Ijumaa, 21 Septemba 2018

DK.SHEIN AWEKA JIWE LA MSINGI SKULI YA SEKONDARI KINUNI.


 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiweka Jiwe la Msingi Skuli ya Sekondari ya Kinuni.

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiwahutubia wananchi katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la msingi Skuli ya Sekondari Kinuni.
 WANAFUNZI wa Skuli ya Sekondari ya Kinuni wakiwa katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la msingi la Kinuni.
 WAZIRI wa Elimu Zanzibar , Mhe Riziki Pembe akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi katika hafla hiyo.


 KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu Zanzibar Dkt. Idrissa Muslim Hija akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Skuli hiyo.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi akisalimiana na wananchi walioudhuria katika hafla hiyo.
 BAADHI ya Wananchi walioudhuria katika Hafla hiyo ya uwekaji wa Jiwe la Msingi Skuli ya Kinuni.


 JENGO la Skuli ya Sekondari ya Kinuni lililowekwa Jiwe la Msingi.

 VIONGOZI mbali mbali wa CCM walioudhuria katika Hafla hiyo.

 VIONGOZI wa CCM na Wananchi kwa Ujumla wakiimba Wimbo wa Mashujaa katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi katika Skuli ya Sekondari Kinuni.




NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amesema mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Elimu nchini yanatokana na Utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Kauli hiyo ameitoa wakati akiweka jiwe la msingi katika Skuli ya Sekondari ya Kinuni iliyopo Wilaya ya Magharibi ‘’B’’ Unguja, amesema ujenzi wa skuli hiyo ya Ghorofa ambayo ni ya kisasa ni hatua kubwa ya kimaendeleo katika sekta ya elimu.

Alisema CCM kupitia Ilani yake imeahadi kuimarisha Sekta ya Elimu kwa kuimarisha miundombinu ya upatikanaji wa elimu ikiwemo kujenga majengo ya kisasa yanayoendana na kasi ya maendeleo katika zama za sasa.

Alibainisha kuwa Serikali ya awamu ya saba inaendeleza kwa vitendo falsafa ya elimu bila ya malipo iliyoasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Aman Karume kwa lengo la kukuza kiwango cha elimu.

Alisema serikali ya ASP ilitangaza elimu bure kwa lengo la kuwakomboa watoto wa Waafrika waliokoseshwa fursa ya elimu kwa makusudi na utawala uliokuwa ukitawala kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Dk.Shein alisema pamoja na maendeleo yanayopatikana katika sekta za elimu bado zipo changamoto zinazoendelea kutatuliwa zikiwemo upungufu wa madarasa, madawati pamoja na upungufu wa walimu hasa wa masomo ya Sayansi.

Alisema Zanzibar kwa sasa imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika sekta ya elimu ikilinganishwa na kabla ya Mapinduzi kwani na skuli za msingi 62 na skuli za sekondari nne lakini kwa sasa idadi imekuwa ni kubwa hadi hatua ya kuwa na Vyuo vikuu vinavyozalisha wataalamu wa kada tofauti kila mwaka.

Alisema serikali inawasomesha walimu wa masomo ya Sayansi kupitia Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) ili watakapohitimu masomo yao wafundishe katika skuli mbali mbali za msingi na sekondari kwa lengo la kumaliza tatizo la kutofaulu masomo ya Sayansi kutokana na upungufu wa walimu kwa baadhi ya Skuli.

Pamoja na hayo alieleza kuwa katika juhudi za kutatua changamoto ya upungufu wa madawati serikali imeagiza Madawati 22,000 kutoka nchini China,  yatakayogawiwa katika Skuli zenye changamoto hiyo nchi nzima.

“Elimu ndio msingi wa maendeleo ya mwanadamu yeyote na ndio maana baada ya waasisi wetu kufanya Mapinduzi ya Mwaka 1964, kwa lengo la kuondosha vitendo vya ubaguzi na kuwapatia elimu vijana wa makundi yote bila ubaguzi.”, alisema Dk. Shein.

Dk.Shein alipiga marufuku ya tabia ya kuchangishwa fedha kwa wanafunzi na kueleza kwamba mwalimu au kiongozi yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Pia ameziagiza Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar kujenga barabara ya lami ya Kinuni ndani inayofika katika Skuli hiyo.  

Akizungumza Waziri wa Elimu Zanzibar  Riziki Pembe Juma, alisema Wizara hiyo inaendelea na mikakati endelevu ya kufanya mageuzi makubwa ya kimaendeleo katika sekta ya elimu nchini.

Waziri Riziki alieleza kuwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 Serikali imeahidi kujenga skuli 10 za Ghorofa na kwa sasa tayari tisa zinajengwa ambapo skuli ya kumi nayo itaanza kujengwa siku za hivi karibuni.

Awali akizungumza Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Zanzibar  Dkt. Idrissa Muslim Hija amesema ujenzi wa skuli hiyo mpya ya Sekondari ya Kinuni ni miongoni mwa Skuli Tisa zinazojengwa nchini ambapo kwa upande wa Unguja zinajengwa tano na kwa upande wa Pemba zinajengwa nne.

Alisema Skuli hizo zinajengwa kwa ushirikiano wa karibu baina ya SMZ na wadau wa maendeleo ambapo jumla ya Dola milioni 10.2 zimetolewa na shirika la Opec Fund for internation Development kati ya hizo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa asilimia 11.17 na zaidi ya bilioni 2.8 zitatumika katika ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Kinuni.

Pamoja na hayo alisema Skuli ya Kinuni itakuwa ya Ghorofa moja yenye Madarasa 14, Maabara tatu, Maktaba moja, Ofisi za Walimu pamoja na miundombinu ya Watu wenye ulemavu.

Dkt. Idrissa alifafanua kwamba lengo la ujenzi wa Skuli hizo ni kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani ili wapate mazingira rafiki ya kujifunza na kufaulu vizuri katika mitihani.

Akizitaja skuli tisa zinazojengwa kupitia mradi huo Unguja ni Skuli za Sekondari Kinuni, Fuoni, Mwembe shauri, Chumbuni na Bububu kwa upande wa Pemba ni Skuli za Wale,mwambe, Kizimbani na Micheweni.

Uwekaji wa Jiwe la msingi katika skuli ya Kinuni ni miongoni mwa maadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya Elimu bila malipo Zanzibar, na Skuli zote tisa zinatarajiwa kuzinduliwa rasmi katika sherehe za kilele cha Maadhimisho ya miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar  Januari 12, mwaka 2019.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni