Jumanne, 29 Agosti 2017

DKT. MABODI "Miradi inayopeleka majimboni iwanufaishe wananchi wote."

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka  wabunge, wawakilishi na madiwani kuhakikisha miradi wanayopeleka majimboni inawanufaisha wananchi wote.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dkt. Abdulla Juma  Mabodi wakati akikabidhi matrekta madogo ya mkono (Power tillers) mbili na mashine ya umeme wa solar moja kwa wakulima wa jimbo la Chaani zilizotolewa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Nadir Abdul-Latif Yussuf.

Dkt. Mabodi alisema ahadi zinazotekelezwa na viongozi mbali mbali wa majimbo nchini ni lazima ziwanufaishe wananchi wote ili kufikia malengo ya mapinduzi kwa vitendo.

Alieleza kuwa vifaa hivyo vya kilimo vilivyotolewa na mwakilishi huyo vinatakiwa kutumiwa vizuri na wakulima ili visaidie shughuli za kilimo katika jimbo hilo.

Aidha Dkt. Mabodi aliwasisitiza viongozi na watendaji wapya waliochaguliwa katika uchaguzi unaoendelea hivi sasa ndani ya chama na jumuiya zake kufanya kazi za taasisi hiyo kwa bidii ili  chama hicho kiweze kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.

“ Nawapongeza viongozi wanaotekeleza Ilani ya Uchaguzi  wa CCM ya mwaka 2015/2020 kwa kasi ili wananchi waweze kunufaika na fursa  mbali mbali za maendeleo zinazofanywa na viongozi wao.”, alisema Mabodi.

Naye  Mwakilishi  wa Jimbo  hilo ,  Nadir Abdul-Latif Yussuf alisema vifaa hivyo vilivyokabidhiwa vyenye thamani ya shilingi milioni 21 ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi alizotoa kwa wananchi wa jimbo hilo wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita.

Nadir aliwapongeza wananchi wa jimbo hilo kwa kumuunga mkono katika masuala mbali mbali ya kijamii hali inayompa nguvu za kuendelea kutatua kero zinazowakabili katika nyanja za kijamii na kiuchumi.

Alisema lengo la kutoa vifaa hivyo kwa wananchi wa jimbo hilo ni kupunguza changamoto za upungufu wa pembe jeo za kilimo zilizokuwa zikiwakabili wakulima wa jimbo hilo kwa muda mrefu.Jumapili, 27 Agosti 2017

Dk. Ali Mohamed Shein, apongeza juhudi zinazochukuliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amepongeza juhudi zinazochukuliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), katika kuuimarisha umoja huo na kusisitiza kuwa kuna kila sababu ya kuendelea kuunga mkono kwa nguvu zote ili uzidi kupata mafanikio.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo katika hafla ya chakula cha hisani cha kuchangia mfuko wa Maendeleo ya Umoja wa Wanawake Tanzania, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, kikwajuni mjini Unguja.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Kamati iliyoratibu shughuli hiyo chini ya Mwenyekiti wake Dk. Maua Abeid Daftari na Makamo wake Mahmoud Thabit Kombo kwa kufanikisha hafla hiyo na kuweza kufikia lengo lililokusudiwa.

Katika hotuba yake fupi mara baada ya harambee hiyo, Dk. Shein alieleza kuvutiwa kwake na harambee hiyo ilivyoendeshwa vizuri sambamba na mnada wa vitu mbali mbali zikiwemo picha za kuchora kwa mkono ikiwemo picha ya Rais Dk. Shein na ile ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.

Aliwapongeza waalikwa kwa kuchangia na kueleza kuwa wamethitisha usemi usemao ‘kutoa ni moyo na si utajiri’ huku akiamini kuwa dhamira ya Umoja huo itafikiwa kutokana na malengo yao ya kuchangisha milioni 300 ambapo baada ya harambee hiyo fedha zilizopatikana zilivuka kiasi hicho za fedha.

Akitangaza fedha zilizopatikana katika michango ya hafla hiyo Dk. Shein alizitaja kuwa ni TZS milioni 300,752,000 ambapo fedha zilizopatikana katika harambee kabla ya kuingiza mchango wake zilikuwa ni TZS 290,752,000 na baada ya yeye pamoja na Mama Shein kuchagia milioni 10 taslim zilifikia kiwango hicho na kuvuka lengo lililokusudiwa na Umoja huo za kupata milioni 300 katika harambee hiyo.

Akichanganua fedha hizo, Dk. Shein alisema kuwa katika mnada wa vitu mbali mbali vilivyouzwa ukumbini hapo fedha zilizopatikana ni TZS 69,600,000 ambapo michango iliyopitia Benki pamoja na fedha taslim ni TZS  221,152,000. 

Mapema Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa (UWT) kwa upande wa Zanzibar Tunu Juma Kondo alimpongeza Dk. Shein kwa kuendelea kuwajali wanawake sambamba na kuwaunga mkono katika harakati zao za kujiletea maendeleo.

Kondo alisema kuwa hatua yake hiyo ni muendelezo wa nia yake njema ya kuona wanawake wanafanikiwa katika kujiletea maendeleo huku akitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa jinsi Dk. Shein anayotekeleza kwa vitendo tena bila ya ubaguzi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Kaimu Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza lengo lao la kukusanya TZS milioni 300 katika harambee hiyo ili ziweze kuchangia katika mfuko wao wa maendeleo.  

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya shughuli hiyo, Dk. Maua Abeid Daftari, ambaye pia ni Mshauri wa Rais Pemba alitoa pongezi kwa niaba ya Kamati yake kwa miongozo na busara walizozipata kutoka kwa Dk. Shein ambazo zimeweza kuwafikisha katika malengo waliyoyakusudia.

Aliongeza kuwa jumuiya ya UWT imekuwa na mapenzi makubwa kwa Dk. Shein kutokana na juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi wote bila ubaguzi hatua inaonesha kuwa mbali ya wanawake wa Tanzania na hata wanaume wa Tanzania nao wanaridhika na uongozi wake na kuahidi kuendelea kumuunga mkono.

Aidha, Dk. Daftari alieleza kuwa Umoja huo utaendelea kumuunga mkono Dk. Shein kwani wanaridhika na utendaji wake wa kazi huku akitoa pongezi kwa Mama Mwanamwema Shein kwa kuendelea kuunga mkono Umoja huo kwa hali na mali.

Akitoa neno la shukurani Katibu Mkuu wa UWT Amina Makilagi aliwahakikishia wachangiaji wote waliouchangia Umoja huo katika hafla hiyo kuwa fedha zilizopatikana zitafanyiwa yale yote yaliokusudiwa.

Katika hafla hiyo, kundi la Taraab la Culture lilitoa burudani ya pekee kwa nyimbo zake mbali mbali zikiwemo nyimbo laini sambamba na zile za asili zilizoipelekea hadhira kushindwa kutulia katika viti vyao na hasa pale ilipoimbwa nyimbo ya “Mpewa hapokonyeki”.Jumatano, 23 Agosti 2017

Majengo na Matawi ya CCM, Yaendane na kasi ya chama


MAKAMO Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema lazima majengo na matawi ya CCM, yaendane na kasi ya chama hicho kwa kujenga majengo ya kisasa.

Alieleza kuwa wakati wa uongozi wa Chama cha ASP na TANU, wanachama na viongozi wa vyama hivyo, walijitahidi kujenga majengo, ambayo kwa sasa yamerithiwa na CCM, hivyo lazima kuwe na majengo yanayofanana na wakati uliopo.

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, alieleza hayo kwenye tawi la CCM la Pandani Jimbo la Mgogoni, kabla ya kuweka jiwe la msingi la tawi hilo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake kiswani Pemba kwa  kuangali utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Alisema, huu ni wakati wa CCM, hivyo majengo yaliorithiwa kutokwa kwa ASP kwa Zanzibar na TANU kwa Tanzania bara kama hayaendani na kasi, ni vyema yakajengwa mengine ili yafanane na wakati na hadhi iliopo.

Alieleza kuwa, ujenzi wa tawi hilo jipya uliofanywa na wanaCCM wenyewe na viongozi wao wengine, unafaa kuungwa mkono na kila mmoja, maana wajenzi wa matawi hayo ni wanaCCM wenyewe, kama walivyofanywa waasisi wa chama hicho kutoka TANU na ASP kwa wakati wao.

“Wana wa ASP na TANU, walijenga matawi ya chama kwa njia ya kuchangishana, na leo hii tumeyarithi tukiwa na CCM, hivyo lazima na sisi tuliopo ndani ya CCM, tujenge majengo ya kisasa, ili yafanane na hadhi na ukubwa wa chama chetu”,alieleza.

Katika hatua nyengine, Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, amemshauri Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mberwa Hamad Mberwa, kuhakikishga shilingi milioni 26, zinapatikana.
Alisema kwa vile taarifa ya ujenzi inaonyesha bado shilingi milioni 36 ili kukamilisha ujenzi huo hadi kuhamia, yeye atawasilisha shilingi milioni 10, na fedha nyengine zilizobakia lazima uongozi wa mkoa uzipate kwa kuchangishana ilikulijenga tawi hilo.

Alifahamisha kuwa, kwa upande wa Mwakilishi wa Jimbo la Mgogoni Shehe Hamad Matari, ameshajitahidi kuchangia asilimia 75 ya gharama zilizofikiwa, hivyo ni vyema na uongozi wa Mkoa huo, kuhakikisha unazipata fedha nyengine.

“Mwenzetu Mwakilishi wa Jimbo hili la Mgogoni, ameshajitolea na sasa na wewe Mwenyekiti wa CCM Mkoa lazima shilingi ,milioni 26, zitafuteni na zangu shilingi milioni 10 zipo, wakati wowote hata leo”,alisisitiza.

Wakati huo huo, Dk Shein alizindua jengo jipya la skuli la madarasa manne ya Mgogoni, na kuwataka wanafunzi kusoma na kueleza kuwa kazi iliopo mbele yao ni kusoma na sio vyenginevyo, kwani elimu ndio msingi wa maisha yao ya baadae.

Aidha aliendelea na kauli yake, ya kuwataka waalimu kuingia madarasani na kuwasomesha wanafunzi hao, na kuweka kando siasa zao wanapokuwa madarasani. “Tumeshawawekea mazingira mazuri ya kusomesha kwa ufunguzi wa jengo jipya, sasa acheni siasa ingieni madarasani kwa wakati ili kuwapa vijana elimu”,alifafanua.

Hata hivyo, aliendelea na msimamo wake wa kumtaka Mkuu wa Mkoa kufanya ziara za mara kwa mara kwenye skuli mbali mbali, na iwapo watawabaini waalimu watoro awasiliane na Waziri husika, kwa hatua.

Aliongeza kuwa yeyote aliyekuwa hawezi kusomesha aseme kwani kuna kundi kubwa la walimu waliomaliza masomo katika vyuo vikuu vya hapa nchini na bado hawajaajiriwa. Pia, aliwasisitiza wasichanganye elimu na siasa wakati wakiwasomesha wanafunzi na kuwaeleza walimu kuwa wawasomeshe wanafunzi kama walivyosomeshwa wao.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Khadija Bakari alisema kuwa ujenzi wa madarasa hayo ulianza kwa nguvu za wananchi mnamo mwaka 2010 waliochangia TZS milioni 7.5 na baadae Serikali ikamalizia kwa kiasicha TZS milioni 64.6 na hadi kukamilika zimetumika TZS milioni 72.4. 

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Riziki Pembe Juma, alisema kuwa anajiskia faraja kuona rais huyo, anazindua majengo mapya ya skuli, ambapo hiyo ni ishara ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Mapema Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri asiekuwa na wizara Maalum Said Soud Said, alisema ujenzi wa masoko na skuli ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, chama ambacho ndio kilichoshinda kwenye uchaguzi mkuu.

“CCM ndio chama kilichoshinda na mimi na mwengine yoyote lazima atekeleze Ilani yake, na asietaka akae pembeni, maana uchaguzi mwengine hakuna hadi mwaka 2020”,alifafanua  Said Soud.

Nao viongozi wakiwemo Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Washauri wa Rais, Makatibu Wakuu nao waliwasisitiza wanafunzi kusoma kwa juhudi na Serikali yao itaendelea kuwaunga mkono kwa kuwajengea majengo bora ya skuli ili kuwapa elimu bora. 

Akiwa kwenye ukaguzi wa ununuzi wa karafuu kwenye kituo cha ZSTC Bandarini Wete, Rais Dk. Shein, ameutaka uongozi wa ZSTC, kuhakikisha karafuu zilizokamatwa kutoka Mkoani Tanga, hazichanganywi na karafuu za Zanzibar. 

Aidha, aliutaka uongozi wa Mkoa wa kaskazini Pemba, kufauta taratibu za kisheria juu ya chombo aina ya jahazi kilichokamatwa hivi karibuni na karafuu zilizodaiwa kutaka kusafirishwa kimagendo.

Dk. Shein aliutaka uongozi wa Polisi katika Mkoa huo kumpa taarifa ndani ya wiki mbili juu ya hatua zilizofikiwa kwa watu waliotajwa ambao wamekimbia baada ya chombo chao kukamatwa kikiwa kinasafirisha karafuu kwa njia ya magendo. 

Rais Dk Ali Mohamed Shein, ataendelea na ziara yake ya siku tano kisiwani Pemba, kwa kumalizia Mkoa wa kusini Pemba, ambapo awali, atapokea taarifa ya kikazi ya mkoa huo, ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi.

Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar akisalimia na Mwenyeji wake Ndg. Haji Mkema mara tu baada ya kuwasili Pandani ambao Mhe. Rais ataweka jiwe la Msingi katika Tawi la CCM la Pandan
Waziri wa Fedha Dkt. Khalid akijitambulisha mbele ya wananchi, walimu na wanafuzi wa skuli ya mgogoni


Mhe. Rais akiwasili hapo Junguni kwa ajili ya uzinduzi wa kituo kipya cha Afya ya Mama na Mtoto

Dkt. Shein akisalimiana na baadhi na watumishi na wageni mbali mbali mara tu baada ya kuwasili hapo junguni
Dkt. Shein akisalimiana na baadhi na watumishi na wageni mbali mbali mara tu baada ya kuwasili hapo junguni
Dkt. SHEIN akizindua rasmi kituo cha afya ya mama na mtoto hapo junguni
Mhe. Rais akisalimia na Viongozi mbali mbali mara tu baada ya kufika hapo Bandarini wete kwa leongo la kuangalia shughuli zaununuzi wa zao la karafuu