Jumatano, 1 Agosti 2018

DK.MABODI AKABIDHI MAGARI MATATU KWA WANANCHI WA MAJIMBO YA KIJITOUPELE NA PANGAWE.


 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akizindua moja ya gari aina ya Canter zilizotolewa na Mbunge wa Majimbo ya Kijitoupele na Pangawe Shamsi Vuai Nahodha.

 

 Dk.Abdulla Juma Mabodi akiendesha basi la Wanafunzi kuashiria makabidhiano ya magari hayo yatakayotumiwa na wanafunzi wa Majimbo hayo  pamoja na wananchi kwa ujumla.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla ‘’Mabodi’’ akizungumza na wananchi wa majimbo ya Kijitoupele na Pangawe katika hafla ya kuwakabidhi magari matatu ambayo ni mabasi mawili na Canter moja yaliyotolewa na Mbunge wa Majimbo hayo Shamsi Vuai Nahodha. 

 MBUNGE wa majimbo ya Kijitoupele na Pangawe, Shamsi Vuai Nahodha akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano ya Maghari hayo.


NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla ‘’Mabodi’’ akikagua maendeleo ya ujenzi wa Skuli ya msingi ya Kwarara inayojengwa na viongozi wa jimbo hilo. 

  MAGARI matatu yakionekana pichani  yaliyotolewa na Mbunge wa Kijitoupele na Pangawe Shamsi Vuai Nahodha.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla ‘’Mabodi’’  akiendesha gari aina ya Canter iliyotolewa na Mbunge huyo.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar, Dk.Abdulla Juma Mabodi amewataka Wabunge na Wawakilishi nchini kuongeza kasi ya kutatua kero za wananchi kwa wakati kama walivyowaahidi katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Kauli hiyo ameitoa mara baada ya kukabidhi magari matatu kwa wananchi wa majimbo ya Kijitopele na Pangawe ambapo Magari hayo yana thamani ya shilingi milioni 128 yaliyotolewa na Mbunge wa Majimbo hayo, Shamsi Vuai Nahodha.

Akizungumza katika ziara yake ya kutembelea majimbo hayo   iliyofanyika katika uwanja wa mpira wa Magirisi uliopo Kijitoupele, Dk.Mabodi  alisema huu ndio wakati wa viongozi wa majimbo kutekeleza kwa kasi Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020.

Akizungumzia vitendea kazi hivyo ambavyo ni magari matatu yakiwemo mabasi ya Wanafunzi mawili na  moja ambalo ni Canter kwa ajili ya shughuli za kijamii, aliwambia wananchi kuwa wanakiwa kuthamini  juhudi za kiongozi huyo aliyetekeleza ahadi zake kwa vitendo.

Dk. Mabodi alieleza kwamba malengo ya Chama Cha Mapinduzi ni kuhakikisha wananchi wa mijini na vijijini wanaondokana na changamoto mbali mbali za kijamii kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Alisema mabasi yaliyotolewa yatawasaidia wanafunzi wote wa majimbo hayo bila kujali tofauti za kisiasa.

kiongozi huyo katika ziara yake ya kutembelea miradi mbali mbali ya Chama iliyokutekeleza ahadi walizowaahidi wananchi katika kampeni  amesema wananchi wanakiamini na kukiunga mkono Chama kutokana na kutatua kwa wakati kero zinazowakabili wananchi.

“ Miradi mbali mbali ya maendeleo inayotekelezwa majimboni na viongozi wa CCM ni kwa ajili ya wananchi wote, na tunaomba wananchi muendelee kutuamini na hatimaye mwaka 2020 mkichague Chama chetu kiendelee kuongoza dola.”, alisema Dk. Mabodi.

Pamoja na hayo aliwapongeza viongozi wa Majimbo ya kijitoupele na Pangawe hasa  Mbunge na Wawakilishi wote wawili kwa kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu pia alitembelea ujenzi wa Kituo cha Afya katika Jimbo la Kijitoupele ambacho kimejengwa na Mwakilishi wa jimbo hilo, Ali Suleiman Ali ‘’Shihata’’ kupitia mfuko wa jimbo wa mwakilishi ambacho hadi kukamilika kwake kitatumia zaidi ya shilingi milioni 59.

Akikagua kituo hicho cha Afya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dk. Mabodi  ameahidi kutoa mipira ya kusambazia maji na pampu kwa lengo la kuhakikisha kituo hicho kinapata kwa wakati huduma ya Maji safi na Salama.

Pia Naibu Katibu Mkuu Dk. Mabodi alitembelea Shule ya Sekondari Kwarara na Kituo cha elimu na habari  sambamba na kukagua ujenzi wa shule ya msingi ya Kwarara itakayotumia shilingi bilioni 1.3 hadi ujenzi wake kukamilika.

Alisema maendeleo yaliyofikiwa katika majimbo hayo ni moja ya muendelezo wa kutekeleza malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwa kuwa kuimarisha ustawi wa kijamii na kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Naye Mbunge wa majimbo hayo, Shamsi Vuai Nahodha alisema CCM imeendelea kuwa na mvuto kwa jamii kutokana na ukweli na dhamira ya dhati ya viongozi wake kuwatumikia wananchi kwa vitendo.

Mbunge huyo Naohodha ambaye pia ni Waziri Kiongozi Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema kwa kushirikiana na viongozi wengine wa majimbo mawili anayoyatumikia wamefanikiwa kutatua kero za wananchi kwa kiwango kikubwa.

Shamsi alisema na kuongeza kuwa wameimarisha huduma muhimu za kijamii zikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, ujenzi wa vituo vya Afya pamoja na ujenzi wa shule za kisasa za msingi na sekondari.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni