NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ''Mabodi'' akifungua mfereji wa maji safi na salama mara baada ya uzinduzi wake uko shehia ya Magogoni Zanzibar. |
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma
Saadalla’’Mabodi’’ akiwahutubia wananchi wa Wadi ya Ijitimai shehia ya Magogoni
katika hafla ya uzinduzi wa kisima cha maji safi na salama kitachowahudumia
zaidi ya wananchi 2000.
MKURUGENZI wa shirika la Direct AID la nchini Kuwait,
Ayman Mohamed akizungumza katika hafla hiyo ambao ni wadau wa maendeleo
walioshirikiana na SMZ kuchimba kisima hicho.
DIWANI wa wadi ya Ijitimai, Asha Hassan Juma akizungumza katika hafla hiyo. |
BAADHI ya viongozi na wananchi walioudhuria hafla hiyo ya uzinduzi wa kisima. |
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka wananchi kisiwani humo kupuuza hoja dhaifu zinazotolewa
na baadhi ya wanasiasa waliofilisika kisiasa na kifikra ambao wanajali maslahi
yao binafsi kuliko maendeleo ya wananchi.
Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla
Juma Saadalla ‘’Mabodi’’ katika hafla ya uzinduzi wa kisima cha Maji safi na
salama huko shehia ya Magogoni Wadi ya Ijitimai, amesema wanasiasa wa aina hiyo
hawafai kuaminiwa wala kupewa dhamana ya uongozi katika jamii.
Dk. Mabodi alisema suala la kuimarisha miundombinu ya maji
safi na salama limo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, na
linatekelezwa kwa kasi kubwa katika maeneo mbali mbali nchini.
Pia amefafanua kwamba huo ndio ungwana wa CCM
kwani inaahidi na inatekeleza kwa vitendo sio maneno matupu kama wanavyofanya baadhi
ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wanaobeza kila maendeleo yanayoletwa Chama
Cha Mapinduzi kupitia serikali.
Amewambia wananchi hao kuwa CCM kwa sasa inashughulika zaidi
kutatua kero za wananchi, na sio kuangaika na wanasiasa walioshindwa kujenga
hoja zao sehemu husika na badala yake wanatafuta makubaliano sehemu
zisizostahiki.
“Kuna watu mpaka sasa wanaota ndoto za mchana kwa kusema kuwa
eti 2020 hakuna uchaguzi sasa nawambia kama 2016 walitia mpira kwapani
wakakimbia na uchaguzi ukafanyika na huo pia wa 2020 utafanyika na hakuna wa
kuzuia.
CCM tunawambia tutaendelea kuwaletea wananchi
maendeleo na kulinda amani na utulivu wa Zanzibar kwa gharama yoyote na
anayetaka kuhatarisha amani basi ajaribu na aone .”, amesisitiza Dk. Mabodi.
Naibu Katibu Mkuu huyo Dk.Mabodi aliwasihi wananchi
kuendelea kuiunga mkono CCM kwani hakuna mtu yeyote wa kuzuia Serikali chini ya
Chama Chama Mapinduzi isitekeleze wajibu wake wa kuleta maendeleo endelevu kwa
wananchi wake.
Akizungumzia uzinduzi huo wa maji safi na salama, Dk.
Mabodi aliwapongeza washirika wa maendeleo wa kampuni ya Direct AID kutoka
nchini Kuwait kwa kuchimba kisima hicho kitakachotoa huduma ya maji kwa
wananchi wa shehia ya magogoni na maeneo jirani.
Alieleza na kuongeza kuwa wadau wa maendeleo
wanavutiwa kuwekeza katika miundombinu ambayo ni muhimu kwa maisha ya kila siku
kwa wananchi kutokana na sera mazingira rafiki ya uwepo wa Amani na Utulivu wa
kudumu unaoletwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aliwataka wananchi wa Wadi ya Ijitimai na shehia zake
kulinda na kukitunza kisima hicho kisiharibiwe na baadhi ya watu wanaohujumu
maendeleo ya serikali kwa makusudi.
Dk.Mabodi aliahidi kuwa Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar
chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Dk.Ali Mohamed Shein itachangia mipira ya
kusambazia maji kutoka katika kisima hicho kwenda kwa wananchi.
Pamoja na hayo alisema serikali kupitia mamlaka ya
Maji Zanzibar (ZAWA) inatekeleza mradi mkubwa wa maji safi na salama nchini
ambao utakamilika kabla ya mwaka 2020 ili wananchi waendelee kupata huduma hiyo
kwa uhakika.
Dk.Mabodi amekemea tabia ya baadhi ya wananchi
wanaochimba visima vya maji na kugawa maji hayo kwa misingi ya itikadi za
kisiasa, jambo ambalo alidai kuwa sio utamaduni mzuri.
Alisema utekelezaji wa miradi mbali mbali inayofanywa
na Serikali ya CCM ni moja ya malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyokuwa na
dhamira ya kuleta usawa, ustawi wa kijamii, maendeleo kwa wote na wananchi
kujitawala kiuchumi na kijamii.
Kupitia hafla
hiyo pia Dk. Mabodi alitoa zawadi ya nguo mbali mbali kwa niaba ya shirika la
Direct AID, zitakazowasaidia wananchi wa maeneo hayo.
Katika Risala ya wananchi wa shehia ya Magogoni,
wameshukru wadau nwa maendeleo wa Direct AID kwa kushirikiana na serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuchimba kisima hicho kitakachopunguza tatizo la ukosefu wa maji wananchi wa shehia
hiyo na shehia jirani.
Kwa upande wake Diwani wa Wadi ya Ijitimai, Asha
Hassan Juma alisema uchimbaji wa kisima hicho ni mwendelezo wa utekelezaji wa
miradi mbali mbali ya kijamii inayotekelezwa katika wadi hiyo.
Naye Mkurugenzi wa shirika la Direct Aid kutoka nchini
Kuwait, Ayman Mohamed alisema kisima hicho ni mwendelezo wa visima mbali mbali
vilivyojengwa nchini kwa ajili ya kuondosha tatizo la maji kwa jamii.
Alisema kwamba shirika hilo litaendelea kushirikiana
kwa karibu na serikali kutatua changamoto za kijamii zikiwemo kuchimba visima
vya maji safi na salama ambavyo ni miongoni mwa sadaka ya kuendelea kwa
wananchi wa makundi yote.
Kisima hicho kilichogharimu milioni 50 kinatarajia
kuwahudumia wananchi zaidi ya 2000 wa maeneo mbali mbali ya wadi ya ijitimai na
shehia zake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni