BAADHI ya waalikwa mbali mbali wakiwemo wazee, walezi, walimu na viongozi wa Chama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walioudhuria katika hafla hiyo ya makabidhiano. |
MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Mjini, Talib Ali Talib, akihutubia katika hafla hiyo na kuelezea kwa upana utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020. |
WANAFUNZI wa Shule ya msingi ya Wazazi wakisoma utenzi uliokuwa na ujumbe unaohusu mafanikio, changamoto na hatua za kimaendeleo za shule hiyo |
VITABU vilivyotolewa na uongozi wa CCM Mkoa wa mjini. |
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mjini kimekabidhi vitabu 2,415 vyenye
thamani ya shilingi milioni 17 kwa shule ya msingi ya Wazazi inayomilikiwa na
taasisi hiyo.
Vitabu hivyo ni miongoni mwa mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020,inayotekelezwa kwa kasi na kwa ufanisi
mkubwa katika jamii.
Akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Mjini, Talib Ali Talib katika hafla hiyo iliyofanyika ukumbi wa CCM Mkoa wa
Mjini uliopo Amani Zanzibar.
Talib alisema utoaji wa vitabu hivyo ni miongoni mwa utekelezaji wa
ahadi zilizotolewa na Chama katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita kwa
kuimarisha sekta mbali mbali za umma, hasa elimu ambayo ndio nyenzo muhimu ya
kuharakisha maendeleo ya nchi.
Aliwataka walimu wa shule hiyo kuvitunza na kusimamia vizuri matumizi
ya vitabu hivyo ili wanafunzi waweze kupata muda mrefu wa kusoma na kupata
uelewa mpana wa masomo yao.
Pia alieleza kuwa shule hiyo imekuwa na historia ya kushika nafasi bora
za ufaulu katika mitihani ya taifa, hivyo walimu, wazee na walezi wanatakiwa
kuendeleza ushirikiano wa malezi ya pamoja kwa lengo la kuendeleza sifa hiyo ya
ufaulu kwa wanafunzi hao.
“Vitabu hivi ni vya masomo yote yanayofundishwa katika shule hii
natarajia vitapunguza ama kumaliza kabisa changamoto ya ukosefu wa vitabu, na
wanafunzi watapata kusoma kwa bidii.
Dhamira ya Chama Cha Mapinduzi ni kuimarisha miundombinu ya shule ya
Wazazi iwe ya kisasa na yenye kutoa elimu bora kwa watoto ambao ndio viongozi
na wataalamu wa fani mbali mbali wa baadae.”, alisema Mwenyekiti huyo.
Aidha aliahidi kuhakikisha shule hiyo inapata usajili wa ngazi ya
sekondari ili wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi waweze kujiunga moja kwa
moja na shule ya sekondari.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Khamis Kheir Ame alitoa shukrani kwa
uongozi wa CCM Mkoa wa mjini kwa busara na ubunifu wao wa kutoa msaada wa
vitabu kwa taasisi hiyo ya kitaaluma.
Alisema msaada huo unathamani kubwa sana katika sekta ya elimu kutokana
na umuhimu wake unaomwezesha mwanafunzi kupata nyenzo ya kujifunzia wakati
wowote akiwa shuleni ama nyumbani.
Akisoma risala mwalimu wa shule hiyo, Swaum Othman Juma alizitaja
changamoto zinazowakabili katika shule hiyo kuwa ni pamoja na upungufu wa
madawati, kuchelewa kwa usajili wa shule ya sekondari pamoja na walimu hao
kupewa mshahara ndogo usiokidhi mahitaji
yao ya kila siku.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni