Alhamisi, 17 Agosti 2017

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein ameutaka Uongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja kutangaza na kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuenzi dhana ya Utalii kwa wote.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein ameutaka Uongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja kutangaza na kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuenzi dhana ya Utalii kwa wote. Kauli hiyo aliitoa katika majumuisho ya ziara ya Mkoa huo iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), alisema dhana ya utalii wa ndani ni muhimu kuendelea kutangawa kwani imebeba fursa zitakazoongeza pato la taifa kupitia sekta ya utalii nchini. 

 Dkt. Shein alipongeza hatua za maendeleo zilizofikiwa na Mkoa huo katika sekta za kilimo, utalii, afya, miundombinu na hatua zilizowekwa za kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabia nchi. Kupitia majumuisho hayo Dkt. Shein aliwaagiza Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga utamaduni wa kutembea vijijini kwa lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya fursa zinazopatikana katika wizara hizo ili wananchi wazifahamu na kuzichangamkia. “ Bado kuna wananchi hawajui kama serikali ina mfumo wa uwezeshaji unatoa mikopo kwa wajasiriamali na vikundi vingine vyenye malengo ya kujikomboa kiuchumi, na hadi hivi sasa tayari zaidi ya bilioni mbili wamekopeshwa wananchi wa maeneo mbali mbali hapa nchini”, alieleza Dkt. Shein na kuitaka Wizara ya kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibar kutangaza kuwafikia wananchi wa vijijini ili wanufaike na mfuko huo. Dkt. Shein aliwapongeza wakulima wa zao la ndimu ndani ya mkoa huo na kuitaka Wizara inayohusika na masuala ya kilimo kutumia wataalamu wake kuwafundishe wananchi mbinu bora za kilimo cha kisasa. 

 Hata hivyo alisema licha ya Mkoa huo kupata mafanikio mbali mbali bado wanatakiwa kuzidisha bidii katika kudhibiti vitendo vya magendo ya bidhaa mbali mbali vinavyoikosesha serikali mapato. Dkt. Shein ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alizindua jengo la Tawi la CCM Kizimkazi Dimbani ndani ya Mkoa huo, na kuwasihi viongozi wa chama hicho kutumia vikao vya kikatiba wakati wa kufanya maamuzi yanayohusu taasisi hiyo badala ya kufanya maamuzi binafsi.

 Aliwasihi wazee wa CCM kuendeleza utamaduni wa kuwafundisha itikadi vijana ili waweze kujua historia ya chama na nchi ilipotoka kabla na baada ya mapinduzi ya mwaka 1964. Aliwambia wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kuwa Chama cha Mapinduzi kinapoahidi kinatekeleza kwa wakati kwani miradi yote inayozinduliwa hivi sasa imetokana na usimamizi mzuri wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2016. 

Ziara hiyo ya siku mbili katika Mkoa wa Kusini, Dkt. Shein alikagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu katika kijiji cha Kitogani, alitembelea wajasiriamali wa Saccos ya AMCO na kuona mazao wanayozalisha yakiwemo Matikiti maji, mihogo, ndimu na Tungule huko Mtule kijiji cha Paje. Miradi mingine iliyotembelewa na Dkt. Shein ni kukagua mradi wa kisima cha maji safi na salama huko katika mapango ya Mnywambiji pamoja na kuweka jiwe la msingi katika nyumba za kuishi za madaktari wa Vituo vya Afya vya Kajengwa na Muyuni ‘B’ Wilaya ya Kusini Unguja.

















Hakuna maoni:

Chapisha Maoni