MWAKILISHI wa Jimbo la Kwahani, Mhe Ali Salum Haji akifungua mafunzo ya Darasa la Itikadi katika Tawi la CCM Sebleni. |
KATIBU wa Siasa na Uenezi CCM Wilaya ya Mjini, Ndugu Fatma Haji Mohamed akizungumza na vijana na Wana CCM katika hafla hiyo ya ufunguzi wa Darasa la Itikadi. |
MWALIMU wa Darasa hilo Ndugu Abdallah Juma Nafaika akitoa nasaha zake katika hafla hiyo. |
BAADHI ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia kwa makini nasaha mbali mbali zinazotolewa na viongozi katika hafla hiyo. |
NA
IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
VIJANA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameshauriwa
kujiunga na madarasa ya itikadi ili kunufaika na fursa mbali mbali zikiwemo kujua
historia halisi ya Zanzibar, mwenendo wa kisiasa, uzalendo pamoja na elimu ya kujitambua.
Ushauri huo umetolewa na Mwakilishi wa Jimbo la
Kwahani Zanzibar Ali Salum Haji wakati
akifungua mafunzo ya darasa la Itikadi katika Tawi la CCM Sebleni Zanzibar.
Amesema baadhi ya vijana wa CCM wanapoteza muda katika
vikundi visivyokuwa na faida badala ya kujiunga na madarasa hayo kwa lengo la kupata
elimu juu ya masuala ya siasa na
historia.
Amefafanua kuwa mafunzo ya itikadi ndio njia mbadala ya kuwakomboa kifikra vijana wa Chama Cha Mapinduzi ili wawe makada imara wenye misimamo isiyoyumba kisiasa, kiungozi na kiitikadi.
“ Vijana someni
historia ya nchi yetu kwani kuna mambo mengi yanayopotoshwa na wapinzani kwa
makusudi ili vijana mtoke katika msimamo wenu wa kulinda na kutetea maslahi ya
Chama Cha Mapinduzi.”, amesema Salum.
Kupitia ufunguzi wa mafunzo hayo Mwakilishi huyo amesisitiza umuhimu
wa Wana CCM kuifanyia kazi falsafa ya siasa na uchumi ili kuwa wabunifu wa
kutumia vizuri fursa zilizowazunguka katika mazingira wanayoishi kwa lengo kujipatia
kipato cha kujikwamua kiuchumi.
Pia ameahidi kuwalipia mafunzo ya ujasiriamali vijana wote
watakaohitimu mafunzo hayo ya itikadi ili baada ya kupata ujuzi wajiajiri
wenyewe.
Naye Katibu wa Siasa na Uenezi CCM Wilaya ya Mjini, Fatma
Haji Mohamed amesema ufunguzi wa darasa hilo ni miongoni mwa mikakati
ya kudumu iliyopangwa na Wilaya hiyo kupitia mpango kazi wao.
Amesema lengo
la kuanzia mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo vijana na wananchama juu ya kutambua masuala ya Itikadi na Siasa zinazoendana na zama za sasa katika ushindani wa
kisiasa.
Amesema mpango huo utakuwa endelevu katika Matawi na Wadi
zote za Wilaya hiyo sambamba na kuwapatia vijana hao elimu ya ujasiria mali.
Jumla ya vijana 76 wameanza mafunzo hayo katika Tawi
la Sebleni, na yatachukua muda wa miezi mitatu.