NAIBU Katibu Mkuu wa
CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi (aliyevaa kanzu na koti nyeusi)
akimfariji ndugu Ali Omar Risasi ambaye ni miongoni mwa majeruhi wa ajali hiyo.
NA IS-HAKA OMAR,
ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa
Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi
amezitembelea na kuzifariji familia za ndugu wa watu watatu waliofariki kwa
ajali ya gari aina ya noah na wengine wanne
kujeruhiwa vibaya.
Waliofariki katika
ajali hiyo ni Francis Haroun (28), Yoana Antony (20) na Suleiman Abdalla Miraj
(18) ambapo majeruhi ni Jabir Ali Mtonga (29), Ali Omar Risasi (17), Said
Masoud (14) na Mudrick Salum Dude.
Akizungumza na
familia hizo Naibu Katibu Mkuu huyo Dk.Mabodi huko katika kijiji cha Ndagaa
Wilaya ya kati Mkoa wa Kusini Unguja alisema CCM imepokea kwa mshutuko,majonzi
na uzuni mkubwa taarifa za ajali hiyo
iliyopoteza maisha ya watu muhimu katika ujenzi wa maendeleo ya kitaifa.
Dk. Mabodi alisema
Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed
Shein amesikitishwa na msiba huo mzito na kuzipa pole familia zote ambazo ndugu
zao wamepata ajali hiyo.
Aliziomba familia
zote ambazo ndugu zao wamefariki kutokana na matukio mbali mbali ya ajili
zilizosababisha vifo hivyo kuwa na subra na uvumilivu kwa kipindi hiki kigumu
na kuwaombea dua na ibada marehemu hao ili mwenyezi mungu awasamehe madhambi
yao na kuwalaza mahali pema peponi amin.
Naibu katibu Mkuu
huyo aliwasihi madaktari na wauguzi wanaowatibu majeruhi walionusurika kifo
kupitia ajali hiyo kuhakikisha wanawafanyia vipimo vya mara kwa mara sambamba
na kutibu majeraha waliyoyapata kwa umakini ili watu hao wapone haraka na
kuendelea na shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Pia Naibu Katibu Mkuu
huyo ameitembelea familia ya marehemu bi.Agata Francis Pius (48) aliyeuawa kwa
kukatwa na mapanga na watu wasiojulikana siku za hivi karibuni.
Akizungumza na ndugu
wa marehemu huyo, Dk.Mabodi amelitaka jeshi la Polisi nchini kukamilisha kwa
wakati upelelezi wa mauaji hayo na kuwakama watu wote waliosababisha kifo hicho
ili wafikishwe katika vyombo vya kisheria.
“ Wananchi wote wa
kijiji cha Ndagaa na vijiji jirani nakupeni pole sana na mendelee kuamini
kwamba CCM ipo pamoja nanyi kwani hiki ni Chama cha kisiasa kilichotokana na
wakwezi na wakulima, na ndio maana tupo karibu na wananchi wa makundi yote bila
kujali tofauti za kisiasa na kidini.”, alisema Dk.Mabodi akiwa katika hali ya
uzuni mkubwa juu ya misiba hiyo.
Mara baada ya
kumaliza ziara maalum ya kuzifariji familia hizo, Dk.Mabodi alizungumza na
Kamati ya siasa ya Tawi la CCM Ndagaa na kuwaagiza viongozi wake kujenga
utamaduni wa kuwatembelea mara kwa mara wananchi wa maeneo hayo ili kubaini
changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.
Alisema kwa sasa
hakuna nafasi ya viongozi na watendaji wa CCM na jumuiya zake kulala na
kusubiri kazi za maofisini bali wanatakiwa kwenda kwa wananchi kuratibu na
kubaini kasoro zilizopo kwa wananchi ili zitatuliwe na taasisi husika.
Mapema akizungumza
Mwenyekiti wa Tawi la CCM Ndagaa, Abdulrahman Abdallah Said alisema kwa niba ya
kamati ya siasa ya Tawi hilo watalifanyia kazi agizo hilo lenye lengo la
kuongeza ufanisi ndani ya Chama Cha Mapinduzi.
Naye Mwenyekiti wa
CCM Mkoa wa Kusini, Ndugu Ramadhan Abdullah Ali alimpongeza Naibu Katibu Mkuu
wa CCM Zanzibar Dk. Mabodi kwa utaratibu wake wa kuwa karibu na wananchi wa
rika zote wakati wote.
Mwenyekiti huyo
alikiri kuwa ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu watatu kwa wakati mmoja na
kuongeza kuwa imeuweka katika simanzi Mkoa huo na kuwasihi madereva wote wa
gari na pikipiki kuendesha vyombo vyao kwa mwendo wa kawaida ili kuepuka na
ajali.
Ajali hiyo iliyotokea
ilitokea katika eneo la Kibuteni Augost 9 mwaka huu ambapo gari aina ya Noah
iliyokuwa na abiria 15 kati ya hao watatu wamefariki hapo hapo na sita
kupelekwa hospitalini wakitoka kijiji cha Ndagaa Wilaya ya Kati na kwenda
kijiji cha Makunduchi harusini.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni