Jumatatu, 22 Juni 2015

Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein aongaoza kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC)



ZANZIBAR.

KIKAO cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC), kilifanyika jana, chini ya Mwenyekiti wake Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Mhe. Waride Bakari Jabu (Mb.), amesema kikao hicho cha kawaida cha siku moja, pamoja na mambo mengine, kimempongeza kwa dhati kabisa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa uamuzi wake wa kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM, ili aweze kugombea kwa mara ya pili Kiti cha Rais wa Zanzibar, katika Uchaguzi Mkuu wa Dola wa mwaka 2015, na hivyo aendelee kuiongoza Zanzibar na kuwaletea Wazanzibari maendeleo, kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.

Kikao pia kimempongeza Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Abdulrahman Omar Kinana, kwa kukamilisha ziara katika Mikoa na Wilaya za Zanzibar, yenye lengo la kuimarisha Uhai wa Chama kwa mafanikio makubwa.

Aidha, kimempongeza Ndugu Kinana kwa kushiriki kikamilifu kazi za Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 - 2015 wakati wote wa ziara yake hiyo, Mikoani humo.

KUHUSU KUJAZA NAFASI WAZI ZA UONGOZI.
Kikao kilipokea na kujadili majina ya wana CCM kumi na wanane (18) waliojitokeza kuomba kujaza nafasi wazi za Ungozi katika Mikoa ya Kichama ya Magharibi na Kusini, Unguja.

Mhe. Waride, amezitaja nafasi hizo kuwa ni Ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) kupitia Wilaya za Kichama za Dimani na Mfenesini (Magharibi) pamoja na Katibu wa Siasa na Uenezi (Kusini) na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu ya CCM ya Taifa, kwa hatua zinazofuatia.

KUHUSU UANDIKISHAJI WA DAFTARI LA WAPIGA KURA.
Kikao kimewahimiza wananchi wote wenye sifa ya kuandikishwa katika daftari hilo la kudumu la wapiga kura  kwa mujibu wa sheria wanapata nafasi ya kujiandikisha bila ya kusumbuliwa na mtu yeyote.

Aidha, kikao kimeviomba vyombo vya dola kusimamia ipasavyo suala zima la wananchi wote wanafuata sheria zilizopo sio tu katika kipindi hiki cha uandikishaji wa daftari la kudumu bali pia wakati wa kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Sambamba na hilo, kikao kimesikitishwa sana na vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baadhi ya watu  kwa lengo la kutaka kuwanyima haki watu wenye sifa ya kuandikishwa katika daftari la wapiga na badala yake kuandikishwa watu ambao wanakosa sifa kwa mujibu wa sheria.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni