Jumanne, 12 Juni 2018

UVCCM JIMBO LA MTONI WATOA SADAKA KWA WAGONJWA NA WAZEE WASIOJIWEZA

 MWENYEKITI wa UVCCM Jimbo la Mtoni Ibrahim Mtumwa Saleh akizungumza na wajumbe wa Kamati ya siasa ya umoja huo katika jimbo hilo katika kikao cha mipango ya utoaji wa sadaka za mchele na unga wa ngano kwa wagonjwa na wazee wasiojiweza katika shehia tano za jimbo la Mtoni Unguja.

 
KATIBU wa UVCCM Halima Khamis Ali akizungumza katika kikao hicho.

 
MWENYEKITI wa Jimbo hilo Ibrahim  akitoa maelezo juu ya sadaka hizo akiwa na viongozi wengine wa UVCCM na CCM.

 MWENYEKITI wa UVCCM Ibrahim Mtumwa na Katibu  wa UVCCM Jimbo la Mtoni Halima Khamis Ali (kushoto) wakimkabidhi sadaka hizo  Bi. Ghanima   Mohamed Omar  kwa niaba ya Mzee Msham Mbwana(kushoto).

 
BAADHI wa UVCCM na CCM walioshiriki katika zoezi hilo la utoaji wa sadaka kwa wagonjwa na wazee wasiojiweza.

 
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.


UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi ( UVCCM) Jimbo la Mtoni umesema utaendelea kuwasaidia watu wasiojiweza ambao ni wazee na wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu ili waweze kujivua uwepo wa umoja huo katika jimbo hilo.

Kauli hiyo ameitoa Mwenyekiti wa UVCCM wa jimbo hilo Ibrahim Mtumwa Saleh wakati akiwakabidhi sadaka za mchele na unga wa ngano kwa ajili ya Mwezi Mtukufu wa ramadhani na siku kuu ya Idd Fitri wazee na wagonjwa wa shehia tano za Jimbo la Mtoni Unguja.

Amesema licha ya UVCCM kukabiliwa na majukumu ya kisiasa ya kusimamia miongozo ya kikanuni ya umoja huo na CCM hasa kwa rika la vijana bado  wana jukumu kubwa la kutatua changamoto zinazowakabili wazee.

Mwenyekiti huyo alieleza kwamba kundi hilo linahitaji msaada  msaada na uangalizi wa karibu, jambo ambayo imepelekea Umoja huo kuona kuna umuhimu wa kusaidia kundi hilo hasa kwa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa ramadhani kama walivyo watu wengine katika jamii.

“ UVCCM chini ya ulezi wa CCM tunajali  na kuthamini mchango wa makundi yote katika jamii hasa wazee ambao walitumikia taifa hili kwa muda mrefu, hivyo sisi vijana ni wajibu wetu kuwasaidia mahitaji mbali mbali ambayo yapo ndani ya uwezo tu ili nao wajivunie uwepo wetu ndani ya jamii”, alisema Ibrahim.

Alisema utamaduni huo wa kutoa sadaka kwa makundi mbali mbali katika jamii hasa yenye mahitaji maalum  utakuwa endelevu, na kuwaomba viongozi mbali mbali wa Chama, Jumuiya, Serikali na watu wenye uwezo kuendeleza utaratibu huo.

 Amebainisha kuwa CCM na jumuiya zake ni taasisi bora ya kisiasa iliyokuwa karibu na wananchi wa makundi yote kuliko chama chochote cha kisiasa toka kuanzishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Naye Katibu wa CCM wa Jimbo hilo Khamis Omar Khamis, alipongeza juhudi za uchapakazi na ubunifu unaofanywa na UVCCM jimbo hilo kwa kuendeleza kwa vitendo harakati na vugu vugu za kujitolea zilizowahi kufanywa na vijana wa enzi za ASP.

Alisema vijana ndio nguzo ya CCM hivyo wanatakiwa kuwa mfano bora wa kutenda na kutekeleza mambo mema yanayoenda sambamba na matakwa ya kanuni, miongozo na sera Chama Cha Mapinduzi katika kutekeleza falsafa ya siasa za maendeleo kwa wote.

Akitoa shukrani zake Bi. Ghanima  Mohamed kwa niaba ya Mzee Msham Mbwana Saleh ambaye ni mgonjwa kwa muda mrefu, alisema sadaka hiyo itatumiwa vizuri ili imsaidie mgonjwa huyo.

 Sadaka hizo  zimetolewa na umoja huo kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa na wazee wenye mahitaji maalum wa shehia tano za jimbo la Mtoni.