KATIBU mpya wa Idara
hiyo Ndugu Kombo Hassan Juma akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Ofisi ya Idara ya Siasa na uhusiano wa Kimataifa (SUK) CCM Zanzibar. |
KATIBU mstaafu wa Idara hiyo Eng. Hamad Yussuf Masauni(kushoto) akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano, Katibu mpya wa Idara hiyo Ndugu Kombo Hassan Juma(kulia aliyekaa). |
BAADHI ya Maafisa wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa(SUK) CCM Zanzibar. |
Afisa wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa
Kimataifa(SUK) CCM Zanzibar Ndugu Mzee
Khatib Abdallah akifuatilia kwa makabidhiano hayo.
NA IS-HAKA OMAR,
ZANZIBAR.
KATIBU wa Kamati Maalum
ya NEC, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa CCM Zanzibar, Ndugu Kombo
Hassan Juma amesema ushindani wa kisiasa na mbinu za upinzani zinazidi
kuongezeka hivyo Chama tawala ni lazima kiwe imara kukabiliana na mabadiliko
yanayotokea katika uwanja wa kisiasa nchini.
Kauli hiyo ameitoa leo
katika hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi ya Idara hiyo yaliyofanyika katika
Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, amesema wanachama, viongozi na watendaji
wa Chama Cha Mapinduzi wanatakiwa kubadilika na kuondokana na mazoea ya siasa
za wakati wa mfumo wa chama kimoja na badala yake waendane na siasa za ushindani.
Ameeleza kuwa ni lazima
CCM iendelee kujifunza baadhi ya mbinu na mikakati ya kisiasa iliyopo katika vyama
vingine vya kisiasa ili Chama kiweze kukabiliana na sera za vyama vyenye lengo
la kukikondosha madarakani.
Katibu huyo mpya wa
Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ndugu Kombo alisema kazi kubwa ya CCM
ni kusimamia viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali waliopewa dhamana ya
uongozi na wananchi wahakikishe wanatekeleza wajibu wao kwa ufanisi.
“ Tutaendelea
kuikumbusha serikali mara kwa mara waendelee na kasi hiyo hiyo ya utekelezaji
wa Ilani kwani ndio sehemu pekee ya mtaji wetu kisiasa ambao tunaamini ipo siku
wananchi watahoji nini tumetekeleza katika maeneo yao”, amesema Ndugu Kombo.
Aidha Ngugu Kombo
amemshukuru Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa
kumuamini kwa kumteuwa awe Mkuu wa Idara hiyo na kuongeza kuwa atafanya kazi
kwa bidii ili CCM ishinde na kubaki madarakani katika uchaguzi Mkuu ujao.
Naye Katibu Mstaafu wa
Idara hiyo Eng. Hamad Yussuf Masauni amesema ana imani kuwa idara hiyo
ameikabidhi mikononi mwa Kiongozi makini mwenye uzoefu na weledi mkubwa ndani
ya CCM na Serikali kwa ujumla.
Amesema Idara hiyo ndio
moyo wa Chama kwani ina dhamana ya kufuatilia hali ya kisiasa nchini pamoja na kuendeleza
mahusiano mazuri na taasisi na wadau mbali mbali wa Kimataifa ili kukuza
urafiki na ustawi wa kijamii baina ya Chama na taasisi hizo.
Hata hivyo amewasihi
watendaji wa SUK Chama na Jumuiya kwa ujumla kumpa ushirikiano Katibu mpya ili
kuimarisha shughuli za kisiasa na kiuchumi ndani na nje ya CCM.
Mapema Mkuu wa Sehemu
katika Idara hiyo Ndugu Khamis Haji Khamis amesema makabidhiano hayo ni fursa
kwa watendaji hao kutumia ujuzi na uzoefu wao katika kubuni mipango mbali mbali
ya kiutendaji itakayoleta maendeleo ndani ya CCM.
Hafla hiyo imekuja mara
baada ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kuteuwa Wakuu
wa Idara mbali mbali za Chama ikiwemo Idara ya Siasa na uhusiano wa
Kimataifa Zanzibar(SUK) ili waongoze idara hizo kwa miaka mitano ijayo.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni