NA EMMANUEL MOHAMED, ZANZIBZR
NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa wa Chama Cha Mapinduzi(CCM),Najma Murtaza Giga, amewataka mawakili wa kujitegemea kutojiingiza katika kuwatetea watu wanaofanya vitendo vya udhalilishaji.
Amesema vitendo hivyo vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku visiwani humu ambapo imefika wakati watu hao wasionewe aibu ama muhali kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.
Hayo aliyasema jana katika ufunguzi wa kikao cha Baraza la Jumuiya hiyo Mkoa wa Mjini, Naibu huyo alisema baada ya wananchi kupata elimu ya kutosha katika kujitokeza kutoa ushahidi sasa imebakia vyombo vya sheria kutoa ushirikiano kwao.
Najma aliongeza kuwa miongoni mwa majukumu ya jumuiya hiyo ni kukemea hali hiyo ambapo ni sehemu ya mmonyoko wa maadili kwa jamii na kwamba jumuiya inapaswa kuwa mstari wa mbele katika mapambano hayo.
"Sisi kama wanajumuiya tunawataka mtu ambaye amefanya vitendo hivyo wasisitetewe kutokana na nafasi yake ama kwa sababu anafanya kazi kutoka serikalini au sekta binafsi hivyo suala hili halitakiwi kuacha kiholela,"alisema
katika maelezo yake Naibu huyo alisema jambo hili haitakiwi kutetewa ama kukingiwa kifua mtu ambaye anafanya vitendo hivyo akiwa ana nafasi ya kiongozi ama vyovyote vile.
"CCM tushatoa tamko kuwa yeyote aliyefanya akiwa mfanyakazi wa serikali ama kiongozi hatakiwi kutetewa mtu yeyote atakayekuwa anafanya vitendo hivyo,"alisema
Kwa upande wake Katibu wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Zanzibar, Kombo Hassan Juma, alisema jukumu la jumuiya ya wazazi ni kuhakikisha maadili ya jamii hayaharibiki.
Alisema jumuiya ya wazazi ina kazi ya kuwalea watoto na kwamba inapaswa kuwahamasisha vijana kutambua maadili ya jamii na kufanya kila mbinu kutekeleza kwa vitendo maneno yanayosemwa samaki mkunje angali mbichi.
Katibu huyo aliongeza kuwa jumuiya hiyo inapaswa kuwaaminisha vijana kuwa bila ya CCM nchi haitawezekana kwa kufanya hivyo itasaidia kurahisisha kazi za chama.
Awali Katibu huyo wa Idara hiyo alikabidhiwa gari aina ya "Hiace Custom" kwa jumuiya hiyo ya mkoa wa Mjini kwa ajili ya shughuli za kikazi ambapo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Najma.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mjini, Ali Othaman, alishukuru kwa kupewa gari hilo ambalo litasaidia kurahisisha shughuli za kikazi za jumuiya hiyo.
Mwenyekiti huyo alisema gari hilo litatumika kwa utaratibu ambao utakuwa rahisi kutumika kwa kila ngazi ikiwemo jimbo, tawi, jumuiya hadi chama na kwamba ikiwezekana kukodisha kwa ajili ya biashara na kitakachopatikana kitagawewa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni