MJUMBE wa Halmashauri kuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Amin Salmin Amour amewataka viongozi wa Majimbo kupita kwa Wananchi kusikiliza kero zinazowakabili na kuweza kuzipatia ufumbuzi ili kuepukana na malalamiko.
Ameyasema hayo huko katika Tawi la CCM Mtoni Wilaya ya Magharibi ‘’A’’,wakati alipokuwa akizungumza na vingozi wa Matawi, Wadi na Jimbo la Mtoni.
Amesema Wawakilishi, Wabunge na Madiwani wanafanya kazi kubwa katika kuleta maendeleo ya Wananchi lakini baadhi yao hawashuki ngazi za chini na kuwaeleza wananchi wanachokifanya.
Ameeleza kuwa matatizo kama vile miondombinu ya maji, Umeme, Barabara, vikundi vya ushirika na ajira hivyo juhudi za makusudi za kutatua matatizo hayo zinahitaji kuchukuliwa na viongozi hao.
Aidha amewataka Viongozi hao kuwa bega kwa bega na Wananchi ili waweze kuleta maendeleo na kukipatia ushindi chama cha Mapinduzi ifikapo 2020.
Mbali na hayo amewataka kuacha makundi kwani ni kikwazo cha kuleta maendeleo kwa Wananchi na Chama kwa Ujumla.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) Galos Nyimbo amesema lengo la kufanya ziara hiyo ni kuimarisha Chama katika ngazi ya Matawi, Wadi na Majimbo ili kuweza kubaini mapungufu yaliopo na kuweza kuyafanyia kazi kabla ya Uchaguzi wa mwaka 2020.
Mbali na hayo amewaomba Wananchi kutoa mashirikiano mazuri kwa Viongozi wao kwa kuwa pamoja na kuziibuwa Changamoto zilizopo na kuzifanyia kazi ili kuimarisha Chama hicho na kuendelea kushika dola.
Mbunge wa Jimbo la Bububu Mwantakaje Haji Juma amesema ametekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa zaidi ya asilimia 80 katika sekta ya elimu, maji. Afya, njia za ndani na mambo maengine lakini kinachohitajika ni Wananchi kutoa ushirikiano kwa Viongozi wao.
Amesema wanafanya vikao vya mara kwa mara na kuelezea walichokifanya lakini baadhi ya mahudhurio ya wanachama yamekuwa madogo na kupelekea kutofahamu juhudi zinazofanywa na Viongozi hao.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Mtoni Hussein Ibrahim Makungu “BHAA” amewataka Wananchi kutumia fursa yao ya kikatiba kwa kuwakosoa wanapokosea na kuwapongeza wanapofanya vizuri ila katika vikao halali sio kukaa vibarazani na kuwapaka matope Viongozi wao kwani kufanya hivyo ni kuwapa nguvu wapinzani.
Nao viongozi wa Matawi, Wadi na Jimbo la Mtoni wamewapongeza wajumbe wa NEC kufanya ziara hiyo kwani itaweza kuwa chachu ya kukiengezea nguvu chama cha mapinduzi na kuendelea kushika dola.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni