Jumatatu, 6 Agosti 2018

DK.MABODI ATAKA WATOTO YATIMA KUTHAMINIWA

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akizungumza na Watoto yatima wanaolelewa na Kituo kinachomilikiwa na shirika la Direct AID, kilichopo Ijitimai ya zamani Mwanakwerekwe
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi  amesema taasisi hiyo inathamini juhudi na mchango wa kuwasadia watoto yatima zinazofanywa na wadau wa maendeleo kutoka nchi mbali mbali duniani.
Hayo aliyasema wakati alipotembelea Kituo cha kulelea watoto yatima kinachomilikiwa na shirika la Direct AID kutoka nchini Kuwait kilichopo mtaa wa Ijitimai ya zamani Mwanakwerekwe Unguja, Dk. Mabodi alieleza kuwa ameridhishwa na juhudi za kituo kinachowapatia malezi bora watoto yatima wanaolelewa na shirika hilo.
Alisema shirika hilo limekuwa likifanya kazi kubwa ya kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya kijamii hasa uimarishaji wa huduma za maji safi na salama na elimu.
Dk.Mabodi alisema kwamba CCM ikiwa ni taasisi ya kisiasa itaendelea kuwa karibu na mashirika mbali mbali yenye dhamira ya kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali, katika kutatua kero na changamoto za jamii.
Amefafanua kwamba watoto ambao wazazi wao wamefariki wasipotunzwa na kuhudimiwa vizuri wanaweza kukosa haki zao za msingi zikiwemo malezi mazuri na elimu bora.
Alitoa wito kwa wananchi wa maeneo mbali mbali kuwa karibu na Watoto yatima kwani wengi wao wanakuwa wakitengwa na kufanyiwa vitendo vya udhalilishwaji hata kukosa fursa ya kupewa huduma muhimu za kibinadamu.
"CCM tutakuwa karibu zaidi na Direct AID kwani mmeamua kuisaidia jamii yetu nasi lazima tuonyeshe ungwana wetu wa kushirikiana nanyi kutatua changamoto zinazowakabili katika upangaji wa mikakati yenu ya kuisaidia jamii.", alisema Dk. Mabodi.
 Naye Mkurugenzi wa shirika hilo, Nd. Ayman Mohamed alisema shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kuwapatia elimu watoto hao ili waweze kuwa na uwezo wa kujitegemea wenyewe mara baada ya kumaliza muda wa kuishi katika kituo hicho.
Alisema kituo hicho kimeweza kutoa vijana wengi wasomi wanaofanya kazi katika sekta mbali mbali za serikali na binafsi.
Nd.Ayman aliyataja malengo ya shirika hilo kuwa ni kujenga Vituo vya kisasa vya kulelea watoto yatima vitakavyokuwa na shule, vituo vya Afya na vyuo vya masomo ya dini ya kiislamu kwa Unguja na Pemba.
Akizungumza mmoja ya vijana waliolelewa katika Kituo hicho, Mhandisi  Abdulahi Salum Kassim alisema kituo hicho kimemlea akiwa na umri mdogo na kumsomesha hadi ngazi ya elimu ya juu ambapo hivi sasa ni mtumishi serikalini.
Alikiri kuwa mafanikio hayo yametokana na utaratibu mzuri uliowekwa na serikali wa kuruhusu shirika la Direct AID kuwasaidia watoto yatima.
" Shirika hili limenilea nikiwa mtoto mdogo na kunisomesha mpaka nimekuwa mtu mzima mwenye familia ambaye pia nawasaidia vijana wenzangu ambao nao wazazi wao walifariki wakiwa wadogo.", alifafanua Mhandisi Abdulahi.
 Naye Diwani wa Wadi ya Meli nne, Saleh Juma Kinana ambaye pia ni miongoni mwa vijana waliolelewa katika Kituo hicho, alisema watoto yatima wanatakiwa kulelewa na kuthaminiwa kama walivyo watoto wengine katika jamii.
Kituo hicho kinafuata malezi na miongozo ya dini ya Kiislam kina jumla ya watoto 44 ambao ni watoto yatima.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi, akisalimiana na viongozi mbali mbali wakiwemo wa Direct AID na Chama Cha Mapinduzi mara baada ya kuwasili katika kituo hicho.

BAADHI ya watoto yatima wanaolelewa katika Kituo hicho kilichopo chini ya Shirika la Direct AID.

MKURUGENZI wa shirika Direct AID, Ndg.Ayman Mohamed akielezea mikakati ya shirika hilo katika kusaidia
masuala mbali mbali ya kijamii.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akizungumza na Watoto yatima wanaolelewa na Kituo kinachomilikiwa na shirika la Direct AID, kilichopo Ijitimai ya zamani Mwanakwerekwe

Picha ya pamoja ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi, viongozi wa CCM, wasimamizi na walimu wa kituo pamoja na watoto yatima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni