Jumapili, 5 Agosti 2018

BALOZI SEIF ALI IDD AMEITAKA JAMII IJITATHIMINI KUPOROMOKA KWA MAADILI.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar ,  Balozi Seif akilifungua Kongamano la Maadili ya Mtanzania lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mjini  na kufanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakili Kikwajuni.


 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi katika Kongamano la Maadili ya Mtanzania lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi CCM ya  Wilaya ya Mjini.

 MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa Mjini Nd. Ali Othman Said akiwatambulisha Viongozi wa ngazi ya juu walioshiriki na kualikwa kwenye kongamano hilo.

 AKISOMA  Taarifa ya Kongamano hilo Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM  Wilaya ya Mjini, Salama Abass. 

 BAADHI ya washiriki wa kongamano hilo la Maadili ya Mtanzania.

 MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif akiagana na baadhi ya Viongozi wa Kidini walioshiriki katika Kongamano la Maadili mara baada ya kulifungua Rasmi Kongamano hilo.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.


MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi alisema ukosefu wa malezi mazuri ya watoto  katika jamii ndio chanzo cha kuporomoka kwa maadili na utamaduni wa nchi.

Amesema kila mtu anatakiwa kulinda maadili ya nchi kuanzia ngazi za familia kwa lengo la kudhibiti changamoto ya ukiukaji wa maadili isiedelee katika jamii.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua Kongamano hukusu Maadili ya Mtanzania kwa Wilaya ya Mjini lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakili Balozi Seif Ali Iddi amebainisha kuwa  suala la kulinda maadili ya nchi linatakiwa kupewa kipaumbele  kwa kujadiliwa kwa kila ili kulipatia ufumbuzi wa kudumu.

Ameeleza kuwa madhara ya kushuka kwa maadili nchini ni pamoja na kuongezeka kwa vitendo viovu  vikiwemo wizi wa  kutumia nguvu, utumiaji wa Dawa za kulevya, Ubakaji, Ulawiti, unyanyasaji wa Wanawake na Watoto vinaonyesha wazi hali isiyo shuwari kwa upande wa Maadili ya Taifa.

Balozi Seif amesema hali iliyopo ya mmong’onyoko wa Maadili inayoendelea hivi sasa Jamii yenyewe inapaswa iangalie ilipokosea na kutafuta mbinu za haraka za kuirejesha katika hali nzuri.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ambaye pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, alionyesha kukerwa zaidi na vitendo vya udhalilishwaji wa watoto wadogo hasa ubakaji na ulawiti vinavyofanywa na watu wazima ambao ndio waliotegemewa kulinda na kutetea haki za watoto.

“ Taifa linalotokana na mkusanyiko wa Familia nyingi zilizopata malezi ya msingi hujenga Taifa madhubuti lililosheheni Maadili mema yanayokubalika Kitaifa.”, amesema Balozi Seif.

Balozi Seif amefafanua kwamba wimbi kubwa la mtikisiko wa maadili uliojichomoza hivi karibuni katika ngazi ya Familia unaosababishwa na uvunjikaji wa ndoa na kusambaratisha baadhi ya familia.

Balozi Seif alizitaja takwimu za kuvunjika kwa ndoa ambapo jumla ya Talaka 1,819 zimetolewa  hukumu katika kipindi cha Miaka Mitatu kuanzia Januari 2016 hadi Julai 2018 kwa Mahakama ya Mwanakwerekwe pekee.

Amesena na kuongeza kuwa Watoto hasa wale wanaokosa matunzo ya pamoja ya Wazazi wao wote wawili kwa sababu ya kutelekezwa na Baba zao huishia vijiweni na kulelewa na wanavijiwe ambao mara nyingi sio Watu wema.

Akitoa Taarifa ya Kongamano hilo Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM  Wilaya ya Mjini, Salama Abass amesema Wilaya ya Mjini licha ya jitihada zinazochukuliwa na Serikali pamoja na jumuiya hiyo  bado changamoto ya uvunjifu wa maadili inaendelea kuongezeka kwa baadhi ya maeneo.

“ Kufanyika kwa kongamano hili ni utekelezaji wa maagizo ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. John Pombe Magufuli aliyeagiza kila Wilaya ndani ya Jumuiya ya Wazazi ifanye madadiliano ya kutafuta sululisho la kudumu la kurejesha hali ya maadili kuanzia ngazi za familia hadi kitaifa.”, alisema Salama.

Akitoa salamu kwenye Kongamano hilo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma  Saadalla ‘Mabodi’,  alisema kuongezeka kwa vitendo vya kuporomoka kwa maadili vinachafua sifa hadhi ya Zanzibar.

Dk.Mabodi ameeleza kuwa mbali na changamoto hiyo bado pia kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa na kauli zisizofaa zinazohamasisha vurugu na utenfano katika jamii, jambo ambalo pia ni ufunjifu wa maadili.

“Katika jitihada za kulinda dhana ya Mapinduzi ya mwaka 1964 ni lazima kwa pamoja tuenzi na kuendeleza sifa na tabia njema walizotuachia wazee wetu, na kuchukia vikali vitendo viovu vinavyolenga kuangamiza taifa letu vinavyosababishwa na Mmong’onyoko wa Maadili., alieleza Dk. Mabodi.

Wakizungumza kwa wakati tofauti baadhi ya washiriki wa kongamano hilo, wamesema kupotea kwa maadili katika nchi kunachangia kushuka kwa uchumi wan chi pamoja na kupungua kwa nguvu kazi ya vijana ambao ndio waathirika wakubwa wa vitendo vinavyotokana na kuporomoka kwa maadili.

Kongamano hilo kuhusu Mmong’onyoko wa Maadili ya Mtanzania lililoandaliwa na Jumuiya ya wazazi ya CCM Wilaya ya Mjini pamoja na mambo mengine liomejadili mada mbali mbali zikiwemo muelekeo wa mapambano dhidi ya mporomoko wa Maadili, Dawa za Kulevya pamoja na Ukimwi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni