Jumapili, 27 Agosti 2017

Dk. Ali Mohamed Shein, apongeza juhudi zinazochukuliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amepongeza juhudi zinazochukuliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), katika kuuimarisha umoja huo na kusisitiza kuwa kuna kila sababu ya kuendelea kuunga mkono kwa nguvu zote ili uzidi kupata mafanikio.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo katika hafla ya chakula cha hisani cha kuchangia mfuko wa Maendeleo ya Umoja wa Wanawake Tanzania, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, kikwajuni mjini Unguja.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Kamati iliyoratibu shughuli hiyo chini ya Mwenyekiti wake Dk. Maua Abeid Daftari na Makamo wake Mahmoud Thabit Kombo kwa kufanikisha hafla hiyo na kuweza kufikia lengo lililokusudiwa.

Katika hotuba yake fupi mara baada ya harambee hiyo, Dk. Shein alieleza kuvutiwa kwake na harambee hiyo ilivyoendeshwa vizuri sambamba na mnada wa vitu mbali mbali zikiwemo picha za kuchora kwa mkono ikiwemo picha ya Rais Dk. Shein na ile ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.

Aliwapongeza waalikwa kwa kuchangia na kueleza kuwa wamethitisha usemi usemao ‘kutoa ni moyo na si utajiri’ huku akiamini kuwa dhamira ya Umoja huo itafikiwa kutokana na malengo yao ya kuchangisha milioni 300 ambapo baada ya harambee hiyo fedha zilizopatikana zilivuka kiasi hicho za fedha.

Akitangaza fedha zilizopatikana katika michango ya hafla hiyo Dk. Shein alizitaja kuwa ni TZS milioni 300,752,000 ambapo fedha zilizopatikana katika harambee kabla ya kuingiza mchango wake zilikuwa ni TZS 290,752,000 na baada ya yeye pamoja na Mama Shein kuchagia milioni 10 taslim zilifikia kiwango hicho na kuvuka lengo lililokusudiwa na Umoja huo za kupata milioni 300 katika harambee hiyo.

Akichanganua fedha hizo, Dk. Shein alisema kuwa katika mnada wa vitu mbali mbali vilivyouzwa ukumbini hapo fedha zilizopatikana ni TZS 69,600,000 ambapo michango iliyopitia Benki pamoja na fedha taslim ni TZS  221,152,000. 

Mapema Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa (UWT) kwa upande wa Zanzibar Tunu Juma Kondo alimpongeza Dk. Shein kwa kuendelea kuwajali wanawake sambamba na kuwaunga mkono katika harakati zao za kujiletea maendeleo.

Kondo alisema kuwa hatua yake hiyo ni muendelezo wa nia yake njema ya kuona wanawake wanafanikiwa katika kujiletea maendeleo huku akitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa jinsi Dk. Shein anayotekeleza kwa vitendo tena bila ya ubaguzi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Kaimu Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza lengo lao la kukusanya TZS milioni 300 katika harambee hiyo ili ziweze kuchangia katika mfuko wao wa maendeleo.  

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya shughuli hiyo, Dk. Maua Abeid Daftari, ambaye pia ni Mshauri wa Rais Pemba alitoa pongezi kwa niaba ya Kamati yake kwa miongozo na busara walizozipata kutoka kwa Dk. Shein ambazo zimeweza kuwafikisha katika malengo waliyoyakusudia.

Aliongeza kuwa jumuiya ya UWT imekuwa na mapenzi makubwa kwa Dk. Shein kutokana na juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi wote bila ubaguzi hatua inaonesha kuwa mbali ya wanawake wa Tanzania na hata wanaume wa Tanzania nao wanaridhika na uongozi wake na kuahidi kuendelea kumuunga mkono.

Aidha, Dk. Daftari alieleza kuwa Umoja huo utaendelea kumuunga mkono Dk. Shein kwani wanaridhika na utendaji wake wa kazi huku akitoa pongezi kwa Mama Mwanamwema Shein kwa kuendelea kuunga mkono Umoja huo kwa hali na mali.

Akitoa neno la shukurani Katibu Mkuu wa UWT Amina Makilagi aliwahakikishia wachangiaji wote waliouchangia Umoja huo katika hafla hiyo kuwa fedha zilizopatikana zitafanyiwa yale yote yaliokusudiwa.

Katika hafla hiyo, kundi la Taraab la Culture lilitoa burudani ya pekee kwa nyimbo zake mbali mbali zikiwemo nyimbo laini sambamba na zile za asili zilizoipelekea hadhira kushindwa kutulia katika viti vyao na hasa pale ilipoimbwa nyimbo ya “Mpewa hapokonyeki”.























Hakuna maoni:

Chapisha Maoni