Alhamisi, 8 Oktoba 2020

DK.MWINYI- ATAKA WAWEKEZAJI WACHANGIE MAENDELEOMGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM amesema endapo atapewa ridhaa ya kuwa rais wa zanzibar,atahakikisha wawekezaji wanachangia maendeleo ya jamii inayowazuka.

 Alisema katika utawala wake ni lazima kila mwekezaji anachangia maendeleo ya kijamii kwa kujenga shule,hospitali na miundombinu ya maji safi na salama. 

 Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na makundi mbalimbali ya kijamii ya wafanyabiashara wadogowadogo wakiwemo mama lishe,walinzi wa mahoteli, wavuvi na wafanyabisha za maduka ya vileo katika Kijiji cha Kiwengwa Wilaya ya Kaskazini "B" Unguja. 

 Dk.Mwinyi, alisema haiwezekani wawekezaji wanufaike na rasilimali za nchi huku wenyeji wakibaki katika lindi la umaskini. 

 "Sekta ya utalii ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu, hivyo ni lazima matokeo ya uwepo wa sekta hiyo yaonekane kuanzia kwa jamii zilizopo katika ukanda wa utalii ziwe na miundombinu bora na rafiki ya kijamii. 

 sio dhambi wawekezaji kusaidia maendeleo katika maeneo waliyowekeza japokuwa wapo baadhi wanatoa wanaotoa michango yao lakini wengi bado hawajahamasika",alisema Dk.Mwinyi.

 Akizungumzia suala la ajira kwa walinzi wa mahoteli Dk.Mwinyi, alisema atahakikisha watu hao wanapatiwa mikataba inayozingatia haki na maslahi yao pindi wanapomaliza mikataba hiyo ama kustaafu.

 Aidha,akizungumzia suala la Kodi na leseni kwa wafanyabiashara ndogondogo,alifafanua kuwa atahakikisha panatengenezwa mfumo mmoja wa ulipaji wa kodi kulingana na kipato cha mfanyabiashara sambamba na kupatiwa kipambulisho maalum kitakacholipiwa kila mwaka.

 "Nimeambiwa tayari serikali imeanza mchakato wa kutoa vitambulisho kwa kila mfanyabiashara na kuweka kiwango maalum cha ulipaji wa Kodi ambacho kitaondosha kero hiyo.",alisema Dk.Mwinyi.

 Akijibu hoja za wananchi Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi,alisema lengo la ziara hiyo ni kusikiliza changamoto za wafanyabiashara wadogo wadogo.

 Alisema kero za wafanyabiashara amezisikia hasa kuhusu suala la Kodi hivyo amesema kuwa akipata ridhaa naa kuwa rais suala Hilo atalitafutia ufumbuzi. 

 Alisema lengo la kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar ni kuhakikisha kila mwananchi anapata haki na kudhibiti vitendo vyote vya dhuruma. 

 Aliwambia wananchi hao kuwa katika utawala wake hatoruhusu vitendo vya uvunjaji wa sheria kwa wananchi vinavyosadikiwa kufanywa na viongozi ama watendaji wa serikali. 

 Alisema vitendo vya ubaguzi hatoruhusu viendelee kwani wananchi wa Tanzania ni wamoja na kwamba ubaguzi ni adui wa maendeleo. 

 Akizungumzia wajasiriamali alisema katika serikali yake watapatiwa mafunzo,watapewa mikopo na mitaji ya masharti nafuu na kuwatafutia masoko ya uhakika. 

 Dk.Mwinyi, akizungumza na waendesha pikipiki wa wilaya hiyo(bodaboda), aliwambia atahakikisha wanatambuliwa kisheria,kupewa mikopo ya masharti nafuu na kupatiwa huduma ya bima ya Afya ili pindi wanapopata ajali wawe na uhakika wa kupata matibabu.

 Katika maelezo yake Dk.Hussein,alisema suala la uvuvi wa kisasa ni sehemu ya ajenda ya serikali ijayo kupitia mfumo wa uchumi wa blue(blue economy), kwa kufanya uvuvi wa kisasa mpaka ufugaji wa samaki sambamba na kuwawezesha nyenzo za kisasa za uvuvi.

 Aliwambia wajasiriamali wa kuanika na kuuza dagaa kuwa atatatua changamoto zao kwa kuwawekea miundombinu rafiki katika utendaji wa kazi zao za kila siku.

 Pia alikemea tabia ya rushwa kwa baadhi ya watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo wanaotuhumiwa na kujihusisha na rushwa. 

 Alitumia nafasi hiyo kuomba kura na kuwaombea wagombea wote wa CCM kura za ndio ifikapo octobar 20, mwaka huu ili Chama kiendelee kuongoza dola. 

 Mama lishe Zainab Hussein,amesema wanakabiliwa na changamoto ya Halmashauri kuwatoza fedha nyingi ambazo ni shilingi 5000 kwa mwezi. 

 Alisema kila mwaka wanalipa shilingi 10,000 kwa leseni,wahudumu wa migahawa wanapimwa Afya kwa gharama za shilingi 60,000. 

 kwa upande wa Mama lishe Zuwena Kassim, wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa maji safi na salama kwa zaidi ya miaka 20. 

 Alisema wanakabiliwa na changamoto ya kuwa vibarua bila kupewa mikataba ya kulinda maslahi yao na kukosa michango ya kuweka katika mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar (ZSSF) na kiinua mgongo.

 "Tunabaguliwa sana sisi jamii ya wamasai Kama vile sio binadamu Kama walivyo wengine tunaomba sana ukiwa rais uweke mazingira ya kulinda haki zetu,''alisema john. 

 Alisema kuwa katika eneo la Kiwengwa maeneo mengi hayana vyoo Jambo ambalo ni hatari kiafya.

 Alisema kuwepo kwa utalii ni Jambo Jema lakini wengine wanauza hadi chakula cha mama lishe na wengine kufanya kazi ambazo wenyeji wanaweza kufanya.

 Katibu wa jumuiya ya waanika dagaa Saleh Khatib Makame, kuwa na eneo maalum la godown,kujengewa ofisi ya jumuiya ya waanika dagaa na kupunguziwa Kodi na Halmashauri ya wilaya hiyo.

DK.MWINYI-ASEMA ATATATUA CHANGAMOTO ZA WAWEKEZAJI

 


MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar, ataweka misingi imara kwa wafanyabiashara ili wafanye biashara zitakazoleta tija nchini.

Dk. Mwinyi alisema hayo alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara kusikiliza changamoto zinazowakabili ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za mgombea huyo, mkutano uliofanyika katika hoteli ya Golden Tulip, Malindi.

Alisema sekta biashara ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi na kuongeza pato la taifa hivyo atahakikisha anafungua milango ili wafanyabiashara waitumie kuimarisha mifumo ya biashara.

Dk. Mwinyi alisema ni vyema kwa wafanyabiashara wa ndani kuwa tayari kuitumia milango hiyo kwa kufanya biashara kubwa ndani ya nchi na kutokaa pembeni kupoteza fursa zitakazojitokeza.

“Ninagombea nafasi hii, kwa lengo la kuwatumikia wananchi na wafanyabiashara ni sehemu muhimu ya wananchi hivyo ninawaomba mjipanga vyema tukashirikiane na kwenda sambamba na matakwa ya wanachi wetu,” alieleza Dk. Mwinyi.

Alisema ili kufikia azma hiyo, serikali atakayoiongoza itashirikiana na jumuiya za wafanyabiashara na kuangalia sheria, kanuni, masuala ya kodi na ukataji wa leseni za biashara ili kuondoa vikwazo katika shughuli za biashara na viwanda nchini.

Akizungumzia sekta ya utalii, Dk. Mwinyi alisema ataiendeleza ili kuinua kiwango cha idadi ya watalii wanaoingia nchini lakini pia kuongeza thamani na aina za utalii kama njia moja wapo ya kuongeza mapato yanayotokana na sekta hiyo.

Alisema pamoja na Zanzibar kuendelea kuwa sekta kiongozi katika kuchangia pato la taifa, bado inapaswa kutangaza vivutio ilivyonavyo zikiwemo fukwe na kwa kuwekewa mipango madhubuti itakayowavutia watalii kuongezeka.

Kwa upande wa maendeleo ya viwanda, Dk. Mwinyi alisema sekta hiyo inahitaji mapinduzi makubwa ili isaidia ustawi wa wananchi wote wakiwemo wawekezaji wazawa kuwekeza kupitia sekta hiyo.

“Sekta ya viwanda itakapoimarika, wakulima na wafanyabiashara wadogo wataweza kutumia viwanda kwa kazi tofauti ili zilete tija kwao na taifa kwa ujumla,” aliemeza Dk. Mwinyi.

Mapema Akiwazungumza katika mkutano huyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC), Ally Amour, alisema serikali ya awamu ya saba imefanya mengi kwa wafanyabiashara hali ambayo imepelekea kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi wa nchi.

Alisema ni vyema anapoingia madarakani kiongozi huyo kusaidia kutayarisha mazingira mazuri ya biashara ili nchi iweze kusonga mbele zaidi kimaendeleo.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo, walimuomba kiongozi huyo kuzipa kipaumbele baadhi ya changamoto zilizobakia hususani kupitia sekta ya kilimo kwa kukipa kipaumbele kilimo cha umwagiliaji maji ili kuongeza uzalishaji utakaokidhi mahitaji ya ndani chakula.

Mbali na hayo walimuomba akiingia madarakani kulipatia ufumbuzi tatizo ufungaji wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ya watu binafsi kwani imechangia kuvuruga mfumo wa maisha na biashara za baadhi nya wafanyabiashara wanaofanya shughuli hizo.