Jumapili, 30 Juni 2019

MHE.BALOZI SEIF ALI IDD AONGOZA HITMA YA DK.BADRIYA-UNGUJA.


 MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd,akiongoza Kisomo cha Hitma ya Marehemu Dk.Badriya Abubakar Gurnah aliyekuwa Mke wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi, kilichofanyika katika Msikiti wa Mwushawal Mwembe Shauri Unguja.

 WAUMINI mbali mbali wa Dini ya Kiislamu wakishiriki Kisomo cha Hitma ya Marehemu Dk.Badriya Abubakar Gurnah, kilichofanyika katika Msikiti wa Mwushawal Mwembe Shauri Unguja.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi, akiwashukru Waumini wa Dini ya Kiislamu wakiwemo Viongozi wa Dini,Serikali,Chama Cha Mapinduzi na Wananchi wote walioshiriki Kisomo cha Hitma ya Mkewe Marehemu Dk.Badriya Abubakar kilichofanyika Msikiti wa Mwushawal Mwembe Shauri Unguja.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi (kulia), akisalimiana na kupewa Mkono wa Pole na Wananchi na Viongozi mbali mbali mara baada ya kumalizika Kisomo cha Hitma katika Msikiti wa Mwushawal Mwembe Shauri Unguja. 

 MKE wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Idd, akijumuika na Wananchi katika kisomo cha Hitma ya Marehemu Badriya Abubakar kilichofanyika kwa upande wa Wanawake Nyumbani kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi, Rahaleo Unguja.


MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, ameongoza Kisomo cha Hitma ya Mke wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi Marehemu Dk.Badriya Abubakar Gurnah kilichofanyika katika Msikiti wa Mwushawal uliopo Mwembe Shauri Unguja.

Kisomo hicho kimeudhuriwa na Waumini wa Dini ya Kiislamu,Viongozi wa Dini,Kiserikali na Chama Cha Mapinduzi pamoja na Wananchi kwa ujumla.

Akitoa Mawaidha Sheikh Norman Jongo, amewasihi Waumini hao kuendelea kumuombea dua mara kwa mara Marehemu Dk.Badriya ili awe miongoni mwa Waja Wema katika Pepo ya Mwenyezi Mungu.

Akitoa shukrani Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi, amewashukru Wananchi walioshiriki katika kisomo hicho na harakati zingine za kumsaidia Dk.Badriya Enzi za Uhai wake.

Sambamba na hayo pia amewashukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Joseph Magufuli kwa mchango walioutoa kabla na baada ya Kifo cha Dk.Badriya.

Wakati huo huo Wananchi,Viongozi wa Dini ya kiislamu, Kiserikali na Chama cha Mapinduzi kwa upande wa Wanawake nao wameshiriki kisomo hicho cha Hitma ya Dk.Badriya Abubakar hapo Nyumbani kwa Dk.Mabodi  Mtaa wa Raha leo Unguja.

Mwenyezi Mungu amlaze mahala Pema Peponi Amin.

Jumamosi, 29 Juni 2019

MHE.ASHA 'MSHUA'- ATAKA WANAWAKE WAWE CHACHU YA USHINDI 2020,ATOA VITENDEA KAZI TSH.MILIONI 1.5

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini Mhe.Asha Abdalla Juma "Mshua' na Katibu wa UWT Wilaya ya Amani Ndugu Asha Mzee wakiwa wamebeba Vitendea kazi vilivyotolewa na Mhe.Asha kwa ajili ya kufanikisha kazi za UWT.

  MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini Mhe.Asha Abdalla Juma "Mshua',akikabidhi Vitendea kazi kwa Katibu wa UWT Wilaya ya Amani Ndugu Asha Mzee ambavyo ni Komputa Moja na Printer Moja ya Kisasa vyenye Thamani ya Shilingi Milioni 1.5

 BAADHI ya Wajumbe wa Baraza la UWT Wilaya ya Amani wakisikiliza nasaha za Mgeni rasmi, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini Mhe.Asha Abdalla Juma "Mshua' 


KATIBU wa CCM Wilaya ya Amani Ndugu Ali Salum Suleiman akitoa shukrani kwa Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Mjini Mhe.Asha Abdalla Juma na kuahidi kuwa miongozo aliyotoa kupitia hotuba yake itafanyiwa kazi kwa Vitendo. 


MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini Kichama Mhe.Asha Abdalla Juma ‘Mshua’,amewataka Wanawake katika Nchini kuamini,kulinda na kuipigania CCM na kuhakikisha inashinda kwa kishindo mwaka 2020 kuliko Chaguzi zote zilizopita toka kuanzishwa Mfumo wa Vyama Vingi Mwaka 1992.

Amesema Serikali za Awamu ya Saba ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini wa Marais wake ambao ni Dk.Ali Mohamed Shein na Dkt.John Pombe Magufuli Viongozi waliosimamia Vyema utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Hayo ameyasema leo wakati akihutubia katika ufunguzi wa Baraza la UWT Wilaya ya Amani kilichofanyika katika Ofisi za Wilaya hiyo Sebleni Amani Unguja.

Mhe.Asha amesema Serikali hizo zimeimarisha Huduma za Afya,Miundombinu ya Barabara,Umeme,Elimu,Mikopo kwa Wanawake yenye masharti nafuu pamoja na kutoa fursa za  Uongozi kwa Wanawake katika Chama na Serikali zote mbili.

Amesema Wanawake wanatakiwa kuunganisha nguvu zao bila ya kujali bila ya kujali tofauti za Vyeo,rangi na kabila wahakikishe CCM inashinda kwa ngazi zote katika Uchaguzi Mkuu ujao, hiyo ndio itakuwa njia pekee ya kuthamini kwa vitendo juhudi zinazofanywa na Serikali.

Kupitia Mkutano huo amewasihi Wajumbe hao kuendeleza Umoja na Mshikamano katika kutekeleza majukumu yao ya kisiasa ndani na nje ya UWT, kwa lengo la kuandaa mazingira rafiki ya kisiasa yatakayoimarisha CCM.

Amesema pamoja na majukumu waliyokuwa nayo Akina Mama hao pia wanatakiwa kuwalea Watoto katika Maadili mema na kuhakikisha Wanakua Salama bila kufanyiwa Vitendo vya Udhalilishwaji.

Akizungumzia suala Uimarishaji wa Chama na Jumuiya hiyo, Mhe.Asha amesisitiza umuhimu wa kuongeza Wanachama Wapya wenye Sifa kisheria za kuipigia kura CCM kwa kila Uchaguzi wa Dola.

“Kila Mwanachama kwa nafasi yake aanze kuwatafuta Wapiga kura Wapya wa makundi yote wenye Sifa za kupiga kura, waelezeni mazuri mengi yanayopatikana ndani ya CCM japokuwa mengi wanayaona na kuyatambua lakini bado tuna jukumu la kuwakaribisha kwa ukarimu kwani CCM ni Chama cha Wote,,,Nyumbani kumenoga.”,amesema Mhe.Asha.

Kupitia Kikao hicho Mhe.Asha,alikabidhi Komputa Moja na Printer Moja ya Kisasa ya rangi zenye Thamani ya Shilingi Milioni 1.5 kwa Uongozi wa UWT Wilaya hiyo ili watekeleze kwa ufanisi shughuli mbali mbali za kiutendaji.  

Naye Katibu wa UWT Wilaya hiyo Ndugu Asha Mzee,akisoma taarifa ya Utendaji wa kazi za UWT, alisema Viongozi,Watendaji na Wanachama wanashirikiana vizuri huku wakijipanga vizuri kukabiliana na dalili zozote za upinzani ili CCM ishinde katika uchaguzi ujao.

Amesema katika mikakati ya kuimarisha Jumuiya wamesimamia vizuri vikao vya ngazi za Matawi hadi Wilaya kuhakikisha vinafanyika kwa mujibu wa Katiba sambamba na kufanya ziara,vikao na mafunzo ya kuwajenge uwezo Akina Mama juu ya masuala mbali mbali ya kisiasa na kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza Mjumbe wa Mkutano huo ambaye pia ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Mgeni Hassan Juma, aliupongeza Uongozi wa Wilaya hiyo kwa kutekeleza masuala ya msingi ya kiutendaji yenye dhamira ya kuimasha UWT na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla.

Kwa upande wake Mjembbe wa Mkutano huo ambaye pia ni Mwakilishi wa Viti Maalum kupitia Mkoa huo Mhe.Saada Ramadhan Mwendwa amesema Mkutano huo ulioambatana na Utoaji wa Mada mbali mbali za kuwajengea uwezo Viongozi wa Baraza hilo ili wakirudi katika maeneo yao watekeleze kwa ufanisi majukumu yao.



  

Jumapili, 16 Juni 2019

NDG.THUWAYBA NA MHE.ANGELINA WAWAPIGA MSASA WANAWAKE WA KASKAKAZINI UNGUJA.

 MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Edington Kisasi akifungua mafunzo ya kuhamasisha daftari la wapiga kura na suala la mikopo kwa wanawake viongozi wa UWT mkoa mkoa wa Kaskazini Unguja. Kulia ni Mbunge wa viti maalumu wa mkoa huo, Angelina Adam Malembekakushoto ni Mwenyekiti wa UWT Mkoani humo Maryam Muharami Shomari


 MBUNGE wa viti maalumu mkoa wa Kaskazini Unguja, Angelina Adam Malembeka (kulia) akihamasisha jambo kwenye mkutano mafunzo ya kuhamasisha daftari la wapiga kura na suala la mikopo kwa wanawake viongozi wa UWT mkoa mkoa wa Kaskazini Unguja. 




 VIONGOZI na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja wametakiwa kuwasaidia viongozi waliochaguliwa kuteleleza ilani na ahadi walizozitoa wakati wa uchaguzi uliopita badala ya kukumbatia wagombea wa uchaguzi ujao.

Akifungua mafunzo ya siku moja yaliyoshirikisha viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa CCM mkoani humo, Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Eddington Kisasi alieleza kuwa kufanya hivyo kunapelekea viongozi waliopo madarakani kushindwa kusimamia ahadi zao.

Alisema wapo baadhi ya viongozi wa chama lkatika ngazi mbali mbali wameanza kuwakumbatia wanachama 'wanaojipitishapitisha' kwa lengo la kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao watambue kuwa kufanya hivyo wakati huu ni kukiuka kanuni za uchaguzi za chama hicho.

Mafunzo hayo yaliyolenga kuhamasisha ujasiriamali na mikopo kwa wanawake na uimarishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yaliandaliwa kwa pamoja kati ya mbunge wa viti maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja Angelina Adam Malembeka na UWT Mkoa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi iliyoagiza kuinuliwa kwa hali za kiuchumi za wanawake katika ngazi zote.

Alisema kanuni za uchaguzi za CCM zinakataza mtu kufanya kampeni kabla ya wakati hivyo viongozi wanaoandaa wagombea na kupanga nao mikakati wanapaswa kujua kuwa wanachochea vurugu ambazo zinakwaza kasi ya utekelezaji wa ilani na kuchelewesha upatikanaji wa maendeleo ya jamii.

"Chama kiliweka muongozo na ndio maana Mwenyekiti wetu (Dk. John Magufuli) alikataza Mambo ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ili tupate kuteleleza ahadi tulizoweka kwa wananchi wetu na nyinyi no mashahidi kwamba kabla ya 2020 tumeshatekeleza ilani kwa zaidi ya asilimia 90 Tanzania bara na Zanzibar", alieleza Kisasi.

Aidha aliwataka viongozi hao kuwa mabalozi wazuri na kuisambaza elimu waliyopatiwa kwa wanachama wenzao kwani yana umuhimu mkubwa katika maendeleo ya jamii na siasa za Tanzania.

"Tuliahidi kuinua uchumi wa wanawake katika ilani ya uchaguzi kupitia njia mbali mbali zikiwemo za ujasiriamali na uanzishwaji wa viwanda hivyo mafunzo haya yana mchango mkubwa katika kuendeleza vikundi vya kiuchumi tulivyonavyo katika shehia, wadi, wilaya na mikoa yetu", alisema Makamu huyo wa Mwenyekiti.

Aidha aliwataka wajasiriamali nchini kutumia fursa ya marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki iliyoanza Juni mosi mwaka huu Tanzania bara, kutengeneza mifuko mbadala ya kubebea bidhaa na kuipeleka huko ili kujiendeleza kiuchumi.

Akizungumzia uimarishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Kisasi aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii kwenda kuhakikisha taarifa zao na kuwasaidia vijana wenye sifa waweze kujiandikisha.

"Utekelezaji wa ibara ya 5 ya katiba ya chama chetu wa kushinda uchaguzi haupo wakati wa uchaguzi pekee bali huanza mapema na huu ndio wakati wake ili kuzichungachunga kura za ushindi wetu ifikapo 2020", alieleza Makamu Mwenyekiti huyo.

Akiwasilisha mada juu ya ujasiriamali na mikopo Mkurugenzi wa taasisi inayojihusisha na elimu ya ujasiriamali na utoaji wa mikopo ya jijini Dar es salam Nickson Martin alisema ili kuwa na uzalishaji wenye tija ipo haja ya wajasiriamali kuzingatia elimu na uwekaji kumbukumbu za biashara zao kujua maendeleo ya shughuli zao.

"Ni lazima mkubali kubadilika na kuweka mikakati kuzifikisha ndoto zenu na za serikali yetu ya kuimarisha uchumi wa watu wake kupitia uchumi wa viwanda", alisema Nickson.

Nae Katibu Msaidizi wa CCM mkoani humo Shafi Hamad Ali akiwasilisha mada ya umuhimu wa daftari la kudumu alisema viongozi wa ngazi zote za chama hicho wanapaswa kujidhatiti na kuhakikisha wanatekeleza maagizo na maelekezo ya chama kama inavyoelekezwa na katiba ya CCM na ya jumuiya zake.

"Msingi wa ushindi katika uchaguzi wa chama chetu ni umoja na mshikamano na ndio maana sote tunawajibika kuhakikisha chama kinashinda katika chaguzi za kutafuta dola na daftari ndio chanzo cha ushindi siku zote", alisema Shafi.

Akitoa shukran za washiriki wa mafunzo hayo Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja Angelina Adam Malembeka alieleza kuwa ataendelea kuwatafutia wanawake wa mkoa huo fursa za kujikomboa kiuchumi ili waweze kujitegemea na kusaidia maendeleo ya familia zao.

Alisema iwapo wanawake hao watatumia kikamilifu fursa za mikopo inayotolewa na taasisi za serikali na za binafsi wanaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda.

Alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo aliyowahi kuwapatia wananchi wa mkoa huo kwsa kushirikiana na wadau mbali mbali ambapo hapo awali makundi mbali mbali ya wanawake yalipatiwa mafunzo ya utengenezaji chaki na mishumaa ili kujiongezea kipato.

"Baada ya kupata mafunzo yale nimeona nije na haya ya kuwaonesha fursa za kuendeleza miradi yetu ili siku moja tuwe na viwanda vidogo vidogo na vya Kati, hapo tutakuwa tumejikomboa kiuchumi kweli kweli", alisema Malembeka.

Alizungumzia mafunzo hayo mmoja ya washiriki wa mafunzo hayo ambae ni Katibu wa UWT jimbo la Kijini Maryam Rashid Mussa alisema yamewasidia kuziona na kutambua fursa za misaada na kwamba watayatumia kuimarisha mitaji yao na chama kwa ujumla.

Mafunzo hayo yalishirikisha jumla ya viongozi wajumbe wa mkutano mkuu wa mkoa  huo 120 yalifungwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa anaetokea jumuiya ya wazazi Tanzania Suleiman Juma Kimea ambae aliwasisitiza washiriki mafunzo hayo kusimamamia misingi na maadili ya chama hicho ili kuepuka mizozo isiyo ya lazima.

NDG: ZAINAB: ATAKA NGAZI ZA WADI ZA UWT ZIFANYE VIKAO.



 MWENYEKITI wa UWT Mkoa wa Magharibi Unguja Ndugu Zainab Ali Maulid,akiwahutubia Wajumbe wa Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe mara baada ya kufungua Kikao cha Baraza hilo kwa niaba ya Wadi 14 za UWT za Wilaya ya Dimani zilizofanya Vikao leo Tarehe 16/06/2019.
 
 KATIBU wa UWT Wadi ya Mwanakwere Ndugu Khadija Seif akisoma Taarifa ya Utendaji wa Majukumu mbali mbali ya Wadi hiyo mara baada ya kufunguliwa kwa Kikao hicho cha Baraza la UWT ngazi ya Wadi huko katika Ukumbi wa Mikutano wa Tawi la Mwanakwerekwe 'A'.

 WAJUMBE wa Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe wakisikiliza nasaha zinazotolewa na Viongozi wao kupitia Kikao hicho.

 MJUMBE wa Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe ambaye pia ni Mwakilishi wa Viti Maalum Mhe.Mwanaidi Kassim Mussa akitoa maoni juu ya Taarifa ya Utekelezaji ya UWT Wadi hiyo iliyowasilishwa katika Kikao hicho.
 BAADHI ya Viongozi wa UWT walioudhuria Kikao hicho cha Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe.
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Tanzania Mkoa wa Magharibi Unguja Ndugu Zainab Ali Maulid, amezitaka Ngazi za Wadi ndani ya Mkoa huo kufanya Vikao vya Kawaida na Kikatiba kwa Mujibu wa Miongozo na Kanuni ya Umoja huo.

Wito huo aliutoa wakati akiwahutubia Wajumbe wa Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe katika Mkutano wa Baraza hilo uliozinduliwa  kwa kuiwakilisha Mikutano yote iliyofanyika leo ya Mabaraza 14 yaliyomo katika Wilaya ya Dimani Unguja.

Amesema ufanisi wa kiutendaji ndani ya Umoja huo unatokana na Utekelezaji wa maelekezo ya Vikao halali vinavyotoa maazimio na maelekezo ya utatuzi wa Changamoto mbali mbali zinazowakabili Wanachama,Viongozi na Watendaji wa UWT.

Ameeleza kuwa Vikao ndio sehemu pekee ya kujitathimini na kupanga Mikakati ya Utendaji wa shughuli mbali mbali za UWT na CCM, hasa katika wakati wa sasa wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Dola wa Mwaka 2020.

Amesema kila Mwanamke ndani ya Umoja huo anatakiwa kuwahamasisha Wanawake wengine ambao hawajajiunga na UWT na CCM wajiunge na Taasisi hizo ili wanufaike na Siasa Bora zinazoendeshwa na Chama Cha Mapinduzi.

Mwenyekiti huyo amewakumbusha  Akina Mama hao kwamba wanatakiwa kujipanga vizuri juu ya kuwahamasisha Wanawake kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura pindi wakati wa zoezi hilo utakapofika.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo Zainab, amewasihi Wanawake kushiriki katika harakati za kukemea na kupambana na Vitendo vya Udhalilishaji wa Kijinsia kwani vinakwamisha malengo ya Vijana hasa wa Kike katika Safari yao ya kusaka Elimu.

Naye Mwenyekiti wa Wadi hiyo, Ndugu Amina Khalfan ameahidi kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na mgeni rasmi watayafanyia kazi kwa vitendo ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao za Kiutendaji.

Akizungumza Mjumbe wa Baraza hilo ambaye pia ni Mwakilishi wa Viti Maalum Mhe.Mwanaidi Kassim Mussa amewashauri Viongozi wa Wadi hiyo kuendelea kuwa Wabunifu na kushirikiana na Viongozi mbali mbali wa ngazi za juu za Umoja huo ili wasaidie kutatua kwa haraka changamoto zinazowakabili.

Jumamosi, 15 Juni 2019

DK.MABODI: ATOA MAAGIZO CCM MFENESINI.



 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi,akiwahutubia Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Mfenesini na Wageni Waalikwa katika Mkutano wa kawaida wa Halmashauri hiyo uliofanyika leo katika ukumbi wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Magharibi 'A' Unguja.



NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,amewataka Wanachama,Viongozi na Watendaji wa CCM Wilaya ya Mfenesini kuhakikisha Taasisi hiyo inashinda Majimbo yote ya Uchaguzi ndani ya Wilaya hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa Dola Mwaka 2020.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akifungua Mkutano wa kawaida wa Halmashauri Kuu ya Wilaya hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Magharibi 'A' Unguja.

 Amesema Viongozi na Watendaji hao kwa kushirikiana na Wanachama na Makada  mbali mbali wanatakiwa kuendelea kufanya kazi mbali mbali zikiwemo za kuelezea kwa kina namna Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 inavyotekelezwa katika maeneo yao.

Amesema Viongozi hao wanatakiwa kuwahamasisha Vijana na Makundi mengine yaliyomo katika jamii wajiunge na CCM ikiwa ni sehemu ya kuongeza Wanachama wapya waliotimiza umri wa kupiga kura kwa mujibu wa Sheria za Nchi, ambao ndio Mtaji wa kudumu wa CCM watakaoleta ushindi wa Chama katika Uchaguzi Mkuu wa Dola Mwaka 2020.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi,amefafanua kuwa Serikali ya Awamu ya Saba chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, amekuwa ni Muadilifu na kinara wa kuenzi na kudumisha Amani na Utulivu wa Nchi hali inayochochea Maendeleo Endelevu ya Zanzibar.

Ameeleza kuwa Tunu hiyo ya Amani inatakiwa kulindwa kwa gharama yoyote na kila Mwananchi bila kujali tofauti za Kidini,Kisiasa na Kikabila kwani ndio chimbuko la mafanikio katika Nyanja mbali mbali za Kiuchumi,Kijamii na Kisiasa.

Dk.Mabodi amesema Chama Cha Mapinduzi kinawathamini Wananchi Wote bila kujali tofauti zao za Kisiasa ndio maana kinasimamia Sera zake zitekelezwe kila eneo linalohitaji huduma za Kijamii na Kiuchumi.

Sambamba na hayo amewasihi Viongozi hao kuendeleza Utamaduni wa kufanya Vikao vya Kikatiba kwa Wakati husika ili kutoa fursa pana ya ngazi mbali mbali za Uongozi kujadili na kufanya Maamuzi ya kuimarisha Chama.

Amekumbusha kuwa CCM haitovumilia Mwanachama yeyote atayetumika kufanya ama kufanyiwa kampeni za kugombea nafasi za Uongozi mwaka 2020,kabla ya Chama kutangaza kufanyika kwa mchakato huo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Ndugu Mohamed Rajab Soud,amesema kufanyika kwa Mkutano huo kunatoa nafasi pana kwa Ngazi ya Mkoa ya Kichama kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Mohamed amesema kuwa Hali ya Kisiasa ndani ya Mkoa huo kwa sasa ipo vizuri na inaimarika zaidi kutoka na juhudi za Viongozi wa Majimbo ambao ni Wabunge na Wawakilishi kutekeleza Wajibu wao kwa Jamii.

Awali akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mfenesini Ndugu Kesi Mashaka Ngusa,amesema kuwa  Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo imeendelea kutekeleza kwa ufanisi masuala mbali mbali ya kuleta Maendeleo ndani ya Wilaya sambamba na kuwajenga Kiitikadi na Kiuongozi Wanachama wa CCM hasa Vijana na Wanawake.