Jumatatu, 22 Juni 2015

Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein aongaoza kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC)ZANZIBAR.

KIKAO cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC), kilifanyika jana, chini ya Mwenyekiti wake Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Mhe. Waride Bakari Jabu (Mb.), amesema kikao hicho cha kawaida cha siku moja, pamoja na mambo mengine, kimempongeza kwa dhati kabisa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa uamuzi wake wa kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM, ili aweze kugombea kwa mara ya pili Kiti cha Rais wa Zanzibar, katika Uchaguzi Mkuu wa Dola wa mwaka 2015, na hivyo aendelee kuiongoza Zanzibar na kuwaletea Wazanzibari maendeleo, kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.

Kikao pia kimempongeza Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Abdulrahman Omar Kinana, kwa kukamilisha ziara katika Mikoa na Wilaya za Zanzibar, yenye lengo la kuimarisha Uhai wa Chama kwa mafanikio makubwa.

Aidha, kimempongeza Ndugu Kinana kwa kushiriki kikamilifu kazi za Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 - 2015 wakati wote wa ziara yake hiyo, Mikoani humo.

KUHUSU KUJAZA NAFASI WAZI ZA UONGOZI.
Kikao kilipokea na kujadili majina ya wana CCM kumi na wanane (18) waliojitokeza kuomba kujaza nafasi wazi za Ungozi katika Mikoa ya Kichama ya Magharibi na Kusini, Unguja.

Mhe. Waride, amezitaja nafasi hizo kuwa ni Ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) kupitia Wilaya za Kichama za Dimani na Mfenesini (Magharibi) pamoja na Katibu wa Siasa na Uenezi (Kusini) na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu ya CCM ya Taifa, kwa hatua zinazofuatia.

KUHUSU UANDIKISHAJI WA DAFTARI LA WAPIGA KURA.
Kikao kimewahimiza wananchi wote wenye sifa ya kuandikishwa katika daftari hilo la kudumu la wapiga kura  kwa mujibu wa sheria wanapata nafasi ya kujiandikisha bila ya kusumbuliwa na mtu yeyote.

Aidha, kikao kimeviomba vyombo vya dola kusimamia ipasavyo suala zima la wananchi wote wanafuata sheria zilizopo sio tu katika kipindi hiki cha uandikishaji wa daftari la kudumu bali pia wakati wa kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Sambamba na hilo, kikao kimesikitishwa sana na vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baadhi ya watu  kwa lengo la kutaka kuwanyima haki watu wenye sifa ya kuandikishwa katika daftari la wapiga na badala yake kuandikishwa watu ambao wanakosa sifa kwa mujibu wa sheria.

Alhamisi, 18 Juni 2015

MBIO ZA URAIS CCM

 

Wanafunzi wa Madrasat Swifat Nabawiyyal Karima {Msolopa} wakitumbuiza katika sherehe ya uchukuaji fomu
Add captionMakamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, akiongozana  na Mkewe Mwanamwema Shein akiwapungia mkono wana CCM waliofurika Viwanja vya Afisi Kuu ya CCM Zanzibar tayari kwa kuchukua Fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama chake kugombea Kiti cha Rais wa Zanzibar. Kulia - Naibu Katibu Mkuu wa CCM - Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai.


Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein akisalimiana na Mjumbe wa Kamati Kuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi.

Makamu  Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mhe. Dkt. Ali MOhamed Shein akikaribishwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndugu. Vuai Ali Vuai kabla tayuari kwa kuchukua Fomu - Afisi Kuu ya CCM - Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar akimkabidhi Fomu Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mhe. Dkt. Ali MOhamed Shein akiwa ndani ya ukumbi wa mkutano tayari kwa kuzungumza na Viongozi wa Ngazi mbali mbali  za CCM Zanzibar.

Jumatatu, 15 Juni 2015

TAMKO LA PAMOJA LA VIONGOZI


TAMKO LA PAMOJA LA VIONGOZI, WATENDAJI WA CHAMA CHA MAPINDUZI NA JUMUIYA ZAKE  WA MIKOA SITA YA KICHAMA YA ZANZIBAR LA KUKUOMBA MAKAMU MWENYEKITI WA CCM NA RAIS WA ZANZIBAR MHE. DKT. ALI MOHAMED SHEIN KUCHUKUA FOMU YA KUOMBA KUTEULIWA KUGOMBEA KITI CHA RAIS WA ZANZIBAR KUPITIA CHAMA CHA MAPINDUZI KATIKA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2015


Kwa niaba ya Viongozi, Watendaji wa Chama na Jumuiya zake wa Mikoa sita ya Kichama ya Zanzibar,  tunayo heshima kubwa leo kusimama hapa kwa niaba yenu ili kuwasilisha tamko letu hili lenye nia na madhumuni ya kumuomba kiongozi wetu mpendwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, kwenda kuchukua Fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya kiti cha Rais wa Zanzibar, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Awali ya yote ninapenda kutumia fursa hii kumshukuru Mola wetu mtukufu mwingi wa rehema na muumba mbingu na ardhi pamoja na vyote viliyomo, kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kukusanyika hapa leo hii kwa salama na amani.

Kwa niaba ya wanachama wa CCM, Jumuiya   pamoja na wananchi wote wapenda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa wa Mikoa na Wilaya zote za Zanzibar, sisi Viongozi wa Chama, Jumuiya pamoja na Watendaji  wa CCM kutoka Mikoa sita ya kichama ya Unguja na Pemba, leo hii tarehe 14 Juni 2015, tumekutana hapa kwenye ukumbi wa Nyumba za Wazee Sebleni Unguja, ili kutafakari na kujenga mustakabali wa uhai wa Chama chetu.

Kama tunavyofahamu kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, mwaka huu wa 2015 tunakabiliwa na Uchaguzi Mkuu wa kumchagua Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Madiwani.  Huu ni uchaguzi mkuu wa tano (5) tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa Tanzania hapo mwaka 1992. 

Aidha, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) tayari imeshatangaza ratiba ya uchaguzi huo ambao utafanyika tarehe 25 Oktoba 2015.  Vile vile hivi karibuni CCM imetangaza ratiba ya mchakato wa uteuzi wa mgombea wake katika uchaguzi huo pamoja na ule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Ratiba hiyo imeanza tarehe 3 Juni 2015 hadi tarehe 2/7/2015.

Hadi kufikia jana tarehe 13 Juni 2015, wakati idadi ya wanachama wa CCM waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefikia 32, hakuna mwanachama wa CCM hata mmoja aliyejitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Rais wa Zanzibar, hali ambayo inathibitisha kwamba, wana CCM wote hapa Zanzibar bado tunaridhika na uongozi wa Mhe. Dkt. Shein.  Hivyo sisi viongozi wa CCM wa Mikoa na Wilaya kwa kushirikiana na Jumuiya zetu pamoja na wazee wetu tumeona tunao wajibu wa kukutana ili kutafakari hali hiyo na kuipatia majibu.


Kwa kuzingatia historia ya Chama chetu na uzito wa changamoto iliyo mbele yetu tumeamua kukutana pahala hapa (Nyumba za Wazee Sebleni) ili kujikumbusha wajibu wetu kama viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, walinzi na watetezi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964 ambayo ndio chimbuko la majengo haya.

Baada ya kutafakari kwa kina na kupima kazi iliopo mbele yetu katika kusimamia maendeleo ya wananchi, kudumisha umoja, amani, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na Mapinduzi yetu matukufu ya tarehe 12 Januari 1964, kwa kauli moja tumekubaliana kumuomba kiongozi wetu mpendwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa mara nyingine tena ajitokeze kwenda kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi.

Kwa hakika tunazo sababu nyingi za kumuomba afanye hivyo, lakini kwa ajili ya kuokoa muda ninaomba nizitaje chache kwa umuhimu wake, nazo ni kama zifuatazo:-
    a)    Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein bado anakidhi vigezo na sifa zote zinazohitajika kwa mujibu wa Katiba na sharia za uchaguzi.

   b)   Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ameonesha uwezo mkubwa wa kuongoza nchi yetu na kusimamia kwa ufanisi mkubwa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 – 2015.

    c)    Anao uwezo mkubwa wa kuwaunganisha Wazanzibari na kudumisha umoja, amani, na Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar.
  
    d)   Ameiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye mfumo wa umoja wa kitaifa kwa weledi mkubwa na kuwa mfano bora wa kuigwa na Mataifa mengine duniani.

    e)    Ana tabia ya upole, uadilifu, uaminifu na unyenyekevu kwa wananchi wa rika na jinsia zote.

   f)     Hana makuu wala ubaguzi wa aina yoyote.  Ni mpenda maendeleo na mwanamapinduzi wa kweli.

    g)    Ni mwenye msimamo thabiti.  Katika masuala ya msingi yanayohusu nchi na wananchi hayumbi na wala hayumbishwi.

   h)   Kuanzia tarehe 17/11/2014 hadi tarehe 4/12/2014, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, alitembelea Mikoa na Wilaya zote za Kichama hapa Zanzibar.  Katika ziara hizo alikutana na kuzungumza na viongozi wa mashina (Mabalozi) na Maskani zote za CCM Unguja na Pemba.  Kwa kupitia mikutano hio viongozi hao ambao ni kundi kubwa la wana CCM walimuomba Dkt. Ali Mohamed Shein, afikirie kugombea tena nafasi hii ya Rais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Kama nilivyoeleza hapo juu, kwa hakika sababu ni nyingi inatosha tu kusema kwamba, kwa maoni yetu Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, bado ni jembe la kujivunia na tunaimani kubwa ya kwamba, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ataendelea kutuvusha na hakuna mbadala wake kwa sasa.

Hivyo kwa heshima na unyenyekevu mkubwa tunamuomba atukubalie ombi letu hili na kwa mara nyingine tena akachukue Fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea kiti cha Rais wa Zanzibar kupitia CCM!

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Ijumaa, 12 Juni 2015

CCM yazipongeza kamati za siasa za Mikoni Pemba


CHAMA Cha Mapinduzi Zanzibar kimezipongeza Kamati za Siasa za Mikoa ya Pemba kwa kusimamia vyema zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura lililofanyika Kisiwani pemba hivi karibuni.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai ametoa kauli hiyo huko, wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati za Siasa za Mikoa miwili ya Pemba, huko Chake chake.
Alisema mafanikio yote hayo yamekuja kutokana na mashirikiano mazuri yaliopo baina ya Viongozi na Watendaji wa Mikoa hiyo, hatua ambayo inaleta matumaini makubwa  na matarajio mazuri zaidi ya ufanisi wa kazi.

“Nimefarajika mno na hatua mliyochukua nyinyi Viongozi wa Chama chetu wa Mikoa yote miwili ya kisiwa cha Pemba kwa kusimamia kwa mafanikio makubwa zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ndani ya mikoa yenu, hivyo nawasihi kutumia ari hiyo kuendeleza suala zima la mshikamano kama hatua mojawapo itakayoleta ushindi wa kishindo kwa Chama chetu kwenye uchaguzi mkuu wa dola wa Oktoba 25, mwaka huu”. Alisisitiza Vuai.

Aliwakumbusha Viongozi na Watendaji wa CCM kufanya kazi kwa kujituma zaidi huku wakijuwa kwamba malengo makubwa ya Chama hicho si jengine bali ni kuendelea wimbi la ushindi katika uchaguzi mkuu na kushika hatamu ya dola Tanzania Bara na zanzibar.

Katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa pia na wajumbe wa halmashauri kuu ya chama cha Mapinduzi wa mikoa miwili kichama,Vuai aliwataka viongozi hao kuendeleza  mshikamano wao kuhakikisha kwamba chama cha Mapinduzi kinanyakua baadhi kama si majimbo yote ya 18 ya uchaguzi yaliopo Kisiwani humo.

“Ile kauli wanayotamka viongozi na wafuasi wa CUF kwamba majimbo ya Pemba ni hatimiliki yao imepitwa na wakati kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ifanya mabadiliko makubwa ya kimaendeleo kila pembe ya kisiwa cha Pemba sambamba na wananchi walio wengi wamekuwa wakijiunga na CCM pamoja na kuanzisha maskani za CCM kwa wingi”. Alidai naibu Katibu Mkuu huyo.

Mapema Vuai alipata nafasi ya kutembelea zoezi la uandikishaji  wa daftari la kudumu la wapiga kura katika vituo vya mkoa wa kaskazini Pemba ikiwemo jimbo la Mtambile ambapo aliridhishwa na zoezi hilo linalofanyika katika mazingira ya amani.

Zoezi la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura ni kwa ajili ya wapiga kura wapya ambao hawajasajiliwa katika daftari hilo kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

'Nimefurahishwa na zoezi la daftari la kudumu la wapiga kura lilivyoendeshwa katika kisiwa cha Pemba kwa utulivu mkubwa hatua ambayo ilitoa nafasi kwa wananchi kushiriki vizuri bila ya pingamizi'alisema.

Vituo vilivyotembelewa na naibu katibu mkuu wa CCM ni pamoja na Kituo cha Kengeja,shule ya msingi ya Mizingani.Chokocho ,Mkanyageni hadi Michenzani.

Wakati huohuo,Naibu katibu mkuu wa chama cha mapinduzi Zanzibar Vuai Ali Vuai amewataka wanachama wa chama hicho kufanya kazi ya kuimarisha chama na kuingiza wanachama wapya kufuatia kuimarika kwa mazingira ya utulivu wa kisiasa Pemba.

Vuai alisema hayo wakati akipandisha bendera katika maskani ya 'Mbili za tosha' hapo Kinyasini Mgogoni mkoa wa kaskazini Pemba,ambapo alisema moja ya faida kubwa ya kuwepo kwa Serikali ya umoja wa kitaifa ni kuweka mazingira mazuri ya vyama vya siasa kufanya kazi zao bila ya usumbufu kama ilivyokuwa zamani.

Alisema mabadiliko makubwa yamepatikana katika kisiwa cha Pemba ikiwemo wananchi pamoja na wafuasi kujiunga katika chama cha Mapinduzi bila ya woga wala kujali vitisho vya wapinzani.

'Ile dhana kwamba kisiwa cha Pemba ni kambi ya upinzani ya CUF sasa imeanza kuondoka kidogo kidogo kwa sababu unaona vijana leo hii wameamuwa kuweka maskani kwa hiari yao'alisema.

Vuai alisema amefurahishwa na uamuzi ambao unaonesha kwamba wananchi wa Pemba wamebadilika baada ya kuchochwa na vituko na visa pamoja na uongo wa wapinzani waliokuwa wakisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya chama cha Mapinduzi haijafanya jambo lolote.

'Nyote ni mashahidi barabara za mkoa wa kaskazini zilivyotandikwa kwa lami huku huduma zote muhimu za usambazaji umeme vijijini na maji safi zikipatikana bila ya matatizo.....nauliza hiyo ni kazi ya nani kama si CCM'alisema Vuai.

Mapema Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi mkoa wa kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa aliwataka wananchi kuacha kudanganywa na wapinzani ambao hivi sasa wamo katika Serikali wakitekeleza ilani ya uchaguzi ya chama cha Mapinduzi kwa utii na uaminifu.

Akisoma risala,Mwenyekiti wa maskani hiyo alisema kwamba wameanzisha maskani hiyo kwa kuijenga siku moja baada ya kuchochwa na kelele za wapinzani katika jimbo hilo.

'Sisi vijana tunaahidi kwamba tutakuwa watiifu kwa chama cha Mapinduzi na kuhakikisha tunakuwa wanachama watiifu na kushiriki katika uchaguzi mkuu kwa kupiga kura ya ndiyo'alisema.

mapema mwenyekiti wa maskani hiyo Omar Yussuf alisema wameamuwa kwa hiari yao kuanzisha maskani hiyo bila ya ushawishi wa mtu baada ya kuridhishwa na utendaji wa ilani ya chama cha mapinduzi.

Omar alisema wanakiunga mkono chama cha Mapinduzi huku wakiahidi kupiga kura ya ndiyo katika uchaguzi mkuu pamoja na kuiunga mkono katiba inayopendekezwa ambayo imeinufaisha zaidi Zanzibar.

'Mheshimiwa naibu sisi wanachama wa maskani ya 'mbili za tosha' tunaahidi tutapiga kura ya ndio kwa katiba inayopendekezwa pamoja na kuhakikishia chama ushindi katika uchaguzi mkuu'alisema.

Katika sherehe hizo Vuai alipandisha bendera katika maskani hiyo pamoja na kutoa jezi seti moja na mipira kwa ajili ya vijana hao ambao wanashiriki katika ligi kuu ya kanda Pemba.

Jumamosi, 6 Juni 2015

Wanawake wamepongezwa kwa kutumia nafasi iliopo katika katiba

Mhe. Vuai Ali Vuai akisalimiana na Mhe. Amina Salum Ali, Hapo Afisi Kuu CCM - Zanzibar


Mhe. Amina akisaini katika kitabu ambacho wageni huwa wanasaini pindi tu wanapofika hapo

Mhe. Naibu Katibu Mkuu akitoa nasaha kwa Mgombea ambae aliyefika hapo Afisi Kuu CCM - Zanzibar kwa ajili ya kusalimiana nae

Mhe. Amina Salum Ali akizungumza na waandishi wa habari hapo katika Afisi Kuu CCM - Zanzibar
Wanawake wamepongezwa kwa kutumia nafasi iliopo katika katiba ya kuwania nafasi za juu za uongozi kwa ajili ya kuleta mabadiliko na maendeleo katika taifa.

Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Vuai Ali Vuai wakati akisalimiana na mgombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano aliyechukuwa fomu kuwania kinyanganyiro hicho Amina Salum Ali ambaye alifika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui kwa ajili ya kujitambulisha.

Alisema
Chama Cha Mapinduzi ni miongoni mwa taasisi zenye demokrasia pana ya kutoa nafasi kwa viongozi wake katika makundi mbali mbali kuchukuwa fomu na kuwania nafasi za juu za uongozi bila ya vikwazo.

'Kwa niaba ya
Chama Cha Mapinduzi tunakupongeza kwa kuamuwa kujitokeza kuchukuwa fomu ya urais wa Zanzibar hatua ambayo inadhihirisha mshikamano uliopo ndani ya chama na nafasi yake kwa watu mbali mbali kuwania nafasi za uongozi bila ya vikwazo'alisema.

Mapema Amina alikipongeza
Chama Cha Mapinduzi kwa demokrasia yake iliopo ambayo imetoa nafasi kubwa kwa wanwake kugombea nafasi mbali mbali za juu za uongozi.

Alisema ameamuwa kuchukuwa fomu kuwania nafasi ya juu ya uongozi katika chama cha Mapinduzi kwa ajili ya kutimiza matakwa ya demokrasia iliopo ndani ya chama ambayo ni kubwa.

'Nakipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kujenga demokrasia pana ambayo leo hii imeniwezesha kuchukuwa fomu kuwania nafasi ya juu ya urais wa muungano'alisema.

Aliwataka wanawake wenzake kuitumia fursa ya demokrasia iliopo katika
Chama Cha Mapinduzi ambayo ni ya kupigiwa mfano yenye malengo ya kuzishirikisha jinsia zote katika uongozi wa nchi.

Mapema Amina alifika katika afisi kuu ya CCM Kisiwandui na kupokewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai na kutoa salamu zake za shukrani kwa chama cha Mapinduzi kwa kumpa kila aina ya ushirikiano.

Mgombea huyo alisema ameanza safari ya kutembea mikoa ya Tanzania ikiwemo Pemba kwa ajili ya kusaka wadhamini ambao watamuwezesha kukamilisha masharti ya fomu ya kuwania nafasi ya urais.