Jumapili, 16 Juni 2019

NDG: ZAINAB: ATAKA NGAZI ZA WADI ZA UWT ZIFANYE VIKAO.



 MWENYEKITI wa UWT Mkoa wa Magharibi Unguja Ndugu Zainab Ali Maulid,akiwahutubia Wajumbe wa Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe mara baada ya kufungua Kikao cha Baraza hilo kwa niaba ya Wadi 14 za UWT za Wilaya ya Dimani zilizofanya Vikao leo Tarehe 16/06/2019.
 
 KATIBU wa UWT Wadi ya Mwanakwere Ndugu Khadija Seif akisoma Taarifa ya Utendaji wa Majukumu mbali mbali ya Wadi hiyo mara baada ya kufunguliwa kwa Kikao hicho cha Baraza la UWT ngazi ya Wadi huko katika Ukumbi wa Mikutano wa Tawi la Mwanakwerekwe 'A'.

 WAJUMBE wa Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe wakisikiliza nasaha zinazotolewa na Viongozi wao kupitia Kikao hicho.

 MJUMBE wa Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe ambaye pia ni Mwakilishi wa Viti Maalum Mhe.Mwanaidi Kassim Mussa akitoa maoni juu ya Taarifa ya Utekelezaji ya UWT Wadi hiyo iliyowasilishwa katika Kikao hicho.
 BAADHI ya Viongozi wa UWT walioudhuria Kikao hicho cha Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe.
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Tanzania Mkoa wa Magharibi Unguja Ndugu Zainab Ali Maulid, amezitaka Ngazi za Wadi ndani ya Mkoa huo kufanya Vikao vya Kawaida na Kikatiba kwa Mujibu wa Miongozo na Kanuni ya Umoja huo.

Wito huo aliutoa wakati akiwahutubia Wajumbe wa Baraza la UWT Wadi ya Mwanakwerekwe katika Mkutano wa Baraza hilo uliozinduliwa  kwa kuiwakilisha Mikutano yote iliyofanyika leo ya Mabaraza 14 yaliyomo katika Wilaya ya Dimani Unguja.

Amesema ufanisi wa kiutendaji ndani ya Umoja huo unatokana na Utekelezaji wa maelekezo ya Vikao halali vinavyotoa maazimio na maelekezo ya utatuzi wa Changamoto mbali mbali zinazowakabili Wanachama,Viongozi na Watendaji wa UWT.

Ameeleza kuwa Vikao ndio sehemu pekee ya kujitathimini na kupanga Mikakati ya Utendaji wa shughuli mbali mbali za UWT na CCM, hasa katika wakati wa sasa wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Dola wa Mwaka 2020.

Amesema kila Mwanamke ndani ya Umoja huo anatakiwa kuwahamasisha Wanawake wengine ambao hawajajiunga na UWT na CCM wajiunge na Taasisi hizo ili wanufaike na Siasa Bora zinazoendeshwa na Chama Cha Mapinduzi.

Mwenyekiti huyo amewakumbusha  Akina Mama hao kwamba wanatakiwa kujipanga vizuri juu ya kuwahamasisha Wanawake kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura pindi wakati wa zoezi hilo utakapofika.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo Zainab, amewasihi Wanawake kushiriki katika harakati za kukemea na kupambana na Vitendo vya Udhalilishaji wa Kijinsia kwani vinakwamisha malengo ya Vijana hasa wa Kike katika Safari yao ya kusaka Elimu.

Naye Mwenyekiti wa Wadi hiyo, Ndugu Amina Khalfan ameahidi kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na mgeni rasmi watayafanyia kazi kwa vitendo ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao za Kiutendaji.

Akizungumza Mjumbe wa Baraza hilo ambaye pia ni Mwakilishi wa Viti Maalum Mhe.Mwanaidi Kassim Mussa amewashauri Viongozi wa Wadi hiyo kuendelea kuwa Wabunifu na kushirikiana na Viongozi mbali mbali wa ngazi za juu za Umoja huo ili wasaidie kutatua kwa haraka changamoto zinazowakabili.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni