Jumanne, 4 Septemba 2018

DK.SHEIN AZINDUA JENGO LA KISASA LA USAJILI WA VITAMBULISHO

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Vituo vya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibar na Uzinduzi wa Uimarishaji Mfumo wa Usajili kieletroniki, kushoto Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Haji Omar Kheri, na kushoto Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, wakishuhudia hafla hiyo iliofanyika katika viwanja vya Ofisi hiyo Dunga Wilaya ya Kati Unguja.

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza kwenye uzinduzi wa jengo la Ofisi mpya ya Wilaya na Uimarishaji wa Mfumo wa Matukio ya Kijamii katika hafla iliyofanyika jana huko Dunga wilaya ya Kati. Kulia Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar Dk.Hussein Khamis Shaaban na (kushoto) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheri.



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema serikali inahitaji viongozi na watendaji wenye uadilifu na uaminifu, ili malengo yanayopangwa na kutekelezwa yaweze kufikiwa kwa ufanisi.

Dk. Shein ameeleza hayo wakati akizindua uimarishaji wa mfumo wa usajili, zoezi la kuimarisha taarifa za vitambulisho na Ofisi za Usajili za wilaya za wakala wa usajili wa matukio ya kijamii Zanzibar, huko Dunga wilaya ya Kati.

Amesema lazima watu wafanyekazi kwa kuheshimu na kuzingatia misingi ya utawala bora, miongozo ya kisheria na kuepuka vitendo vya upendeleo, kwani haviwezi kuleta mafanikio.

Dk. Shein amewataka watendaji wanaosimamia usajili kutekeleza vyema majukumu yao ya kazi, kwa kuongozwa na weledi bila ya kuwa na woga kwani wanajukumu la kukusanya takwimu sahihi.

Amesema mipango mizuri ya serikali katika masula ya kuimarisha maendeleo na huduma za wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na upatikanaji wa maji safi na salama inafikiwa kwa upatikanaji wa takwimu zilizosahihi.

Amewataka kutoruhusu utoaji mwanya kwa watu wanaotaka kughushi taarifa za kijamii, kwani itachangia kuharibu usalama wa nchi.

Amesema Zanzibar inahitaji amani na utulivu katika uimarishaji wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi hivyo wahakikishe lazima watu wote wanatoa taarifa vizuri na kwa usahihi.

Sambamba na hilo, amewataka watendaji kuhakikisha wakati wanapowahudumia wananchi wanatumia lugha nzuri zenye busara na hekma na ni vyema kuepuka tabia ya kuwakaripia.

Dk.Shein amesema, anafahamu katika utekelezaji wa mfumo huo mpya wa usajili kutajitokeza changamoto nyingi, hivyo aliwataka wasiogope na wahakikishe wanazipatia ufumbuzi kwa maslahi ya taifa.

Aidha amesema anafahamu jitahada zilizofanyika katika kuwasajili Wazanzibari 712,982 na kukusanya mapato ya milioni 154.726 katika mwaka 2017 hadi 2018 kutokana na malipo mbali mbali.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni