KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa Dk. Bashiru Ally. |
NA IS-HAKA OMAR,
ZANZIBAR.
KATIBU Mkuu wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) Dk.Bashiru Ally anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku
nne visiwani humu Agosti 17 hadi 20 mwaka huu.
Dk.Bashiru anafanya ziara
hiyo kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo Mei mwaka huu baada
ya aliyekuwa Katibu Mkuu Abdulrahman Omar Kinana kustaafu.
Akitoa taarifa ya ziara
hiyo ya Katibu Mkuu huyo, Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu Taifa(NEC),Idara
ya Itikadi na Uenezi CCM, Zanzibar Catherine Peter Nao, alisema CCM Zanzibar
tayari kimekamilisha maandalizi yote ya mapokezi ya kiongozi huyo.
Catherine alisema katika
ziara yake hiyo pamoja na mambo mengine anatarajia kuzungumza na viongozi mbalimbali
wa CCM na jumuiya zake na makundi ya kutoka taasisi za vijana visiwani humu.
Aliongeza kuwa ziara
hiyo ya Dk.Bashiru itakuwa ni ya kikazi na kujitambulisha kwa wana-CCM ambapo wanatakiwa
kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Katibu Mkuu huyo ambapo atawahutubia
wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla katika uwanja wa Ofisi Kuu ya CCM
Kisiwandui saa 9 alasiri.
“Tunawaomba wanachama
wote tujitokeze kwa wingi kushiriki mapokezi hayo ya kiongozi wetu mpendwa ambaye
ni mara ya kwanza kuja tukitambulisha na kuzungumzia sera na masuala mbalimbali
ya kuimarisha CCM na Jumuiya zake, alisema Catherine.
Akizungumzia ratiba
ya ziara hiyo Katibu huyo wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar,Catherine
alisema siku ya siku ya kesho Agosti 17 mwaka huu katibu Mkuu huyo atakutana na
kuzungumza na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Katibu huyo aliongeza
kuwa Dk.Bashiru anatarajia kukutana na na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye
pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.
Alisema mchana wa
siku hiyo ya ijumaa atazuru Kaburi la Muasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar
Hayati Mzee Abeid Karume na kuzungumza na watumishi pamoja na Wazee wa CCM
Zanzibar ambapo jioni atazungumza na Viongozi na wanachama wa Mikoa minne ya
CCM Unguja hapo katika viwanja vya CCM Kisiwandui.
Catherine aliendelea
kueleza kuwa jumamosi ya Agosti 18 mwaka huu Katibu Mkuu huyo atazungumza na
Wenyeviti wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Makatibu wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Kamati
za siasa za Mikoa na Wilaya, Wabunge, Wawakilishi na madiwani katika ukumbi wa
Kamati Maalum Kisiwandui pamoja na kuzungumza na makundi ya vijana katika
ukumbi wa CCM Mkoa wa mjini.
Aliongeza kuwa siku
ya Jumapili Agosti 19, mwaka huu Katibu Mkuu huyo asubuhi atasafiri kuelekea
Pemba kwalengo la kuendelea na ziara yake hiyo ambapo atazungumza na Watumishi
wa CCM na wazee wa Pemba katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Kitengo.
Katibu huyo alisema
Dk.Bashiru anatarajia kuzungumza na viongozi na wanachama wa CCM wa Mikoa miwili
katika ukumbi wa skuli ya Fidel Castro Mkoa wa Kusini Pemba na jioni
anatazungumza na Wenyeviti wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Makatibu wa CCM wa Mikoa
na Wilaya, Kamati za siasa za Mikoa na Wilaya, Wabunge, Wawakilishi,madiwani na
maafisa wadhamini katika ukumbi wa Makonyo Pemba.
Katibu Mkuu huyo atahitimisha
ziara yake hiyo siku ya Juma tatu Agosti 20 mwaka huu, kwa kuzuru kaburi la Dk.Omar
Ali Juma kisiwani Pemba na kumalizia ziara yake kwa kuzungumza na makundi ya vijana ambapo jioni atasafiri
kuelekea Dar es salaam kuendelea na majukumu mengine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni