Ijumaa, 25 Machi 2016

ZUBEIR MAULID AIBUKA KIDEDEA USPIKA BLW



WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi watokanao na Chama Cha Mapinduzi Zanzibar leo wamefanya Uchaguzi wa kumpata mjumbe atakaye peperusha bendera ya CCM katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Spika wa Baraza hilo kwa kipindi cha mwaka 2015 - 2020.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Itikadi na Uenezi  Mhe. Waride Bakari Jabu, amesema uchaguzi huo ulioendeshwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, ulifanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Mjini Unguja.

Mwenyekiti wa Uchaguzi huo, uliojumuisha wajumbe 72, alimtangaza Zubeir Ali Maulid kuwa mshindi baada ya kupata kura 55 na kuwashinda wapinzani wake wawili aliyemaliza muda wake Pandu Ameir Kificho aliyepata kura 11 na Jaji Janeth Nora Sekihola aliyepata 4, na kura mbili ziliharibika.
Jumla ya wanachama wa tisa (9) walijitokeza kuomba ridhaa ya CCM ili wagombee nafasi hiyo ya Spika .

Katika kikao cha Kamati Maalum kilichofanyika Machi 24, mwaka huu, Afisi Kuu ya CCM Zanzibar, ilipitisha majina matatu ikiwa ni pamoja na Pandu Ameir, Zubeir Ali Maulid na Janeth Nora Sekihola, ambapo uchaguzi wake umefanyika leo.
Akitoa neno la shukrani, Zubeir Ali Maulid, aliwashukuru wajumbe hao kwa imani yao kwake na kuwataka wampe kila aina ya mashirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Naye aliyekuwa Spika wa Baraza hilo Pandu Ameir Kificho, amekubali kushindwa na kumuahidi kumpa msaada wowote atakaohitaji, iwapo atatakiwa kufanya hivyo.
Uchaguzi huo wa Spika unatarajiwa kufanyika mara tu baada ya kuitishwa kwa Baraza jipya la Wawakilishi.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.
Sgd.

 (Waride B. Jabu),
Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi - CCM,
ZANZIBAR.
25/03/2016.