KAMATI Kuu ya CCM Zanzibar
imemteuwa Juma Ali Juma kuwa mgombea Ubunge kwa Tiketi ya
Chama hicho katika Jimbo la Dimani, Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai
Ali Vuai aliwambia waandishi wa Habari kuwa uamuzi huo umefikiwa katika kikao
cha Kamati hiyo iliyokutana jana chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Makamo
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein.
Alisema Kikao hicho ambacho
kilikasimiwa madaraka na kikao Cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya kufanya uamuzi
huo, na wajumbe walipitia mapendekezo yaliyotolewa na vikao vya ngazi ya jimbo,
wilaya na Mkoa juu ya wanachama 25 waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.“ kikawaida halmashauri kuu ya taifa
ndiyo inayofanya uteuzi wa mwisho, lakini ilikasimu madaraka yake kwa
kamati maalum baada ya kuomba ili kwenda na wakati uliopangwa.
Pia baada ya taratibu zote kwa ngazi
husika kukamilisha hatimaye Kamati Maalum imefanya maamuzi ya mwisho ya kumpata
Mgombea atakayeweza kupeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi mdogo wa Jimbo
la Dimani Unguja,”. Alisema Vuai na kuongeza kuwa kazi iliyobaki kwa Sasa
ni Wana CCM na Wananchi kwa ujumla wanaopenda maendeleo ya jimbo hilo kumuunga
mkono mgombea huyo ili apate kushinda kwa kishindo .
Alieleza kuwa pamoja na wagombea wote
waliochukua fomu kuomba nafasi hiyo walikuwa na sifa lakini kutokana na
utaratibu wa CCM umemteuwa mgombea mmoja ambaye atakayeweza kutumia tiketi ya
Chama hicho katika uchaguzi huo na wagombea wengine ambao hawakubahatika kupata
nafasi hiyo wasikate tamaa badala yake waendelee kukiunga mkono chama.
Vuai alieleza kuwa matarajio ya CCM
katika Uchaguzi huo ni mgombea wa Chama hicho kushinda kwa kura nyingi kwani
ana sifa na vigezo vinavyotakiwa na wananchi wa jimbo hilo ikiwemo uaminifu,
weledi, utendaji bora na hana sifa za ufisadi wala tuhuma yoyote mbaya kwa
jamii.
Aliongeza kwamba jukumu la kampeni za
Uchaguzi wa jimbo hilo utasimamiwa na Mkoa wa Magharibi kwa kushirikiana na Afisi
Kuu CCM Zanzibar ili kuhakikisha mgombea wake anashinda na kuendelea kuandika
historia ya CCM katika uwanja wa siasa za ndani na nje ya nchi.
Aidha aliwasihi wafuasi wa chama
hicho na wananchi kwa ujumla kukiunga mkono chama hicho kuanzia kampeni hadi Uchaguzi
kwa lengo la kuhakikisha CCM inashinda ili iweze kuendeleza utekelezaji mzuri
wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2016 katika jimbo hilo.
Akijibu hoja za baadhi ya waandishi wa
Habari kuhusu ushiriki wa Chama cha CUF chini ya mwavuli wa UKAWA katika Uchaguzi
wa Jimbo hilo, Vuai alifafanua kwamba CCM inafurahi kuwepo na Chama cha
Upinzani katika uchaguzi huo kwani itaongeza ushindani pamoja na hamasa
kwa chama cha mapinduzi kuendelea kufanya siasa za kistaarabu na
kujitathimini kisiasa.
Pamoja na hayo alieleza kuwa viongozi,
wanachama na watendaji wa CCM wameelimishwa vizuri juu ya kuepuka athari za
makundi baada ya kumalizika hatua ya kura za maoni ambapo kwa sasa
wanachama wote wanasimama kwa timu moja ambayo ni Chama Chama Mapinduzi kwa
kuhakikisha mgombea aliyeteuliwa anashinda kwa kura nyingi.
Kwa masikitiko makubwa Naibu Katibu
Mkuu huyo alitumia nafasi hiyo kuwaeleza waandishi wa habari juhudi
zilizofanywa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Marehemu Hafidh Ali Tahir kuwa
alikuwa ni kiongozi bora aliyepigania maendeleo ya wananchi wa jimbo lake na
jamii kwa ujumla bila kuchoka.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani unafanyika baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo Hafidh Ali Tahir, kupitia tiketi ya CCM kufariki dunia mapema mwaka huu baada ya kuuguwa ghafla akiwa Mbungeni Dodoma.
Kutokana na kifo
hicho Tume ya Uchaguzi ya Taifa Tanzania (NEC), tayari imetangaza kufanyika kwa
uchaguzi mdogo , January 22 mwakani.
"KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI"
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni