Jumapili, 28 Oktoba 2018

MWAKILISHI MTEULE JIMBO LA JANG'OMBE AKABIDHIWA CHETI CHA USHINDI.


  AFISA wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Wilaya ya Mjini Mwanapili Khamis Mohamed (kulia) akimkabidhi  Cheti cha udhibitisho wa ushindi wa nafasi ya Uwakilishi   Mwakilishi mteule wa Jimbo la Jang’ombe Ramadhan Hamza Chande (kushoto) , aliyekuwa Wakala wa Mgombea wa CCM katika Uchaguzi huo Rajab Uweje Yakoub (wa pili kushoto).

 ALIYEKUWA Wakala wa Mgombea Uwakilishi wa CCM Ndugu Rajab Uweje Yakoub (wa pili kushoto) katika Uchaguzi huo akisaini Cheti cha udhibitisho wa ushindi wa Uwakilishi cha Mwakilishi mteule wa CCM Jimbo la Jang’ombe.


AFISA wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Wilaya ya Mjini  Mwanapili Khamis Mohamed (kulia) akisaini Cheti cha udhibitisho wa ushindi wa Uwakilishi cha Mwakilishi mteule wa CCM Jimbo la Jang’ombe. 
MWAKILISHI mteule wa Jimbo la Jang’ombe Ramadhan Hamza Chande akionyesha Cheti cha udhibitisho wa ushindi wa Uwakilishi kupitia Uchaguzi Mdogo wa Jimbo hilo uliofanyika Jana.

  Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ndugu Salum Kassim Ali (kulia) akisalimiana na Mwakilishi mteule wa Jimbo la Jang’ombe Ramadhan Hamza Chande(kushoto) mara baada ya hafla ya kukabidhiwa Cheti cha udhibitisho wa ushindi.
 NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.


MWAKILISHI mteule wa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Jang'ombe Ndugu Ramadhan Hamza Chande leo amekabidhiwa rasmi Cheti cha udhibitisho wa ushindi wa nafasi ya Uwakilishi wa Jimbo hilo.


Hafla hiyo imefanyika katika Ofisi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Wilaya ya Mjini iliyopo Maisara na kuudhuriwa na Viongozi na Wanatendaji wandamizi Tume hiyo na  CCM.


Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Cheti hicho Mwakilishi mteule huyo Ramadhan Hamza ameahidi kufanya kazi kwa uadilifu na kwa kufuata miongozo na taratibu zote za kisheria kwa maslahi ya wananchi wote wa Jimbo hilo.  


Amewashukuru wananchi na wanachama wa CCM wa Jimbo hilo kwa kumpatia ridhaa ya kuongoza Jimbo hilo kupitia  utaratibu halali wa kidemokrasia.


"Nitawatumikia kwa uadilifu wananchi wote wa Jang’ombe bila ya ubaguzi wowote kwani naamini bila nyinyi kuridhia na kunichagua kwa kura nyingi nisingeweza kushinda katika mchakato huu wa kisiasa uliokuwa na ushindani mkubwa.


Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020 tayari nishakabidhiwa muda wowote nitaanza kutekeleza mpango kazi wangu kwa lengo la kutekeleza ahadi nilizoahidi katika kampeni.”,ameeleza Chande.


Kwa upande wake aliyekuwa Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa Jang'ombe ambaye pia ni Afisa wa ZEC Wilaya ya Mjini Bi.Mwanapili Khamis Mohamed amemsisitiza kiongozi huyo kufanya kazi zake kwa majibu wa taratibu na kanuni za kisheria ili kutimiza matakwa ya wananchi waliomchagua.


Mwakilishi huyo aliyeshinda nafasi hiyo jana kwa kura 6,581  sawa na asilimia 90.5 katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Jang'ombe uliofanyika kwa amani bila ya kujitokeza matukio ya uvunjifu wa sheria za Uchaguzi na nchi kwa ujumla.


Jumamosi, 27 Oktoba 2018

RAMADHAN CHANDE - AIBUKA MSHINDI UCHAGUZI WA JANG'OMBE KWA ASILIMIA 90.5

MSHINDI wa Uwakilishi tiketi ya CCM Uchaguzi Mdogo wa Jang'ombe Ndugu Ramadhan Hamza Chande. 


MGOMBEA Uwakilishi katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Jang'ombe Zanzibar  kupitia Chama cha Mapinduzi Ndg Ramadhan Hamza Chande  ameibuka mshinda katika uchaguzi huo kwa ushindi wa Kura 6,581 sawa na asilimia 90.5 ya kura zote halali zilizopigwa ambazo ni 7,274.

Akitangaza matokeo hayo  Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi Jimbo hilo ambaye pia ni Afisa wa Tume ya Uchaguzi Wilaya ya Mjini Unguja, Mwanapili Khamis Mohamed amesema kufuatia matokeo hayo Ramadhan Hamza ameshinda Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Jang'ombe.

Afisa huyo amemtangaza mshindi wa pili kuwa ni Mgombea wa Chama Cha CUF ndugu Mtumwa Ambari Abdalla aliyepata kura 172 sawa na asilimia 2.4.

Aidha ametaja kura za vyama vingine vilivyoshiriki katika mchakato huo wa Uchaguzi ambazo ni ADA-TADEA 131, AFP 58, CCK 72, DP 73, TLP 71, SAU 53 pamoja na NRA 62.
Akizungumza mara baada ya matokeo hayo Mwakilishi wa Mgombea wa chama cha ADA-TADEA Halma Abdalla amesema Uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki hivyo mgombea wa CCM ameshinda kihalali.

Naye Mshindi wa Kiti cha Uwakilishi tiketi ya CCM Jimbo la Jang'ombe ndugu Ramadhan Hamza Chande amewashukuru wananchi wote waliojitokeza kupiga kura hasa wale waliomwamini na kumpa ridhaa ya kuwa Mwakilishi wa kuliongoza Jimbo hilo.

Ameahidi kutekeleza vipaumbele vyake alivyoahidi kupitia katika mikutano mbali mbali ya kampeni za Uchaguzi kwa mujibu wa maelekezo yaliyomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Uchaguzi huo uliofanyika leo Octoba 27, mwaka 2018 umefanyika kutokana na aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo ndugu Abdalla Diwani kuvuliwa uanachama kwa makosa ya ukiukaji wa maadili ndani ya taasisi hiyo.MWANAPILI-ASEMA ZOEZI LA KUPIGA KURA LINAENDELEA VIZURI JANG'OMBE.

 MGOMBEA wa nafasi ya Uwakilishi tiketi ya CCM Jimbo la Jang'ombe Ramadhan Hamza Chande akipiga kura katika Kituo cha Kupigia kura kilichopo Shule ya Jang'ombe Jimbo la Jang'ombe Wilaya ya Mjini Zanzibar.


 BAADHI ya Wananchi wakiangalia majina yao kwa ajili ya kupiga kura katika Kituo cha kupiga kura kilichopo Kidongochekundu zanzibar katika zoezi la uchaguzi jimbo la Jang'ombe linaloendelea katika maeneo mbali mbali ya Jimbo hilo.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

ZOEZI la Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang’ombe wa kumchagua Mwakilishi wa Jimbo hilo unaendelea vizuri bila ya kuwepo na matukio ya vurugu na uvunjifu wa amani katika vituo vya kupigia kura.

 Akizungumza Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi Jimbo hilo ambaye pia ni Afisa wa Tume ya Uchaguzi Wilaya ya Mjini Unguja, Mwanapili Khamis Mohamed, amedhibitisha kuwa zoezi hilo linaendelea vizuri.  

Amesema wananchi wamejitokeza toka saa 1:30 asubuhi walikuwa tayari washafika katika vituo vya kupiga kura na vituo vilipofunguliwa wamepiga kura kwa utulivu na bado wanaendelea kujitokeza.

Afisa huyo wa Tume ya Uchaguzi Wilaya ya Mjini, amewasihi wananchi wenye sifa za kupiga kura kisheria kuendelea kujitokeza kwa wingi kwa lengo la kutekeleza haki yao ya Kidemokrasia.

Aidha amesema mpaka hivi sasa bado hapajatokea changamoto yoyote kwani Tume hiyo imejipanga vizuri hasa katika suala zima la kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa  vifaa pamoja na huduma za msingi za maafisa na wadau mbali mbali walioshiriki katika kufanikisha zoezi hilo.

Akizungumza wakati wa kutembelea Vituo  vya kupigia kura  Mgombea Uwakilishi wa Tiketi ya CCM wa Jimbo la Jang’ombe Ndugu Ramadhan Hamza Chande, ameelezea kuridhishwa kwake na hali ya utulivu katika Vituo vya kupigia kura.

Amewasisitiza wananchi wa Jimbo hilo bila ya kujali tofauti zao za kisiasa wajitokeze  kwa wingi kuchagua mgombea watakayeona ana sifa na vigezo vya kuwaletea maendeleo.

Kwa upande wake mgombea wa nafasi ya Uwakilishi wa Chama cha ADA-TADEA, Sabry Ramadhan Mzee ‘China’ , amewataka wananchi wa Jimbo la Jang’ombe kuendeleza utamaduni wa ustaarabu na utulivu wakati wote wa zoezi hilo la Uchaguzi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi RC-Ayoub Mohamed Mahmoud, amesema Vyombo vya Ulinzi vimejipanga vizuri kukabiliana na changamoto yoyote inayohusu masuala ya ulinzi na usalama ndani ya Jimbo hilo.

Amewasihi wananchi wakimaliza kupiga kura warudi majumbani kwa lengo la kuendendelea na shughuli zao za kujitafutia kipato huku wakisikiliza vyombo vya habari kwa ajili ya kupata matokeo ya Uchaguzi huo.

Uchaguzi huo unaofanyika leo Octoba 27, mwaka 2018 unafanyika kwa lengo la kumpata Mgombea Uwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe kufuatilia aliyekuwa kiongozi wa nafasi hiyo kuvuliwa uanachama na CCM kutokana na kukiuka maadili ya taasisi hiyo.

Jumatatu, 22 Oktoba 2018

MATUKIO KATIKA PICHA MKUTANO WA SITA WA KAMPENI ZA CCM UCHAGUZI WA JANG'OMBE MGENI RASMI MHE.SAMIA SULUHU HASSAN.

 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Baja kwa ajili ya kumnadi mgombea wa CCM wa Jimbo la Jang'ombe Ndugu Ramadhan Hamza Chande.

 BAADHI ya Viongozi na wanachama wa CCM wakiimba wimbo maalum wa Mashujaa katika Mkutano wa Sita wa kampeni za CCM Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Jang'ombe.

 BAADHI wa wanachama wa CCM wakiimba wimbo maalum wa mashujaa katika mkutano wa kampeni za CCM Jimbo la Jang'ombe uliofanyika katika Uwanja wa Baja Ziwani Zanzibar.

 WAKUU wa Idara za  CCM Zanzibar ambao pia ni Wajumbe wa Kamati Maalum ya NEC Taifa Zanzibar wakifuatilia matukio mbali mbali katika Mkutano wa Kampeni za CCM  Jimbo la Jang'ombe uliofanyika katika Uwanja wa Baja.


VIONGOZI mbali mbali wa CCM wakiwa katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi wa Jimbo la Jang'ombe.

 KIKUNDI cha muziki wa Taarab cha Big Star kikitoa burudani katika mkutano huo ambao mgeni rasmi alikuwa ni Mhe. Samia Suluhu Hassan.

 WANA-CCM wakimpungia mikono Mgombea wa CCM Ramadhan Hamza Chande kuashiria kuwa watampigia kura za ndio katika Uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Octoba 27, mwaka 2018.

 VIONGOZI wa CCM wakimtuza fedha msoma utenzi  Ndugu Kassim katika mkutano huo wa Kampemi uliofanyika katika Uwanja wa Baja.

 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi na Wana-CCM katika mkutano wa kampeni za CCM Jimbo la Jang'ombe.

 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Samia Suluhu Hassan(kulia) akimkabidi  Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 pamoja na Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2017 Mgombea wa Uwakilishi Jimbo la Jang'ombe Ndugu Ramadhan Hamza Chande (kushoto)  ambazo ni nyenzo za kufanyia kazi katika Jimbo la Jang'ombe. 

 Mgombea wa Uwakilishi Jimbo la Jang'ombe Ndugu Ramadhan Hamza Chande kionyesha Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na Katiba mara baada ya kukabidhiwa na mgeni rasmi.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akizungumza na kumuombea kura mgombea wa CCM Ramadhan Hamza Chande.

 MWENYEKITI wa Mkoa wa Mjini Talib Ali Talib akimuombea kura za ndio mgombea wa CCM.

 KATIBU wa CCM Mkoa wa Mjini Ndugu  Mohamed Nyawenga akizungumza na kuwatambulisha wageni mbali mbali katika mkutano huo wa Kampeni.

 MJUMBE wa Kamati Maalum ya NEC Taifa Zanzibar  Mhandisi  Nassir Ally Juma akimuombea kura Mgombea wa CCM Jimbo la Jang'ombe.

 MJUMBE wa Baraza la Wawakilishi  ambaye pia ni Naibu Waziri  wa Nchi  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar  Mihayo Juma Nhunga akimuombea kura mgombea wa CCM  Jimbo la Jang'ombe Ramadhan Chande.

 MGOMBEA mwenza wa Ramadhan Chande katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM Lilian Limo akimuombea kura za ndio mgombea Uwakilishi Jimbo la Jang'ombe Zanzibar.

 MBUNGE Mteule wa Jimbo la Liwale Mkoani Lindi Ndugu Zubeir Mohamed aliyehama katika Chama cha CUF hivi karibuni na kujiunga na CCM akimuombea kura za ndio mgombea uwakilishi wa Jimbo la Jang'ombe.

 MBUNGE wa Jimbo la Jang'ombe Ali  Hassan Omar 'King' akimuombea kura za ndio mgombea  uwakilishi wa Jimbo hilo Ramadhan Hamza Chande, (Picha na Is-haka Omar-AKZ).

Jumapili, 21 Oktoba 2018

MWL.RAYMOND AITIKISA JANG'OMBE , AWASIHI VIJANA KUMPIGIA KURA ZA NDIO RAMADHAN CHANDE.


 KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi  Mwl. Raymond Mwangwala akiwahutubia wananchi na kumwombea kura za ndio Mgombea wa CCM Ramadhan Chande  kupitia Mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang'ombe Zanzibar, uliofanyika katika Uwanja wa Tawi la CCM Kidogo chekundu.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi  Mwl. Raymond Mwangwala amewasihi wananchi wa jimbo la Jang’ombe hasa vijana kumchagua kwa kura za ndio mgombea wa tiketi ya CCM Ramadhan Hamza Chande.

Wito huo ameutoa leo alipokuwa akimnadi  na mgombea wa CCM Jimbo la Jang’ombe huko katika Mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika katika Tawi la Kidongo Chekundu Unguja.

Amemtaja mgombea huyo wa CCM kuwa ni mgombea pekee mwenye sifa na vigezo vya kuleta mabadiliko chanya ya maendeleo katika Jimbo hilo.
Mwl. Raymond amesema viongozi mbali mbali wa CCM katika Jimbo la Jang’ombe wametekelea kwa ufanisi miradi ya maendeleo na kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto sugu za jimbo.

Pia ameongeza kuwa  Serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na  Rais wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein ametekeleza kwa ufanisi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2016  hatua ambazo zinastahiki kuungwa mkono na wananchi wote hasa wa Jimbo hilo.

Katibu Mkuu huyo wa UVCCM Raymond, amebainisha kwamba mafanikio hayo yatakuwa endelevu endapo wanachama na wananchi wa Jang’ombe watamchagua mgombea anayetokana na Chama Cha Mapinduzi chenye sera imara na historia ya kuwatumikia wananchi wa rika zote hasa vijana.

Katika maelezo yake Katibu Mkuu huyo alisema kupitia Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 2018/2019  zimetengwa jumla ya shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kusaidia kundi la Vijana hatua ambayo inatakiwa kuthaminiwa na kundi hilo.

Amesema mbali na fedha hizo pia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayotokana na CCM inajenga viwanja vya kisasa vya michezo kwa kila Wilaya Zanzibar kwa lengo la kuwawezesha vijana wajiajiri kupitia sekta ya michezo mbali mbali.

Aidha amesisitiza kuwa CCM ina matarajio makubwa ya kushinda kwa asilimia kubwa katika uchaguzi huo kutokana na Wananchi hasa kuiamini na kuiunga mkono tasisi hiyo kwani ushahidi wa tathimini hizo umeonekana wazi katika Chaguzi  za Majimbo mbali mbali ya Tanzania bara ambayo chama hicho kimeshinda kwa kishindo.

“Mgombea wetu anauzika ana mvuto na pia ana sifa ya utendaji na uchapakazi uliotuka hivyo nakuombeni wananchi wa Jimbo la Jang’ombe hasa Vijana Wenzangu Octoba 27, mwaka huu tumchague ndugu Ramadhan Hamza kwa kura nyingi  za ndio”, alisema Mwl. Raymond.

Ameongeza kuwa Vyama vya upiunzani kwa sasa havina sera na vimepoteza dira ya kisiasa kwa kutawaliwa na migogoro na visasi vya wenyewe kwa wenyewe hali inayovikosesha sifa ya kuongoza nafasi yoyote katika jamii.

Akizungumza Mgombea wa Uwakilishi tiketi ya CCM  Ramadhan Hamza Chande, amewaomba  kura za ndio wanachama na wananchi wote wa Jimbo hilo.

Amesema  kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi atakuwa mstari wa mbele kushirikiana na makundi yote hasa vijana  kutekeleza mikakati ya maendeleo.

Akizungumza Mjumbe wa Kamati Maalum ya NEC Taifa Zanzibar kupitia kundi la Vijana Ndugu Abdulghafari Idissa amesema CCM ndio Chama chenye dhamira ya kweli ya kuwaletea wananchi wote maendeleo.

Naye Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Salha Mohamed Mwinjuma amewaomba Vijana na wanawake siku ya kupiga kura wajitokeze kwa wingi kumchagua mgombea wa CCM kwani ana uwezo mkubwa wa kubuni mbinu mbadala za kuwaletea maendeleo.

Uchaguzi huo unafanyika kutokana na aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe Ndugu  Abdallah Diwani kuvuliwa uanachama baada ya kukiuka maadili ya Chama Cha Mapinduzi.

MATUKIO KATIKA PICHA KAMPENI ZA CCM JIMBO LA JANG'OMBE MGENI RASMI KATIBU MKUU WA UVCCM MWL.RAYMOND.


 MGOMBEA wa  tiketi ya CCM  uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang'ombe Ramadhan Hamza Chande akiwasalimia wanachama wa CCM mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Mkutano wa kampeni uliofanyika Tawi la CCM Kidogo Chekundu.

 MGOMBEA wa CCM Ramadhan Chande pamoja na Katibu Mkuu wa UVCCM Mwl. Raymond wakicheza mziki wa kizazi kipya katika mkutano wa kampeni.

 MSOMA Utenzi katika Mkutano huo

 KATIBU Mkuu wa UVCCM Mwl. Raymond  Mwangwala akihutubia na kumnadi mgombea katika Mkutano uliofanyika Tawi la Kidongo chekundu.

 MGOMBEA wa CCM katika Uchaguzi wa Jang'ombe Ramadhan Hamza Chande akiomba kura za ndio kwa wananchi wa Jang'ombe Shehia ya Kidongo chekundu.

 MWENYEKITI wa UVCCM Mkoa wa Mjini Kamaria Suleiman Nassor akiwatambulisha viongozi mbali mbali na kumuombea kura mgombea wa CCM.

 MWENYEKITI wa UVCCM Jimbo la  Jang'ombe akifungua Mkutano huo wa Kampeni.

 ALIYEKUWA Mgombea mwenza katika mchakato wa kura za maoni CCM ndugu  Othman  Shaaban Kibwana akimuombea kura Mgombea wa Uwakilishi Jimbo la Jang'ombe.

 WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi nafasi za Vijana wakimuombea kura mgombea wa CCM katika mkutano huo.

 MADIWANI wa Wadi za Jang'ombe wakimuombea kura Mwakilishi wa Jang'ombe.

 WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar nafasi za Vijana wakimuombea kura za ndio mgombea uwakilishi Jang'ombe.

   Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais – Mhe. Mihayo Juma Nhunga akimuombea kura mgombea uwakilishi wa CCM Jimbo la Jang'ombe.

 BAADHI ya Wana-CCM wakimpungia mkono mgombea uwakilishi jimbo la Jang'ombe (hayupo pichani).

 WABUNGE  wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia nafasi za UVCCM wakimuombea kura za ndio mgomea uwakilishi wa CCM, (PICHA NA IS-HAKA OMAR-AKZ).


MTATIRO - ASEMA SERA NZURI ZA CCM NDIO CHIMBUKO LA MAENDELEO YA TANZANIA

 KADA wa CCM Julius Mtatiro akizungumza na Vyombo vya Habari vya Zanzibar kwa mara ya kwanza toka alipohama katika Chama cha CUF.

 BAADHI ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Kada wa CCM Julius Mtatiro katika Mkutano uliofanyika katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.


KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Julius Mtatiro amesema viongozi mbali mbali wanahama katika  Vyama vya upinzani kutokana na taasisi hizo kushindwa kuwatumikia wananchi na badala yake ajenda zao zinatekelezwa na CCM.

Amesema mifumo imara ya kisiasa, kidemokrasia,uwazi, uwajibikaji, utendaji  na utawala bora iliyopo ndani ya CCM na Serikali zake mbili ya Zanzibar na  Jamhuri ya muungano ndio chanzo cha wanachama na viongozi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akizungumza na waandishi wa Habari huko Afisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui, aliwambia wanachama mbali mbali wa vyama vya upinzani hasa CUF na CHADEMA kujiunga na CCM mapema ili wanufaike na demokrasia pamoja na siasa zenye sera halisi za maendeleo.

Kupitia mkutano huo, Mtatiro aliyewahi kushika nyadhifa za ngazi za juu ndani ya CUF na kwa sasa amehamia CCM, alisema amepoteza  miaka 10 akiwa kiongozi ndani ya CUF na UKAWA ambapo hana jambo lolote analoweza kujivunia zaidi ya kuwa muhanga  wa kutatua migogoro ndani ya taasisi hizo iliyotokana na uchu wa madaraka.

Ameeleza kwamba licha ya vyama vya upinzani kuwa mstari wa mbele kukosoa na kubeza kila jambo linalofanywa na Serikali lakini ukweli na kwamba ndani ya vyama hivyo kuna mifumo ya rushwa, ufisadi, ukandamizaji wa demokrasia, pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu.

Akijibu baadhi ya hoja za waandishi wa habari , Mtatiro amesema kila mtu ana haki ya kuhama chama kimoja kwenda kingine na yeye amefanya hivyo baada ya kuvutiwa na mfumo imara wa kisiasa  ndani ya CCM chini ya Mwenyekiti wa Chama hicho Dkt. John Pombe Magufuli.

“ Kama niliweza kukaa ndani ya CUF miaka 10, basi hata CCM Mwenyezi Mungu akinipa uzima nitakaa zaidi ya miaka 60 kwani Chama hiki kimetekeleza mambo mengi mazuri kwa muda mfupi ambayo nilitamani yafanyike kwa Taifa letu”, alisema Mtatiro.

Amesema kuwa atabaki kuwa mwanasiasa mwenye msimamo na asiyeyumba katika kueleza ukweli na kuonyesha njia ya mafanikio kwa wananchi wenzake.

Akizungumzia hali ya maisha ya wananchi hasa wa Vijijini amesema yameimarika kwani huduma muhimu za kijamii na kiuchumi zimeboreshwa hasa Barabara Afya , Elimu , Umeme, Maji safi na salama.

Pia akizungumzia Sera ya Tanzania ya Viwanda Mtatiro, amesema mkakati huo ndio chimbuko la kukuza kwa kasi uchumi wa Taifa na kuongeza kuwa sera hiyo inatakiwa kwenda sambamba na kampeni uzalishaji mkubwa wa malighafi kupitia Sekta ya Kilimo.

Amesema Mataifa yaliyoendelea yamewekeza zaidi katika ujuzi na ufundi hasa kwa kundi la vijana ambalo ndio nguvu kazi ya uzalishaji katika Sekta mbali mbali za umma na binafsi.

Katika maelezo yake mtatiro, ameshauri CCM kupitia Serikali zake kuaulisha changamoto za ajira kwa vijana kupitia mfumo wa kujenga Vyuo vingi vya Ufundi na Ujasiriamali ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kutengeneza bidhaa mbali mbali zitakazochangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

“ Nazishauri Serikali zetu badala  ya kutumia fedha nyingi kuwasomesha vijana Vyuo Vikuu pia waangazie katika ujenzi wa Vyuo vya Ufundi na Ujasiriamali kila Kata na Shehia ili tupate vijana wengi wenye ujuzi ambao wataweza pia kujiajiri wenyewe kwani mataifa mengi yaliyoendelea kiuchumi kama China,Marekani  na India wametumia mfumo huo na wameweza kufika mbali kiuchumi.”, ameshaSEuri Mtatiro.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mchambuzi, mtafiti na mwandishi wa makala mbali mbali za Kisiasa nchini amezungumza na Vyombo vya Habari  vya Zanzibar kwa mara ya kwanza toka alipohama CUF na kujiunga na CCM mnamo  Desema 11, mwaka 2018.


Alhamisi, 18 Oktoba 2018

DK.MABODI AANIKA NJAMA CHAFU ZA VYAMA VYA UPINZANI, MTATIRO AJUTIA MIAKA 10 ALIYOHUDUMU CUF.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla 'Mabodi' akihutubia wananchi na Wana-CCM katika Mkutano wa kampeni za CCM uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang'ombe uliofanyika uwanja wa Kwaalinatu.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amewatahadharisha wanachama wa chama hicho, kuwa makini kwa kuepuka propaganda na njama chafu zinazofanywa na viongozi wakuu wa CUF waliotengeneza migogoro bandia ili waweze kupata huruma ya wananchi kuingia madarakani.

Tahadhari hiyo aliitoa wakati akimnadi mgombea wa nafasi ya Uwakilishi kwa tiketi ya CCM Ramadhan Hamza Chande katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Jang’ombe huko katika Uwanja wa Kwaalinatu.

Amesema CUF wametengeneza mgogoro bandia wenye lengo la kuiyumbisha CCM mwaka 2020 mbinu dhaifu ambazo hazitoweza kufanikiwa mbele ya CCM ya sasa iliyokuwa imara na inayokwenda sambamba na ulimwengu wa siasa za Kisayansi.

Dk. Mabodi amesema ushahidi pekee wa kuonyesha kuwa viongozi wa CUF hawana uadui kwa upande wa Zanzibar na Tanzania bara ni pale waliposhirikiana  kumnadi mgombea wa Chama hicho katika kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Liwale ambao mgombea wa CCM ameibuka mshindi.

Akimnadi na kumuombea kura Mgombea wa CCM katika Uchaguzi wa mdogo wa Jimbo la Jang’ombe Ramadhan Hamza Chande, Dk. Mabodi amewasihi Wana-CCM na wananchi wa Jimbo hilo kumchagua mgombe huyo ili aendeleze mambo mema yaliyoasisiwa na viongozi wa waliopita wa nafasi hiyo.

Amesema CCM imempitisha Ramadhan ikiamini kuwa ana uwezo na anafaa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa kasi kubwa.

Akieleza namna Chama kilivyojipanga kuwaletea maendeleo Wananchi, Dk.Mabodi alisema CCM inafanya siasa za kuimarisha maendeleo katika sekta zote Mijini na Vijijini ili kumaliza ahadi zote zilizotolewa katika Uchaguzi mkuu uliopita kabla ya mwaka 2020.

Dk.Mabodi ameongeza kuwa Chama kimekuwa kikishuka kwa wananchi wa makundi yote kwa lengo la kuratibu changamoto na kuzitatua kwa wakati.

Naye Mgombea wa tiketi ya CCM katika Uchaguzi mdogo wa Jang’ombe Ramadhan Hamza Chande, amewaomba wananchi na wanachama wa CCM wa jimbo hilo kukichagua Chama Cha Mapinduzi kupitia mgombe huyo aweze kuwatumikia na kuharakisha maendeleo ya Jang’ombe.

Katika maelezo yake Ramadhan amesema atakapopewa rdhaa na wananchi hao ya kuwa kiongozi atashirikiana nao kupanga mikakati ya kupanga mikakati yenye tija ndani ya Jimbo hilo.

Awali Mke wa Rais mstaafu wa awamu ya nne ya Jamhuri ya Tanzania Mama Salma Kikwete, amesema matunda yanayotokana na sera na mipango endelevu ya CCM yanaonekana wazi wazi kwani Zanzibar na Tanzania bara zote zinang’ara kwa miundombinu ya kisasa ya barabara na kuimarika kwa Sekta za Elimu, Afya pamoja na Maji safi na Salama.

Amesema CCM imekuwa ikiendeleza misingi ya maendeleo iliyoasisiwa na Vyama vya ukombozi vya ASP na TANU vilivyoungana na kuunda taasisi hiyo kwa nia ya kuongeza nguvu za kusimamia ufanisi sera na mipango ya maendeleo kwa wananchi wote.

Akizungumza katika Mkutano huo wa kampeni aliyekuwa kiongozi wa ngazi za juu wa CUF Julius Mtatiro aliyejiunga na CCM, amewaomba wananchi wa Jang’ombe kumchagua mgombea wa CCM kwani vyama vya upinzani hasa CUF vina matatizo na migogoro isiyoweza kutatulika kutokana na ubinafsi na sera za ubaguzi za viongozi wa vyama hivyo.

Mtatiro ametumia  mkutano huo kuwaomba radhi Watanzania hasa Vijana wa CCM kuwa kipindi yupo upinzani alitumiwa vibaya na CUF kukwamisha mipango ya maendeleo iliyokuwa ikitekelezwa na Serikali zote mbili za Chama Cha Mapinduzi.

Amesema kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 aliyohudumu katika CUF, hakuna hata siku moja Chama cha CUF ama UKAWA waliyoweza kushauri ama kupongeza mambo mema yanayofanywa na CCM badala yake waliponda na kupotosha umma kwa makusudi.

Akizungumza Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Abdallah Hasnuu Makame, akimuombea kura mgombea wa CCM katika mkutano huo wa kampeni amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana yametokana uwepo wa tunu za Taifa  ambazo ni Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 pamoja na Muungano wa Serikali mbili.

Amesema wananchi wa Jimbo la Jang’ombe hawatojutia maamuzi yao endapo watamchagua mgombea wa CCM aweze kuwaongoza kwa kipindi cha miaka miwili kufika 2020, kwani historia ya siasa za Tanzania toka mwaka 1992 ulipoasisiwa mfumo wa vyama vingi CCM ndio Chama pekee kilichoweza kutimiza kwa vitendo matakwa ya wananchi katika mfumo wa vyama vingi.

Akizungumza Mwakilishi wa Viti Maalum CCM Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Faida Mohamed Bakari, amewaomba  wanawake na vijana wa Jang’ombe kumchagua Ramadhan awe mwakilishi kwani ana uwezo mkubwa wa kusimamia maslahi ya makundi hayo sambamba na kuanzisha miradi mbali mbali itakayoweza kuwanufaisha wananchi.

Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang’ombe unatarajiwa kufanyika Octoba 27, mwaka 2018, kufuatia aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo Abdallah Diwani kuvuliwa uanachama kwa makosa ya ukiukaji wa maadili ya Chama Cha Mapinduzi.