazazi Wilaya ya  Wete Pemba, Bi. Mariam Ali Said  amemshukru Naibu Katibu Mkuu wa Wazazi Zanzibar kwa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo na kuongeza kuwa vifaa hivyo vitamaliza changamoto za uchapaji wa nyaraka za kiofisi masafa ya mbali.

Akizungumza Kaimu  Naibu Katibu Mkuu  Wazazi Zanzibar, Nd. Mustafa Rashid Kumwalu  kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo Bi. Najma Gina mara  baada ya kukabidhi  Komputa  hizo ametoa wito kwa watendaji wa umoja huo kutumia komputa hizo kwa matumizi yaliyokusudiwa  ili shughuli za kiutendaji ndani ya umoja huo zifanyike kwa wakati na kwa ufanisi.

Nd. Rashid  alieleza kuwa  lengo la umoja huo ni kuhakikisha watendaji wake wanapata vitendea kazi vya kisasa vitakavyosaidia  kutekeleza kwa wakati shughuli za kiutendaji  kwa lengo la kwenda sambamba na matakwa  ya Katiba ya CCM iliyofanyiwa mabadiliko miezi kadhaa iliyopita.

Aidha amefafanua kwamba Komputa zilizokabidhiwa leo ni 6 ambapo awali alikabidhi tatu hivyo zimekuwa ni tisa na bado kumi kwa mujibu wa idadi ya komputa zilizoahidiwa na Naibu katibu Mkuu wa Umoja huo.

Komputa hizo zina thamani zaidi ya shilingi milioni Saba zimekabidhiwa kwa  Wilaya  6  za  Umoja  wa  Wazazi  CCM Wilaya ya Amani, Wilaya ya Mfenesini, Wilaya ya Kati, Wilaya ya Kaskazini “B”, Wilaya ya Wete na Wilaya ya Chake Chake Pemba.

Jumapili, 11 Juni 2017

UWT ZANZIBAR YAPIGA MSASA VIONGOZI WAPYA WA MATAWI YA MAJIMBO YA MKWAJUNI NA CHAANI UNGUJA


 Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar, Bi.Salama Aboud Talib akiwahutubia viongozi wapya wa Matawi ya Majimbo ya Chaani na Mkwajuni Kaskazini “A” kichama Unguja.
 Katibu wa Idara ya Organazesheni wa UWT Zanzibar, Tunu Juma Kondo akizungumza na viongozi hao kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar, Bi.Salama Aboud Talib huko  Gamba Ofisi ya Wilaya Kaskazini “A” Gamba Unguja.
Mmoja wa Viongozi wa Tawi la Chaani Mcheza Shauri Jimbo la Chaani Bi. Fatma akitoa akizungumza katika Mkutano huo. 
Naibu Katibu Mkuu huyo Bi. Salama Aboud akitoa sadaka ya fedha kwa Akina Mama wa UWT kwa ajili ya futari  ya Mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja 
 Bi. Mtumwa Suleiman akimuunga  mkono  Naibu Katibu Mkuu wa UWT Z'bar Bi. Salama kwa kuongeza sadaka ya fedha kwa Akina Mama wa UWT kwa ajili ya futari  ya Mwezi mtukufu wa ramadhani.
Baadhi ya viongozi mbali mbali UWT wa ngazi za matawi wa Majimbo ya Chaani na Mkwajuni  Wilaya ya Kaskazini “A” wakifuatilia kwa makini nasaha zinazotolewa na viongozi wakuu wa UWT katika Mkutano huo.



      UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT), umewataka viongozi waliochaguliwa kwa ngazi za matawi ya umoja huo na chama kwa ujumla kuongeza idadi ya wanachama hai watakaoiwezesha CCM kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.  

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa UWT  Zanzibar, Bi. Salama Aboud Talib katika ziara ya kuwapongeza na kuwahamasisha  viongozi wapya wa ngazi za matawi waliochaguliwa hivi karibuni katika Majimbo ya Chaani na Mkwajuni Wilaya ya Kaskazini “A” kichama Unguja.

Amewataka  viongozi hao kujua idadi kamili ya wanachama na kubaini ni wanachama wangapi wamefariki ili watolewe katika orodha ya wanachama hai kwa lengo la kupata idadi ya uhakika ya  wanachama watakaoendelea kuibeba CCM katika  michakato mbali mbali ya kisiasa.

Amesema   viongozi waliochaguliwa wameaminiwa hivyo wanatakiwa kuwatumikia na kuwaongoza vizuri  wanachama waliowachagua kwa kutetea maslahi ya CCM kwa vitendo.

Aidha  Bi. Salama Aliwataka wanawake hao kuwa na masimamo imara wa kuendelea kuwachagua viongozi wenye sifa na uwezo wa kuzitumikia chama na jumuiya kwa uadilifu badala ya kuwatumikia watu wachache wenye nguvu za kisiasa na uwezo wa kifedha.

Hata hivyo kupitia ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu huyo amesisitiza kudumishwa dhana ya umoja ndani ya jumuiya hiyo ili wasimamie ipasavyo matakwa ya Katiba ya CCM na Jumuiya waweze kufanikisha majukumu mbali mbali ya kuendelezwa kwa dhana ya umoja na mshikamano ndani ya jumuiya hiyo .

Mapema Katibu wa Idara ya Organazesheni wa UWT Zanzibar,  Bi. Tunu Juma Kondo, akimkaribisha  Naibu Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa matarajio ya CCM na UWT kutoka kwa viongozi wapya wa umoja huo wa ngazi za matawi ni kuona mabadiliko ya haraka ya kiutendaji yatakayoongeza ufanisi ndani ya taasisi hiyo.

Naye Bi.Fatma Khamis mussa kutoka Tawi la Chaani, amewasihi viongozi wa ngazi za juu wa umoja huo pamoja na chama kufanya ziara za mara kwa mara katika ngazi za Matawi ili kuongeza hamasa ushirikiano kwa wanachama na viongozi wa ngazi hizo.

Pamoja na hayo katika  mkutano huo Naibu Katibu Mkuu huyo Bi. Salama Aboud kwa kushirikiana na Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja  Bi. Mtumwa Suleiman wametoa sadaka ya fedha kwa akina Mama wa UWT kwa ajili ya futari  ya Mwezi mtukufu wa ramadhani.


Alhamisi, 8 Juni 2017

DR.MABODI NA BALOZI SEIF ALI IDD WASHIRIKI MAZISHI YA KADA MKONGWE WA CCM PEMBA.











Mwanasiasa Mkongwe wa Zanzibar Mzee Khamis Mkadara  aliyefariki Dunia mapemba jana asubuhi amezikwa Kijijini kwake Wawi Mkoa wa Kusini Pemba maziko yaliyohudhuriwa na Mamia ya Waumini wa Dini ya Kiislamu, Wananchi  pamoja na Viongozi wa Kiserikali na Kisiasa.   

Mzee Khamis Mkadara alikuwa akisumbuliwa na Maradhi ya kawaida pamoja na uzee alifariki nyumbani kwake Mtaa wa  Wawi Wilaya ya Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika mazishi hayo aliiwakilisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Chama cha Mapinduzi akijumuika  na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Juma Abdulla Mabodi na baadhi ya watendaji wa Serikali.

Marehemu Mzee Khamis Juma Mkadara alizaliwa Mwaka 1927 na kuanza elimu ya Quran katika Madrasa mbali mbali za Wilaya ya Chake chake ambapo baadaye katika ujana wake akajishughulisha na masuala ya Kisiasa katika dhana nzima ya kudai Uhuru wa Visiwa vya Zanzibar.

Katika kipindi hicho ya kutaka kujikomboa Mzee Mkadara alikuwa muanzilishi wa Chama cha Shirazy Association na baadaye kukiunganisha na chama cha African Association na Kuzaliwa kwa Chama cha Afro Shirazy Party.

Katika utumishi wa Chama Mzee Khamis Juma Mkadara aliwahi kuwa Mwenyekiti wa ASP wa Wilaya ya Chake chake mwaka 1973 na baada  ya kuzaliwa Chama cha Mapinduzi mwaka 1977 aliendelea na wadhifa huo hadi mwaka 1997.

Mbali ya wadhifa huo wa Kichama Mzee Mkadara pia aliwahi kuwa Diwani wa Wadi ya Wawi mwaka 1995.

Mwanasiasa huyo mkongwe Kisiwani Pemba alikuwa mstawi wa mbele katika utetezi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar akiwa miongoni mwa Wazee waliotumikia kwa kiindi kirefu Taifa hili la Tanzania.

Utumishi huo uliweza kumpatia fifa na ushujaa uliopelekea kutunukiwa nishani na Rais Mstaafu wa Tanzania Awamu ya Nne Dr. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar wa Awamu ya Sita Dr. Aman Abeid Karume.

Mzee Khamis Juma Mkadara  aliyefikisha umri wa Miaka 90 ameacha Kizuka Mmoja, Watoto Wanane na Wajukuu 33.

Mwenyezi Muungu ailaze roho ya Mwanasiasa huyo Mkongwe Mzee Khamis Juma  Mkadara mahali pema peponi-Amin.