Alhamisi, 8 Oktoba 2020

DK.MWINYI -AWEKA WAZI NEEMA KWA WANANCHI WA KASKAZI 'B' UNGUJAMGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi, amesema endapo atakuwa rais wa Zanzibar atahakikisha anajenga bandari mpya ya kisasa ya mafuta na gesi asililia ili kukuza uchumi wa nchi. 

 Alisema ujenzi wa bandari hiyo hautoathiri shughuli za wananchi hasa wanaojishughulisha na uvuvi katika maeneo ya wilaya hiyo. 

Ahadi hiyo ameitoa katika mwendelezo wa mikutano ya kampeni za CCM katika wilaya ya Kaskazini ‘B’ huko katika skuli ya bumbwini Wilaya ya kaskazini ‘B’ Unguja.

 Alisema bandari hiyo ikikamilika itakuwa ndio kitovu cha uchumi wa nchi kwani itasaidia kutoa ajira nyingi.

 Aidha, alisema atavipa kipaumbele vikundi vya ujasiriamali kwa kuvipatia mikopo na mafunzo ili wanufaike na fursa hizo. 

 Alisema atahakikisha wananchi wa wilaya hiyo wananufaika na ufugaji wa kisasa wa samaki ili waende sambamba na dhana ya uchumi.

 Pia alijiombea kura na kuwaombea kura wagombea wote wa CCM ili CCM iendelee kuongoza dola.

Pamoja na hayo aliwataka wananchi walinde amani ya nchi na wasikubali kuchokozeka na vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wapinzani.

Alisema atajenga hospitali ya wilaya,kununua vifaa tiba vya kisasa na kuajiri wafanyakazi wa sekta ya afya ili huduma zitakazotolewa zikidhi mahitaji ya wakaazi wa wilaya ya kaskazini ‘B’ Unguja. 

 Pia ameahidi kujenga barabara ya bumbwini hadi mahonda ili kukuza uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.

 Aidha alisema watajenga skuli ya ghorofa na daharia pamoja na kuthibiti changamoto ya wizi wa mifugo ili wananchi wanufaike na fursa za ufugaji.

 Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, alisema historia ya Zanzibar imeanzia mbali kwani toka utawala wa wareno na waoman.  

Dk.Shein, alisema toka mwa 1957 zilifanyika chaguzi mbalimbali lakini wazawa hawakuwahi kushinda uchaguzi huo kutokana na kuwepo kwa njama za ukandamizaji.

 Alisema baada ya utawala wa ukandamizaji wa wakati huo,Wazee wa kiafrika chini ya uongozi wa marehemu Abeid Amani Karume wakaamua kuondosha utawala huo kupitia mapinduzi ya mwaka 1964.

 Dk.Shein, alisema baada ya mapinduzi hayo nchi ilikuwa huru na kuweka viongozi kwa awamu mbalimbali toka awamu ya kwanza mpaka hivi sasa tunaelekea awamu ya nane.

 Alisema kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wanajifanya hawatambui mapinduzi kutokana na sababu zao za kisiasa. 

Alisema kwa sasa nchi ipo katika harakati za uchaguzi hivyo wananchi, wasikubali kuongozwa na watu wabaguzi wa kidini.kikabila na kisiasa. 

Alieleza kuwa CCM imemteua Dk.Mwinyi kwa kuwa ana sifa zinazokubalika ndani ya jamii yake sambamba na kuwa na sifa za ziada za kuwa mpole,mvumilifu,mcheshi,mcha mungu na mwadilifu.

 Alisema Dk.Hussein, ana sifa nyingine tofauti na wagombea wengine mwani ana uzoefu wa kiutendaji ndani ya serikali na ni msomi wa fani ya udaktari. 

 Alieleza kuwa CCM imemkabidhi Dk.Mwinyi, bendera na ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025 ili vimuongoze katika kusimamia maslahi ya CCM. 

Dk.Shein, alisema ushindi wa CCM wa mwaka huu ni mkubwa ambao utakuwa ni wa kihistoria katika siasa za afrika mashariki kwani CCM imejipanga vizuri kuhakikisha inashindwa kwa njia za kidemokradsia. 

Alisema hakuna njia ya mkatoa ya kuingia ikulu na kwamba ni lazima chama kishinde kupitia uchaguzi huru na wa haki. 

Alieleza kuwa kwa mara ya kwanza Zanzibar itaendesha uchaguzi kwa fedha zake za ndani bila ya kutegemea ufadhili, hatua ambayo ni kubwa kimaendeleo.

Pamoja na hayo aliwaombea kura za ndio wagombea wote wa CCM wakiwemo wagombea wa nafasi za Urais,wabunge,wawakilishi na madiwani.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla, alisema kuwa CCM imetekeleza ilani yake kwa zaidi ya asilimia 100 kwa kuwafikishia wananchi huduma zote za msingi.

Alisema Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Shein, aliasisi mfumo wa kupunguza masafa baina ya chama na serikali kwa kwa kufuatana na viongozi wa CCM kila anapofanya ziara zake za kikazi.

Alisema CCM inaendelea kufanya kampani zake za kisayansi za kuwafuata wananchi katika maeneo yao na kuwaeleza sera zake na namna kitakavyotekeleza miradi mipya ya maendeleo kwa maslahi ya wananchi wote. 

“ Tumetekeleza kwa kiwango kikubwa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 na mengine mazuri yamo katika ilani mpya ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025”, alisema Dk.Mabodi. 

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Unguja ,Idd Ali Ame alisema wananchi wa mkoa huo wanamshukru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015/2020. 

Alisema serikali ya awamu ya saba imetekeleza mambo mengi ya maendeleo zikiwemo utengenezaji wa barabara za kisasa,vituo vya afya,majengo ya kisasa ya skuli za msingi na sekondari, ujenzi wa kituo cha mafunzo ya amali, huduma za maji safi na salama. 

Alisema wananchi wa mkoa huo watafikisha shukrani zao kupitia upigaji wa kura za ndio kwa kuwachagua wagombea wa CCM ili chama kishinde na kuendelea kuongoza dola.

Akizungumza kwa niaba ya wagombea wa nafasi ya uwakilishi, mgombea uwakilishi jimbo la Donge, Dkt.Khalid Salum Mohamed alisema wanamshukru Rais wa Zanzibar Dk.Shein kwa kuasisi ujenzi wa bandari kubwa katika maeneo ya bumbwini kwani itasaidia kuongeza ajira kwa wananchi wa maeneo hayo na vijiji jirani.

Pia alisema wamejipanga kutekeleza kwa vitendo falsafa ya uchumi wa kupitia rasilimali za bahari(blue economy), na kwamba wananchi wa maeneo hayo ya kaskazini Unguja wananufaika na bahari. 

Pamoja na hayo aliwasihi wananchi kuwapigia kura za ndio wagombea wote waliosimamishwa na Chama Cha Mapinduzi na kuhakikisha wanashinda.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Anna Agata msuya ,amesema amani ya Tanzania inategemea Zanzibar hivyo ni muhimu wananchi kuwapigia kura nyingi za ndio wagombea walioteuliwa na CCM.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni