Alhamisi, 29 Juni 2017

DKT.MABODI: AWATAKA WANANCHI SHEHIA YA NDAGONI PEMBA WASIHARIBU MIUNDOMBINU YA MAJI.



NAIBU  Katibu  Mkuu   wa  CCM Zanzibar  Dkt. Abdulla  Juma  Saadalla “ Mabodi”  amewasihi  wananchi  wa  shehia ya Ndagoni  Mkoa wa Kusini Pemba kulinda miundombinu ya maji safi na salama isiharibiwe na baadhi ya watu wenye tabia  ya kuhujumu  miundombimu hiyo kwa makusudi.

Nasaha hizo  amezitoa  wakati  akikagua  miundombinu ya maji iliyotengenezwa na Mamlaka ya Maji Pemba baada ya kuharibiwa na watu wasiojulikana  ambayo  kwa sasa  imerudiswa katika hali ya kawaida na wananchi  wameanza kupata  huduma hiyo.

Dkt. Mabodi  alisema nishati ya maji ni muhimu kwa maisha ya kila siku kwa wananchi wote hivyo ni lazima miundombinu yake ithaminiwe na kuwekewa ulinzi wa kudumu  kwani  ikikosekana  wanaoteseka ni wananchi waiokuwa na hatia hasa wagonjwa na wazee wasiojiweza .

Naibu Katibu Mkuu huyo aliwambia wananchi hao kuwa siasa za chuki na migogoro zimepitwa na wakati hivyo  wabadilike  na kuanza kuishi kwa misingi ya umoja  na ushirikiano kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya  kisiwa hicho.

Aidha alieleza kwamba dhamira ya CCM ni kufanya siasa zenye ushindani  wa kutatua kero za wananchi ili waweze kupata huduma bora za kijamii zitakazowanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha  Dkt. Mabodi   ametoa  pole kwa wananchi wa Kisiwa Cha Pemba waliopata mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa za masika na kusababisha uharibifu wa mali na vifo, kuwambia kuwa  CCM inashirikiana kushirikiana na serikali kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hao.

“Mwezi mmoja uliopita nilikuja hapa na kutoa agizo kwa ZAWA washughulikie tatizo hili na wananchi wapate maji safi na salama, nakupongezeni kwa kutekeleza agizo langu kwa wakati na pia naendelea kupita katika maeneo  mengine kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM umefikia katika hatua gani”., alisema Dkt. Mabodi.

Pamoja na  hayo  Dkt. Mabodi alisema mbali na changamoto hizo  Chama hicho kitaendea   kuishauri serikali itafute ufumbuzi wa kudumu wa kumaliza  changamoto za masuala ya kilimo zinazowakabili wananchi wa Jimbo la Ole na vitongoji vyake.

Akizungumza katika  ziara hiyo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Pemba,  Bw. Omar  Mshindo alisema  mamlaka hiyo haitomvulimia mtu yeyote anayefanya vitendo vya uharibifu wa miundo mbinu hiyo na  atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.

Mapema  Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Pemba , Bi. Salama  Mbarouk  Khatib alimpongeza  Naibu Katibu Mkuu huyo kwa juhudi  zake za kusimamia utekelezaji  wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 ili wananchi wa mijini wapate maendeleo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni