Jumanne, 6 Machi 2018

KATIBU WA IDARA YA ORGANAZESHENI CCM Z'BAR ,BAKARI-AFANYA ZIARA MKOA WA KASKAZINI UNGUJA

 VIONGOZI  wa CCM Wilaya ya Kaskazini ‘A’ wakimkaribisha mgeni rasmi ambaye ni Katibu wa Kamti Maalum ya NEC, Idara ya organazesheni CCM Zanzibar ndugu Bakari Hamad Khamis katika ziara ya kujitambulisha kwa Secretarieti ya CCM ngazi za majimbo na Wilaya.

 BAADHI ya wajumbe wa Sekreterieti za majimbo na Wilaya ya Kaskazini ‘A’ wakimlaki mgeni rasmi mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Wilaya iliyopo Gamba Mkoa wa Kaskazini Unguja.

 KATIBU mwenezi CCM Wilaya kASKAZINI ''A'' Ali Chum Haji(kulia aliyesimama akizungumza), Katibu wa idara ya organazesheini CCM Zanzibar Bakar Hamad (katikati).

 Katibu wa Kamti Maalum ya NEC, Idara ya organazesheni CCM Zanzibar ndugu Bakari Hamad Khamis akizungumza na watendaji hao katika ziara ya kujitambulisha kwa Secretarieti ya CCM ngazi za majimbo na Wilaya ya Kaskazini ‘’A’’.

 KATIBU wa CCM Wilaya ya Kaskazini ‘’B’’ Ndugu Subira Mohamed Ameir (kulia) akizungumza baada ya mgeni rasmi kuwasili katika Wilaya hiyo kwa lengo la kujitambulisha.

 KATIBU wa Kamti Maalum ya NEC, Idara ya organazesheni CCM Zanzibar,ndugu Bakari Hamad Khamis  akizungumza na Kamati za Secretarieti ya CCM ngazi za majimbo na Wilaya.

BAADHI ya wajumbe wa Sekreterieti za majimbo na Wilaya ya Kaskazini ‘A’ wakimlaki wakisikiliza na kufuatilia nasaha za mgeni rasmi.
 KATIBU wa Kamti Maalum ya NEC, Idara ya organazesheni CCM Zanzibar ndugu Bakari Hamad Khamis akisisitiza umuhimu wa watendaji kuisoma na kuielewa Katiba ya CCM ya mwaka 1977.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.


KATIBU wa  Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar ,Ndugu Bakari  Hamad Khamis amesema wanachama na watendaji wa CCM wanatakiwa kuandaa mipango endelevu ya kuhakikisha Chama kinashinda na kubaki madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Rai hiyo ameitoa katika ziara yake ya kujitambulisha kwa watendaji wa Chama na Jumuiya zake ambao ni wajumbe wa Sekreterieti za Wilaya na Majimbo ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, amesema Chama Cha Mapinduzi ili kishinde ni lazima maandalizi ya ushindi wake yaanze kwa sasa.

Alieleza kuwa pamoja na mambo mengine lengo la ziara hiyo ni kuwakumbusha watendaji hao majukumu yao ya msingi wanayotakiwa kuyafanyia kazi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Amesema CCM ikiwa katika mfumo wa vyama vingi vya siasa ni lazima ifanye kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi wote bila ya ubaguzi.

Katibu huyo wa NEC ndugu Bakari, aliwambia Watendaji hao kuwa wanatakiwa kutumia uwezo wao wa kisiasa kuhakikisha baadhi ya majimbo yaliyopo katika mikono ya wapinzani yanarudi katika milki ya   Chama Cha Mapinduzi.  

“Dhana ya CCM mpya na Tanzania mpya sio upya wa kuwa ndio kimezaliwa leo bali ni kufanya kazi kwa bidii ili wananchi wanufaike na fursa zinazopatikana kwa serikali iliyotokana na Chama Cha Mapinduzi”, alisema Bakari.

Pia alisisitiza umuhimu wa viongozi na watendaji wa Chama na Serikali kutekeleza kwa wakati ahadi zilizotolewa katika kampeni za Uchaguzi uliopita kwa lengo la kumaliza madeni hayo ya kisiasa.

Aliwataka watendaji hao kusimamia utaratibu wa uimarishaji wa maskani za Chama hasa za vijana kwa lengo la kuongeza wanachama hai watakaofuata itikadi na siasa za CCM kwa vitendo.

Pia aliwaagiza Makatibu hao kuhakikisha wanaimarisha vikundi vya hamasa na burudani katika maeneo yao ili wanachama na wananchi kwa ujumla wapate sehemu ya kukutana mara kwa mara na kubadilishana mawazo.

Alisema  mabadiliko ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 yamebeba dhamira ya kuleta mageuzi ya kiutendaji kwa kila ngazi ya Chama na Jumuiya zake.

Sambamba na hayo amewataka baadhi ya watendaji wa ngazi za matawi hadi Mkoa wenye tabia za kutofungua Ofisi zao kwa wakati kuacha utamaduni huo na badala yake watekelezze wajibu wao ili wanachama wapate sehemu ya kuwasilisha changamoto zao.

Naye Katibu mwenezi Wilaya ya Kaskazini ‘A’  Ndugu Ali Chum Haji, alisema maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu huyo wa Idara ya orgazanesheni yatafanyiwa kazi kwa wakati ili kwenda sambamba na siasa za maendeleo kwa jamii.

Kwa upande wake  Katibu wa CCM Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Ndugu Subira Mohamed Ameir amesema Wilaya hiyo inakabiliwa na Changamoto mbali mbali za kijamii na kisiasa zinazotakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu kupitia busara, hekima na uadilifu wa viongozi wakuu wa Chama na Serikali kabla ya uchaguzi Mkuu ujao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni