Jumapili, 28 Februari 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu waandishi wa habari,
Imekuwa kawaida yetu kukuiteni kila inapotokezea haja ya kufanya hivyo kuzungumzia mambo tofauti, ikiwemo kutoa ufafanuzi au kujibu hoja za wapinzani zinazokigusa chama chetu Chama Cha Mapinduzi. Nichukue fursa hii kuwashukuruni sana kwa ushirikiano mnaotupa. Kwa kweli kila tunapowahitaji mnakuja bila ya kujali shughuli zenu nyengine mlizonazo. Hili linatupa faraja sana na tunaomba tuendelee kushirikiana na hasa katika kipindi hiki ambapo tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa marejeo. 

Ndugu Waandishi, 
Maudhui ya mkutano wetu huu wa leo ni kutoa ufafanuzi kuhusiana na propaganda za uongo zinazosambazwa na Chama Cha Upinanzi cha CUF dhidi ya Chama chetu cha CCM, kama zilivyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Ahmed Nassor Mazrui ambaye amekihusisha Chama chetu na hujuma ya kuchoma moto Tawi la CUF lilioko Dunga Kiembeni na kwamba kitendo hicho kinaweza kuchochea amani na utulivu uliopo. Ndugu Waandishi, Napenda kuchukua fursa hii kuwaambia wananchi lakini hasa CUF kwamba, CCM haina sababu yoyoye ya kukifanyia hujuma chama hicho kutokana sababu nyingi zikiwemo zifuatazo:-
 • Serikali za CCM Tanzania Bara na Zanzibar ndizo zilizokubali kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa. 
• CCM kinauwezo wa kushinda kwa kishindo uchaguzi wa marudio bila ya hujuma, hila wala ghilba zozote.
• CUF ni chama dhaifu kinachoongozwa na kumilikiwa na mtu mmoja kinyume na CCM ambacho ni chama imara na kilichokomaa kisiasa na kimejengeka vyema kiuongozi. 
• CUF hakijawahi na kamwe hakiwezi kukishinda CCM katika uchaguzi ambao ni huru na wa haki.
• CUF ni chama ambacho tayari kimeshaonesha mwelekeo wa kumalizika kisiasa kutokana na kutokuwa na msimamo; kimetangaza kutoshiriki uchaguzi wa marejeo huku wagombea wakihangaika kushawishi wanachama na wafuasi wao kujitokeza kwenda kupiga kura. 

 Hivyo, kauli iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF ya kuihusisha CCM na hujuma dhidi ya Chama hicho haina mashiko na ni msururu wa propaganda za uongo zinazoenezwa na CUF kwa lengo la kujaribu kurejesha imani za wanachama na wafuasi wake, ambao kuna kila dalili zinazoonesha kuchoshwa na ahadi za uongo ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi wao.

Aidha, shutuma hizo zinalenga kukipaka matope Chama Cha Mapinduzi na Serikali mbele ya Jumuiya ya kimataifa, na wakati huo huo kuishawishi Jumuiya hiyo kuamini kwamba CUF hakitendewi haki Zanzibar. Mazrui ameonya na kutahadharisha kuwa iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa, vitendo hivyo vya hujuma wanavyofanyiwa CUF vinaweza kuchochea uvunjifu wa amani na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ndugu Waandishi, 
Naomba nichukue fursa hii kumtoa wasi wasi kiongozi huyo wa CUF na wananchi wote kwa jumla kwamba CCM ni chama mahiri sana na kwamba Serikali zake zote mbili; ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hii ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa muda wa miaka 52 sasa kimejijengea sifa kubwa ya kulinda amani, utulivu na pia kuheshimu haki za binadamu. CCM kimekuwa chama cha kupigiwa mfano miongoni mwa vyama vilivyoleta ukombozi katika Bara la Afrika. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Amiri jeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi na Usalama ameshawahakikishia watanzania kuwa ni jukumu lake kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo nchini kote Bara na Zanzibar. Aidha, kauli kama hiyo imekuwa ikirejewa mara kadhaa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.Lakini CCM na wananchi wengi wa Zanzibar wamekuwa wakijiuliza masuala mengi juu ya dhamira ya kweli ya Chama hicho cha CUF kudumisha amani na utulivu kwani kauli na vitendo vya viongozi wa chama hicho havioneshi dhamira hiyo. Tokea kumalizika kwa uchaguzi mkuu kumekuwa na matukio mengi yanayofanywa na chama hicho ambayo moja kwa moja yanaashiria uvunjifu wa amani ya nchi. 
Kwa mfano; 
 • kitendo cha Maalim Seif kujitangaza Urais tarehe 26 Oktoba, 2015 kabla ya kura hizo kuhakikiwa na kutangazwa na Tume ni kinyume na sheria ya uchaguzi ya Zanzibar na kingeweza kuleta mtafaruk wa kisiasa.
 • Kitendo cha Maalim Seif kutoa shinikizo kwa Tume kumtangaza yeye kuwa mshindi kutokana na matokeo aliyokuwa nayo yeye mikononi hakikuwa kitendo cha kikawaida
 • Kitendo cha kumpa muda wa saa 24 Rais wa nchi kuondoka madarakani ni jambo kubwa kiusalama na kisheria, na kwa vyovyote haliwezi kumithilishwa na kitendo cha kuchoma moto tawi la chama cha siasa hata kama lingefanywa na mfuasi wa chama chochote cha siasa.
 • Yapo matukio mengine mengi ya hujuma yanayotishia amani ambayo yamefanywa na CUF katika kijiji cha Tumbatu, Kengaja Pemba na sehemu nyingi. Pamoja kutiliwa alama za X katika baadhi ya Nyumba za wanachama wetu huko Pemba Ni dhahiri mambo hayo yalihitaji busara na uvumilivu mkubwa kisiasa na kiutawala. 

Ndugu Waandishi,
Katika kipindi hiki tokea kufanyika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015 uliofutwa, CCM imeshuhudia mambo ya aibu na ya ajabu ya uvunjifu wa sheria yaliyofanywa na watu wenye akili timamu walioshiriki kwenye uchaguzi na vile vile waliopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi. Tunatangaza rasmi kwamba Chama Cha Mapinduzi kinasubiri wakati muwafaka, kimedhamiria kuzishinikiza mamlaka zote husika kuhakikisha kuwa zinawatafuta popote walipo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, wale wote waliohusika kuharibu uchaguzi uliofutwa na kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha za wananchi kwa ajili ya uchaguzi wa marejeo. Iwapo kweli nchi hii imeamua kufuata utawala wa sheria na demokrasia, haiwezekani hata siku moja watu wanaofanya makosa makubwa ya jinai kuachwa kudunda mitaani na wengine masikini, wanyonge wa Mungu kupewa adhabu kali ikiwemo kuswekwa makorokoroni. 

Mwisho, tunachukua fursa hii kuwaomba wanachama wetu wote wa CCM na Wananchi kwa jumla, wapenda amani na utulivu waendelee kuwa watulivu, kujiweka tayari na hatimaye wajitokeze kwa wingi kwenye uchaguzi wa marudio, ili kukiletea ushindi wa kishindo Chama Cha Mapinduzi. Aidha, wajiepushe na vitendo vyenye mwelekeo wa uvunjifu wa amani, Umoja na Mshikamano wetu. Naomba kuwasilisha.

Jumatatu, 22 Februari 2016

DR SHENI ASEMA MUUNGANO NA MAPINDUZI KWANZA MENGINE YATASUBIRI.

Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Jumuiya ya Umoja wa Vijana UVCCM Mkoa wa Mjini kichama leo katika ukumbi wa CCM Amani Mjini Unguja na kuwataka Vijana kulinda Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar,ikiwa ni katika hatua za uimarishaji wa Chama cha Mapinduzi kuelekea uchaguzi wa marudio wa Machi 20, 2016.

Jumatano, 10 Februari 2016

CCM YALAANI KUCHOMWA MOTO TAWI LAKE PEMBA

Na: Ally Ndota
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimelaani vikali kitendo cha kuwekwa alama ya X nyumba kadhaa za wafuasi wake Kisiwani Pemba hivi karibuni.

Aidha, kimesikitishwa na kulaani vikali kitendo cha kuchoma moto Tawi la CCM la Kengeja, kilichofanywa na watu wasiojulikana usiku wa kumkia leo.  

Hayo yamesema na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Bibi Waride Bakari Jabu, alipokuwa akizungumza na Wanahabari hapo Afisini kwake  Kisiwandui, Mjini Unguja.

Amesema kitendo cha kuweka  alama ya X kwenye nyumba za wafuasi wa CCM pekee katika maeneo ya Mtambile, Kengeja, Minazini na Kangani Wilayani Mkoani sio tu kina lengo la kuvunja amani iliyopo nchi bali pia  kinakwenda kinyume na sheria na taratibu za Taifa letu.

“Kwa niaba ya CCM nachukua nafasi hii kulaani vikali na kuwataka wale wote waliohusika na vitendo hivyo, waache mara moja, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria na taratibu za nchi yetu” na kuongeza kusema kuwa kinapaswa kulaaniwa na kila mpenda amani na ustawi wa demokrasia ya kweli nchini”. Alidai Bi. Waride.

Ametoa wito kwa Wazanzibari hasa wafuasi wa CCM kupuuza vitendo hivyo, na badala yake waelekeze nguvu zaidi katika maandalizi ya uchaguzi wa marudio uliotangazwa kufanyika Machi 20, ili kukiletea ushindi wa kishindo Chama hicho (CCM).

Kuhusu kuchomwa moto Tawi la CCM Kengeja, Bibi Waride amesema Chama Cha Mapinduzi kimeshtushwa na kitendo hicho, kwani sio tu kinarejesha nyuma maendeleo ya chama, bali pia kinawatia hofu wana CCM wa maeneo husika.

Amesisitiza haja kwa Vyombo vya Ulinzi hasa Jeshi la Polisi kuwatafuta wale wote waliohusika na hujuma hiyo, na kuwafikisha mbele ya  Vyombo vya Dola ili Sheria iweze kuchukua mkondo wake.