NA EMMANUEL MOHAMED, ZANZIBAR.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,
Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar,Catherine Peter Nao,ametaja kipaumbele
chake ambacho anatarajia kuanza nacho katika utendaji wake ndani ya Chama Cha
Mapinduzi(CCM), kuwa atatekeleza kwa vitendo Ibara ya 5 ya Katiba ya Chama ya
mwaka 1977.
Amesema idara hiyo inawajibu wa
kutekeleza ibara hiyo inayoelekeza kufanya kazi ya kuhakikisha CCM inashinda
katika kila uchaguzi na kwamba ndio sehemu muhimu ya Chama kuwa na mafanikio
kisiasa.
Hayo ameyasema wakati
akikabidhiwa rasmi Ofisi, Kisiwandui na aliyekuwa Katibu wa Kamati Maalum ya
NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM, Zanzibar, Waride Bakari Jabu,ambaye ni
Mjumbe wa Halimashauri Kuu ya Chama (NEC).
Katibu huyo amewakumbusha
watumishi hao wa Idara hiyo kuwa wanatakiwa kutambua kuwa wako kwenye hatua ya
kuhakikisha wanatekeleza ibara hiyo ya Tano na si vinginevyo.
Katika maelezo yake hayo Katibu
huyo ameongeza kuwa Ibara hiyo inaeleza wazi na kutaka kuwa kila Uchaguzi
ukifika CCM inashinda katika serikali za mitaa hadi serikali kuu na kwamba kazi
ya Chama cha siasa ni kushinda na kushika Dola.
"Tuko hapa katika kutekeleza
ibara hii ya tano na kuwa lengo kuu ambalo linatukutanisha ni kukipigania Chama
chetu kishinde kwa kila Uchaguzi.
Pia namshukuru sana Makamu
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein kwa kuniamini na
akanichagua katika nafasi hii "alisema Katibu.
Mbali na hilo, Katibu huyo
amemshauri Katibu mstaafu wa Idara hiyo Bi. Waride kuendelea kutoa ushirikiano wake
kwa Idara na Chama kwa ujumla.
"Kuondoka kwako hapa
usinifungie milango bado ninakuitaji hii namna ya utaratibu wa chama chetu
katika kuhamishana mtu kutoka sehemu moja kwenda nyingine na ifahamike kuwa
bado una nafasi kubwa ya uongozi tena ya kimaamuzi ya juu ya chama bado
tutakuhitaji kwa namna moja ama nyingine,"amesema.
Amesema anatarajia kuendeleza mambo
mema yaliofanywa na mtangulizi wake huku akibuni mikakati mipya itakayosaidia
kurahisisha utendaji wa shughuli za Chama na Idara kwa ujumla.
Naye aliyekuwa Katibu wa Idara
hiyo Waride amesema katika kipindi cha muda wake wa kufanya kazi kwenye idara
hiyo alifanya jitihada za kuhakikisha chama inamiliki vyombo vyake vya habari
ikiwemo radio ya bahari ili kurahisisha kazi ya Uenezi.
Ameeleza kuwepo kwa vyombo vya
habari vya Chama, idara hiyo itasaidiwa kurahisisha utendaji wake wa kazi
ikiwemo kusambaza mambo mazuri yanayofanywa na CCM pamoja na Rais Dk.Shein na
kwamba imefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Waride amesema licha ya kuwepo na
changamoto mbali mbali za kiutendaji na kisiasa uongozi wake ulijitahidi kuimarisha
mazingira mazuri ya kusambaza taarifa na shughuli za Chama ili Wana CCM na
wananchi wajue utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2015/2020.
Hata hivyo Bi.Waride amemshauri Katibu
huyo mpya kuhakikisha anafanya kazi kwa ushirikiano na Watendaji wa ngazi mbali
mbali za Chama na Jumuiya zake kwa lengo la kufanikisha kwa ufanisi shughuli za
Chama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni