Jumamosi, 14 Julai 2018

MABODI AZINDUA MRADI WA VISIMA VYA MAJI MAGOMENI


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Zanzibar, Dk.Abdalla Juma Sadala 'Mabodi' amesema mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa wananchi(MKUZA) na pensheni za wazee ni matunda ya mapinduzi ya mwaka 1964.

Amesema matunda hayo ya mapinduzi yameanza kuwanufaisha mpaka wananchi wa kaya maskini ambapo wanapewa fedha za watoto kwa ajili ya kwenda shule.

Hayo aliyasema jana wakati akizindua mradi wa visima saba Jimbo la Magomeni,ambapo aliwataka wanachama waende kuzungumza kwa watu wengine kuhusu mafanikio hayo ya matunda ambayo yananufaisha kaya maskini.

Dk.Mabodi aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) kupitia Rais Dk.Ali Mohamed Shein amehakikisha anawapatia matunda ya mapinduzi hayo kwa kuwapatia pensheni ambayo inawasaidia kuendeshea maisha yao ya uzeeni.

"Matunda ya Mapinduzi yamepatikana na kwamba yanawanufaisha wananchi wote wa Zanzibar kwa kupitia ilani madhubuti ya CCM ambapo ilani ya uchaguzi ibara ya 69,104 na 109 zote zinazungumzia masuala ya kuwaletea maendeleo wananchi hususan katika sekta ya maji,"alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Alisema katika ilani hiyo CCM inatekeleza haadi zake ambazo zilitoa wakati wa uchaguzi hivyo wafadhili wa maendeleo pia wanatekeleza ilani ya CCM hususan katika miradi ya maji.

"Katika muongozo wa ilani inaelekeza kuwa Serikali na wafadhili wa maendeleo watashirikiana katika kuhakikisha wanaleta maendeleo kwa wananchi hivyo tunaona huduma hizi zinafika lakini inatokana na ilani ya CCM,"alisema Dk.Mabodi

Mbali na hilo, Naibu Katibu Mkuu huyo alikabidhi gari aina ya Canter Mistubishi lilogharimu sh.milioni 35 kwa jimbo hilo la Magomeni huku upande wa mradi wa visima hivyo vimegharimu milioni 93 kwa ufadhili wa shirika la Direct Aid kwa kushirikiana na Mbunge wa jimbo hilo.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo, Jamal Kassim Ali, alisema baada ya uchaguzi aliwahaidi kuwatatulia changamoto ya upatinakaji wa huduma ya maji safi na salama hivyo mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM.

Alisema hatua inayofuata ni kuwasogezea huduma hiyo ya maji safi na salama majumbani mwao na kuwatoa katika huduma ya upatikanaji wa visimani.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni