KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Ikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Bi, Catherine Peter Nao akizungumza mara baada ya kuwasili katika studio za Swahiba Fm iliyopo Mbweni Zanzibar. |
KATIBU wa Kamati
Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndugu Catherine Peter
Nao akizungumza mara baada ya kuwasili katika studio za Chuchu FM iliyopo
Mlandege Zanzibar. |
MKUU wa Vipindi Chuchu Fm, Mulhat Doria(wa kwanza kulia aliyevaa mtandio wa rangi nyekundu) akizungumza na ujumbe wa ugeni huo kutoka CCM Zanzibar. |
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
TASNIA ya Habari ni sekta muhimu inayoziwezesha Serikali mbali mbali Duniani kuimarisha dhana ya Demokrasia kupitia matangazo na taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Chama tawala, miongozo na mipango ya maendeleo ili wananchi wajue uwajibikaji wa serikali yao na kupima uhalisia wa sera zinazotekelezwa kama zinakidhi mahitaji yao.
Maelezo hayo yametolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Bi. Catherine Peter Nao katika mwendelezo wa ziara yake katika vyombo Zanzibar, kutokana na umuhimu wa sekta hiyo Katibu huyo ameagiza viongozi na watendaji wa Chama na Serikali kupanga utaratibu wa kuzungumza na vyombo vya Habari mara kwa mara ili waweze kuwaeleza wananchi utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku katika taasisi zao.
Catherine amesema kiongozi yeyote mwenye dhamana ya kutoa taarifa za Chama ama Serikali atakayekataa kuzungumza na vyombo vya habari atakuwa anaenda kinyume na falsafa ya CCM mpya na Tanzania mpya inayotaka Chama kirudi mikononi mwa wananchi kwa kuanza na hatua ya kuwapatia taarifa sahihi zinazohusu masuala ya maendeleo.
Amesema kiongozi anayetekeleza wajibu wake vizuri hawezi kuwa na hofu ya kuzungumza na vyombo vya habari, hivyo ni lazima watumishi hao wa umma kukubali mabadiliko ya zama mpya za utandawazi zinazotoa fursa ya wananchi kuhoji na kudadisi viongozi waliowapa dhamana nini wamefakanya katika maeneo yao.
“Serikali ya Mapiunduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein imefanya mambo mengi mazuri lakini cha kusikitisha wananchi wengi hawajui serikali yao nini inafanya kutokana na baadhi ya Viongozi wenye dhamana ya kuzungumza wapo kimya”, alisema Catherine.
Agizo hilo limetolewa baada ya Vyombo vya Habari mbali mbali nchini kulalamikia urasimu usikuwa na tija wa baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Chama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kutotoa ushirikiano kwa taasisi za kihabari hali inayosababisha baadhi ya vyombo hivyo kutoa taarifa za upande mmoja baada ya kukosekana ushirikiano kutoka kwa viongozi wa umma.
Pia amewapongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa juhudi zao za kusimamia na kutekeleza ilani ya CCM kwa kasi kubwa hatua inayoleta furaha ya kudumu kwa wananchi.
Hata hivyo Katibu huyo amesema licha ya kuwepo na changamoto mbali mbali za kiutendaji bado CCM inaendelea kubaki katika msimamo wake kwa mujibu wa Ibara ya tano ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 kwa kuhakikisha mwaka 2020 CCM inashinda katika Uchaguzi wa ngazi zote na kubaki madarakani.
Ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kujitambulisha kwa vyombo hivyo ambavyo ni wadau wakubwa wa Chama Cha Mapinduzi ili waweze kufanya kazi kwa ushirikiano kwa maslahi ya wananchi.
Akizungumza Mkurugenzi wa Swahiba FM Radio, Maalim Kassim Mohamed Kassim alisema Vyombo vya habari vipo kwa ajili ya wananchi hivyo kiongozi yeyote aliyepewa dhamana na wananchi ana wajibu wa kutoa ushirikiano kwa taasisi hizo.
Mkurugenzi huyo amekishauri Chama Cha Mapinduzi kukaa pamoja na viongozi wa Serikali hasa mawaziri na wakurugenzi kuwasihi watoe ushirikiano kwa kituo chake pindi wanapohitajika kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala mbali mbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Naye Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, Yussuf Khamis Yussuf amesema Shirika hilo litaendelea kutoa habari mbali mbali zinazohusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, huku wakizingatia kanuni na miongozi ya maadili ya Tasnia ya habari.
Naye Meneja wa Chuchu Fm Salma Ahmed Alley, amesema pamoja juhudi za taasisi hiyo katika kuelimisha, kuhabarisha, kukosoa na kuhamasisha amani na utulivu bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa matangazo ya biashara kutoka Serikalini na taasisi zingine hali inayosababisha baadhi ya wakati chombo hicho kuyumba kifedha.
Pamoja na hayo Salma amesifu juhudi za Katibu huyo wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Bi. Catherine kwa ujasiri wake wa kuvithamini vyombo vya habari na kufungua milango ya ushirikiano wa kudumu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni