MWENYEKITI wa Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)
Taifa Kheir James amewataka vijana wasomi nchini kuhakikisha tija ya elimu
waliyonayo inanufaisha jamii iliyowazunguka kwa maslahi ya vizazi vya sasa na
vijavyo.
Rai hiyo ameitoa leo katika hafla ya kuwapongeza wanafunzi waliofaulu mtihani wa kidatu cha Sita Zanzibar mwaka 2018 kwa kiwango cha daraja la kwanza, la pili na tatu (Division I,II na III) hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Z-Ocean iliyopo Bububu Wilaya ya Magharibi ‘’A’’ Zanzibar.
Ameeleza kuwa endapo vijana hao watashindwa kuzitumia vizuri elimu
zao kwa kuzinufaisha jamii zilizowazunguka basi elimu hizo zitakuwa hazina
maana kwao wao na taifa kwa ujumla.
Amesema serikali zote mbili ambazo ni Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinaendelea
kuthamini vijana kwa kuwawezesha kupitia nyanja mbali mbali hasa za kitaaluma.
Amewataka vijana hao ambao watajiunga na elimu ya juu katika
vyuo mbali mbali nchini kuwa wanatakiwa kusoma masomo ambayo wana uwezo nayo ili
waweze kufaulu vizuri katika masomo ya elimu ya juu na wawe wataalamu wenye
uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Mwenyekiti huyo Kheir amefafanua kwamba CCM na serikali zake
mbili inawaamini vijana kwa kuwapatia nafasi mbali mbali za uongozi sio kwa
sababu za kujuana bali ni kutokana na sifa walizokuwa nazo kitaaluma.
“ CCM haina vijana wa ovyo ovyo kama zilivyo taasisi zingine
za kisiasa bali ina vijana madhubuti, wazalendo,weledi na wenye sifa na kila
vigezo vinavyokubalika katika nyanja mbali mbali za uongozi na utendaji katika
taasisi za serikali na binafsi.”amefafanua Mwenyekiti huyo.
Alisema taasisi yoyote isiyokuwa na utaratibu wa kurithisha
uongozi kutoka kizazi kimoja kwenda kingine basi taasisi hiyo itakuwa ni sawa
na mfu na ndio maana CCM inaendeleza utaratibu wa kuwarithisha na kuwaanda
vijana wake kiungozi ili waweze kuwa viongozi bora ndani na nje ya Serikali
zao.
Ameeleza kuwa suala la vijana kupendana ni lazima na sio
hiari kwani endapo kundi hilo litaendekeza tabia ya kufanyiana fitna, majungu
na kuchafuana hawatokuwa na uwezo wa kulinda rasilimali za taifa kwani nguvu
nyingi watakuwa wanazitumia kuchafuana badala ya kufanya mambo ya maendeleo.
Pia amewataka viongozi wa serikali kuendeleza utamaduni wa
kusema na kutangaza mambo mema yanayofanywa na serikali kwa wananchi pamoja na
kutoa ufafanuzi wa masuala mbali mbali yanayopotoshwa na baadhi ya watu wasioitakia
mema CCM na serikali zake.
Pamoja na hayo aliwambia viongozi vijana walioaminiwa na
kupewa nafasi za uongozi ndani ya Chama na Serikali wafanye kazi zao kwa
uadilifu ili vijana na wananchi kwa ujumla waendelee kuwaamini na kujifunza
mambo mema kutoka kwao.
Mwenyekiti huyo amekemea vikali tabia za baadhi ya vijana
wanaopenda kulalamika bila ya kujituma kufanya kazi kwa kubuni mambo mbali
mbali ya kuwaingizia kipato pamoja na kulitumikia taifa kwa maendeleo endelevu.
Kupitia hafla hiyo ameipongeza CCM Zanzibar kwa juhudi
zake za kuendeleza utamaduni wa
kuwaamini vijana wasomi kwa kuwapatia fursa mbali mbali zinazowasaidia kupata
elimu ya juu na mafunzo ya ujasiriamali bila ya usumbufu.
Aidha Kheir amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein kwa kuipa kipaumbele sekta ya elimu pamoja na kuimarisha Amani na Utulivu wa Zanzibar hatua ambayo imechangia kuharakisha maendeleo ya nchi.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma
Saadalla (Mabodi) amesema Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kulea kitaaluma
vijana wa makundi yote ili waweze kunufaika na rasilimali za nchi.
Amesema CCM Zanzibar inatekeleza mipango mbali mbali ya kuwawezesha
vijana kwa kuwajengea mazingira bora yatakayowawezesha kujiajiri wenyewe na
kuwasaidia vijana wenzao ambao bado hawajafika ngazi ya elimu ya juu.
Pia ameeleza kwamba
taasisi hiyo pia inaendelea na mikakati ya kuanzisha miradi mikubwa ya
ujasiriamali itakayowezesha vijana ambao hawakufika elimu ya juu kuweza
kujiajiri wenyewe.
“Chama chetu kinajali vijana wa makundi yote na sio wasomi
pekee na ndio maana mipango yetu ya kuwajengea uwezo ipo kwa vijana wa makundi
yetu na ndio maana hata nchi yetu imekombolewa na vijana waliokuwa wakwezi na
wakulima.”, amesema Dk.Mabodi.
Mapema Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Tabia Maulid Mwita amesema vijana hao wapo tayari kutumia uwezo wao wote kulinda na kuthamini
mambo mema yanayotekelezwa na Serikali zote mbili chini ya usimamizi wa Chama
Cha Mapinduzi.
Hafla hiyo imeandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar kwa kushirikiana na UVCCM kwa lengo la kuwapongeza vijana 470 wa kidato
cha sita Zanzibar waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza, pili na tatu (Division
I,I na III) mwaka 2018.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni