Ijumaa, 12 Juni 2015

CCM yazipongeza kamati za siasa za Mikoni Pemba


CHAMA Cha Mapinduzi Zanzibar kimezipongeza Kamati za Siasa za Mikoa ya Pemba kwa kusimamia vyema zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura lililofanyika Kisiwani pemba hivi karibuni.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai ametoa kauli hiyo huko, wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati za Siasa za Mikoa miwili ya Pemba, huko Chake chake.
Alisema mafanikio yote hayo yamekuja kutokana na mashirikiano mazuri yaliopo baina ya Viongozi na Watendaji wa Mikoa hiyo, hatua ambayo inaleta matumaini makubwa  na matarajio mazuri zaidi ya ufanisi wa kazi.

“Nimefarajika mno na hatua mliyochukua nyinyi Viongozi wa Chama chetu wa Mikoa yote miwili ya kisiwa cha Pemba kwa kusimamia kwa mafanikio makubwa zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ndani ya mikoa yenu, hivyo nawasihi kutumia ari hiyo kuendeleza suala zima la mshikamano kama hatua mojawapo itakayoleta ushindi wa kishindo kwa Chama chetu kwenye uchaguzi mkuu wa dola wa Oktoba 25, mwaka huu”. Alisisitiza Vuai.

Aliwakumbusha Viongozi na Watendaji wa CCM kufanya kazi kwa kujituma zaidi huku wakijuwa kwamba malengo makubwa ya Chama hicho si jengine bali ni kuendelea wimbi la ushindi katika uchaguzi mkuu na kushika hatamu ya dola Tanzania Bara na zanzibar.

Katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa pia na wajumbe wa halmashauri kuu ya chama cha Mapinduzi wa mikoa miwili kichama,Vuai aliwataka viongozi hao kuendeleza  mshikamano wao kuhakikisha kwamba chama cha Mapinduzi kinanyakua baadhi kama si majimbo yote ya 18 ya uchaguzi yaliopo Kisiwani humo.

“Ile kauli wanayotamka viongozi na wafuasi wa CUF kwamba majimbo ya Pemba ni hatimiliki yao imepitwa na wakati kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ifanya mabadiliko makubwa ya kimaendeleo kila pembe ya kisiwa cha Pemba sambamba na wananchi walio wengi wamekuwa wakijiunga na CCM pamoja na kuanzisha maskani za CCM kwa wingi”. Alidai naibu Katibu Mkuu huyo.

Mapema Vuai alipata nafasi ya kutembelea zoezi la uandikishaji  wa daftari la kudumu la wapiga kura katika vituo vya mkoa wa kaskazini Pemba ikiwemo jimbo la Mtambile ambapo aliridhishwa na zoezi hilo linalofanyika katika mazingira ya amani.

Zoezi la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura ni kwa ajili ya wapiga kura wapya ambao hawajasajiliwa katika daftari hilo kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

'Nimefurahishwa na zoezi la daftari la kudumu la wapiga kura lilivyoendeshwa katika kisiwa cha Pemba kwa utulivu mkubwa hatua ambayo ilitoa nafasi kwa wananchi kushiriki vizuri bila ya pingamizi'alisema.

Vituo vilivyotembelewa na naibu katibu mkuu wa CCM ni pamoja na Kituo cha Kengeja,shule ya msingi ya Mizingani.Chokocho ,Mkanyageni hadi Michenzani.

Wakati huohuo,Naibu katibu mkuu wa chama cha mapinduzi Zanzibar Vuai Ali Vuai amewataka wanachama wa chama hicho kufanya kazi ya kuimarisha chama na kuingiza wanachama wapya kufuatia kuimarika kwa mazingira ya utulivu wa kisiasa Pemba.

Vuai alisema hayo wakati akipandisha bendera katika maskani ya 'Mbili za tosha' hapo Kinyasini Mgogoni mkoa wa kaskazini Pemba,ambapo alisema moja ya faida kubwa ya kuwepo kwa Serikali ya umoja wa kitaifa ni kuweka mazingira mazuri ya vyama vya siasa kufanya kazi zao bila ya usumbufu kama ilivyokuwa zamani.

Alisema mabadiliko makubwa yamepatikana katika kisiwa cha Pemba ikiwemo wananchi pamoja na wafuasi kujiunga katika chama cha Mapinduzi bila ya woga wala kujali vitisho vya wapinzani.

'Ile dhana kwamba kisiwa cha Pemba ni kambi ya upinzani ya CUF sasa imeanza kuondoka kidogo kidogo kwa sababu unaona vijana leo hii wameamuwa kuweka maskani kwa hiari yao'alisema.

Vuai alisema amefurahishwa na uamuzi ambao unaonesha kwamba wananchi wa Pemba wamebadilika baada ya kuchochwa na vituko na visa pamoja na uongo wa wapinzani waliokuwa wakisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya chama cha Mapinduzi haijafanya jambo lolote.

'Nyote ni mashahidi barabara za mkoa wa kaskazini zilivyotandikwa kwa lami huku huduma zote muhimu za usambazaji umeme vijijini na maji safi zikipatikana bila ya matatizo.....nauliza hiyo ni kazi ya nani kama si CCM'alisema Vuai.

Mapema Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi mkoa wa kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa aliwataka wananchi kuacha kudanganywa na wapinzani ambao hivi sasa wamo katika Serikali wakitekeleza ilani ya uchaguzi ya chama cha Mapinduzi kwa utii na uaminifu.

Akisoma risala,Mwenyekiti wa maskani hiyo alisema kwamba wameanzisha maskani hiyo kwa kuijenga siku moja baada ya kuchochwa na kelele za wapinzani katika jimbo hilo.

'Sisi vijana tunaahidi kwamba tutakuwa watiifu kwa chama cha Mapinduzi na kuhakikisha tunakuwa wanachama watiifu na kushiriki katika uchaguzi mkuu kwa kupiga kura ya ndiyo'alisema.

mapema mwenyekiti wa maskani hiyo Omar Yussuf alisema wameamuwa kwa hiari yao kuanzisha maskani hiyo bila ya ushawishi wa mtu baada ya kuridhishwa na utendaji wa ilani ya chama cha mapinduzi.

Omar alisema wanakiunga mkono chama cha Mapinduzi huku wakiahidi kupiga kura ya ndiyo katika uchaguzi mkuu pamoja na kuiunga mkono katiba inayopendekezwa ambayo imeinufaisha zaidi Zanzibar.

'Mheshimiwa naibu sisi wanachama wa maskani ya 'mbili za tosha' tunaahidi tutapiga kura ya ndio kwa katiba inayopendekezwa pamoja na kuhakikishia chama ushindi katika uchaguzi mkuu'alisema.

Katika sherehe hizo Vuai alipandisha bendera katika maskani hiyo pamoja na kutoa jezi seti moja na mipira kwa ajili ya vijana hao ambao wanashiriki katika ligi kuu ya kanda Pemba.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni