Alhamisi, 26 Julai 2018

CCM MKOA MJINI YATOA VITABU VYENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 17

 MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Mjini, Talib Ali Talib(kulia),akimkabidhi vitabu vya kusomea na kufundishia Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi  Khamis Kheir Ame (kushoto), hafla hiyo ilifanyika Amani katika ukumbi wa CCM Mkoa Amani.


 BAADHI ya waalikwa mbali mbali wakiwemo wazee, walezi, walimu na  viongozi wa Chama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walioudhuria katika hafla hiyo ya makabidhiano.

 MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Mjini, Talib Ali Talib, akihutubia katika hafla hiyo na kuelezea kwa upana utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

 WANAFUNZI wa Shule ya msingi ya Wazazi wakisoma utenzi uliokuwa na ujumbe unaohusu mafanikio, changamoto na hatua za kimaendeleo za shule hiyo

 VITABU vilivyotolewa na uongozi wa CCM Mkoa wa mjini.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mjini kimekabidhi vitabu 2,415 vyenye thamani ya shilingi milioni 17 kwa shule ya msingi ya Wazazi inayomilikiwa na taasisi hiyo.

Vitabu hivyo ni miongoni mwa mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020,inayotekelezwa kwa kasi na kwa ufanisi mkubwa katika jamii.

Akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini, Talib Ali Talib katika hafla hiyo iliyofanyika ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini uliopo Amani Zanzibar.

Talib alisema utoaji wa vitabu hivyo ni miongoni mwa utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Chama katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita kwa kuimarisha sekta mbali mbali za umma, hasa elimu ambayo ndio nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo ya nchi.

Aliwataka walimu wa shule hiyo kuvitunza na kusimamia vizuri matumizi ya vitabu hivyo ili wanafunzi waweze kupata muda mrefu wa kusoma na kupata uelewa mpana wa masomo yao.

Pia alieleza kuwa shule hiyo imekuwa na historia ya kushika nafasi bora za ufaulu katika mitihani ya taifa, hivyo walimu, wazee na walezi wanatakiwa kuendeleza ushirikiano wa malezi ya pamoja kwa lengo la kuendeleza sifa hiyo ya ufaulu kwa wanafunzi hao.

“Vitabu hivi ni vya masomo yote yanayofundishwa katika shule hii natarajia vitapunguza ama kumaliza kabisa changamoto ya ukosefu wa vitabu, na wanafunzi watapata kusoma kwa bidii.

Dhamira ya Chama Cha Mapinduzi ni kuimarisha miundombinu ya shule ya Wazazi iwe ya kisasa na yenye kutoa elimu bora kwa watoto ambao ndio viongozi na wataalamu wa fani mbali mbali wa baadae.”, alisema Mwenyekiti huyo.

Aidha aliahidi kuhakikisha shule hiyo inapata usajili wa ngazi ya sekondari ili wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi waweze kujiunga moja kwa moja na shule ya sekondari.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Khamis Kheir Ame alitoa shukrani kwa uongozi wa CCM Mkoa wa mjini kwa busara na ubunifu wao wa kutoa msaada wa vitabu kwa taasisi hiyo ya kitaaluma.

Alisema msaada huo unathamani kubwa sana katika sekta ya elimu kutokana na umuhimu wake unaomwezesha mwanafunzi kupata nyenzo ya kujifunzia wakati wowote akiwa shuleni ama nyumbani.

Akisoma risala mwalimu wa shule hiyo, Swaum Othman Juma alizitaja changamoto zinazowakabili katika shule hiyo kuwa ni pamoja na upungufu wa madawati, kuchelewa kwa usajili wa shule ya sekondari pamoja na walimu hao kupewa mshahara  ndogo usiokidhi mahitaji yao ya kila siku.


Jumatatu, 23 Julai 2018

CCM Z'BAR YAWAPONGEZA WALIOPATA DIVISION I,II&III KIDATO CHA SITA-2018


KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya siasa na uhusiano wa kimataifa CCM Zanzibar ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa  Mwl. Kombo Hassan Juma, akizungumza na wanafunzi wa kidato cha Sita Unguja waliofaulu mtihani mtihani wa taifa kiwango cha daraja la kwanza hadi la tatu.

 WANAFUNZI wa kidato cha Sita waliofaulu mtihani wa taifa mwaka 2018, wakisikiliza kwa makini nasaha za viongozi mbali mbali wa CCM katika Kikao cha kuwapongeza kilichofanyika Afisi Kuu CCM, Kisiwandui Zanzibar
 KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya siasa na uhusiano wa kimataifa CCM Zanzibar ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa  Mwl. Kombo Hassan Juma, akizungumzia umuhimu wa vijana kuthamini elimu. BAADHI ya wanafunzi waliofaulu kidato cha sita mwaka 2018.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewapongeza wanafunzi waliofaulu mtihani wa taifa wa kidato cha sita mwaka 2018, waliopata kiwango cha  daraja la kwanza, pili na tatu (Division I,II&III).

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya siasa na uhusiano wa kimataifa CCM Zanzibar ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa  Mwl. Kombo Hassan Juma,  alipokutana na wanafunzi 450 waliofaulu mtihani huo kwa upande wa Unguja, huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.

Mwl. Kombo alisema Chama Cha Mapinduzi kinawapongeza wanafunzi hao kwa juhudi zao za kusoma kwa bidii hadi wakafaulu mtihani huo.

Alieleza kwamba licha ya CCM kuwa taasisi ya kisiasa bado ina jukumu la msingi la kufuatilia,kuhakiki na kutathimini mwenendo wa hali ya elimu nchini.

Alieleza kwamba maendeleo ya nchi yoyote duniani yanatokana na fikra na ubunifu wa wasomi wa fani mbali mbali zinazosaidia kuharakisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi.

Mwl. Kombo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya ajira, elimu na mafunzo Afisi kuu CCM Zanzibar aliwambia wanafunzi hao kwamba CCM itaendelea kuwaunga mkono katika safari yao ya kielimu ili waweze kuhitimu elimu ya juu na kuwa wataalam watakaoitumikia nchi kwa uadilifu.

“ Wazee na walezi sote tunatakiwa kuwajibika  katika kusimamia na kuwalea katika maadili mema vijana wetu ili waweze kujifunza na kusoma kwa bidii na kufaulu vizuri katika mitihani mbali mbali ya kitaifa.

Serikali zote mbili ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania na Zanzibar zinaendelea kuimarisha sekta ya elimu hasa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi waliofaulu kujiunga na Vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu.”, alisema Mwenyekiti huyo na kuwasisitiza wanafunzi nchini kusoma kwa bidii ili wanufaike na fursa hiyo.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Laila Burhan Ngozi aliwashauri wanafunzi mbali mbali wa ngazi za sekondari nchini kuepuka vikundi viovu badala yake wasome kwa bidii kwa lengo la kuwa na umahiri wa kumudu masomo ya Chuo kikuu.

Pia aliwasihi wanafunzi ambao viwango vyao vya ufaulu havikukidhi vigezo vya kuendelea na elimu ya juu wasikate tamaa bali wajiendeleze kitaaluma na kuweza kukamilisha malengo yao waliojiwekea.

Katika kikao hicho pia waliudhuria wanafunzi wawili wa Zanzibar waliofanya vizuri zaidi katika mtihani wa kidato cha Sita mwaka huu, ambao ni Ndugu Biubwa Khamis Ussi kutoka shule ya Sekondari ya SOS na Ndugu Fahad Rashid Salum kutoka Shule ya Sekondari Lumumba.

Ijumaa, 20 Julai 2018

WANEC CCM WAENDELEA KUKAGUA UTEKEWLEZAJI WA ILANI YA CCM MAJIMBONI
MJUMBE wa Halmashauri kuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Amin Salmin Amour amewataka viongozi wa Majimbo kupita kwa Wananchi kusikiliza kero zinazowakabili na kuweza kuzipatia ufumbuzi ili kuepukana na malalamiko.

Ameyasema hayo huko katika Tawi la CCM Mtoni Wilaya ya Magharibi ‘’A’’,wakati alipokuwa akizungumza na vingozi wa Matawi, Wadi na Jimbo la Mtoni.

Amesema Wawakilishi, Wabunge na Madiwani wanafanya kazi kubwa katika kuleta maendeleo ya Wananchi lakini baadhi yao hawashuki ngazi za chini na kuwaeleza wananchi wanachokifanya.

Ameeleza kuwa matatizo kama vile miondombinu ya maji, Umeme, Barabara, vikundi vya ushirika na ajira hivyo juhudi za makusudi za kutatua matatizo hayo zinahitaji kuchukuliwa na viongozi hao.

Aidha amewataka Viongozi hao kuwa bega kwa bega na Wananchi ili waweze kuleta maendeleo na kukipatia ushindi chama cha Mapinduzi ifikapo 2020.

Mbali na hayo amewataka kuacha makundi kwani ni kikwazo cha kuleta maendeleo kwa Wananchi na Chama kwa Ujumla.

Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) Galos Nyimbo amesema lengo la kufanya ziara hiyo ni kuimarisha Chama katika ngazi ya Matawi, Wadi na Majimbo ili kuweza kubaini mapungufu yaliopo na kuweza kuyafanyia kazi kabla ya Uchaguzi wa mwaka 2020.

Mbali na hayo amewaomba Wananchi kutoa mashirikiano mazuri kwa Viongozi wao kwa kuwa pamoja na kuziibuwa Changamoto zilizopo na kuzifanyia kazi ili kuimarisha Chama hicho na kuendelea kushika dola.

Mbunge wa Jimbo la Bububu Mwantakaje Haji Juma amesema ametekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa zaidi ya asilimia 80 katika sekta ya elimu, maji. Afya, njia za ndani na mambo maengine lakini kinachohitajika ni Wananchi kutoa ushirikiano kwa Viongozi wao.

Amesema wanafanya vikao vya mara kwa mara na kuelezea walichokifanya lakini baadhi ya mahudhurio ya wanachama yamekuwa madogo na kupelekea kutofahamu juhudi zinazofanywa na Viongozi hao.

Nae Mwakilishi wa Jimbo la Mtoni Hussein Ibrahim Makungu “BHAA” amewataka Wananchi kutumia fursa yao ya kikatiba kwa kuwakosoa wanapokosea na kuwapongeza wanapofanya vizuri ila katika vikao halali sio kukaa vibarazani na kuwapaka matope Viongozi wao kwani kufanya hivyo ni kuwapa nguvu wapinzani.

Nao viongozi wa Matawi, Wadi na Jimbo la Mtoni wamewapongeza wajumbe wa NEC kufanya ziara hiyo kwani itaweza kuwa chachu ya kukiengezea nguvu chama cha mapinduzi na kuendelea kushika dola.


CCM Z'BAR YAWAPIGA MSASA VIONGOZI NA WATENDAJI WA JUMUIYA ZAKE. 

Wakuu wa Idara za CCM Zanzibar pamoja na Makamu Wenyeviti wa Jumuiya za CCM Taifa wakiimba nyimbo za CCM  mara baada ya kuingia katika ukumbi wa Mkutano wa Afisi Kuu CCM Kisiwandui Zanzibar, kwa ajili ya kikao.

 

BAADHI ya viongozi na Watendaji hao wa Jumuiya za Chama cha Mapinduzi wakifuatilia kwa makini maelekezo yanayotolewa na viongozi wa CCM kupitia Kikao hicho, kilichofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.


 Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mgeni Hassan Juma akitoa nasaha kwa viongozi na watendaji hao juu ya uimarishaji wa CCM na Jumuiya zake.

 
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Ndugu Catherine Peter Nao (aliyesimama katikati), akizungumza na viongozi na watendaji wa Jumuiya tatu za CCM Z’bar wakiwemo Wabunge na Wawakilishi wa Viti Maalum.

 BAADHI ya viongozi na watendaji mbali mbali wa Jumuiya tatu za CCM wakiimba nyimbo za Chama cha Mapinduzi baada ya viongozi wa Chama kufika ukumbini.
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar kimewataka watendajii na viongozi wa Jumuiya zote za Chama kufanya kazi zao kwa ushirikiano ili taasisi hiyo iendelee kuwa kinara wa kusimamia na kutekeleza kwa ufanisi sera na mikakati yake ya  maendeleo kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Ndugu Catherine Peter Nao wakati akizungumza na Viongozi mbali mbali wa Jumuiya tatu za Chama cha Mapinduzi wakiwemo Makamu Wenyeviti, Wabunge na Wawakilishi wa viti maalum pamoja na Makatibu wa Jumuiya hizo huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.

Katibu huyo  wa Kamati Maalum ya NEC, Catherine alisema uimara wa CCM unatokana na ushirikiano uliotukuka unaofanywa na viongozi na watendaji wa ngazi mbali mbali za Chama na Jumuiya zake, ambao kimsingi ndio nyenzo pekee ya kusimamia sera za Chama zitekelezwe kwa ufanisi.

Catherine ambaye toka ateuliwe kushika nafasi hiyo hicho ni Kikao chake cha mwanzo kuzungumza na viongozi hao, alisisitiza kuwa kila kiongozi kwa sasa anatakiwa kutekeleza wajibu wake katika kupanga na kubuni mikakati endelevu ya kufanikisha ushindi wa CCM mwaka 2020.

“ Kila tunapokutana tukiwa ni viongozi tuliaminiwa na Wana- CCM kuwa tunaweza kuongoza kwa uadilifu jahazi hili mpaka mwaka 2022 ni lazima tujadili kwa kina namna ya kutekeleza kwa vitendo Ibara ya 5 ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2012, inayoeleza kuwa ushindi wa CCM ni lazima katika uchaguzi Mkuu na wa serikali za mitaa.”, aliwakumbusha viongozi hao Catherine.

Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, aliwapongeza wabunge na wawakilishi wanaofuata nyayo za Rais wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ambaye pia Makamu Mwenyekiti wa CCM wanaotekeleza kwa kasi Ilani hiyo kwa kuwaletea wananchi maendeleo.

Pia aliwataka wabunge na wawakilishi wa viti Maalum kwenda sambamba na kasi hiyo ya utekelezaji wa Ilani ili Chama Cha Mapinduzi kiweze kutatua kwa kiwango kikubwa kero zinazowakabilli wananchi kabla ya mwaka 2020.

Aidha Ndugu Catherine aliwambia viongozi hao kwamba pia wana jukumu la kushiriki ipasavyo katika mipango ya kukijenga Chama hasa katika mipango ya kuongeza wanachama wapya ambao ndio rasilimali ya kudumu ya kisiasa kwa Chama cha Mapinduzi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Taifa,  Ndugu Abdallah Haji Haidar alisema kila kiongozi aliyepewa dhamana ya uongozi anatakiwa kutekeleza wajibu wake kwa kufanya kazi za Chama kwa bidii ili taasisi hiyo iendelee kuongoza dola.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Ndugu Tabia Maulid Mwita alisema vijana wapo tayari kufanya kazi za Chama na za ujenzi wa Taifa muda wowote kwani wapo kwa ajili ya kulinda na kutetea mambo mema yaliyoasisiwa na Vijana wa ASP kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Naye Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Mgeni Hassan Juma alisema maelekezo yaliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi watayafanyia kazi ili kwenda sambamba na siasa za ushindani wa kisera na utatuzi wa changamoto za wananchi kwa wakati.

Nao Wawakilishi na Wabunge hao wa viti maalum, waliahidi kuendeleza ushirikiano na viongozi wenzao katika kutekeleza mambo mema yatakayoimarisha CCM katika nyanja za kisiasa na kiuchumi.

Jumamosi, 14 Julai 2018

MABODI AZINDUA MRADI WA VISIMA VYA MAJI MAGOMENI


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Zanzibar, Dk.Abdalla Juma Sadala 'Mabodi' amesema mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa wananchi(MKUZA) na pensheni za wazee ni matunda ya mapinduzi ya mwaka 1964.

Amesema matunda hayo ya mapinduzi yameanza kuwanufaisha mpaka wananchi wa kaya maskini ambapo wanapewa fedha za watoto kwa ajili ya kwenda shule.

Hayo aliyasema jana wakati akizindua mradi wa visima saba Jimbo la Magomeni,ambapo aliwataka wanachama waende kuzungumza kwa watu wengine kuhusu mafanikio hayo ya matunda ambayo yananufaisha kaya maskini.

Dk.Mabodi aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) kupitia Rais Dk.Ali Mohamed Shein amehakikisha anawapatia matunda ya mapinduzi hayo kwa kuwapatia pensheni ambayo inawasaidia kuendeshea maisha yao ya uzeeni.

"Matunda ya Mapinduzi yamepatikana na kwamba yanawanufaisha wananchi wote wa Zanzibar kwa kupitia ilani madhubuti ya CCM ambapo ilani ya uchaguzi ibara ya 69,104 na 109 zote zinazungumzia masuala ya kuwaletea maendeleo wananchi hususan katika sekta ya maji,"alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Alisema katika ilani hiyo CCM inatekeleza haadi zake ambazo zilitoa wakati wa uchaguzi hivyo wafadhili wa maendeleo pia wanatekeleza ilani ya CCM hususan katika miradi ya maji.

"Katika muongozo wa ilani inaelekeza kuwa Serikali na wafadhili wa maendeleo watashirikiana katika kuhakikisha wanaleta maendeleo kwa wananchi hivyo tunaona huduma hizi zinafika lakini inatokana na ilani ya CCM,"alisema Dk.Mabodi

Mbali na hilo, Naibu Katibu Mkuu huyo alikabidhi gari aina ya Canter Mistubishi lilogharimu sh.milioni 35 kwa jimbo hilo la Magomeni huku upande wa mradi wa visima hivyo vimegharimu milioni 93 kwa ufadhili wa shirika la Direct Aid kwa kushirikiana na Mbunge wa jimbo hilo.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo, Jamal Kassim Ali, alisema baada ya uchaguzi aliwahaidi kuwatatulia changamoto ya upatinakaji wa huduma ya maji safi na salama hivyo mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM.

Alisema hatua inayofuata ni kuwasogezea huduma hiyo ya maji safi na salama majumbani mwao na kuwatoa katika huduma ya upatikanaji wa visimani.


" VIONGOZI JIPIMENI KATIKA UTENDAJI WENU WA KAZI " ND. BAKARI

Katibu wa Oganization  CCM Zanzibar Nd. Bakari  akizungumza na wanaCCM wa Tawi la Shaurimoyo ' B'


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar, kimewataka viongozi wa wa chama visiwani humu kujipima katika utendaji wao wa kutoa huduma kwa wananchi. 

Kauli hiyo ameitoa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Organaizesheni,Zanzibar,Bakari Hamad Khamis wakati akizungumza wanachama wa tawi la Shauri Moyo 'B', mjini Unguja alisema endapo inaridhisha iongezwe juhudi zaidi.

Alisema na kama viongozi hao utendaji wao haujiridhishi inapaswa kujiuliza sababu ambazo zinasababisha kutofanikiwa kufikia malengo yaliowekwa. 

"Lakini si viongozi pekee bali wanachama wote tunawajibika kufanya kazi hiyo kwa mantiki ya kuimarisha chama chetu pamoja na kuhudumisha Zanzibar yetu,"alisema Katibu huyo 

 Katika maelezo yake Katibu Bakari alisema wanachama wanatakiwa kuwa wa moja ili kukijenga chama na kwamba endapo wakianza kuunga mkono hoja za wapinzani hivyo kwa kufanya hivyo ni kutoisaidia Serikali ambayo inaongozwa na CCM.

 "Sisi viongozi tunatakiwa tuelewe kuwa ni watu wa kwanza katika kukisimamia chama na kuisimamia Serikali kazi moja ya serikali ni kutekeleza majukumu waliopewa na chama na ndio maana ikifika wakati wa uchaguzi tunaanda ilani,"alisema Katibu huyo 

 Aliongeza kuwa lazima wanachama wae na umoja ili kuhakikisha chama kinabaki kuendelea kushika dola na kuwatatulia matatizo wananchi na kuwaletea maendeleo.

Katibu wa Oganization CCM Zanzibar Nd. Bakari akiwasili katika  Tawi la Shaurimoyo ' B' kwa ajili ya kuzungumza na wanachama wa CCM Tawi  hilo

Katibu wa Oganization  CCM Zanzibar Nd. Bakari  akipokea risala kutoka kwa Nd. Arafa Juma Faki 
ambae ni Katibu wa CCM Tawi la Shaurimoyo ' B'

Katibu wa Oganization  CCM Zanzibar Nd. Bakari  akizungumza na wanaCCM wa Tawi la Shaurimoyo ' B'Kaimu Katibu wa Wilaya ya Amani ambae pia ni Katibu wa Wazazi wilaya ya Amani Nd.Mwanaisha Ame Moh'd akitoa nasaha zake kwa Wanachama hao wa CCM wa Tawi la Shaurimoyo ' B'

Add caption

Jumatatu, 9 Julai 2018

MAMA SAMIA AONGOZA KIKAO CHA KAMATI MAALUM YA HALMASHAURI KUU YA CCM TAIFA ZANZIBAR


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo Julai 9, mwaka 2018 ameongoza Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar.

Makamu wa Rais Mhe. Samia ameongoza kikao hicho baada ya kupendekezwa na wajumbe wa kikao kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Ibara ya 108 (4) ili aongoze kikao hicho kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Dk. Ali Mohamed Shein aliyesafiri nje ya nchi kikazi. 

 Kikao hicho kimefanyika kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi hadi saa 7:30 mchana katika ukumbi wa Mikutano wa Afisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Kisiwanduzi Zanzibar.

Pamoja na mambo mengine kikao hicho kilikuwa na ajenda moja ya kujadili kwa kina majina 19 ya Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi waliojitokeza kugombea nafasi ya uwakilishi katika jimbo la Jang’ombe Zanzibar. 

 Wanachama hao 19 walioomba nafasi hiyo na kupendekezwa katika ngazi za jimbo, wilaya na Mkoa, Kikao hicho kimeweka alama zinazostahiki kwa wagombea wote na kupendekeza kwa Kamati Kuu ya CCM Taifa ili irejeshe majina matatu au kama itakavyoona inafaa kwa ajili ya kura ya maoni kwa lengo la kumpata mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi mdogo wa jimbo hilo. Kikao hicho ni maalum kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2017, ibara ya 109 (1) na 7(b).

 Mchakato huo unafanyika kutokana na Jimbo la Jang’ombe kuwa wazi baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo Abdalla Diwani kufukuzwa uanachama wa CCM hivi karibuni baada ya kukiuka maadili na miongozo ya Chama.

  MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akisalimiana na Wajumbe wa Kamati Maalum ya NEC Taifa Zanzibar  kilichofanyika leo  katika ukumbi wa Afisi Kuu CCM Kisiwandui.

 
 MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan  akiingia Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar kwa ajili ya kuongoza kikao cha NEC Taifa Zanzibar.
BAADHI ya Wajumbe wa Kikao hicho 

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akisoma ajenda za Kikao cha Kamati Maalum ya NEC Taifa Zanzibar cha kujadili majina ya Wana CCM waliowania kugombea nafasi ya uwakilishi jimbo la Jang'ombe.

WAGOMBEA 19 wa CCM wanaowania nafasi ya uwakilishi wa Jimbo la Jang'ombe wakiwa katika picha ya Pamoja.