Jumapili, 23 Septemba 2018

KAMATI MAALUM YA NEC CCM TAIFA Z'BAR YATOA MILIONI TANO KWA AJILI YA RAMBIRAMBI ZA AJALI YA MV.NYERERE.

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akiongoza Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar,  kilichofanyika leo Afisi Kuu ya CCM iliyopo Kisiwandui Zanzibar.
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akisoma ajenda za Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar, kilichofanyika leo Afisi Kuu ya CCM iliyopo Kisiwandui Zanzibar.


 MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein(aliyekuwepo katikati),Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (wa pili kushoto), Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd(wa kwanza kushoto)pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi(wa kwanza kulia) wakiwa wamesisima kwa ajili ya kutoa heshima na kuomboleza Maafa ya Ajali ya Kivuko cha MV.Nyerere iliyotokea Mkoani Mwanza Septemba 20, mwaka 2018 katika Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar kilichofanyika leo katika Afisi Kuu ya CCM iliyopo Kisiwandui Zanzibar.

 MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein akizungumza na Wajumbe wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar katika Kikao kilichofanyika leo Kisiwandui kwa ajili ya kujadili majina ya Wagombea Uwakilishi wa CCM katika Jimbo la Jang'ombe.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla (kushoto) akisalimiana na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd (kulia) mara baada ya kuwasili Afisi Kuu CCM kwa ajili ya Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar.

 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa  CCM Zanzibar Mwl.Kombo  Hassan Juma (kushoto) akisalimiana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan baada ya kuwasili katika Mkutano wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya  CCM  Taifa  Zanzibar. 
 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Katibu wa Kamati  Maalum ya NEC, Idara ya Uchumi na Fedha CCM Zanzibar  Ndugu Hafadhali Taibu Hafadhali (kushoto) akisalimiana na Makamu wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd(kulia) baada ya kuwasili Kisiwandui kwa ajili ya Kikao cha Kamati Maalum ya  Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar. 


 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikabidhi Mabati 180 ya kuezekea Tawi la CCM Urusi lililopo Jang'ombe ikiwa ni Utekelezaji wa ahadi zake alizotoa katika ziara yake ya Kichama Zanzibar April 6, mwaka 2018.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar kilichofanyika Kisiwandui. Picha na Afisi Kuu CCM Zanzibar.



KAMATI Maalum ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa Zanzibar,imetoa salamu za rambi rambi kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk.John Magufuli kwa kutokea na ajali ya kivuko cha MV Nyerere ambayo imesababisha vifo vya zaidi ya watu 100 katika kisiwa cha Ukara.

Akitoa salamu hizo leo katika kikao cha Kamati hiyo Mjini Unguja Makamu Mwenyekiti wa CCM, Dk.Ali Mohamed Shein ambaye ni Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
amesema kamati hiyo imesikitishwa na ajali hiyo ambayo imetokea Septemba 20 mwaka huu katika kisiwa hicho Mkoani Mwanza.

Makamu huyo Mwenyekiti wa Taifa CCM aliongeza kuwa taarifa hiyo ya ajali ambayo imesababisha vifo vya watu wengi imewasikitisha wana-CCM kwa upande wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) na kwamba Zanzibar iko pamoja katika kuomboleza msiba huo mkubwa wa taifa.

"Taarifa iliotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Dk.John Magufuli ya uamuzi wa Serikali kuomboleza siku nne ni dhahiri kuwa ni msiba mkubwa kwa Tanzania sisi kwa upande wa Zanzibar tulikuwa na sherehe mbili kubwa tumeziharisha zote kwa kuwa tunaomboleza kwa maagizo ya Rais Dk.Magufuli,"amesema Dk.Shein

Rais Dk.Shein amesema ilitarajiwa kufanywa sherehe kubwa za Elimu bila malipo na kuwatunuku zawadi wanafunzi wa kidato cha sita waliofaulu lakini shughuli hizo zimeaharishwa kutokana na ukubwa jambo hilo.

Dk.Shein ameeleza kuwa sherehe zote zilizotakiwa kufanyika visiwani humu zimeharishwa kutokana na kuwepo kwa msiba huo mkubwa na kwamba Zanzibar inaungana na ndugu na jamaa katika kuomboleza.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM,Zanzibar Dk.Abdulla Saadalla Juma 'Mabodi' kwa niaba ya Kamati hiyo Maalum ya Halmashauri Kuu amesema imetoa shilingi milioni tano kwa ajili ya mchango wa rambirambi wa msiba huo na kwamba kiasi hicho ni cha kuanzia.

Alisema CCM kwa upande wa Zanzibar ina ungana na wafiwa wote wa msiba huo na kwamba chama kitaendelea kutoa mchango wake kadri mahitaji yatakapohitaji.

"Kabla ya kuanza kikao chetu tumefungua kwa dua ya kuwaombea waliofariki katika ajali hiyo na hatujaishia hapo tumetoa tamko rasmi la kuhusu msiba huu kwa ujumla tunawapa pole na tunawaomba kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu,"alisema Dk.Mabodi

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo ameleeza kwamba CCM kwa upande wa Zanzibar inawaomba watanzania kutotumia msiba huo kwa kuwagawa wananchi kisiasa na hivyo wanatakiwa kuwa wamoja.

Amesema Kamati Maalum inawaomba wanafamilia,ndugu na jamaa wa marehemu na majeruhi katika ajali hiyo kuendelea kuwa na hali ya subira wakati wa kipindi hicho cha msiba huo mkubwa.

"CCM kinaamini kuwa Serikali itafanya uchunguzi wa kina wa tukio hili ili kubaini kilichotokea na kwamba watebdaji wetu watakwenda kuungana na viongozi wenzetu huko Tanzania bara katika kusaidia kuungana kuomboleza,"ameeleza Dk.Mabodi

Ajali hiyo imetokea Septemba 20 mwaka huu katika majira ya saa 6 mchana katika ziwa Victoria wakati ikiwa kwenye safari yake ya kutoka Bugorola kuelekea kisiwa cha Ukara.

Mbali na hilo, Naibu huyo Katibu Mkuu amefafanua kuwa katika kikao hicho cha kamati Maalum ya Halmashauri kuu kilichokutana mjini Unguja pia kimewajadili wagombea watatu wa nafasi ya uwakilishi jimbo la Jangombe katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 27 mwaka huu.

Dk.Mabodi amesema  baada ya wajumbe wa kamati hiyo kuwapa alama wagombea hao ndipo majina hayo yatapelekwa Kamati Kuu kwa ajili ya kuchagua jina moja litakalopeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo.

Pia ameeleza kuwa maandalizi ya kampeni katika jimbo hilo la Jangombe yako vizuri na kwamba CCM itashinda kwa asilimia kubwa kwenye uchaguzi huo.  

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan amekabidhi mabati 180 kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM,Zanzibar Dk.Abdulla Saadalla Juma 'Mabodi' ikiwa sehemu ya utekelezaji wake wa ahadi aliyotoa katika ziara yake ya Kichama aliyofanya miezi kadhaa iliyopita huko katika Tawi la CCM Urusi Jang'ombe.

Makamu huyo wa Rais amesema katika ziara yake ya kichama Pemba na Unguja matawi mengi ya vijijini na mjini waliomba msaada wa mabati hayo kwa ajili ya kuyaweka katika matawi hayo.

Ijumaa, 21 Septemba 2018

DK.SHEIN AWEKA JIWE LA MSINGI SKULI YA SEKONDARI KINUNI.


 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiweka Jiwe la Msingi Skuli ya Sekondari ya Kinuni.

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiwahutubia wananchi katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la msingi Skuli ya Sekondari Kinuni.
 WANAFUNZI wa Skuli ya Sekondari ya Kinuni wakiwa katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la msingi la Kinuni.
 WAZIRI wa Elimu Zanzibar , Mhe Riziki Pembe akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi katika hafla hiyo.


 KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu Zanzibar Dkt. Idrissa Muslim Hija akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Skuli hiyo.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi akisalimiana na wananchi walioudhuria katika hafla hiyo.
 BAADHI ya Wananchi walioudhuria katika Hafla hiyo ya uwekaji wa Jiwe la Msingi Skuli ya Kinuni.


 JENGO la Skuli ya Sekondari ya Kinuni lililowekwa Jiwe la Msingi.

 VIONGOZI mbali mbali wa CCM walioudhuria katika Hafla hiyo.

 VIONGOZI wa CCM na Wananchi kwa Ujumla wakiimba Wimbo wa Mashujaa katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi katika Skuli ya Sekondari Kinuni.




NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amesema mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Elimu nchini yanatokana na Utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Kauli hiyo ameitoa wakati akiweka jiwe la msingi katika Skuli ya Sekondari ya Kinuni iliyopo Wilaya ya Magharibi ‘’B’’ Unguja, amesema ujenzi wa skuli hiyo ya Ghorofa ambayo ni ya kisasa ni hatua kubwa ya kimaendeleo katika sekta ya elimu.

Alisema CCM kupitia Ilani yake imeahadi kuimarisha Sekta ya Elimu kwa kuimarisha miundombinu ya upatikanaji wa elimu ikiwemo kujenga majengo ya kisasa yanayoendana na kasi ya maendeleo katika zama za sasa.

Alibainisha kuwa Serikali ya awamu ya saba inaendeleza kwa vitendo falsafa ya elimu bila ya malipo iliyoasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Aman Karume kwa lengo la kukuza kiwango cha elimu.

Alisema serikali ya ASP ilitangaza elimu bure kwa lengo la kuwakomboa watoto wa Waafrika waliokoseshwa fursa ya elimu kwa makusudi na utawala uliokuwa ukitawala kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Dk.Shein alisema pamoja na maendeleo yanayopatikana katika sekta za elimu bado zipo changamoto zinazoendelea kutatuliwa zikiwemo upungufu wa madarasa, madawati pamoja na upungufu wa walimu hasa wa masomo ya Sayansi.

Alisema Zanzibar kwa sasa imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika sekta ya elimu ikilinganishwa na kabla ya Mapinduzi kwani na skuli za msingi 62 na skuli za sekondari nne lakini kwa sasa idadi imekuwa ni kubwa hadi hatua ya kuwa na Vyuo vikuu vinavyozalisha wataalamu wa kada tofauti kila mwaka.

Alisema serikali inawasomesha walimu wa masomo ya Sayansi kupitia Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) ili watakapohitimu masomo yao wafundishe katika skuli mbali mbali za msingi na sekondari kwa lengo la kumaliza tatizo la kutofaulu masomo ya Sayansi kutokana na upungufu wa walimu kwa baadhi ya Skuli.

Pamoja na hayo alieleza kuwa katika juhudi za kutatua changamoto ya upungufu wa madawati serikali imeagiza Madawati 22,000 kutoka nchini China,  yatakayogawiwa katika Skuli zenye changamoto hiyo nchi nzima.

“Elimu ndio msingi wa maendeleo ya mwanadamu yeyote na ndio maana baada ya waasisi wetu kufanya Mapinduzi ya Mwaka 1964, kwa lengo la kuondosha vitendo vya ubaguzi na kuwapatia elimu vijana wa makundi yote bila ubaguzi.”, alisema Dk. Shein.

Dk.Shein alipiga marufuku ya tabia ya kuchangishwa fedha kwa wanafunzi na kueleza kwamba mwalimu au kiongozi yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Pia ameziagiza Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar kujenga barabara ya lami ya Kinuni ndani inayofika katika Skuli hiyo.  

Akizungumza Waziri wa Elimu Zanzibar  Riziki Pembe Juma, alisema Wizara hiyo inaendelea na mikakati endelevu ya kufanya mageuzi makubwa ya kimaendeleo katika sekta ya elimu nchini.

Waziri Riziki alieleza kuwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 Serikali imeahidi kujenga skuli 10 za Ghorofa na kwa sasa tayari tisa zinajengwa ambapo skuli ya kumi nayo itaanza kujengwa siku za hivi karibuni.

Awali akizungumza Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Zanzibar  Dkt. Idrissa Muslim Hija amesema ujenzi wa skuli hiyo mpya ya Sekondari ya Kinuni ni miongoni mwa Skuli Tisa zinazojengwa nchini ambapo kwa upande wa Unguja zinajengwa tano na kwa upande wa Pemba zinajengwa nne.

Alisema Skuli hizo zinajengwa kwa ushirikiano wa karibu baina ya SMZ na wadau wa maendeleo ambapo jumla ya Dola milioni 10.2 zimetolewa na shirika la Opec Fund for internation Development kati ya hizo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa asilimia 11.17 na zaidi ya bilioni 2.8 zitatumika katika ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Kinuni.

Pamoja na hayo alisema Skuli ya Kinuni itakuwa ya Ghorofa moja yenye Madarasa 14, Maabara tatu, Maktaba moja, Ofisi za Walimu pamoja na miundombinu ya Watu wenye ulemavu.

Dkt. Idrissa alifafanua kwamba lengo la ujenzi wa Skuli hizo ni kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani ili wapate mazingira rafiki ya kujifunza na kufaulu vizuri katika mitihani.

Akizitaja skuli tisa zinazojengwa kupitia mradi huo Unguja ni Skuli za Sekondari Kinuni, Fuoni, Mwembe shauri, Chumbuni na Bububu kwa upande wa Pemba ni Skuli za Wale,mwambe, Kizimbani na Micheweni.

Uwekaji wa Jiwe la msingi katika skuli ya Kinuni ni miongoni mwa maadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya Elimu bila malipo Zanzibar, na Skuli zote tisa zinatarajiwa kuzinduliwa rasmi katika sherehe za kilele cha Maadhimisho ya miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar  Januari 12, mwaka 2019.


Jumapili, 16 Septemba 2018

MAANGAIKO YATWAA UBINGWA MABODI CUP.


 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi (kushoto) akimkabidhi Kombe la ushindi nahodha wa Timu ya Maangaiko ndugu Mkongea Mohamed Hamada (kulia) mara baada ya timu  hiyo kushinda wa penalti 4-2 dhidi ya timu ya Ubina katika Fainali ya Ligi ya Mabodi CUP iliyochezwa Kajengwa Makunduchi Unguja.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi (kushoto) akimkabidhi Kombe la ushindi nahodha wa Timu ya Ubina ndugu Haji Kheri Ussi  (kulia) ambaye Timu yake imeibuka msindi wa pili katika ligi ya Mabodi CUP.
WANANCHI wa vijiji mbali mbali vya Jimbo la Makunduchi walioudhuria katika mechi ya Fainali za kombe la Mabodi CUP wakishuhudia utoaji wa zawadi mbali mbali kwa timu zilizoshiriki mashindano hayo.
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akisalimiana na wachezaji wa Timu ya Maangaiko katika Fainali za ligi ya Mabodi CUP.


 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akisalimiana na waamuzi wa mchezo wa Fainali hiyo ya ligi ya Mabodi CUP.


 WASHIRIKI wa mbio za magunia wakionyesha uwezo wao katika kiwanja cha Uhuru katika fainali hizo za Mabodi CUP.


 TIMU za Ubina na Maangaiko wakitimua vumbi katika mchezo huo wa Fainali za ligi ya Mabodi CUP 2017-2018.

WASHIRIKI wa mchezo wa kuvuta kamba wakionyesha uwezo wao katika fainali hizo za Mabodi CUP 2017-2018.





NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla (Mabodi) amewataka vijana kuchangamkia fursa za ajira zilizopo katika sekta ya michezo nchini.

Rai hiyo ameitoa wakati akifunga  fainali ya Mechi za ligi ya Mabodi Cup iliyochezwa katika uwanja wa Uhuru uliopo Kajengwa Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja.

Dk.Mabodi amesema CCM inaendelea kusimamia ipasavyo Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 katika kuimarisha sekta ya michezo kwa kujenga Viwanja  vya kisasa vya michezo katika maeneo mbali mbali nchini.

Akizungumzia historia fupi ya ligi hiyo kuwa imeasisiwa na Marehemu Juma Abdulla Saadalla Mabodi kwa lengo la kudumisha mshikamano kwa wananchi wote wa Vijiji vya Makunduchi.

Alisema ni muhimu kwa wananchi hao hasa vijana kuthamini na kuendeleza tunu za maendeleo zilizoasisiwa na Wazee wa vijiji vya Jimbo la Makunduchi kwa sababu jitihada zao haziwezi kulipwa ila zithaminiwezi kuwarithisha vijana.

"Endelezeni ligi hii iwe  miongoni mwa chachu  za kuleta Umoja na Mshikamano na isiwe chanzo cha mifarakano kwani aliyeasisi ligi hii hakuwa na nia mbaya bali alitaka kuimarisha  Muungamo wa wanavijiji wanaoshi ndani na nje ya makunduchi.

Pia Sekta ya  Michezo inaimarika kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, chini ya Uongozi wa Serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.", alisema Dk.Mabodi.

Alisema Jimbo la Makunduchi limekuwa ni kitovu cha kuenzi utamaduni wa asili ulioasisiwa na wazee wa vijiji vilivyomo katika Jimbo hilo hatua inayotakiwa kuendelezwa kwa vitendo na vijana wa sasa.

"Wazee wetu wametuachia vitu muhimu vya asili tunavyotakiwa kuvienzi kwa mfano ligi hii ya Mabodi Cup, Hasnuu Makame CUP, Sherehe za Mwaka kogwa pamoja na tamasha la vyakula vya asili linalowaunganisha wananchi wa Makunduchi na vijiji jirani." alisema.

Aidha aliwasihi wananchi wa jimbo hilo kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeo yanayoletwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya usimamizi mzuri wa CCM.

Dk.Mabodi  alisikishwa na kukemea vikali kuibuka kwa utashi binafsi wa kuigawa ligi hiyo katika makundi mawili  na kuagiza ligi hiyo iwe na jina moja la Mabodi CUP lenye uongozi mmoja na ligi nyingine yoyote itakayoibuka itafutiwe jina jingine mbadala kwa ajili ya kuimarisha ushindani wa kimichezo.

Dk. Dk.Mabodi aliahidi kushiriki kikamilifu katika kuendeleza ligi hiyo iweze kutoa wachezaji wenye vipaji vya kucheza katika timu kubwa za kitaifa na kimataifa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini Unguja anayekaimu  Wilaya Kusini Unguja Rajab Ali Rajab alisema michezo ni sekta muhimu inayodumisha urafiki na afya za vijana.

Akizungumza Mgeni mwalikwa ambaye ni Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SSP) Mkoa wa Kilimanjaro Haji Miraj Abdallah alisema michezo ni sehemu muhimu ya kuwaunganisha vijana wa vikundi mbali mbali kuwa wamoja katika kulinda maslahi ya nchi.

SSP Haji aliwashauri vijana hao kujiepusha na vikundi viovu badala yake watumie vizuri vipaji vyao  kupitia michezo kwa kujiajiri wenyewe.

Awali mechi hiyo ya fainali katika ligi ya Mabodi CUP 2017-2018 ilizikutanisha timu mbili za Ubina na Maangaiko ambazo zote zilionyesha ujuzi wa soka na kumaliza mechi wakiwa wametoka sare ya 1-1.

Baada ya matokeo hayo mechi hiyo ilienda katika hatua ya penalti ambapo timu ya Maangaiko ilishinda kwa goli 4-2 dhidi ya timu ya Ubina.

Kupitia michuano hiyo Timu ya Maangaiko ambayo ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo walipata zawadi ya Shilingi milioni moja na kikombe cha mshindi wa kwanza na timu ya Ubina imepata shilingi 500,000 pamoja na kikombe cha mshindi wa pili.

Pia mshindi wa tatu alipata shilingi 300,000 mshindi wa nne amepata shilingi 200,000 ambapo timu nne zilizoshiriki mashindano hayo kila timu imepewa kiasi cha shilingi 75,000.

Katika fainali hiyo pia ilipambwa na michezi mingine ikiwemo ya kuvuta kamba pamoja na mbio za magunia ambapo kila mshindi wa kwanza katika timu za michezo hiyo amezawadiwa kiasi cha shilingi 50,000.


Jumatatu, 10 Septemba 2018

CATHERINE: AKEMEA UPOTOSHAJI KUHUSU UUZAJI WA KADI ZA CCM

 KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi Ndugu Catherine Peter Nao.



KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar ndugu Catherine Peter Nao amesema kadi za CCM haziuzwi wala sio kibali cha kutoa ajira bali zinapatikana kwa utaratibu uliowekwa Kikatiba.

Amesema serikali inatoa ajira kwa utaratibu wake iliyojiwekea kwa kuangalia vigezo na sifa za kitaaluma walizonazo waombaji wa ajira hizo lakini sio kwa vigezo vya kuwa na kadi ya Chama Cha Mapinduzi.

Amefafanua kwamba sharti la msingi kwa mtu yeyote kupata kadi ya CCM ni lazima  akubali kupewe mafunzo ya Itikadi kwa muda wa  miezi mitatu na sio kama wanavyopotosha baadhi ya watu wasiyoitakia mema CCM na serikali zake. 

Ufafanuzi huo ameutoa leo wakati akizindua darasa la Itikadi la CCM Mkoa wa Mjini kichama, uliofanyika katika ukumbi wa CCM Mkoa iliyopo Amani. 

Amesema endapo  Chama Cha Mapinduzi  kitabaini kuwepo kwa baadhi ya viongozi ama wanachama wanaojihusisha na vitendo vya kuuza kadi hizo watachukuliwa hatua kali za kimaadili.

Ameongeza kuwa Chama kimeendelea kuimarika na kadi zote za wanachama zitawekwa katika mfumo wa kisasa utakaokuwa na taarifa zote za wanachama na wataweza kuzitumia kadi hizo hata kwa huduma nyingine za kijamii.

“Kadi ya CCM haiuzwi mtaani wala haitowi ajira hivyo wananchi msipotoshwe na baadhi ya wanasiasa waliofilisika kisiasa na kuanza kutengeneza ajenda za upotosha wananchi.”, amesisitiza Catherine.

Katibu huyo wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Cathenine amewataka vijana hao wanaopata mafunzo ya itikadi kuwa wavumilivu wakati wa masomo hayo ili wawe viongozi bora wa sasa na baadae walioiva itikadi, uzalendo, falsafa na historia halisi ya Zanzibar.

Ameeleza kwamba changamoto kubwa iliyopo kwa vijana wa sasa ni kuwa na tamaa ya kupata nafasi za uongozi bila kupitia katika mafunzo mbali mbali ya uongozi na itikadi yanayowajenga kuwa viongozi imara na wenye misimamo isiyoyumba juu ya maslahi ya nchi.

Akizungumzia suala la ajira Catherine ameeleza kuwa licha ya kuwa ajira bni changamoto ya dunia nzima lakini serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeendelea kutoa fursa mbali mbali za ajira kwa vijana kupitia sekta za umma na binafsi.

Catherine amewasihi vijana hao kuendelea kuiamini na kuunga mkono serikali ya awamu ya Saba chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein anayetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa wananchi wote bila ya ubaguzi wa kidini wala kikabila.

Kupitia uzinduzi huo Katibu huyo wa Idara ya itikadi na uenezi Zanzibar amesema CCM imejipanga vizuri kushiriki uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jan’gombe na kuhakikisha mgombea wa Chama hicho anaibuka mshindi na kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.

Katika juhudi za kuunga mkono Darasa hilo la itikadi Katibu huyo ametoa kiasi cha shilingi 350,000 kwa vijana hao ili ziwasaidie kugharamikia mahitaji mbali mbali katika mafunzo hayo.

Akizungumza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Ndugu Talib Ali Talib amesema Mkoa huo utaendelea kuwakusanya vijana mbali mbali kwa lengo la kuwajengea uwezo juu ya mafunzo mbali mbali yatakayowasaidia katika maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wake Katibu wa Siasa na Uenezi wa Mkoa wa Mjini  Ndugu Maulid Issa amesema mbali na vijana hao kupatiwa masomo ya itikadi pia wanapewa mafunzo mbali mbali ya ujasiriamali na mafunzo ya lugha za kigeni ili wanufaike na soko la utalii kwa kujiajiri wenye kwa wale wasiokuwa na ajira.

MATUKIO KATIKA PICHA MAKAMU MWENYEKITI WA UWT TAIFA BI.THUWAYBA AKIWA KTK KAMPENI ZA KUMNADI MGOMBEA UDIWANI WA CCM MONDULI MJINI


 MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa Bi.Thuwayba Kisasi akizungumza katika Mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea udiwani wa CCM Ndugu Julias Kalanga Kata ya Monduli Mjini.

BAADHI ya wananchi wakiwa katika Mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea udiwani wa CCM Julias Kalanga Kata ya Monduli Mjini.


MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa Bi.Thuwayba Kisasi akiwa sokoni kwa lengo la kumuombea kura Mgombea udiwani wa CCM Ndugu Julias Kalanga.

  

Jumanne, 4 Septemba 2018

DK.SHEIN AZINDUA JENGO LA KISASA LA USAJILI WA VITAMBULISHO

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Vituo vya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibar na Uzinduzi wa Uimarishaji Mfumo wa Usajili kieletroniki, kushoto Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Haji Omar Kheri, na kushoto Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, wakishuhudia hafla hiyo iliofanyika katika viwanja vya Ofisi hiyo Dunga Wilaya ya Kati Unguja.

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza kwenye uzinduzi wa jengo la Ofisi mpya ya Wilaya na Uimarishaji wa Mfumo wa Matukio ya Kijamii katika hafla iliyofanyika jana huko Dunga wilaya ya Kati. Kulia Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar Dk.Hussein Khamis Shaaban na (kushoto) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheri.



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema serikali inahitaji viongozi na watendaji wenye uadilifu na uaminifu, ili malengo yanayopangwa na kutekelezwa yaweze kufikiwa kwa ufanisi.

Dk. Shein ameeleza hayo wakati akizindua uimarishaji wa mfumo wa usajili, zoezi la kuimarisha taarifa za vitambulisho na Ofisi za Usajili za wilaya za wakala wa usajili wa matukio ya kijamii Zanzibar, huko Dunga wilaya ya Kati.

Amesema lazima watu wafanyekazi kwa kuheshimu na kuzingatia misingi ya utawala bora, miongozo ya kisheria na kuepuka vitendo vya upendeleo, kwani haviwezi kuleta mafanikio.

Dk. Shein amewataka watendaji wanaosimamia usajili kutekeleza vyema majukumu yao ya kazi, kwa kuongozwa na weledi bila ya kuwa na woga kwani wanajukumu la kukusanya takwimu sahihi.

Amesema mipango mizuri ya serikali katika masula ya kuimarisha maendeleo na huduma za wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na upatikanaji wa maji safi na salama inafikiwa kwa upatikanaji wa takwimu zilizosahihi.

Amewataka kutoruhusu utoaji mwanya kwa watu wanaotaka kughushi taarifa za kijamii, kwani itachangia kuharibu usalama wa nchi.

Amesema Zanzibar inahitaji amani na utulivu katika uimarishaji wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi hivyo wahakikishe lazima watu wote wanatoa taarifa vizuri na kwa usahihi.

Sambamba na hilo, amewataka watendaji kuhakikisha wakati wanapowahudumia wananchi wanatumia lugha nzuri zenye busara na hekma na ni vyema kuepuka tabia ya kuwakaripia.

Dk.Shein amesema, anafahamu katika utekelezaji wa mfumo huo mpya wa usajili kutajitokeza changamoto nyingi, hivyo aliwataka wasiogope na wahakikishe wanazipatia ufumbuzi kwa maslahi ya taifa.

Aidha amesema anafahamu jitahada zilizofanyika katika kuwasajili Wazanzibari 712,982 na kukusanya mapato ya milioni 154.726 katika mwaka 2017 hadi 2018 kutokana na malipo mbali mbali.




THUWAYBA: AHIMIZA MSHIKAMANO

 MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa, Thuwayba Kisasi akizungumza katika moja ya Mkutano wa UWT uliofanyika katika ukumbi wa Wilaya ya Amani, Unguja.


MAKAMU Mwenyekti wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa Taifa, Thuwayba Edington Kisasi amewataka akina mama kuepuka migawanyiko na makundi ndani ya CCM na badala yake kushirikiana katika kukijenga na kukiimarisha chama hicho.


Kisasi ameeleza hayo huko kwenye mkutano wa Baraza la Umoja wa Wanawake (UWT), wilaya ya Amani alipokuwa akifungua mkutano na akinamama wa Jumuiya hiyo.


Amesema iko haja ya kukemewa kuwepo kwa makundi ndani ya jumuiya hiyo, kwani hilo ni tatizo kwa Chama cha Mapinduzi na kwamba chama kinapomaliza uchaguzi kiungane kuwa kitu kimoja.


“Upo mtandao unaoendeleza migawainyiko na makundi ndani chama na jumuiya, lakini niwahakikishie kuwa hatua zitachuuliwa kwa wahusika wote waliounda makundi hayo”, alisema Makamu huyo.


Amewataka akinamama wajitambue thamani yao kwa kuwa ni tegemeo kubwa kwa CCM, familia na jamii, hivyo kanuni za chama hicho ziendelezwe hali ambayo itakifanya kiimarike zaidi.


Amewahimiza wanawake hao kujishughulisha na miradi ya maendeleo ambayo itawawezesha kujipatia kipato, hali itakayowaepusha na utegemezi hasa ikizingatiwa kuwa fursa za kujikomboa zipo.


Thuwaiba amekemea vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto na kuwataka akina mama kuhakikisha wanazidisha uangalizi kwa watoto na kuviripoti kwenye vyombo vya sheria ili wahusika wachukuliwe hatua.